KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Saturday, January 21, 2012

Ujenzi uwanja wa Kaunda kugharimu bil.10/-


KLABU ya Yanga imeingia mkataba na Kampuni ya National Estare & Design Consultancy (NEDCO) kwa ajili ya kuujenga upya uwanja wake wa Karume uliopo Jangwani, Dar es Salaam.
Makubaliano hayo yalitiwa saini mjini Dar es Salaam jana kati ya Mwenyekiti wa Yanga, Lloyd Nchunga na Mkurugenzi wa NEDCO, Ambwene Mwakyusa.
Kwa mujibu wa mkataba huo, ujenzi wa uwanja huo utagharimu sh. bilioni 10 na unatarajiwa kuanza mapema mwakani.
Nchunga aliwaambia waandishi wa habari kuwa, ujenzi wa uwanja huo utaanza baada ya kukamilika kwa upembuzi wa muundo wake.
Mwenyekiti huyo wa Yanga alisema ujenzi huo utakapokamilika, uwanja wa Kaunda utakuwa na uwezo wa kuchukua mashabiki kati ya 10,000 na 15,000.
Nchunga alisema kukamilika kwa ujenzi wa uwanja huo kutaipunguzia klabu yake tatizo la kuhaha kusaka uwanja wa kuchezea wakati wa mashindano mbalimbali.
"Wazo la kujenga uwanja wetu katika hadhi tulikuwa nalo muda mrefu na sasa muda wa kufanya hivyo umefika, hivyo ni matarajio yangu kuwa jambo hili litafanikiwa na kufanikisha ndoto zetu za kumiliki uwanja wa kisasa,”alisema.
Mbali na ujenzi wa uwanja huo, Nchunga alisema klabu yake pia imepanga kujenga jengo la kitega uchumi la ghorofa saba mahali lilipo jengo lake dogo mtaa wa Mafia, Dar es Salaam.
Nchunga alisema ujenzi wa jengo hilo la ghorofa utaanza mara baada ya kukamilika kwa taratibu husika za utekelezwaji wa mpango huo.
Ili kufanikisha ujenzi wa uwanja huo, mwenyekiti huyo wa Yanga alisema klabu hiyo imepata wafadhili kadhaa watakaougharamia, ambao watawekwa hadharani hapo baadae.
Mbali na wadhamini, alisema wanatarajia kuendesha harambee kwa ajili ya kupata sh. milioni 800 zitakazotumika kwa ujenzi huo wakati fedha nyingine zitatafutwa kupitia mpango maalumu wa wanachama kuchangia.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa NEDCO, Mwakyusa alisema kampuni yake itahakikisha inajenga uwanja huo pamoja na jengo la kitega uchumi la Yanga katika hadhi ya pekee.
Mwakyusa alisema kampuni yake itaanza mara moja kukamilisha taratibu nyingine ndogo ndogo kwa ajili ya maandalizi ya ujenzi huo.

No comments:

Post a Comment