'
Thursday, September 19, 2013
SIMBA INATISHA
KUMEKUCHA. Simba inatisha. Hivyo ndivyo unavyoweza kuyayelezea matokeo ya mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara kati ya Simba na Mgambo JKT iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika mechi hiyo, Simba inayoundwa na wachezaji wengi wapya, iliibuka na ushindi mnono wa mabao 6-0 na kuishusha kwenye uongozi wa ligi hiyo, JKT Ruvu, ambayo jana ilichapwa bao 1-0 na ndugu zao wa Ruvu Shooting.
Ushindi huo mnono uliiwezesha Simba kukamata usukani wa ligi hiyo kwa kuwa na pointi 10 baada ya kucheza mechi nn, ikifuatiwa na JKT Ruvu na Ruvu Shooting zenye pointi tisa kila moja baada ya kucheza idadi hiyo ya mechi.
Mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Hamisi Tambwe aliibuka shujaa wa Simba na kuzawadiwa mpira baada ya kupachika wavuni mabao manne kati ya Sita. Mabao mengine mawili yalifungwa na Haruna Chanongo.
Tambwe, amekuwa kama mshambuliaji nguli wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo, ambaye juzi usiku aliiduwaza Galatasaray baada ya kufunga mabao matatu 'hat trick' katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.
Simba ilianza mchezo huo kwa kasi wakati Chanongo, alipobisha hodi langoni mwa Mgambo dakika ya nne kabla ya mabeki kutibua mpango wake ndani ya eneo la hatari.
Mfungaji bora wa Kombe la Kagame mwaka huu alipokuwa na kikosi cha Vital' O ya Burundi, Tambwe alianza kufunga bao dakika ya nne akiunganisha kwa kichwa krosi ya beki wa kushoto, Issa Rashid 'Baba Ubaya'.
Chanongo alifunga bao la pili dakika ya 32 kwa shuti baada ya kupata pasi ya Henry Joseph. Tambwe alipachika mabao mengine dakika za 41 na 44 kabla ya kufunga kwa penalti dakika ya 76.
Katika dakika ya 64, beki wa Mgambo, Bakari Mtama alijifunga wakati akiwa katika harakati za kuokoa shuti lililopigwa na Chanongo na kuipatia Simba bao la tano.
Simba ilicheza mchezo huo ikitokea katika furaha ya ushindi wa mabao 2-0, iliyopata dhidi ya wakata miwa wa Mtibwa Sugar kwenye uwanja huo mwishoni mwa wiki iliyopita.
Mgambo ilikosa bao dakika ya 49 baada ya Mohammed Neto kushindwa kumalizia pasi ya Adam Gila. Dakika ya 68, Salum Kipaga alipiga shuti nje akiwa ndani ya eneo la hatari la Simba.
Simba: Abel Dhaira, Miraji Adam, Issa Rashid, Gilbert Kaze, Joseph Owino, Henry Joseph/Ramadhan Chombo, Jonas Mkude, Amri Kiemba, Betramu Mwombeki, Hamisi Tambwe na Haruna Chanongo.
Mgambo: Kulwa Manzi, Francis Anyosisye, Salum Mlima, Bakari Mtama, Novat Lufunga, Salum Kipaga, Peter Mwalianzi, Mohammed Neto, Fulli Maganga na Salum Gila.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment