KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, January 18, 2012

Sina bifu na Afande Sele-Madee


KIONGOZI wa kikundi cha muziki wa kizazi kipya cha Tip Top Connection, Hamad Ally ’Madee’ amekanusha madai kuwa, haelewani na msanii mwenzake, Selemani Msindi ’Afande Sele’.
Akizungumza mjini Dar es Salaam wiki hii, Madee alisema anamuheshimu Afande Sele kama kaka yake na pia msanii aliyemtangulia kimuziki.
Madee alikuwa akijibu swali aliloulizwa uwapo ni kweli ana bifu na Afande Sele na ndio sababu amekuwa akitunga nyimbo zenye mwelekeo wa kumpiga madongo.
”Hata mimi nimekuwa nikishangazwa na uvumi huu kwa sababu sio kweli kwamba nina bifu na Afande Sele,”alisema.
Madee alisema mara nyingi anapotunga nyimbo zake, halengi kumwimba mtu zaidi ya kutoa elimu kwa wasikilizaji na pia kuwaburudisha.
”Katika muziki wa hip hop, lazima mashairi yawe ya majigambo, lakini kwa kweli silengi kumsema mtu yeyote,”alisisitiza.
Akijibu swali kuhusu sababu za kujiondoa kwa baadhi ya wasanii nyota wa kundi hilo, Madee alisema uamuzi wao huo umelenga kujiongezea maslahi mazuri zaidi.
Hata hivyo, alisema kuondoka kwa wasanii hao hakuwezi kulidhoofisha kundi hilo ndio sababu limeendelea kubaki kama lilivyo na litadumu hivyo.
Baadhi ya wasanii waliojiengua katika kundi hilo ni pamoja na mwanadada Khadija Shaaban ’K-Sher’, Cassim Mganga na MB Dog.
”Hawa wenzetu wanatafuta maisha, huwezi kuwalaumu, lakini Tip Top Connection bado ipo na itaendelea kuwepo,”alisisitiza.
Kwa sasa, Madee anajiandaa kurekodi wimbo wake mpya, utakaojulikana kwa jina la Historia. Amesema wimbo huo umelenga kuelezea historia yake katika maisha ya muziki wa kizazi kipya.

No comments:

Post a Comment