KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, January 12, 2012

Diamond kunusurika kufungwa jela ni utoto, umaarufu au pesa

Diamond na wenzake wakiwa mahakamani mjini Iringa

Diamond na mwenzake wakiwa nje ya mahakama


MSANII nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Naseeb Abdul ‘Diamond’ mwanzoni mwa wiki hii alinusurika kutupwa jela kwa kosa la kumshambulia mwandishi wa habari wa mjini Iringa.
Diamond alinusurika kufungwa baada ya kulipa faini na fidia ya sh. 80,000 kwa mlalamikaji, Francis Godwin, ambaye ni mwandishi wa habari wa kujitegemea wa mjini Iringa.
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo, Masua alisema kutokana na watuhumiwa wote watatu katika kesi hiyo, akiwemo Diamond kukiri kosa, anawahukumu kwenda jela miezi sita au kulipa faini ya sh. 50,000 kila mmoja.
Mbali na kuwatoza faini washtakiwa hao watatu, Hakimu Masua pia alimwamuru Diamond kumlipa mlalamikaji fidia ya sh. 30,000.
Ilidaiwa mahakamani kuwa, Diamond na wacheza shoo wake wawili walimshambulia Godwin na kuharibu kamera yake katika tukio lililotokea Desemba 31 mwaka jana kwenye Uwanja wa Samora mjini Iringa.
Wakitoa utetezi wao, watuhumiwa hao waliiomba mahakama iwapunguzie adhabu kwa vile hawakukusudia kutenda kosa hilo na walikwenda Iringa kwa lengo la kutoa burudani na kwamba tukio hilo lilitokana na ghadhabu walizokuwa nazo.
Diamond alikodiwa kwa ajili ya kufanya onyesho siku hiyo mjini Iringa na kwa mujibu wa ratiba, lilipangwa kuanza saa nane mchana na kumalizika saa 12 jioni.
Hata hivyo, onyesho hilo lilichelewa kuanza baada ya Diamond kufika uwanjani saa 11.50 na mashabiki kuamua kuwavaa waandaaji waliohusika kuchukua pesa za kiingilio.
Mbali na kuhoji kuchelewa kuanza kwa onyesho, mashabiki hao pia walihoji kwa nini tiketi zilizotumika zilikuwa za Chama cha Soka mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) zikionyesha mechi ya kirafiki kati ya Asante Kotoko ya Ghana na Marafiki wa Uhuru, iliyochezwa Novemba 12, 2011 Uwanja wa Taifa kwa kiingilio cha sh. 5,000.
Mara baada ya Diamond na wenzake kufika uwanjani kwa gari aina ya Coaster, mwandishi Godwin aliamua kumfuata na kumuhoji sababu ya kuchelewa, ndipo msanii huyo na wenzake walipomvaa na kuanza kumshambuliaji.
Kufuatia tukio hilo, baadhi ya mashabiki walimvamia Diamond na kuanza kumpiga huku wengine wakimtetea kabla ya polisi kufika uwanjani na kuokoa jahazi.
Katika tukio hilo, Godwin alidai alipoteza camera yake yenye thamani ya sh. milioni 1.5, simu ya mkononi yenye thamani ya sh. 300,000 na pia laptop yake aina ya Acer kuharibiwa.
Godwin aliripoti tukio hilo polisi na kufunguliwa kesi namba IR/RB/7700/2011.
Kutokana na kasheshe hiyo, Diamond alishindwa kufanya onyesho la uzinduzi wa albamu yake mpya, lililopangwa kufanyika Januari Mosi, 2012 kwenye ukumbi wa Maisha Club, Dar es Salaam.
Mbali na sakata hilo, Diamond ni msanii aliyekumbwa na kashfa nyingi katika mwaka 2011 na kutawala kwenye vyombo mbalimbali vya habari nchini, hasa magazeti ya udaku.
Mshindi huyo wa tuzo tatu za muziki za Kilimanjaro mwaka 2010, amekuwa akihusishwa na uhusiano wa kimapenzi na wasanii mbalimbali maarufu wa kike nchini.
Imedaiwa kuwa, tayari Diamond alishamvisha pete ya uchumba mrembo wa Tanzania wa mwaka 2008, Wema Sepetu, lakini wakati huo huo amekuwa na uhusiano wa kimapenzi na mrembo mwengine, Jokate Mwegelo.
Mbali na mabinti hao, Diamond pia amekuwa akidaiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mabinti kedekede, hatua iliyosababishwa apewe majina mbalimbali kama vile ‘mzee wa totoz’.
Hali hiyo imesababisha wadau wengi wa sanaa nchini wahoji, je huu ni utoto wa Diamond, kulewa sifa na umaarufu ama kapagawa kutokana na uwezo wa kipesa alionao sasa?
Hujachelewa Diamond, kutokana na umri wako mdogo, unao muda wa kutosha kuweza kujirekebisha, vinginevyo utakuja kuangukia pia kama wenzake akina Mr. Nice na wengineo.

No comments:

Post a Comment