KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, September 30, 2013

SERIKALI INATUKWAMISHA KUJENGA UWANJA WA KISASA-YANGA


LEO tungependa kupitia kwenu kutoa taarifa kuhusu maendeleo ya mradi wetu wa Uwanja wa kisasa wa mpira katika Jiji la Jangwani kama itakavyojulikana
Mara ya mwisho tuliongea ama kuonana ilikuwa mwezi wa tatu wakati Ndugu zetu wa BCEG walipokabizi Concept design ama Usanifu wa awali na kuanzia sasa tutakuwa tunatoa taarifa za mara kwa mara kuhusu mradi huu. Wahenga walisema UKIACHA KUSEMA HUTATENDA JAMBO lakini pia KUKAA KIMYA SANA kunajenga hisia mbaya na kutoa nafasi ya upotoshwaji wa habari
Kwa kifupi napenda kuwakumbusha kuwa Makubalino ya Awali (Memorandum of Understanding) yalisainiwa 23 Novemba 2012. Pamoja na mengineyo YANGA inatakiwa:
· Kupata na kuwa na eneo la kutoshereza malengo ya mradi
· Kupata ushauri mzuri, michoro mizuri na mkandarasi mzuri wa mradi
· Kupata na kutenga fedha za kukamilisha usanifu na ujenzi wa mradi
Kwa upande wa BCEG wajibu wao ni kuwa na utaalamu na uzoefu wa kutosha. BCEG wameandaa na kukabidhi michoro ya usanifu wa awali kukidhi matakwa ya YANGA. YANGA tunatakiwa kutoa maoni yetu na na kuingia RASMI mkataba wa ujenzi.
Kutokana na kukua kwa Jiji la Dar es Salaam, na katika hali ya kutaka klabu iwe na vitega uchumi klabu imeonelea ni vyema kama ingekuwa na uwanja wa mpira wa karne ya sasa na baadaye ambao pamoja na mambo mengine utakuwa na mioundombinu ifuatayo:-
1. Uwanja wa mpira wenye viti 40,000
2. Hostel ya wachezaji na football academy ya vijana
3. Viwanja vya mazoezi
4. Uwanja wa kutosha kuegesha magari
5. ­­­­­Hoteli na sehemu ya makazi
6. Ukumbi wa mikutano
7. Sehemu ya maofisi, benki, zahanati (sports clinic)
8. Maduka, supermarket na sinema
9. Sehemu za kubarizi, kupumzikia (Recretional and Open spaces)
Mara baada ya azma yetu kukamilika eneo hili litaitwa “Jangwani City” na kufanya wakazi wa maeneo ya Jangwani na sehemu za jirani wasiende maeneo ya mbali kutafuta huduma muhimu za kijamii. Eneo hili litaboresha mandhari nzima ya Jangwani kwa kukuza mazingira na miundombinu. Hii itahusu pamoja na mambo mengine ujazaji udongo (tuta kubwa), upandaji miti, bustani za kubarizi, kuboresha mifereji ya majitaka na kudhibiti mafuriko ya eneo la Jangwani na hivyo kulipatia sura ya kibiashara na kitalii.
Ili kukamilisha azma ya kuwa na Jangwani City itakayo kuwa na miundombinu yote hiyo, Uongozi ulipeleka maombi ya eneo la nyongeza Manispaa ya Ilala na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa barua zenye kumbukumbu namba YASC/ARDHI/MWK/YM/46/2012 na YASC/ARDHI/MWK/YM/47/2012 za 12 Desemba 2012, na mpaka sasa bado maombi yetu hayajajibiwa.
Mwezi wa saba, Wadhamini/Uongozi wa YANGA walimwandikia Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kuomba msaada wake kufanikisha maombi ya nyongeza ya kiwanja yaliyowasilishwa Manispaa ya Ilala na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Klabu ya Yanga ina kiwanja chenye ukubwa wa hekta 3.59 eneo la Jangwani. Kiwanja hiki kina hati miliki kwa miaka 99 toka mwaka 1972 na katika eneo hilo, klabu ilifanikiwa kujenga uwanja wa mpira wa Kaunda na Jengo la klabu la ghorofa tatu. Jengo hili lilijengwa kwa ufadhili mkubwa sana wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume (Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi) na michango ya wanachama na wapenzi wa klabu ambao kila siku wamekuwa wakiamini kuwa haba na haba hujaza kibaba.
Ndugu Wandishi wa habari kwa kifupi tumefikia hapo, zoezi la kutoa maoni yetu kuhusu michoro ya usanifu wa awali na kuingia rasmi mkataba wa ujenzi na BCEG limesimama, likisubiri majibu ya nyongeza la eneo. Ni matumaini yetu zoezi hili litakamilika hivi karibuni na kuendelea na mradi.
 YANGA DAIMA MBELE NYUMA MWIKO
Dar es Salaam, 30 September 2013
Francis Mponjoli Kifukwe

BREAKING NEWSSSSS....MPIGA GITA LA BESI JOSEPH WATUGURU AFARIKI



MPIGA gita la besi wa bendi ya muziki wa dansi ya WK Sound, Joseph Watuguru amefariki dunia.
Watuguru alifariki dunia jana asubuhi nyumbani kwake Mabibo mjini Dar es Salaam baada ya
kuugua ugonjwa wa kifua kikuu.

Mmiliki wa bendi hiyo, Wiston Kagusa alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, marehemu Watuguru alianza kuugua ugonjwa huo wiki mbili zilizopita kabla ya kufariki dunia.

Kwa mujibu wa Kagusa, afya ya Watuguru ilianza kudhoofika mwezi uliopita
na baada ya kwenda kufanyiwa uchunguzi katika hospitali ya Amana, iligundulika kwamba alikuwa na kifua kikuu.

Kwa mara ya mwisho, mwanamuziki huyo alipanda jukwaani na bendi hiyo wiki mbili zilizopita katika ukumbi wa Safari ulioko Mbagala, Dar es Salaam.

Kagusa alisema taratibu za mazishi zinatarajiwa kufanyika kesho nyumbani kwa marehemu.
Marehemu Watuguru alianza kujipatia umaarufu miaka ya 1990 alipokuwa katika bendi ya Mchinga Sound, iliyokuwa ikiongozwa na Muumin Mwinjuma.

Alikuwa mmoja wa wapiga gita mahiri la besi nchini, kiasi kwamba Muumin alikuwa akipenda kutaja jina lake katika nyimbo mbalimbali za Mchinga Sound.

Habari zaidi zitafuata baadaye.

Sunday, September 29, 2013

SIMBA MATAWI YA JUU




MABAO yaliyofungwa na washambuliaji Hamisi Tambwe na Ramadhani Singano 'Messi' leo yameiwezesha Simba kuzidi kujichimbia kileleni mwa ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kuichapa JKT Ruvu mabao 2-0.

Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Simba ilikwenda mapumziko ikiwa mbele kwa bao 1-0.

Tambwe aliifungia Simba bao la kwanza dakika ya 24 kwa njia ya penalti baada ya beki jamal Saidi wa JKT Ruvu kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari. Bao hilo lilikuwa la saba kwa Tambwe msimu huu.

Singano aliihakikishia Simba ushindi dakika ya 49 baada ya kuifungia bao la pili baada ya gonga safi kati ya Tambwe na Abdulrahim Humud.

Ushindi huo umeiwezesha Simba kuendelea kuongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 14 baada ya kucheza mechi sita, ikifuatiwa na Kagera Sugar yenye pointi 11.

Simba: Abbel Dhaira, Haruna Shamte, Adeyoum Seif, Kaze Gilbert, Joseph Owino, Abdulhalim Humud, Amri Kiemba/Ramadhani Singano, Said Ndemla, Betram Mombeki/Miraj Madenge, Amisi Tambwe na Haroun Chanongo/Marcel Kaheza.

JKT Ruvu: Shaaban Dihile, Damas Makwaya, Stanley Nkomola, Omar Mtaki, Jamal Said, Nashon Naftali, Alhaj Zege, Emanuel Swita/Richard Msenya, Bakari Kondo/Paul Ndauka, Salum Machaku na Emanuel Pius.

Katika mechi zingine za ligi hiyo zilizochezwa leo, Azam FC imetoka sare ya 1-1 na Prison wakati Ashanti United imetoka sare ya 2-2 na Mtibwa Sugar.

NGASA AREJESHA NEEMA YANGA



BAO lililofungwa na mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Hamisi Kiiza jana liliiwezesha Yanga kuibuka na ushindi wa pili katika michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kuichapa Ruvu Shooting bao 1-0.

Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Kiiza alifunga bao hilo baada ya kazi nzuri iliyofanywa na Mrisho Ngasa.

Mechi hiyo ilikuwa ya kwanza kwa Ngasa kuichezea Yanga msimu huu baada ya kumaliza adhabu ya kufungiwa kucheza mechi sita na kutozwa faini ya sh. milioni 45.

Ngasa alipewa adhabu hiyo baada ya kubainika kuwa, aliingia mkataba na Simba na kulipwa sh. milioni 30. Alitakiwa kulipa sh. milioni zingine 15 kama riba.

Katika mechi nyingine za ligi hiyo zilizochezwa jana, Mbeya City ilitoka sare ya bao 1-1 na Coastal Union kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.

Coastal walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya saba kupitia kwa Haruna Moshi ‘Boban’ kabla ya Mbeya kusawazisha kupitia kwa Mwagane ‘Morgan’ Yeya dakika ya 70.

Katika mchezo huo, Richard Peter wa Mbeya City na Markus Ndeheli na Haruna Moshi wa Coastal walipewa kadi nyekundu.

Rhino Rangers ya Tabora ilipata kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Kagera Sugar katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.

BINTI WA UFILIPINO ATATWAA TAJI LA MREMBO WA DUNIA 2013




BALI, Indonesia

MREMBO kutoka Philippines, Megan Young jana usiku alitawazwa kuwa mrembo wa 63 kutwaa taji la mrembo wa dunia, baada ya kuwabwaga washiriki wenzake 127 kutoka nchi mbalimbali duniani.

Shindano hilo lililofanyika kwenye kisiwa cha Bali, liliwekewa ulinzi mkali kufuatia maandamano ya kulipinga yaliyofanywa na waislamu wenye msimamo mkali.

"Naahidi kuwa mrembo bora wa dunia, ambaye hajapata kutokea,"alisema Young (23) baada ya kutangazwa kuwa mshindi wa taji hilo.

Kauli yake hiyo ilipokelewa kwa shangwe kubwa na mashabiki kutoka Ufilipino waliosafiri naye kwenda Bali, huku wakirukaruka kwa furaha na kupunga bendera za nchi hiyo hewani.

Licha ya kuwepo kwa tishio la kuvuruga mashindano hayo kutoka kundi la Waislamu wenye msimamo mkali, polisi walisema hakukuwa na maandamano yoyote yaliyofanyika jana.



Kwa wiki kadhaa, kundi hilo lilikuwa likiitaka serikali ifute mashindano hayo kwa sababu yanakwenda kinyume na mafundisho ya dini ya kiislamu.

Washiriki wanne walitolewa mapema kabla ya fainali ya shindano hilo kutokana na kuwa wagonjwa. Washiriki walipita stejini wakiwa wamevaa mavazi ya kutokea nyakati za usiku.

Young, ambaye ametwaa taji hilo kutoka kwa mshindi wa mwaka jana, Wenxia Yu kutoka China, alizaliwa Marekani. Alihamia Philippines akiwa na umri wa miaka 10. Amewahi kushiriki mara kadhaa kwenye vipindi vya televisheni vya nchi hiyo.

Mshindi wa pili wa taji hilo ni Marine Lorphelin (20) kutoka Ufaransa wakati Mghana, Carranzar Naa Okailey Shooter (22) alishika nafasi ya tatu.

Saturday, September 28, 2013

NGASA AKATA MZIZI WA FITINA, AILIPA SIMBA MIL 45/-, KUICHEZEA YANGA LEO


Mrisho Ngasa akikabidhiwa jezi ya Yanga baada ya kurejea rasmi kwenye klabu hiyo msimu huu.


MSHAMBULIAJI Mrisho Ngasa wa Yanga anatarajiwa kuanza kuonekana rasmi uwanjani leo baada ya kulipa deni la sh. milioni 45 kwa klabu ya Simba.

Ngasa atashuka dimbani leo kuichezea Yanga katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Ruvu Shooting, itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mshambuliaji huyo alifungiwa kucheza mechi sita baada ya kamati ya sharia, katiba na hadhi za wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kubaini kwamba alitia saini mkataba wa kuichezea Simba na kulipwa sh. milioni 30.

Kamati hiyo ilimtaka Ngasa arejeshe fedha hizo pamoja na kulipa fidia ya sh. milioni 15 na mshambuliaji huyo, ametekeleza hilo.

Ngasa aliwasilisha fedha hizo makao makuu ya TFF jana saa tisa alasiri akiwa amefuatana na Ofisa Habari wa klabu hiyo, Baraka Kizuguto na Mhasibu, Rose Msamila.

Akizungumza baada ya kukabidhi hundi ya fedha hizo, Ngasa alisema hana kinyongo na Simba licha ya kumsainisha mkataba mpya bila kujijua.

Alisema alikubali kutia saini mkataba huo akielewa kwambani wa mkopo, kumbe Simba walimsainisha mkataba mpya wa mwaka mmoja kinyume na makubaliano kati yao.

Ametoa mwito kwa wanasoka wa Tanzania, wasikubali kutia saini mikataba na klabu bila ya kuwashirikisha wanasheria.

Alisema ni vyema kwa mchezaji kutia saini kitu anachokielewa badala ya kulazimishwa ama kushawishiwa kufanya hivyo bila kujua lolo.

Pambano kati ya Yanga na Ruvu Shooting linatarajiwa kuwa gumu kutokana na kila timu kupania kushinda ili kujiweka kileleni kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Ruvu Shooting inashika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi tisa baada ya kucheza mechi tano, sawa na timu za JKT Ruvu, Azam na Coastal Union. Yanga ni ya tisa ikiwa na pointi sita.
Mrisho Ngasa akikabidhiwa jezi namba 16 ya Simba na aliyekuwa makamu mwenyekiti wa klabu hiyo, Geofrey Nyange 'Kaburu'

KAMATI YA MAADILI TFF YATOA UAMUZI



Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imetangaza hukumu ya mashauri nane yaliyowasilishwa mbele yake kwa kumsafisha mlalamikiwa mmoja, kutowaadhibu zaidi washtakiwa sita na kuahirisha kusikiliza shauri moja baada ya mlalamikiwa kutokuwepo.

Riziki Juma Majala, ambaye ni Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) ndiye pekee aliyesafishwa na Kamati ya Maadili dhidi ya mashtaka ya kutoa kauli zilizosababisha kufunguliwa kwa kesi dhidi ya TFF.

Vilevile Kamati imesita kuwachukulia hatua Shafii Dauda, Nazarius Kilungeja, Wilfred Kidao, Omar Isaak Abdulkadir na Kamwanga Tambwe kutokana na kuridhika kuwa wameshaadhibiwa kwa kuenguliwa kwenye uchaguzi, hivyo hawawezi kuadhibiwa mara mbili.

Pia imesema haiwezi kumuadhibu Richard Julius Rukambura, aliyeshtakiwa kwa kukiuka Katiba ya TFF kwa kosa la kufungua kesi mahakamani, baada ya kubaini kuwa si mwanafamilia wa TFF kutokana na kuenguliwa kwenye uchaguzi.

Hoja hiyo pia ilitumika kutomchukulia hatua Dauda na mwamuzi wa zamani Omar Abdulkadir kwa hoja kuwa walipoteza sifa za kuwa wanafamilia wa TFF baada ya kuenguliwa kwenye uchaguzi na Kamati ya Uchaguzi.

Shauri la Omary Mussa Mkwaruro la tuhuma za kutumia cheti cha elimu kisichotambuliwa na mamlaka husika, limeahirishwa kutokana na Mlalamikiwa kutowasilisha utetezi wake, hivyo Kamati imeagiza Sekretarieti kuwasiliana naye ili awasilishe maelezo yake.

Watu hao walifikishwa mbele ya Kamati ya Maadili baada ya kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi wa TFF na baada ya usaili walibainika kuwa na matatizo ya kimaadili, hivyo ili iamue juu ya hadhi yao katika familia ya mpira wa miguu kwa kuwachukulia hatua au kuwaweka huru.
Katika hukumu iliyotolewa leo (Septemba 26 mwaka huu), Kamati ya Maadili imeeleza kuwa Majala hakiuka Kanuni za Maadili kwa kuwa vielelezo vilivyowasilishwa na TFF vinaonyesha kuwa klabu ya Kiluvya United imesajiliwa na Serikali na vyama wanachama wa TFF.

Kuhusu Rukambura, ambaye alilalamikiwa kwa kuipeleka TFF kwenye mahakama ya kiraia, hivyo kukiuka Kanuni ya 73 (3) (b) ya Kanuni za Maadili, Kamati imesema ushahidi uliowasilishwa na TFF hauonyeshi kama mgombea ni mwanafamilia wa TFF; alishaondolewa katika uchaguzi na hivyo si kati ya wagombea na hivyo mikono ya Kamati kufungwa kwa mujibu wa kanuni ya pili ya Kanuni za Maadili.

Kamati pia imeeleza kuwa Kanuni ya 73 (3) ambayo ingepaswa kutumika kumchukulia hatua, chimbuko lake ni Ibara ya 75 ya Katiba ya TFF ambayo inawalenga wanachama tu na hivyo kuamua kuwa malalamiko hayo hayana mashiko na kwani Rukambura alishapoteza sifa za kuwa mwanafamilia na hivyo kushindwa kumchukulia hatua.

Kidao alishtakiwa kwa kosa la kumiliki nyaraka za Kamati ya Utendaji kinyume na taratibu na pia kuwasilisha malalamiko yake Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) bila ya kufuata taratibu, lakini Kamati imesema kwa vile mlalamikiwa ameenguliwa kwenye uchaguzi, anatumikia adhabu ya kinidhamu na hivyo haiwezi kumuadhibu mara mbili.

Kuhusu Shafii Dauda, Kamati imesema malalamiko dhidi yake hayana mashiko kwa kuwa si mwanafamilia wa TFF na kwamba lalamiko dhidi yake linatupiliwa mbali kwa kuwa tayari ameshaondolewa kwenye uchaguzi kutokana na kosa la kinidhamu.

Kamati iliona hakukuwa na haja ya kushughulikia mashauri dhidi ya Nazarius Kilungeja, ambaye alishtakiwa kwa kukaidi maagizo ya vyombo halali vya TFF, na Kamwanga Tambwe kwa kuwa tayari wawili hao wanatumikia adhabu ya kufungiwa na Kamati ya Nidhamu.

Thursday, September 26, 2013

NGASA KUREJEA DIMBANI JUMAMOSI



MSHAMBULIAJI Mrisho Ngasa wa Yanga anatarajiwa kurejea dimbani keshokutwa wakati timu hiyo itakapomenyana na Ruvu Shooting katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Akizungumza na Burudani mjini Dar es Salaam jana, Ngasa alisema uongozi wa Yanga umekubali kumlipia deni la sh. milioni 45 anazodaiwa na klabu ya Simba pamoja na faini.

Ngasa alisema alifikia makubaliano hayo na Mwenyekiti wa Yanga, Yussuf Manji wakati wa kikao cha faragha kati yao kilichofanyika juzi kwenye hoteli ya Serena mjini Dar es Salaam.

"Namshukuru mwenyekiti wangu kwamba tumeshakubaliana kuhusu suala hilo na pesa hizo zinaweza kupelekwa TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) wakati wowote,"alisema.

Ngasa alifungiwa kucheza mechi sita za ligi na kutakiwa kurejesha sh. milioni 30 alizolipwa na Simba pamoja na faini ya sh. milioni 15. Jumla ya fedha alizotakiwa kulipa ni sh. milioni 45.

Awali, kulikuwepo na taarifa kwamba, Manji alikataa kumlipia Ngasa fedha hizo na kumtaka azilipe mwenyewe. Manji anadaiwa kuweka msimamo huo, alipokutana na Ngasa mjini Mbeya wiki mbili zilizopita.

Lakini baada ya kikao cha juzi, pande hizo mbili zilikubaliana kuhusu taratibu za kulipa fedha hizo ili kumwezesha mchezaji huyo arudi dimbani kuisaidia timu yake.

Ngasa hakuwa tayari kutaja utaratibu huo, lakini habari za uhakika zimeeleza kuwa, amekubali kukatwa sh. 500,000 kila mwezi katika mshahara wake ili kufidia deni hilo. Ngasa analipwa mshahara wa sh. milioni mbili kila mwezi.

Mshambuliaji huyo alimweleza Manji kuwa, ana hamu ya kuanza kuitumikia Yanga baada ya kumaliza adhabu yake ya kutocheza mechi sita aliyopewa na TFF.

Alipoulizwa jana kuhusu makubaliano hayo, Manji alijibu kwa ufupi akisema: "Subirini, akicheza mtamuona."

MANJI ALIPUA BOMU YANGA


MWENYEKITI wa klabu ya Yanga, Yussuf Manji amewataka wachezaji wa timu hiyo kubadilika na kuhakikisha wanashinda mechi zote zilizosalia za michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara.

Manji alitoa agizo hilo juzi alipokutana na wachezaji wa timu hiyo pamoja na benchi la ufundi na kula nao chakula cha usiku kwenye hoteli ya Serena mjini Dar es Salaam.

Habari za uhakika kutoka ndani ya kikao hicho zimeeleza kuwa, Manji aliwaeleza wachezaji pamoja na benchi la ufundi kwamba hajafurahishwa na mwenendo wa timu hiyo katika ligi kuu hadi sasa.

Kwa mujibu wa habari hizo, Manji aliwaeleza wachezaji hao kwamba, timu ilicheza vizuri katika baadhi ya mechi alizozishuhudia, lakini haelewi kwa nini imekuwa ikikosa ushindi.

Mwenyekiti huyo wa Yanga anadaiwa kuwaeleza wachezaji hao kwamba, anahisi kuna njama zinazofanywa na watu wasioitakia mema timu hiyo ili kuihujumu isifanye vizuri katika ligi.

"Manji aliwaeleza wazi wachezaji na baadhi ya viongozi wa Yanga waliokuwepo kwenye kikao hicho kwamba, anahisi anafanyiwa hujuma na watu wanaompinga na alionya kuwa, iwapo wachezaji hawatabadilika, atajiuzulu,"kilisema chanzo cha habari.

Mwenyekiti huyo aliwaeleza wachezaji na viongozi wenzake kwamba yupo tayari kujiuzulu wakati wowote na kuwaachia nafasi watu wengine ya kuiongoza klabu hiyo kongwe nchini.

Chanzo hicho cha habari kilieleza kuwa, Manji aliamua kupasua bomu kwa kuwaeleza wachezaji kwamba, miongoni mwa watu wanaojaribu kuihujumu Yanga ni wale waliokuwa wamezoea kuchota mapato ya mechi za ligi holela.

"Kuna watu najua tumeziba mianya yao ya ulaji, sasa wanahaha kutaka kuikwamisha Yanga, kama na nyie mnatumika, niambieni nijiuzulu sasa hivi,"chanzo hicho cha habari kilimnukuu Manji.

Yanga inashika nafasi ya nane katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa imeambulia pointi sita katika mechi tano, imefunga mabao 10 na kufungwa mabao saba.

Kwa mujibu wa chanzo hicho cha habari, katika kikao hicho, Manji aliwauliza wachezaji matatizo yanayowafanya washindwe kushinda mechi zao na kuelezwa kuwa, hawajalipwa posho za mechi kadhaa.

Alipoulizwa kuhusu kilichojadiliwa kwenye kikao hicho, nahodha wa Yanga, Nadir Haroub 'Cannavaro' alisema yalikuwa masuala ya kawaida, yaliyolenga kujua matatizo na kuimarisha timu yao.

“Lengo la mwenyekiti lilikuwa ni kuhakikisha tunajitazama upya na kuangalia wapi tumejikwaa na baada ya hapo tuendelee mbele,"alisema Cannavaro.

Kufuatia maamuzi yaliyofikiwa kwenye kikao hicho, Cannavaro alisema wameamua kutangaza kiama kwa timu zote watakazokutana nazo katika ligi hiyo kuanzia mwisho wa wiki hii.

Alisema wamepanga kuanza kuonyesha kucha zao keshokutwa katika mechi yao dhidi ya Ruvu Shooting, itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika hatua nyingine, uongozi wa Yanga umeamua kuongeza nguvu kwenye safu yake ya uongozi kwa kumrejesha kundini mwenyekiti wa matawi ya klabu hiyo ya mjini Dar es Salaam, Mohamed Msumi.

Habari zilizopatikana jana zimeeleza kuwa, uongozi wa Yanga umefikia uamuzi huo baada ya kubaini kuwa, Msumi ni mtu muhimu na anakubalika na wanachama wengi kutokana na mchango wake ndani ya klabu.

Msumi aliamua kujiweka kando na masuala ya Yanga kwa kile alichodai kuwa, katiba ya Yanga imekuwa ikikiukwa tangu uongozi wa Manji ulipoingia madarakani mwaka jana.

Viongozi wa matawi ya Yanga wanatarajiwa kukutana kati ya leo na kesho kwa ajili ya kumkabidhi majukumu Msumi ili kuiwezesha timu hiyo kushinda katika mechi zake zilizosalia.

Alipoulizwa kuhusu uamuzi wa kumrejesha kundini, Msumi alisema yupo tayari kuendelea kuitumikia Yanga wakati wowote.

Wednesday, September 25, 2013

LIGI KUU BARA HAITABIRIKI



 

UNAWEZA kuiita kuwa ni ligi isiyotabirika. Ni kutokana na matokeo ya mechi 35 zilizochezwa hadi sasa, zikiwemo zilizowahusisha mabingwa watetezi Yanga na watani wao wa jadi.

Yanga ilianza ligi hiyo kwa kishindo baada ya kuibugiza Ashanti mabao 5-1 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Ni ushindi uliopokelewa kwa furaha na mashabiki wa klabu hiyo kongwe, waliokuwa na imani kubwa kwamba, wangeendeleza wimbi la ushindi kwa kila timu, ambayo wangekutana nayo.

Lakini mambo yaligeuka katika mechi ya pili baada ya mabingwa hao watetezi kulazimishwa sare ya mabao 2-2 na Coastal Union mjini Dar es Salaam, ikalazimishwa sare ya bao 1-1 na Mbeya City mjini Mbeya na kulazimishwa tena sare hiyo ya mabao na Prisons mjini humo.

Hali ilikuwa mbaya kwa Yanga katika mechi yake ya tano iliyochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam baada ya kuchapwa mabao
3-2 na Azam. Ni kipigo kilichopokelewa kwa huzuni kubwa na mashabiki wa klabu hiyo.

Kwa upande wa Simba, ilianza ligi hiyo vibaya baada ya kulazimishwa kutoka sare ya mabao 2-2 na Rhino Rangers mjini Tabora, ikaichapa JKT Oljoro bao 1-0 mjini Arusha, ikaicharaza Mtibwa Sugar mabao 2-0 mjini Dar es Salaam kabla ya kuibugiza Mgambo JKT mabao 6-0.

Kasi ya Simba ilipunguzwa na vijana wa Mbeya City baada ya kulazimishwa kutoka nayo sare ya mabao 2-2 baada ya wakongwe hao kuwa mbele kwa mabao 2-0. Ni moja ya mechi zilizokuwa na msisimko wa aina yake kutokana na timu zote mbili kuonyesha kiwango cha juu cha soka.

Timu zilizoanza ligi hiyo kwa kishindo ni maafande wa JKT Ruvu na Ruvu Shooting, ambazo zinashika nafasi ya pili na ya nne katika msimamo wa ligi hiyo, inayozishirikisha timu 14.
JKT Ruvu ilianza ligi hiyo kwa kishindo baada ya kuwachapa ndugu zao wa Mgambo JKT mabao 2-0 mjini Tanga, ikaitandika Prisons mabao 3-0 mkoani Pwani na kuilaza Ashanti bao 1-0.

Mambo yaligeuka kwa JKT Ruvu katika mechi yake ya raundi ya nne baada ya kukubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa ndugu zao wa Ruvu Shooting kabla ya kupigwa mweleka mwingine wa idadi hiyo ya bao na JKT Oljoro.

Coastal Union nayo ilianza ligi hiyo kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya JKT Oljoro, ikatoka sare ya bao 1-1 na Yanga, ikatoka suluhu na Prisons, ikatoka sare ya bao 1-1 na Rhino Rangers kabla ya kuichapa Ruvu Shooting bao 1-0.

Azam nayo ilianza ligi hiyo kwa kusuasua baada ya kulazimishwa kutoka sare ya bao 1-1 na Mtibwa Sugar, ikaichapa Rhino Rangers mabao 2-0, ikatoka sare ya bao 1-1 na Kagera Sugar, ikalazimishwa sare nyingine ya bao 1-1 dhidi ya Ashanti kabla ya kuzinduka na kuichapa Yanga mabao 3-2.

Mbeya City ndiyo timu pekee iliyoonyesha maajabu hadi sasa baada ya kulazimisha sare dhidi ya vigogo vya ligi hiyo, Yanga, Simba na Mtibwa Sugar. Ilitoka sare ya bao 1-1 na Yanga mjini Mbeya, ilitoka suluhu na Mtibwa mjini Morogoro na pia ilitoka sare ya mabao 2-2 na Simba mjini Dar es Salaam. Pia ilitoka suluhu na Kagera Sugar mjini Mbeya kabla ya kuichapa Ruvu Shooting mabao 2-1.

Mbali na kulazimisha sare, timu hiyo inayoundwa na wachezaji wengi chipukizi, imeonyesha kiwango cha juu cha soka na kuwa kivutio kwa mashabiki walioishuhudia ikicheza dhidi ya Simba na Yanga.

Kwa mujibu wa msimamo wa ligi hiyo, Simba inaongoza kwa kuwa na pointi 11 baada ya kucheza mechi tano, ikifuatiwa na JKT Ruvu, Azam, Ruvu Shooting na Coastal Union zenye pointi tisa kila moja.

Kagera Sugar inashika nafasi ya sita kwa kuwa na pointi nane, ikifuatiwa na Mbeya City yenye pointi saba, Yanga na Mtibwa zenye pointi sita kila moja, Rhino Rangera, JKT Oljoro na Mgambo JKT zenye pointi nne kila moja, Prisons yenye pointi tatu na Ashanti yenye pointi moja.

                                                        Tambwe anatisha
Mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Hamisi Tambwe amedhihirisha kwamba ni moto wa kuotea mbali kwa ufungaji wa mabao baada ya kupachika wavuni mabao sita hadi sasa.

Tambwe, aliyesajiliwa na Simba msimu huu, akitokea Vital'O ya Burundi, aliifungia Simba mabao manne kati ya sita, ilipoinyuka Mgambo JKT mabao 6-0 kabla ya kuongeza mengine mawili wakati Simba ilipotoka sare ya mabao 2-2 na Mbeya City.

Jerry Tegete, Didier Kavumbagu wa Yanga na Haruna Chanongo wa Simba wanashika nafasi ya pili kwa kufunga mabao matatu kila mmoja, wakifuatiwa na wachezaji  sita waliofunga mabao mawili kila mmoja.

Wachezaji waliofunga mabao mawili kila mmoja ni Jonas Mkude wa Simba, Elias Maguri wa Ruvu Shooting, Bakari Kondo wa JKT Ruvu, Paul Nonga wa Mbeya City, Saad KIpanga wa Rhino Rangers, Felix Themi wa Kagera Sugar na Kipre Tchetche wa Azam.

Mbali na kuongoza ligi, Simba pia inaongoza kwa ufungaji mabao baada ya kupachika wavuni mabao 13 katika mechi tano, ikifuatiwa na Yanga iliyofunga mabao 10 na Azam iliyofunga mabao manane.

Ashanti ndiyo pekee iliyofungwa mabao mengi hadi sasa, baada ya kuruhusu nyavu zake kutikisika mara 11, ikifuatiwa na Mgambo JKT iliyofungwa mabao 10 na Rhino Rangers na Yanga zilizofungwa mabao saba kila moja.
                                                    Mitazamo ya makocha
Kocha Mkuu wa Azam, Stewart Hall amesema walianza ligi hiyo kwa kusuasua kutokana na baadhi ya wachezaji kushindwa kucheza kwa kujituma katika mechi za mwanzo.

Hall, ambaye ni rais wa Uingereza, aliwataja wachezaji walioonyesha kiwango cha chini hadi sasa kuwa ni Salum Abubakar 'Sure Boy' na Khamis Mcha 'Viali', ambao aliamua kuwaweka benchi katika mechi dhidi ya Yanga.

Kocha huyo alilazimika kuwatumia kwa mara ya kwanza wachezaji chipukizi, Joseph Kimwaga na Farid Mussa katika mechi dhidi ya Yanga na walioonyesha kiwango cha juu na hatimaye kuisaidia Azam kupata ushindi.

Kimwaga ndiye aliyeifungia Azam bao la tatu dakika za majeruhi baada ya kutanguliziwa mpira mrefu na kipa Aishi Manula na kuwazidi mbio mabeki wa Yanga kabla ya kuukwamisha mpira wavuni.

Farid na Kimwaga waliingizwa kwenye programu ya mchezo huo kwa shinikizo la wakurugenzi wa timu hiyo, ambao wanaheshimu uwezo wao, uliowawezesha kupandishwa kwenye kikosi cha kwanza.
 
"Wachezaji kama Salum Abubakar, Mcha Khamis na Kipre Tchetche walicheza vizuri msimu uliopita, lakini kiwango chao kimeshuka msimu huu, hawajitumi, nadhani wanajiona wana nafasi kubwa kwenye kikosi cha kwanza,"alisema Hall.

Hall alisema mchezo wa soka unahitaji mazoezi na mchezaji kujituma na kwamba hayuko tayari kuwavumilia wachezaji wazembe. Alisema hiyo ndiyo sababu iliyomfanya awaweke pembeni wachezaji hao na kuanza kuwatumia chipukizi.

Kocha Mkuu wa Yanga, Ernie Brandts amekiri kuwa, ligi ya msimu huu inazo changamoto nyingi na imekuwa ikimpa wakati mgumu kutokana na kupata matokeo wasiyoyatarajia.

Brandts, ambaye ni raia wa Uholanzi alisema, ushindani umekuwa mkali zaidi msimu huu ikilinganishwa na msimu uliopita, ndio sababu timu yake imambulia pointi sita katika mechi tano ilizocheza hadi sasa.

Akitoa mfano, alisema katika mechi kati yao na Azam, vijana wake walicheza vizuri, lakini walishindwa kutumia vyema nafasi walizopata kufunga mabao.

Hata hivyo, kocha huyo ameahidi kupambana kufa na kupona kuhakikisha timu yake inafanya vizuri katika mechi zinazofuata

Kocha Mkuu wa Simba, Abdalla Kibadeni anasema kuumia kwa wachezaji wawili, Nassoro Masoud 'Cholo' na Henry Joseph kulichangia kuifanya timu hiyo ishindwe kupata ushindi katika mechi yao dhidi ya Mbeya City.

Kibadeni alisema, iwapo kikosi kilichocheza na Mbeya City kingekuwa kilekile kilichoibamiza Mgambo JKT mabao 6-0, wangeweza kutoka uwanjani na ushindi dhidi ya vijana hao wa Mbeya.

Kocha huyo alikiri pia kuwa, bado wachezaji wake wanakabiliwa na tatizo na kuchoka haraka kipindi cha pili na kuongeza kuwa, ataendelea kulifanyia kazi kwa kuwapa mazoezi na kuongeza stamina na pumzi.

Kocha Juma Mwambusi wa Mbeya City anasema, vijana wake waliweza kuzidhibiti vyema Simba na Yanga kwa vile anazijua vyema mbinu zinazotumiwa na wapinzani wao uwanjani.

Akitoa mfano, alisema wachezaji wa Yanga walicheza kwa woga na kutumia zaidi pasi ndefu walipocheza nayo mjini Mbeya na kwamba kisingizio cha ubovu wa uwanja hakikuwa na maana.
Mwambusi alisema Simba ni timu nzuri, lakini waliweza kuibana kwa kupeleka mashambulizi yao pembeni ya uwanja ili kuwazuia mabeki wa timu hiyo wasipande mbele kusaidia mashambulizi.

Aliitaja mbinu nyingine waliyotumia kuwa ni kuongeza ulinzi, kuziba njia kwa kuboresha winga zake. Anasema hiyo ndiyo sababu iliyowawezesha kusawazisha mabao yote waliyofungwa na Simba.

Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea tena keshokutwa wakati Yanga itakapomenyana na Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Rhino Rangers na Kagera Sugar, Mbeya City na Coastal Union, Mgambo JKT na JKT Oljoro.

Jumapili Ashanti itacheza na Mtibwa Sugar, JKT Ruvu na Simba wakati Prisons itamenyana na Azam.

RATIBA YA MECHI ZIJAZO
Sept 28, 2013
Yanga na Ruvu Shooting
Rhino Rangers na Kagera Sugar
Mbeya City na Coastal Union
Mgambo JKT na JKT Oljoro
Sept 29, 2013
Ashanti na Mtibwa Sugar
 JKT Ruvu na Simba
 Prisons na Azam

Msimamo wa ligi hiyo hadi sasa ni kama ifuatavyo:
  P W D L GF GA PTS
1  Simba SC  5  3  2  0  13  4  11
2  JKT Ruvu  5  3  0  2  6  2  9
3  Azam   5  2  3  0  8  5  9
4  Ruvu Shooting  5  3  0  2  6  3  9
5  Coastal Union  5  2  3  0  5  2  9
6  Kagera Sugar  5  2  2  1  6  3  8
7  Mbeya City  5  1  4  0  5  4  7
8  Young Africans  5  1  3  1  10  7  6
9  Mtibwa Sugar  5  1  3  1  3  4  6
10  Rhino Rangers  5  0  4  1  5  7  4
11  JKT Oljoro  5  1  1  3  3  6  4
12  Mgambo JKT  5  1  1  3  2  10  4
13  Prisons  5  0  3  2  2  8  3
14  Ashanti United  5  0  1  4  2  11  1


LATIFAH ASEMA ATATUMIA PESA ALIZOSHINDA KUJILIPIA ADA, CLARA ATOA YA MOYONI


MSHINDI wa pili wa shindano la kumsaka mrembo wa Tanzania wa 2013, Latifah Mohamed amesema atatumia fedha za zawadi alizopata kujisomesha masomo ya chuo kikuu.

Latifah, ambaye ni mhitimu wa kidato cha sita amesema, hapendi kuendelea kuwasumbua wazazi wake kumlipia ada ya chuo kwa sasa.

Binti huyo alishika nafasi hiyo baada ya kujibu vizuri swali aliloulizwa na jaji. Aliulizwa na kujibu swali hilo kwa lugha ya kiingereza.

Latifah ni miongoni mwa warembo waliokuwa wakishangiliwa kwa mayowe mengi na mashabiki kila alipopita jukwaani. Shindano hilo lilifanyika kwenye ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.

"Nataka wazazi wangu waone nimefanya kitu fulani muhimu katika maisha yangu,"alisema binti huyo, ambaye alizawadiwa pesa taslim sh. milioni 6.2.

Mbali na kutumia pesa hizo kujisomesha, Latifah alisema anatarajia kutumia kiasi kingine kuanzisha biashara. Alisema lengo lake kubwa ni kuwa mfanyabiashara.

"Nitaanzisha biashara yoyote kwa sababu wakati tulipokuwa kambini, tulipewa mafunzo ya jinsi ya kuwa wajasiriamali,"alisema.

Latifah alisema, wakati walipokuwa kambini, alifurahia mafunzo waliyopewa na mshindi wa taji hilo wa mwaka 2004, Faraja Kotta.

"Faraja alituonya, tusitumie urembo kuficha maovu. Alitutaka tujitambue. Kwangu, Faraja na Nancy Sumari ni mfano mzuri wa wanawake,"alisema.

Latifah alisema alifurahi alipotangazwa kuwa mshindi wa pili wa taji hilo kwa vile alikuwa amejiwekea malengo ya kuingia hatua ya tatu bora.

"Kusema kweli sikutarajia kushika nafasi ya pili, lakini namshukuru Mungu kwa sababu ushindani ulikuwa mkali,"alisema.

Latifah alisema alianza kuvutiwa na fani ya urembo tangu akiwa mdogo na alimtaja mrembo wa Tanzania wa 2000, Jacqueline Ntuyabaliwe kuwa ni kichocheo kwake kushiriki shindano hilo.

"Kuna siku nilimwambia baba yangu mzazi, nataka niwe mrembo, akaniambia subiri kwanza umalize shule na sasa nimetimiza ndoto yangu,"alisema.

Binti huyo alisema amemaliza kidato cha sita mwaka huu na kwamba wazazi wake hawakuwa na kinyongo kwake kushiriki katika mashindano ya urembo.

Alisema alipata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa wazazi wake tangu alipoanza kushiriki shindano la Miss Kigamboni na kuibuka mshindi na baadaye shindano la Miss Temeke, ambapo pia aliibuka mshindi.

Wakati huo huo, mshindi wa tatu wa shindano la Miss Tanzania 2013, Clara Bayo amewataka wazazi nchini kuwaruhusu watoto wao wa kike kushiriki kwenye mashindano hayo ili waweze kuonyesha vipaji vyao.

Clara amesema fani ya urembo si ya kihuni kama inavyodhaniwa na wengi na kwamba, iwapo itatumika vizuri, inaweza kuleta manufaa makubwa kwa watoto wa kike.

Mrembo huyo alisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha Usiku wa Habari, kilichorushwa hewani na kituo cha televisheni cha TBC 1.

"Zipo fursa nyingi kwa wasichana wanaoshiriki mashindano ya urembo na si vizuri kuzikosa fursa hizi,"alisema binti huyo, ambaye ni mhitimu wa kidato cha sita.

Clara alisema tangu alipoanza kushiriki kwenye mashindano hayo, kuanzia kitongoji cha Dar City Centre na baadaye Kanda ya Ilala, alikuwa amejiwekea malengo ya kuingia hatua ya tano bora.

"Naweza kusema ilikuwa bahati kwangu kuingia hatua hiyo na tatu bora kwa sababu ushindani ulikuwa mkali,"alisema mrembo huyo.

"Nilifurahi sana kushinda nafasi niliyoipata, namshukuru Mungu,"aliongeza.

Clara alisema mwanzoni alikuwa akiogopa kushiriki kwenye mashindano hayo kutokana na msimamo wa wazazi wake.

"Mwanzoni wazazi hawakutaka kabisa nishiriki mashindano haya, walinishinikiza nisome kwanza. Nimemaliza kidato cha sita hivi karibuni na nilipowaambia nataka kushiriki, waliniunga mkono,"alisema.

Binti huyo mwenye sura yenye mvuto alisema, fani ya urembo si ya kihuni kwa vile uhuni ni tabia binafsi ya mtu.

Alisema wasichana wanaoshiriki kwenye mashindano hayo wanapaswa kuwa makini kwa vile ni rahisi kufuatiliwa na vyombo vya habari kutokana na umaarufu walioupata.

"Ukiwa na tabia nzuri, huwezi kupata matatizo,"alisema.

Alisema anamshukuru mrembo wa Tanzania wa 2005, Nancy Sumari kwa kumpa mafunzo mazuri alipokuwa kambini, ambapo alimtaka kutofautisha urembo na maisha yake binafsi.

KAMWAGA, KINDA WA AZAM ALIYEIZAMISHA YANGA



JINA la Joseph Kamwaga ni geni kwa mashabiki wa soka nchini. Ni mmoja wa wachezaji chipukizi wa Azam waliopandishwa kikosi cha kwanza msimu huu, akitokea kikosi cha pili.

Kabla ya mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara kati ya Azam na Yanga iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Kamwaga hakuwa akifahamika. Ni kwa sababu hakuwa akipata nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo.

Lakini baada ya kucheza mechi hiyo, Kamwaga sasa amekuwa maarufu kutokana na kuifungia Azam bao la tatu na la ushindi dhidi ya Yanga na kuiwezesha kutoka uwanjani na ushindi wa mabao 3-2.

Kamwaga aliingia uwanjani kipindi cha pili kuchukua nafasi ya kinda mwingine wa timu hiyo, Farid Musa na dakika chache baadaye akafanikiwa kuzitikisa nyavu za Yanga na kuamsha shangwe kwa mashabiki wa timu hiyo.

Mpira uliozaa bao hilo ulianzia kwa kipa Aishi Manula, ambaye baada ya kuokoa bao, alirusha mpira mrefu kwa Kamwaga, akawazidi mbio mabeki wa Yanga na kufumua kiki iliyompita kipa Ally Mustapha 'Barthezl na kujaa wavuni.

Kamwaga na Farid walichezeshwa mechi hiyo kwa mara ya kwanza na Kocha Stewart Hall wa Azam kutokana na shinikizo la wakurugenzi wa klabu hiyo baada ya baadhi ya wachezaji wa kikosi cha kwanza kucheza chini ya kiwango.

Katika mechi hiyo dhidi ya Yanga, Stewart aliamua kuwaweka benchi kiungo Salum Abubakar na mshambuliaji Khamis Mcha kutokana na kucheza kwa kiwango cha chini katika mechi dhidi ya Ashanti, nafasi zao zikachukuliwa na Farid na Kamwaga.

Akizungumza na Burudani baada ya mechi hiyo, Kamwaga alisema amejisikia furaha kuifungia Azam bao hilo muhimu kwa vile ilikuwa mara yake ya kwanza kucheza katika ligi na dhidi ya timu kongwe na maarufu.

Alisema siri ya mafanikio yake katika soka ni kufanya mazoezi kwa bidii na kufuata vyema mafunzo ya makocha wake, akiwepo Hall na wale wa kikosi cha pili.

"Hakuna njia ya mkato katika kupata mafanikio zaidi ya  kufanya mazoezi ya nguvu na  kwa bidii,"alisema kinda huyo, ambaye anaamini kuwa, iwapo Stewart ataendelea kumpa nafasi kwenye kikosi cha kwanza, ataweza kuonyesha maajabu.

Alisema kitendo cha kuifungia Azam bao la tatu na la ushindi dhidi ya Yanga kilikuwa cha fahari kubwa kwake kwa vile kimeweza kutangaza jina lake na kumfanya ajulikane na mashabiki.

Kamwaga amewashukuru wachezaji wenzake wa Azam kwa kumpa ushirikiano mkubwa tangu alipopandishwa kikosi cha kwanza na kuongeza kuwa, ndoto yake kubwa ni kuipa mafanikio zaidi timu hiyo.

Aliyataja malengo aliyojiwekea kuwa ni pamoja na kuifungia bao Azam katika kila mechi atakayopangwa na pia kuwatengenezea wachezaji wenzake nafasi za kufunga mabao.

Kinda huyo alisema kikosi cha Azam kilishindwa kufanya vizuri katika mechi za mwanzo za ligi hiyo kutokana na baadhi ya wachezaji muhimu kuwa majeruhi na chipukizi waliopandishwa daraja kutokuwa na uzoefu wa ligi hiyo.

Alisema ana hakika iwapo yeye na chipukizi wenzake watauzoea mfumo wa Kocha Stewart, kikosi hicho kitafanya vizuri zaidi katika mechi zijazo na kutimiza malengo waliyojiwekea ya kutwaa ubingwa msimu huu.

"Unajua wanapoongezeka wachezaji wapya kwenye timu, lazima kunakuwa na mabadiliko kidogo, na hivyo ndivyo ilivyotokea kwa Azam. Bado tunajifunza kutoka kwa wenzetu wazoefu kwenye kikosi cha kwanza,"alisema.

Kinda huyo amekiri kuwa, kucheza kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, mbele ya umati mkubwa wa mashabiki kunataka moyo na uzoefu, vinginevyo kelele za mashabiki zinaweza kumwathiri mchezaji.

Kamwaga amesema anaridhishwa na mafunzo, ambayo yamekuwa yakitolewa na Stewart kwa vile ni kocha mwenye ujuzi na uzoefu na amemuomba awe akiwapatia nafasi ya kucheza kwenye ligi mara kwa mara ili kuwaongezea uzoefu.

Hata hivyo, Kamwaga amekiri kwamba anakabiliwa na changamoto kubwa ya kupata namba kwenye kikosi hicho kutokana na kuwepo kwa wachezaji wazoefu kama vile John Bocco na Kipre Tchetche.

Kamwaga alisema anatamani kuvaa jezi za timu ya Taifa, Taifa Stars na kuongeza kuwa, iwapo atapata nafasi ya kuichezea Azam mara kwa mara, anaamini ipo siku ndoto yake hiyo itatimia.

HAPPINESS: NILIJUA NITASHINDA



MREMBO wa Tanzania wa 2013, Happiness Watimanywa amesema alikuwa na uhakika mkubwa wa kushinda taji hilo kutokana na maandalizi aliyoyafanya na pia kujiamini.

Happiness amesema tangu alipofuzu kuingia fainali ya shindano hilo, alikuwa amejiwekea malengo ya kuingia hatua ya tano bora na tatu bora.

"Nilitarajia kushinda kwa sababu nilijiamini, lakini kuna washiriki wachache tuliokuwa tunachuana kwa sababu tulikuwa na sifa zinazolingana," alisema mrembo huyo alipokuwa akihojiwa na kituo cha televisheni cha TBC 1 mwishoni mwa wiki iliyopita.

Happiness alishiriki katika fainali za mwaka huu za shindano hilo akiwa mshindi wa mkoa wa Dodoma na Kanda ya Kati. Pia alishinda taji la mrembo mwenye mvuto katika hatua ya awali ya shindano la taifa.

Ushindi huo ulimwezesha Happiness kuzawadiwa gari lenye thamani ya sh. milioni 15 pamoja na fedha taslim sh. milioni nane. Shindano hilo lilifanyika kwenye ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.

Mrembo huyo alisema anaamini majaji walitenda haki kwa kumchagua kuwa mshindi kwa vile anazo sifa zote za kumwezesha kuipeperusha vyema bendera ya taifa katika shindano la kumsaka mrembo wa dunia.

"Sijahonga ili nipate ushindi, majaji walitenda haki," alisisitiza huku akiangua kicheko. Happiness alishinda taji hilo baada ya kuwabwaga washiriki wenzake 29 kutoka mikoa mbalimbali nchini.

Mrembo huyo alisema hakuwa akifahamiana na majaji wa shindano hilo kwa vile walitambulishwa kwao wiki moja kabla ya shindano.

"Wapo tuliokuwa tukiwafahamu, lakini wengine hatukuwajua kabisa. Wapo waliokuja kutuona tulipokuwa kambini na kutupa mafunzo juu ya mambo mbalimbali,"alisema mrembo huyo mwenye jisimu lenye mvuto.

Miongoni mwa majaji wa shindano la mwaka huu walikuwa warembo wa Tanzania miaka ya nyuma. Warembo hao ni Faraja Kotta, Nancy Sumari na Jacqueline Ntuyabaliwe.

Kwa mujibu wa Happiness, wazazi na ndugu zake waliupokea ushindi wake kwa furaha kubwa kwa vile mara baada ya kutangazwa mshindi wa taji hilo, walirukaruka kwa furaha ukumbini.

Happiness alisema fani ya urembo si ya kihuni kama watu wengi wanavyofikiria na kwamba uhuni ni tabia ya mtu.

"Iwapo wewe mwenyewe utajitambua na wazazi wako wakikuelewa, watakuruhusu kushiriki mashindano haya. Kama huna tabia ya kihuni, huwezi kufanya vitendo vya kihuni,"alisema.

Alisema baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwazuia watoto wao wa kike kushiriki kwenye mashindano hayo kutokana na tabia na mwenendo wao kuwa mbaya katika jamii.

Happiness alisema anatambua wazi kwamba, jukumu alilonalo kwa sasa ni gumu, lakini atajitahidi kushirikiana na wadhamini, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) na waandaaji, Kampuni ya Lino Agency International kulitimiza.

"Zipo kazi nyingi za kufanya za kijamii mbele yangu, kuna programu binafsi za Miss Tanzania na wadhamini, nitahakikisha zote nazifanya kadri ya uwezo wangu,"alisema.

Mrembo huyo alisema pia kuwa, atashirikiana vyema na kamati na wadhamini kuhakikisha anajiandaa vyema kwa shindano la dunia, litakalofanyika Septemba mwakani nchini Uingereza.

MASHAUZI: SIPENDI KUUMIZWA KIMAPENZI


KIONGOZI wa kikundi cha muziki wa taarab cha Mashauzi Classic, Isha Mashauzi amesema kamwe katika maisha yake hapendi kuumizwa kimapenzi na mwanaume.

Isha amesema anapoachana na mwanaume, huwa hageuki nyuma na kwamba mapenzi kwake ni kitu cha kupita.

"Nikiacha nimeacha, sipendi kuumizwa, kazi yangu mwenyewe inaumiza,"alisema Isha alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha Ng'aring'ari kilichorushwa hewani na kituo cha televisheni cha Clouds TV mwishoni mwa wiki iliyopita.

Isha amesema amewahi kutongozwa na wanaume wengi, lakini kutokana na msimamo alionao kimapenzi, wamebaki kuwa rafiki zake baada ya kuwaeleza ukweli wa mambo.

"Wapo zaidi ya wanaume wanne, ambao walinitongoza na kunitaka kimapenzi, lakini niliwaeleza wazi kwamba, kwa vile kila mmoja ana mkewe nyumbani, siwezi kujihusisha nao katika suala hilo. Hivi sasa ni rafiki zangu wakubwa, huwezi kuamini,"alisema.

Hata hivyo, Isha ametahadharisha kuwa, mwanamke anapoamua kumtolea nje mwanaume, anapaswa kuwa makini ili kuepuka kujiingiza katika matatizo.

Alisema wapo wanaume wanaopenda vibaya na wanaoweza kufanya lolote pale wanapokataliwa kimapenzi, ikiwa ni pamoja na kuua ama kujiua.

"Hata kama humpendi, mchukulie taratibu, usimweleze kwa pupa, wewe ni mwanadamu, siyo ng'ombe, hujui anakupenda vipi,"alisema mwanamama huyo, ambaye alianza kupata umaarufu katika muziki wa taarab alipokuwa kundi la Jahazi.

Isha amekiri kuwa, aliwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Jumanne Tevez, ambaye alipiga naye picha za video ya wimbo wake wa Nakupenda kwa dhati, lakini hawakuwahi kupata mtoto.

Anasema anajuta kumtambulisha Tevez kwa watu wengine kwa sababu baadhi yao walitumia nafasi hiyo kumtaka kimapenzi kwa lengo la kumkomoa.

Licha ya kuachana na Tevez baada ya mpenzi wake huyo wa zamani kuoa mwanamke mwingine, Isha amesema bado wanaendelea kuwasiliana na kuwa na urafiki wa kawaida.

"Hata mkewe tuna uhusiano mzuri na wakati mwingine huwa tunapigiana simu kujulikana hali, namwita wifi naye ananiita wifi,"alisema Isha.

Isha amesema katika maisha yake, kamwe hawezi kupigana na mwanamke mwenzake kwa ajili ya kugombania mapenzi. Alisema tabia hiyo imepitwa na wakati.

Ametoa mwito kwa wanawake wa Kitanzania kujenga utamaduni wa  kupendana na kukosoana badala ya kujengeana chuki bila ya sababu za msingi.

Amesema inapendeza mwanamke anapomuonea mwenzake wivu wa kimaendeleo kwa kufanya kile kilichomvutia kutoka kwa mwenzake hata kama atakuwa anamuiga.

Isha amesema licha ya mkurugenzi mwenzake wa Mashauzi Classic, Thabiti Abdul kuhamia kundi la Five Stars, bado amekuwa akiendelea kufanya maonyesho na kundi hilo.

"Thabiti bado tuko naye, anakuja mazoezini, anapiga kinanda na gita kwenye maonyesho, kwa ujumla bado tuko naye,"alisema.

Isha amesema kwa sasa kundi lake la Mashauzi Classic linajiandaa kuipua albamu mpya, itakayokuwa na nyimbo sita. Amesema albamu hiyo itajulikana kwa jina la Asiyekujua hakuthamini.

Albamu hiyo itakuwa ya pili kwa Mashauzi Classic tangu kundi hilo lilipoanzishwa miaka miwili iliyopita. Albamu ya kwanza inajulikana kwa jina la Si bure una mapungufu, iliyofuatiwa na Viwavi Jeshi. Albamu hizo mbili zilikuwa na nyimbo nne kila moja.

Sunday, September 22, 2013

YANGA PWAA, YAPIGWA 3-2 NA AZAM


Wachezaji wa Azam wakimpongeza mfungaji wao wa bao la tatu katika mechi dhidi ya Yanga leo. Picha kwa hisai ya Bin Zubeiry

MWANZONI ilionekana kama vile hadithi ingekuwa ni ile ya kutangulia si kufika. Ni baada ya Yanga kufunga bao la kusawazisha na hatimaye kuongeza la pili.

Lakini mambo yalibadilika dakika chache baadaye baada ya Azam kufunga bao la kusawazisha na kuongeza la tatu dakika moja kabla ya mchezo kumalizika.

Katika mechi hiyo iliyokuwa na ushindani mkali, Azam iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Yanga na kuzima shangwe na nderemo zilizokuwa zikisikika kutoka kwa wapinzani wao.

Mshambuliaji chipukizi, Joseph Kimwaga ndiye aliyeibuka shujaa wa Azam baada ya kuifungia bao la tatu baada ya kutanguliziwa mpira mrefu uliopigwa na kipa Aishi Manula na kuwazidi mbio mabeki wa Yanga kabla ya kuukwamisha mpira wavuni.

Azam ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 34 lililofungwa na mshambuliaji John Bocco baada ya kuuwahi mpira wa uliokolewa na beki Kevin Yondani wa Yanga. Timu hizo zilikwenda mapumziko Azam ikiwa mbele kwa bao 1-0.

Yanga ilisawazisha dakika ya 48 kwa bao lililofungwa na Didier Kavumbagu aliyeuwahi mpira mrefu, akamkodolea macho kipa Manula kabla ya kuupachika mpira wavuni.

Bao hilo liliiongezea nguvu Yanga, iliyofanikiwa kupata bao la pili lililofungwa na Hamisi Kiiza baada ya kupokea pasi kutoka kwa Simon Msuva.

Kibao kiliwageukia Yanga dakika ya 69 baada ya beki Yondani kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari la Yanga na Kipre Tchetche kuukwamisha mpira wavuni kwa njia ya penalti.

Wakati mashabiki wakiamini pambano hilo lingemalizika kwa sare, ndipo Kamwaga alipoifungia Azam bao la tatu. Kwa matokeo hayo, Azam sasa inazo pointi tisa baada ya kucheza mechi tano wakati Yanga inazo pointi sita.

Yanga SCAlly Mustafa ‘Barthe z’, Mbuyu Twite, David Luhende, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’, Simon Msuva, Frank Domayo, Didier Kavumbangu, Jerry Tegete/Hamisi Kiiza na Haruna Niyonzima.

Azam FC: Aishi Manula, Erasto Nyoni, Waziri Salum, David Mwantika, Joackins Atudo/Said Mourad, Himid Mao, Farid Mussa/Joseph Kimwaga, Kipre Balou, John Bocco, Humphrey Mieno na Brian Umony/Kipre Tchetche.

Katika mechi nyingine za ligi hiyo zilizochezws leo, JKT Ruvu ilifungwa 1-0 na JKT Oljoro Uwanja wa Azam Complex. Bao pekee Oljoro lilifungwa na Paul Malipesa dakika ya 79.

Ruvu Shooting ilishindwa kukwea kileleni baada ya kuchapwa bao 1-0 na Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga. Bao pekee la Coastal Union lilifungwa na Haruna Moshi ‘Boban’ dakika ya 82.

HAPPINESS AWA MISS TANZANIA



Redd's Miss Tanzania 2013,Happiness Watimanywa akipungia mkono mara baada ya kutangazwa mshindi wa Taji hilo kwa mwaka huu.Kushoto ni mshindi wa pili,Latifa Mohamed na kushoto ni mshindi wa tatu,Clara Bayo
Hawa ni warembo walioingia hatua ya tano bor



Hawa ni warembo walioingia hatua ya 15 bora

SIMBA YATOLEWA NISHAI NA MBEYA CITY, LEO NI YANGA NA AZAM


KIUNGO Amri Kiemba wa Simba akiwatoka mabeki wa Mbeya City wakati timu hizo zilipomenyana jana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. (Picha kwa hisani ya Bin Zubeiry Blog)
VIJANA wa Mbeya City jana walidhihirisha kwamba hawakupanda daraja la ligi kuu kwa kubahatisha baada ya kuilazimisha Simba kutoka nayo sare ya mabao 2-2 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Simba itabidi ijilaumu kwa kushindwa kutoka uwanjani na ushindi kwani ilikuwa mbele kwa mabao 2-1 hadi mapumziko, kabla ya vijana wa Mbeya City kuchachamaa na kusawazisha kipindi cha pili.

Kwa matokeo hayo, Simba bado inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 11 baada ya kucheza mechi tano wakati Mbeya City imefikisha pointi saba.

Mshambuliaji Hamisi Tambwe kutoka Burundi aliendelea kung'ara na kuongoza kwa ufungaji mabao baada ya kuifungia Simba mabao yote mawili. Alifunga mabao hayo dakika ya 29 na 33.

Mbeya City, inayofundishwa na kocha mzoefu, Juma Mwambusi, ilipata bao la kwanza dakika ya 37 kupitia kwa Paul Nonga kabla ya Richard Peter kusawazisha dakika ya 69 na kuwaacha mashabiki wa Simba wakiwa wameduwaa.

Katika mechi hiyo iliyokuwa na ushindani mkali, mabao ya Mbeya City yalionekana kuwa ya ufundi zaidi, hasa bao la pili, ambalo lilifungwa kwa mpira wa adhabu, ambao Richard alitanguliziwa kwa mbele na kuunganisha kwa shuti.

SimbaAbbel Dhaira , William Lucian ‘Gallas’, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Kaze Gilbert/Hassan Hatibu dk66, Joseph Owino, Jonas Mkude, Twaha Ibrahim/Ramadhani Chombo ‘Redondo’ dk50, Amri Kiemba/Ramadhani Singano ‘Messi’ dk79, Betram Mombeki, Amisi Tambwe na Haroun Chanongo.

Mbeya City:Dvid Burhan, John Kabanda, Hassan Mwasapili, Deogratius Julius, Antony Matogolo, Yohana Morris, Mwagane Yeya/Richard Peter dk59, Steven Mazanda, Paul Nonga, Deus Kaseke na Yussuf Willson.

Katika mechi zingine za ligi hiyo zilizochezwa jana, Mgambo JKT ilitoka sare ya bao 1-1 na Rhino Rangers mjini Tanga, Prisons ilitoka sare ya bao 1-1 na Mtibwa Sugar mjini Mbeya wakati Kagera Sugar iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Ashanti.

Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea leo wakati Azam itakapomenyana na Yanga kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, JKT Ruvu itacheza na JKT Oljoro kwenye uwanja wa Azam Complex wakati Ruvu Shooting itavaana na Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.

Thursday, September 19, 2013

SIMBA, MGAMBO ZAINGIZA MILIONI 58, MIKATABA YA MAKOCHA LIGI KUU YATAKIWA TFF



Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya Simba na Mgambo Shooting Stars iliyochezwa jana (Septemba 18 mwaka huu) katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 58,365,000.

Watazamaji 10,241 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo namba 23 ya VPL msimu wa 2013/2014 iliyomalizika kwa wenyeji Simba kuibuka na ushindi wa mabao 6-0.

Viingilio katika mechi hiyo vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 13,839,327.45 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 8,903,135.59.

Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 7,036,946.16, tiketi sh. 2,548,890, gharama za mechi sh. 4,222,167.70, Kamati ya Ligi sh. 4,222,167.70, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 2,111,083.85 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 1,641,954.10.
 
MIKATABA YA MAKOCHA VPL, FDL YATAKIWA TFF
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetoa siku 14 kwa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na za Ligi ya Daraja la Kwanza (FDL) kuwasilisha mikataba ya makocha wao.

Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF iliyokutana Septemba 12 mwaka huu imebaini klabu nyingi hazijawasilisha mikataba ya mabenchi yao ya ufundi, kitu ambacho ni matakwa ya kikanuni. Siku hizo 14 zimetolewa kuanzia Septemba 17 mwaka huu.

Kwa klabu ambazo zitashindwa kuwasilisha mikataba hiyo na vielelezo vingine ndani ya mudau huo zitachukuliwa hatua kwa mujibu wa kanuni.

SIMBA INATISHA



KUMEKUCHA. Simba inatisha. Hivyo ndivyo unavyoweza kuyayelezea matokeo ya mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara kati ya Simba na Mgambo JKT iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika mechi hiyo, Simba inayoundwa na wachezaji wengi wapya, iliibuka na ushindi mnono wa mabao 6-0 na kuishusha kwenye uongozi wa ligi hiyo, JKT Ruvu, ambayo jana ilichapwa bao 1-0 na ndugu zao wa Ruvu Shooting.

Ushindi huo mnono uliiwezesha Simba kukamata usukani wa ligi hiyo kwa kuwa na pointi 10 baada ya kucheza mechi nn, ikifuatiwa na JKT Ruvu na Ruvu Shooting zenye pointi tisa kila moja baada ya kucheza idadi hiyo ya mechi.

Mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Hamisi Tambwe aliibuka shujaa wa Simba na kuzawadiwa mpira baada ya kupachika wavuni mabao manne kati ya Sita. Mabao mengine mawili yalifungwa na Haruna Chanongo.

Tambwe, amekuwa kama mshambuliaji nguli wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo, ambaye juzi usiku aliiduwaza Galatasaray baada ya kufunga mabao matatu 'hat trick' katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.

Simba ilianza mchezo huo kwa kasi wakati Chanongo, alipobisha hodi langoni mwa Mgambo dakika ya nne kabla ya mabeki kutibua mpango wake ndani ya eneo la hatari.

Mfungaji bora wa Kombe la Kagame mwaka huu alipokuwa na kikosi cha Vital' O ya Burundi, Tambwe alianza kufunga bao dakika ya nne akiunganisha kwa kichwa krosi ya beki wa kushoto, Issa Rashid 'Baba Ubaya'.

Chanongo alifunga bao la pili dakika ya 32 kwa shuti baada ya kupata pasi ya Henry Joseph. Tambwe alipachika mabao mengine dakika za 41 na 44 kabla ya kufunga kwa penalti dakika ya 76.

Katika dakika ya 64, beki wa Mgambo, Bakari Mtama alijifunga wakati akiwa katika harakati za kuokoa shuti lililopigwa na Chanongo na kuipatia Simba bao la tano.

Simba ilicheza mchezo huo ikitokea katika furaha ya ushindi wa mabao 2-0, iliyopata dhidi ya wakata miwa wa Mtibwa Sugar kwenye uwanja huo mwishoni mwa wiki iliyopita.

Mgambo ilikosa bao dakika ya 49 baada ya Mohammed Neto kushindwa kumalizia pasi ya Adam Gila. Dakika ya 68, Salum Kipaga alipiga shuti nje akiwa ndani ya eneo la hatari la Simba.

Simba: Abel Dhaira, Miraji Adam, Issa Rashid, Gilbert Kaze, Joseph Owino, Henry Joseph/Ramadhan Chombo, Jonas Mkude, Amri Kiemba, Betramu Mwombeki, Hamisi Tambwe na Haruna Chanongo.

Mgambo: Kulwa Manzi, Francis Anyosisye, Salum Mlima, Bakari Mtama, Novat Lufunga, Salum Kipaga, Peter Mwalianzi, Mohammed Neto, Fulli Maganga na Salum Gila.

YANGA MAJANGA





Na Solomon Mwansele, Mbeya

MAMBO bado si shwari kwa Yanga baada ya kuendelea kubanwa katika mechi za ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara.

Mabingwa hao watetezi wa ligi kuu, jana walilazimishwa kutoka sare ya bao 1-1 na Prisons katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine mjini hapa.

Sare hiyo ilikuwa ya pili mfululizo kwa Yanga baada ya mwishoni mwa wiki iliyopita kulazimishwa kutoka sare hiyo ya mabao na Mbeya City kwenye uwanja huo.

Kwa matokeo hayo, Yanga imeambulia pointi sita katika mechi nne ilizocheza, ikiwa imefungana na timu za Azam, Coastal Union na Mbeya City. Prisons ni ya pili kutoka mwisho ikiwa imeambulia pointi mbili.

Yanga ilihesabu bao la kuongoza dakika ya 41 lililofungwa na Jerry Tegete, aliyeunganisha wavuni kwa kichwa krosi maridadi iliyopigwa na  Simon Msuva kutoka pembeni ya uwanja.

Bao la kusawazisha la Prisons lilifungwa na Peter Michael dakika ya 77 baada ya kuunganisha kwa kichwa mpira wa kona uliopigwa na Omega Seme.

Pambano hilo lilihudhuriwa na mashabiki wachache, tofauti na siku Yanga ilipocheza na Mbeya City na timu hizo kutoka sare mwishoni mwa wiki iliyopita.

Katika dakika 30 za kwanza, timu zote mbili zilicheza kwa kasi ndogo huku zikisomana na kufanya mashambulizi machache ya kushtukiza. Timu hizo zilikwenda mapumziko Yanga ikiwa mbele kwa bao 1-0.

Prisons ilipata nafasi nzuri ya kusawazisha dakika ya 48 baada ya Six Ally kuwatoka mabeki wa Yanga na kufumua shuti kali, lakini lilikwenda moja kwa moja mikononi mwa kipa Ally Mustapha.

Yanga: Ally Mustapha, Mbuyu Twite, David Luhende, Nadir Haroub, Kelvin Yondan, Athumani Iddi, Simon Msuva/ Nizar Khalfan, Salum Telela/Frank Dumayo, Didier Kavumbagu, Jerry Tegete/Saidi Bahanuzi, Haruna Niyonzima.

Prisons:Benno David, Salum Kimenya, Mika Shaban, Jumanne Elfadhili, Nurdin Issah, Lugano Mwangama, Jimmy Shoji, Freddy Chudu, Ibrahim Issaka, Six Ally/Peter Michael na Jeremiah Juma/ Omega Seme.

Wakati huo huo, JKT Ruvu jana ilishushwa kileleni mwa ligi hiyo baada ya kupigwa mweleka wa bao 1-0 na ndugu zao wa Ruvu Shooting katika mechi iliyopigwa kwenye uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi mkoani Pwani.

Azam imeendelea kuchechemea katika ligi hiyo baada ya kulazimishwa kutoka sare ya bao 1-1 na Ashanti katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.

Kipre Tchetche aliifungia Azam bao la kuongoza kipindi cha kwanza kabla ya Anthony Matangalu kuisawazishia Ashanti kipindi cha pili.

Azam ililazimika kumaliza mechi hiyo ikiwa na wachezaji 10 baada ya beki  wake, Aggrey Morris kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kucheza rafu mbaya.

Katika mechi nyingine za ligi hiyo zilizochezwa jana, Coastal Union ilitoka sare ya bao 1-1 na Rhino Rangers katika mechi iliyopigwa kwenye uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga wakati Mtibwa Sugar ilitoka suluhu na Mbeya City kwenye uwanja wa Manungu ulioko Turiani Morogoro.

Tuesday, September 17, 2013

KAYUNI KUHUDHURIA KOZI YA WAKUFUNZI CAF


Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Sunday Kayuni atashiriki warsha ya wakufunzi wa makocha wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) itakayofanyika kuanzia Oktoba 22-24 mwaka huu.

Warsha hiyo iliyoandaliwa na CAF kwa ajili ya wakufunzi wake itafanyika nchini Cameroon. Wakufunzi 18 wa CAF kwa upande wa makocha watahudhuria warsha hiyo.

Madhumuni ya warsha hiyo ni kuainisha majukumu yao, kubadilishana uzoefu. Pia kuwapa methodolojia mpya ya ufundishaji na muongozo kuhusu mfumo wa leseni za makocha ambao watautumia katika nchi wanazotoka.

Mbali ya Kayuni Tanzania, wakufunzi wengine ni Ahmed Babiker (Sudan), Amadou Shaibu (Nigeria), Boy Bizzah Mkhonta (Swaziland), Duodu Fred Osam (Ghana), Edussei Anthony (Ghana), Fathi Nossir (Misri), Faouzy Altaisha (Sudan) na Fran Hilton Smith (Afrika Kusini).

Wengine ni Francis Oti-Akenteng (Ghana), Honour Janza (Zambia), Kasimawo Laloko (Nigeria), Mahmoud Saad (Misri), Paul Hamilton (Nigeria), Serame Letsoaka (Afrika Kusini), Shawky Abdel Shafy (Misri), Thondoo Govinder (Mauritius) na Ulric Mathiot (Seychelles),

YANGA, PRISONS KAZI IPO KESHO, SIMBA KUKIPIGA NA MGAMBO JKT



Michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaingia raundi ya nne kesho (Septemba 18 mwaka huu) kwa mechi saba katika viwanja saba tofauti.

Vinara wa ligi hiyo, JKT Ruvu wanaonalewa na Kocha Mbwana Makata watakuwa ugenini Uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi mkoani Pwani dhidi ya Ruvu Shooting ya Charles Boniface Mkwasa.

Mechi hiyo inatarajiwa kuwa kivutio kikubwa kwa washabiki mkoani Pwani kutokana na aina ya soka inayochezwa na timu hizo.

Baada ya sare dhidi ya Mbeya City wikiendi iliyopita, Yanga inaendelea kubaki Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya ambapo itacheza na Tanzania Prisons katika mechi itakayochezeshwa na mwamuzi Simon Mbelwa kutoka Pwani.

Nayo Simba itaumana na Mgambo Shooting Stars ya Tanga katika mechi itakayopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000. Mechi hiyo itakuwa chini ya Kamishna David Lugenge kutoka Iringa.

Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Oljoro JKT kutoka Arusha na wenyeji Kagera Sugar wakati Azam na Ashanti United zitakwaruzana kwenye uga wa Azam Complex ulioko Chamazi jijini Dar es Salaam.

Mwamuzi Jacob Adongo kutoka Mara ndiye atakayechezesha mechi kati ya Coastal Union na Rhino Rangers itakayofanyika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga. Mtibwa Sugar inarejea uwanja wake wa Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro ambapo inaikaribisha Mbeya City ya Kocha Juma Mwambusi.

Wakati huo huo, Ligi Daraja la Kwanza (FDL) nayo inaendelea kesho (Septemba 18 mwaka huu) kwa mechi moja ambapo Lipuli ya Iringa ambayo wikiendi iliyopita ilicheza Mkamba mkoani Morogoro inapita mjini Morogoro kuikabili Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Jamhuri.

UWAKILISHI MKUTANO MKUU TFF WAFAFANULIWA



Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imesema uwakilishi wa ujumbe kwenye Mkutano Mkuu unaanzia kwenye chama cha mpira wa miguu cha mkoa, kufuatiwa na chama shiriki na baadaye klabu ya Ligi Kuu.

Mwongozo huo juu ya uwakilishi wa wajumbe kwenye Mkutano Mkuu umetolewa kutokana na maombi ya Sekretarieti ya TFF kwa kamati hiyo iliyokutana jana (Septemba 16 mwaka huu) baada ya kubaini baadhi ya wajumbe wanashikilia nafasi mbili kwenye vyama tofauti.

Kwa mujibu wa Ibara ya 5 ya Katiba, kuna makundi ya aina tatu ya wanachama wanaounda TFF. Makundi hayo ni vyama vya mikoa, vyama shiriki na klabu za Ligi Kuu.

Sekretarieti ya TFF imebaini kuwa kuna baadhi ya viongozi wa kuchaguliwa wa mikoa ambao pia ni viongozi wa vyama shiriki na klabu za Ligi Kuu, hivyo wana nafasi zaidi ya moja ya kuingia kwenye Mkutano Mkuu.

Hivyo, kutokana na mwongozo huo ushiriki wa wajumbe kwenye Mkutano Mkuu wa TFF utaanzia chama cha mkoa, kufuatiwa na chama shiriki na baadaye klabu za Ligi Kuu.

Pia nafasi ambazo zinaweza kuwakilishwa kwenye Mkutano Mkuu kama mhusika hayupo ni za Mwenyekiti atakayewakilishwa na Makamu Mwenyekiti, na Katibu atakayewakilishwa na Katibu Msaidizi.  Nafasi za ujumbe wa Mkutano Mkuu na ile ya mwakilishi wa klabu hazina uwakilishi kama mhusika hayupo.

Monday, September 16, 2013

PRISCA ATWAA TAJI LA MISS TALENT

 

WAKATI homa ya shindano la Redd’s Miss Tanzania ikiwa inapanda kwa washiriki wote, mrembo Prsica Clement juzi usiku alifanikiwa kutwaa taji la Redd’s Miss Tanzania Talent lililofanyika katika hoteli ya Giraffe iliyopo Kunduchi, Dar es Salaam.

Kutokana na ushindi huo, Prisca ambaye anatokea Sinza akiwakilisha Kanda ya Kinondoni, amefanikiwa kuingia katika hatua ya 15 Bora ya Redd’s Miss Tanzania.

Majaji wa shindano hilo walilazimika kumpa ushindi Prsica kutokana na uhodari wake wa kucheza na moto, hivyo kuwashinda washiriki wote 30 wa shindano hilo.

Watazamaji wengi waliofurika katika ukumbi wa hoteli hiyo, walikubaliana na uamuzi wa majaji wa kumpa ushindi huo.

Shindano la Redd’s Miss Tanzania linatarajiwa kufanyika mwishoni mwa wiki katika Ukumbi wa Mlimani City, uliopo Mwenge, Dar es Salaam ambapo mshindi ataondoka na gari dogo lenye thamani ya Sh milioni 15 na kitita taslimu cha fedha cha Sh milioni 8.

Mbali na mshindi kutwaa zawadi hizo, mshindi wa pili atapata Sh milioni 6.2, mshindi wa tatu Sh milioni , mshindi wa nne Sh milioni 3, mshindi wa tano Sh milioni 2, mshindi wa sita hadi 15 atapata Sh milioni 1.2 na waliobaki watapata Sh 700,000 kila mmoja.

Akizungumzia ushindi huo, Prsica alisema hiyo ni dalili njema kwake ya kutwaa taji hilo na ana uhakika mkubwa atafanikiwa kuwa mshindi.

Naye Meneja wa Redd’s Original, Victoria Kimaro alisema, shindano la mwaka huu limekuwa na msisimko mkubwa zaidi kutokana na washiriki wote kuwa na sifa zinazolingana.

“Mwaka huu Redd’s Miss Tanzania imepata washiriki bomba zaidi na naamini litakuwa na ushindani mkubwa na wa aina yake,” alisema Victoria.

Taji la Redd’s Miss Tanzania kwa sasa linashikiliwa na Brigitte Alfred aliyelitwaa taji hilo mwaka jana na kukabidhiwa gari aina ya Noah pamoja na kitita cha Sh milioni 8.

Shindano la Redd’s Miss Tanzania linadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia kinywaji chake cha Redd’s Original.

Sunday, September 15, 2013

YANGA WATAKA MECHI YAO NA MBEYA CITY IRUDIWE


Wachezaji wa Yanga wakiwa wamemzonga mwamuzi Andrew Shamba baada ya kukataa bao lao

HABARI, PICHA KWA HISANI YA BIN ZUBEIRY
KLABU ya Yanga ya Dar es Salaam, imekata rufani kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ikitaka mchezo wake wa jana wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Mbeya City ulioisha kwa sare ya 1-1 Uwanja wa Sokoine mjini hapa urudiwe katika Uwanja usiofungamana na timu yoyote baina yao.

Pamoja na hayo, Yanga SC pia imeomba mchezo wake mwingine dhidi ya Prisons Jumatano, uchezwe katika Uwanja mwingine badala ya Sokoine. 

Mjumbe wa Sekretarieti ya Yanga, Mkenya Patrick Naggi amewaambia Waandishi wa Habari leo katika Mkutano uliofanyika hoteli ya Paradise mjini kwamba, pamoja na Rufaa hiyo walicheza mechi ya jana chini ya kinga (Under Protest).

Mjumbe wa Sekretarieti ya Yanga SC, Patrick Naggo akizungumza na Waandishi wa Habari katika hoteli ya Paradise leo. Kulia Ofisa Habari wa klabu, Baraka Kizuguto.

“Baada ya vurugu tulizofanyiwa jana wakati tunaingia uwanjani, tuliwasiliana na marefa na Kamisaa tukawapa taarifa ya kucheza chini ya kinga na taratibu zote zilifanyika. Baada ya mechi kumalizika na kuendelea kufanyiwa vurugu, tukakata Rufaa,”alisema Naggi.

Naggi ambaye pia ni Kamisaa wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) alisema wana ushahidi na vielelezo vya kutosha juu ya vurugu walizofanyiwa jana tangu kabla ya mchezo, ikiwemo kushambuliwa kwa mawe wakati wanaingia.

Alisema basi lao lilivunjwa kioo na mashabiki uwanjani na dereva wake kujeruhiwa, hali ambayo iliwatia wasiwasi wachezaji na kucheza kwa woga jambo ambalo lilifanya wacheze ovyo na kulazimishwa sare.

Kwa upande wake, Ofisa Habari wa Yanga SC, Baraka Kizuguto alisema kwamba mapema baada ya kufika Mbeya walijaribu kuwasiliana na uongozi wa Chama cha Soka Mbeya (MREFA) kuhusu mambo mbalimbali ikiwemo usalama wao, lakini walikuwa wakipigwa chenga.

Kizuguto alisema kwamba kwa ujumla baada ya yaliyotokea jana, wameingiwa hofu kubwa kuelekea mchezo wa Jumatano dhidi ya Prisons mjini hapa, hivyo nao pia wameomba uchezwe kwenye Uwanja mwingine. 

“Kwa hali hii kwa kweli tuna wasiwasi sana na tunaona hapa si salama tena kwetu, hivyo tunaomba na mchezo huo uchezwe Uwanja mwingine kwa usalama wetu,”alisema.
Kizuguto pia alimlalamikia refa wa mchezo wa jana Andrew Shamba wa Pwani kwa kukataa bao lao halali lililofungwa na Didier Kavumbangu na kwamba na hilo pia limo kwenye rufaa yao

SIMBA, MTIBWA ZAINGIZA MIL 102, YANGA, MBEYA CITY MIL 100

MECHI ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya Simba na Mtibwa Sugar iliyochezwa jana (Septemba 14 mwaka huu) katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 95,080,000.

Watazamaji 16,507 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo namba 15 ya VPL msimu wa 2013/2014 iliyomalizika kwa wenyeji Simba kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Viingilio katika mechi hiyo vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 23,018,077.45 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 14,503,728.81.

Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 11,704,107.18, tiketi sh. 2,548,890, gharama za mechi sh. 7,022,464.31, Kamati ya Ligi sh. 7,022,464.31, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 3,511,232.15 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 2,730,958.34.


Wakati huo huo, mchezo mwingine wa ligi hiyo jana kati ya Yanga na Mbeya City uliingiza kiasi cha Sh. Milioni 100, kutokana na watu 20,000 walioingia uwanjani.

Kati ya hizo, Sh. Milioni 18 ni makato ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), gharama za tiketi Milioni 37, ghrama za Uwanja Milioni 6, MREFA wamepata Milioni 2.5, TFF Milioni 3.5, Kamati ya Ligi Milioni 7,  na kila timu imepata Sh. Milioni 23.6.

Taarifa hiyo ni kwa mujibu wa Mwenyekiti MREFA, Elias Mwanjala. 

SIMBA YANGURUMA, YANGA, AZAM ZABANWA


MSHAMBULIAJI Haruna Shamte wa Simba akiruka juu kukwepa kwanja la beki Hassan Ramadhani timu hizo zilipomenyana jana katika mechi ya ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

MABINGWA watetezi wa ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara, Yanga jana walilazimishwa sare ya bao 1-1 na watoto wa mjini, Mbeya City katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.

Wakati Yanga walilazimishwa sare, watani wao wa jadi Simba waliendelea kung'ara baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mtibwa Sugar katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Pambano kati ya Yanga na Mbeya City lilikuwa na ushindani mkali kutokana na timu zote mbili kucheza soka ya kuvutia, kushambuliana kwa zamu na kuwa na uchu wa kufunga mabao. Timu hizo zilikwenda mapumziko zikiwa suluhu.

Mbeya City ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 50 lililofungwa na Mwigane Yeya baada ya mabeki wa Yanga kujichanganya.

Bao la kusawazisha la Yanga lilifungwa na Didier Kavumbagu dakika ya 71 alipounganisha kwa kichwa mpira wa adhabu ndogo.

Kwa upande wa Simba, mabao yake yalifungwa na Henry Joseph na Betram Mombeki dakika ya 67 na 89.

Wakati huo huo, Azam jana iliendelea kubanwa katika ligi hiyo baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na Kagera Sugar katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

Kagera ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa Themi Felix dakika ya 25 kabla ya Khamis Mcha kuisawazishia Azam dakika ya 55.

Katika mechi zingine za ligi hiyo zilizochezwa jana, Coastal Union ilitoka suluhu na Prisons mjini Tanga wakati Rhino Rangers ilitoka sare ya bao 1-1 na JKT Oljoro mjini Arusha.

MWAKYEMBE AWAPA SHAVU SIKINDE

WAZIRI wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe (mwenye suti nyeusi katikati waliosimama) akiwa katika picha ya pamoja na wanamuziki wa bendi ya muziki wa dansi ya Mlimani Park Orchestra baada ya kukutana na kuzungumza nao ofisini kwake mjini Dar es Salaam juzi. (Picha na Emmanuel Ndege).

ALLY BUSHIRI: STARS INACHEZA SOKA YA ULAYA ILIYOTUSHINDA


KUTOLEWA mapema kwa timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars katika michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia za 2014, kumepokelewa kwa hisia tofauti na wadau wa michezo nchini. Kocha Msaidizi wa zamani wa timu hiyo, Ally Bushiri ni miongoni mwa, ambao kwa sasa hawafurahishwi na mwenendo wa timu hiyo hivi sasa. Katika makala hii ya ana kwa ana iliyoandikwa na Mwandishi Wetu ATHANAS KAZIGE, kocha huyo anaelezea sababu za kuvurunda kwa timu hiyo.

SWALI: Kwa mara nyingine, timu yetu ya Taifa, Taifa Stars imetolewa mapema katika michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia za 2014. Nini mtazamo wako kuhusu kufanya vibaya kwa timu hiyo katika michuano ya kimataifa?

JIBU: Zipo sababu nyingi, lakini kubwa ninayoiona kwa sasa ni kutoshirikishwa kwa wadau katika muundo unaofaa kutumika katika kuijenga timu hiyo ili iweze kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa.
 
Kwa kipindi kirefu sasa, Taifa Stars imekuwa ikiundwa na wachezaji wengi kutoka timu za Yanga, Simba, Azam na Mtibwa, tofauti na miaka ya nyuma, ambako baadhi ya wachezaji nyota walitoka mikoani kwenye timu, ambazo hazikuwa na majina makubwa.

Binafsi naamini Tanzania inayo hazina ya wachezaji wengi wenye vipaji vya kucheza soka, lakini tatizo kubwa lililopo ni ufuatiliaji wa wachezaji hao na kuwaendeleza. Haiwezekani kwa timu ya Taifa kuundwa na wachezaji kutoka klabu nne tu kila mwaka. Huu ni utaratibu mbovu na hautatuwezesha kufika mbali.

SWALI: Nini kifanyike ili kuondokana na utaratibu huo, ambao umeuelezea kuwa ni mbovu?

JIBU: Nadhani mfumo unaotumika sasa katika uteuzi wa wachezaji wa timu hiyo unapaswa kubadilika. Wakati umefika kwa Kocha Kim Poulsen kuelezwa kwamba, uchezaji wa wachezaji wa Ulaya ni tofauti na wa hapa Tanzania.

Wachezaji wetu wanapenda kucheza mpira wa kasi na kupeana pasi fupi fupi, lakini Poulsen anataka wacheze mfumo wa Kiulaya wa kutumia nguvu, kitu ambacho kwa wachezaji wetu hakiwezekani.

Kiukweli wachezaji wetu wa sasa hawana nguvu kama ilivyokuwa kwa wachezaji wa zamani na hawana uwezo wa kucheza kwa kasi muda wote wa dakika 90. Udhaifu huu ndio umekuwa ukisababisha Taifa Stars ishindwe kufurukuta inapocheza na timu zingine kubwa za Afrika, japokuwa wakati mwingine imekuwa ikionyesha maajabu kama vile kuzifunga Morocco, Zambia na Cameroon.

SWALI: Kwa maana hiyo, unadhani kuna umuhimu kwa Taifa Stars kurudia mfumo wa Kibrazil, ambao wachezaji waliuzoea wakati timu ilipokuwa chini ya Marcio Maximo na wewe ukiwa msaidizi wake?

JIBU: Kwa mtazamo wangu,suala la mfumo linapaswa kuwa ajenda kubwa katika kujadili maendeleo ya timu hiyo. Tunapaswa kutafakari kwa makini ni mfumo upi unaoweza kuifaa timu yetu ya taifa badala ya kubadili mfumo mara kwa mara.

Inawezekana pia kuwa, benchi la ufundi la Taifa Stars halimpi ushirikiano wa kutosha Maximo ili aweze kujua hali halisi ya uchezaji wa soka hapa nchini. Hili ni jukumu la mkurugenzi wetu wa ufundi, Sunday Kayuni na wasaidizi wake. Vinginevyo hadithi itaendelea kuwa ile ile ya kutolewa mapema.

SWALI: Huoni kama wachezaji wetu nao wana matatizo?

JIBU: Hilo lipo kwa sababu baadhi ya wachezaji walioteuliwa kuunda timu hiyo, uwezo wake umeshuka, hawapaswi kuendelea kuwemo kwenye timu hiyo.

Tatizo lingine ni kwamba baadhi ya wachezaji wanaoteuliwa kuunda timu hiyo, hawana mapenzi ya dhati ya kuichezea Taifa Stars. Hawachezaji kwa kujituma kama wanavyofanya wanapokuwa kwenye klabu zao. Wachezaji wa aina hii wanapaswa kuondolewa kwa vile wanawavunja nguvu wenzao.

SWALI: Nini ushauri wako kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)?

JIBU: Naushauri uongozi wa TFF uwashirikishe wadau wake katika kujadili matatizo haya na kupanga mikakati ya kuyatatua. Ni vyema TFF ikutane na wachezaji wa zamani waliowahi kung'ara Taifa Stars ili kupata mawazo na ushauri wao.

Upo umuhimu mkubwa wa kuifanyia marekebisho makubwa timu hiyo, kuanzia katika uteuzi, mafunzo na saikolojia ili kuwafanya wachezaji wacheze kwa ari na kujituma badala ya ilivyo sasa. Binafsi nipo tayari kutoa mchango wangu wa mawazo iwapo nitahitajika.

Nimecheza soka kwa miaka mingi na kwa kiwango cha kimataifa, nimekuwa kocha katika klabu nyingi na hata Taifa Stars ilipokuwa chini ya Maximo, hivyo nina uzoefu wa kutosha.

Tunapaswa kuanza mageuzi haya mapema kwa sababu tunakabiliwa na mashindano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Afrika za 2015, hivyo hatupaswi kurudia makosa. Tunapaswa kusonga mbele.

Haiwezekani tuwe na mashindano mazuri ya Copa Coca Cola na Kombe la Uhai, lakini tunashindwa kuwa na timu nzuri ya taifa. Kuna wakati timu yetu ya Copa Coca Cola iliwahi kutwaa kombe la kimataifa kule Brazil, lakini wale vijana hawajulikani wako wapi?

SWALI: Nini mwito wako kwa serikali kuhusu maendeleo ya soka nchini?

JIBU: Kwanza naipongeza serikali yetu kwa kuwa mstari wa mbele katika kuinua viwango mbalimbali vya michezo nchini, hasa kuajiri makocha kutoka nje kuja kuzifundisha timu zetu za taifa.

Ushauri wangu kwa serikali ni kutoiachia TFF pekee usimamizi wa timu yetu ya taifa. Inapaswa kuwatumia wataalamu wake katika kuisimamia na kutoa ushauri wa kuiboresha timu hii ili kuondokana na hadithi ya 'kichwa cha mwendawazimu'.