KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, January 18, 2012

DOGO JANJA: Sifanyi muziki kushindana na mtu


MSANII chipukizi wa muziki wa kizazi kipya nchini, Aboubakar Chende ‘Dogo Janja’ amesema hafanyikazi ya muziki kwa lengo la kushindana na msanii mwingine.
Amesema muziki kwake ni fani na kwamba siku zote kitu orijino kitabaki kuwa orojino na kitu feki kitakuwa feki.
Dogo Janja, mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Makongo, Dar es Salaam, alisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha televisheni cha Jambo cha TBC 1.
Msanii huyo aliyekuwa na maskani yake Arusha kabla ya kuhamia Dar es Salaam alisema, hapendi kushindanishwa na wasanii wengine wa umri wake kwa sababu kazi zao zinatofautiana.
Alisema anamshukuru Mungu kwamba hadi sasa ameweza kurekodi albamu moja huku baadhi ya nyimbo akiwa amewashirikisha wasanii kadhaa nyota nchini kama vile Dully Sykes, Peter Msechu, Tundaman na wengineo.
Dogo Janja, ambaye analelewa na kundi la Tip Top Connection alisema, nyimbo zote zilizomo kwenye albamu hiyo alizirekodi nyakati za usiku kwa vile ndio muda aliokuwa akipangiwa na wamiliki wa studio.
“Kwangu naona ilikuwa kama bahati kupangiwa muda huo kwa sababu ni muda mzuri, hata wazungu wanapojiliwaza kiakili, hupenda kutazama filamu nyakati za usiku,”alisema.
Msanii huyo alisema mlezi wake, Hamad Ally ‘Madee’ aliamua arekodi albamu hiyo kwa lengo la kutengeneza historia kwa vile mauzo yake huwa si mazuri na wasanii wengi wanalalamika.
“Madee aliniambia mauzo ya albamu si mazuri, lakini lazima nitengeneze historia. Shoo ndizo zinazolipa zaidi,”alisema dogo huyo.
Kwa sasa, Dogo Janja ameachia kibao kipya kinachokwenda kwa jina la Siri zao, akiwa amemshirikisha msanii mkongwe, Chege Chigunda.
Msanii huyo mwenye makeke alisema amerekodi kibao hicho katika studio za Marco Chali na kuongeza kuwa, anatarajia kutengeneza video yake baada ya mwezi mmoja.
Katika wimbo huo, Dogo Janja anasikika kwa sauti yake ya kitoto akitoa ujumbe kuhusiana na mada hiyo ya siri zao huku Chege akiitikia na kuchombeza zaidi.
Alisema ameamua kujipanga kuufanya mwaka 2012 uwe wenye mafanikio zaidi kwake kama ilivyokuwa mwaka 2011 alipojitambulisha kwenye fani hiyo.
“Mimi nataka kuhakikisha kuwa huu mwaka ninafunika na kuweka heshima kubwa katika medani hii ya muziki wa kizazi kipya na ndo kwanza kama unavyoona kazi imeanza,” alisema.
Dogo Janja alitamba kuwa, kwa sasa anastahili kuitwa msanii mkali kwa vile uwezo wake katika muziki wa hip hop umeongezeka maradufu, ikiwa ni pamoja na kurapu kwa lugha za kirangi na kichaga.

No comments:

Post a Comment