KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, January 25, 2012

TBL, SBL ruksa kudhamini michezo Z'bar kwa vinywaji visivyo na kilevi



Na Aboud Mahmoud, Zanzibar
SERIKALI ya Zanzibar imesema kampuni zinazotengeneza pombe nchini zinaruhusiwa kudhamini michezo visiwani humu lakini kwa kutumia vinywaji visivyo na kilevi.
Hayo yalisemwa kwenye kikao cha Baraza la Wawakilishi jana na Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Abdilahi Jihad Hassan alipokuwa akijibu swali la mwakilishi wa Rahaleo, Nassoro Salum Aljazira.
Waziri Jihad alisema serikali haina pingamizi kwa kampuni za bia kudhamini michezo, lakini zinapaswa kufuata taratibu, ikiwa ni pamoja na udhamini wake kuhusisha vinywaji visivyo na kilevi.
Katika swali lake, Aljazira alitaka kujua iwapo serikali ya Zanzibar inaruhusu udhamini wa kampuni za bia katika michezo kwa kutumia vinywaji visivyo na kilevu kama vile Malta Guiness.
Kampuni maarufu kwa kutengeneza pombe nchini ni Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) na Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL).
"Hatuna mashaka kwa michezo kudhaminiwa na vinywaji baridi, lakini kampuni hizo lazima zitimize masharti ya msingi tutakayokubaliana," alisema waziri huyo
Aliongeza kuwa, kwa sasa serikali hairuhusu udhamini wa pombe katika michezo visiwani Zanzibar na kwamba serikali itaendelea kusimamia sera hiyo kwa lengo la kulinda maadili ya Wazanzibar.
Hata hivyo, Jihad alisema kama itatokea kwa timu za Zanzibar kupata udhamini huo, zinaruhusiwa kuutumia kwa michezo itakayofanyika nje ya visiwa hivyo.
Akitoa mfano, alisema hivi karibuni timu ya soka ya Baraza la Wawakilishi iliruhusiwa kutumia jezi zenye nembo ya moja ya kampuni hizo, lakini michezo iliyoshiriki haikufanyika Zanzibar.
Waziri Jihad alisema kila nchi inapaswa kufuata utamaduni wake na kwa Wazanzibar, utamaduni wao hauruhusu unywaji wa pombe hadharani.
Akijibu swali la msingi la Muyuni Jaku Hashim, Naibu Waziri wa wizara hiyo, Bihindi Hamad Khamis alisema kwa mujibu wa sera ya michezo ya mwaka 2007 kifungu cha 2.10.1, ufadhili wa michezo kupitia kampuni za bia haukubaliki katika visiwa vya Zanzibar.
Bihindi alisema agizo hilo linalindwa ndani ya mipaka ya Zanzibar, lakini timu yoyote inaruhusiwa kufanya hivyo nje ya visiwa hivyo.
Katika swali lake, Muyuni alitaka kujua kwa nini timu ya Baraza la Wawakilishi iliruhusiwa kuvaa jezi zenye nembo ya bia wakati ilipocheza na timu ya bunge la Jamhuri ya Muungano.

No comments:

Post a Comment