KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Saturday, January 21, 2012

Twiga Stars yapigwa jeki mil. 11.8/-



KAMPUNI ya ZH Hope Limited ya mjini Dar es Salaam imetoa tiketi nne za ndege zenye thamani ya sh. milioni 11.8 kwa ajili ya waamuzi wanne watakaochezesha mechi kati ya Twiga Stars na Namibia.
Mbali na tiketi hizo, kampuni hiyo pia imejitolea kuwagharamia waamuzi hao huduma ya chakula na malazi kwa siku zote watakazokuwepo nchini kwa ajili ya mechi hiyo.
Twiga Stars na Namibia zinatarajiwa kurudiana Januari 29 mwaka huu, katika mechi ya michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Afrika, itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, mechi hiyo itachezeshwa na waamuzi kutoka Zimbabwe wakati kamishna atatoka Ethiopia.
Aliwataja waamuzi hao kuwa ni Rusina Majo Kuda (mwamuzi wa kati) akisaidiwa na Stellah Ruvinga na Rudo Nhananga. Mwamuzi wa akiba atakuwa Pamela Chiwaya. Kamishna wa mechi hiyo ni Beletsh Gebremariam.
Wambura alisema gharama nzima ya mechi hiyo ya marudiano ni sh. milioni 74.6. Alisema fedha hizo zinajumuisha posho za wachezaji, benchi la ufundi na gharama ya kambi.
Kwa mujibu wa Wambura, gharama zingine ni malazi na chakula kwa msafara wa timu ya Namibia utakaokuwa na watu 25 kwa muda wote itakaokuwepo nchini pamoja na usafiri wa ndani.
Katika mechi ya awali iliyochezwa wiki iliyopita mjini Whindoek, Twiga Stars iliichapa Namibia mabao 2-0.
Kufuatia ushindi huo, Twiga Stars sasa inahitaji sare ya aina yoyote ili iweze kusonga mbele katika michuano hiyo, ambapo itakutana na mshindi kati ya Misri na Ethiopia.

No comments:

Post a Comment