KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, January 25, 2012

Simba raha tupu


VINARA wa ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara, Simba jana waliendelea kujikita kileleni baada ya kuichapa Coastal Union mabao 2-0 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ushindi huo uliiwezesha Simba kuendelea kuongoza ligi hiyo kwa kuwa na pointi 31 baada ya kucheza mechi 14 na kuiacha nyuma Yanga kwa tofauti ya pointi tatu. Yanga inazo pointi 28.
Mabao yaliyoiwezesha Simba kutoka uwanjani na pointi zote yalifungwa na Haruna Moshi na Gervas Kago, moja katika kila kipindi. Coastal ilijipatia bao lake kwa njia ya penalti kupitia kwa Hamisi Shengo.
Simba ilikuwa ya kwanza kulikaribia lango la Coastal Union dakika ya 24 wakati Haruna alipopiga mpira wa adhabu karibu na lango, lakini shuti lake lilitoka nje.
Dakika nane baadaye, Kago aliikosesha bao Simba baada ya kumegewa pasi safi na Juma Jabu, lakini shuti lake lilidakwa na kipa Godson Mmasa wa Coastal Union.
Coastal Union ilijibu mapigo dakika ya 34 wakati Mohamed Ibrahim alipogongeana vizuri na Daniel Lianga, lakini beki Kevin Yondani wa Simba alitokea na kuokoa hatari hiyo.
Simba ilipoteza nafasi nzuri ya kufunga bao dakika ya 36 wakati Haruna alipomtengenezea krosi maridhawa Kago, ambaye alikuwa amebaki ana kwa ana na goli baada ya kipa Mmasa wa Coastal Union kutoka langoni, lakini kichwa chake hakikuweza kulenga lango.
Bao la kwanza la Simba lilifungwa na Haruna dakika tano kabla ya mapumziko kwa shufi hafifu, kufuatia kazi nzuri iliyofanywa na Kapombe.
Ikiwa imesalia dakika moja kabla ya mapumziko, Simba ilipata nafasi nyingine nzuri ya kufunga bao wakati Mafisango alipopewa pasi akiwa ndani ya 18 huku kipa Mmasa akiwa ameanguka chini, lakini shuti lake lilitoka pembeni ya lango. Timu hizo zilikwenda mapumziko Simba ikiwa mbele kwa bao 1-0.
Uzembe wa beki Nassoro Chollo wa Simba nusura uiwezeshe Coastal kupata bao dakika ya 54 baada ya kupangua mpira vibaya, ukamkuta Ibrahim, aliyepiga shuti kali lililopaa juu ya lango.
Lango la Simba lilikuwa hatarini tena dakika ya 68 wakati Benard Mwalala alipojitwisha kwa kichwa mpira wa krosi, lakini ulipanguliwa na kipa Juma Kaseja.
Bao la pili la Simba lilifungwa na Kago dakika ya 77 kwa shuti kali baada ya kazi nzuri iliyofanywa na Haruna.
Coastal Union ilipata bao dakika ya 80 lililofungwa kwa njia ya penalti na Shengo baada ya beki Juma Nyoso kumchezea rafu mbaya Samwel Tennysona katika eneo la hatari.
Wakati huo huo, mashabiki wa Simba jana walikuwa wakigombea kununua jezi za timu ya Zamalek ya Misri, zilizokuwa zikiuzwa uwanjani na baadhi ya wafanyabiashara.
Zamalek inatarajiwa kumenyana na Yanga katika mechi ya raundi ya kwanza ya michuano ya klabu bingwa Afrika, inayotarajiwa kupigwa Februari 19 mwaka huu mjini Dar es Salaam.
Simba: Juma Kaseja, Nassoro Chollo, Juma Jabu, Juma Nyoso, Kevin Yondani, Shomari Kapombe, Mwinyi Kazimoto/ Ramadhani Singano, Jonas Gerrard, Patrick Mafisango, Haruna Moshi, Gervas Kago/ Edward Christopher.
Coastal Union: Godson Mmasa, Mbwana Hamisi, Ramadhani Wasso, Jamal Machelenga, Felix Stanley, Hamisi Shengo, Daniel Lianga/ Lameck Dayton, Mohamed Ibrahim, Benard Mwalala, Samwel Tennysona/ Rashid Mandawa, Salum Gila.

No comments:

Post a Comment