KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, January 25, 2012

Thabiti Abdul azua kasheshe Mashauzi Classic

Thabiti Abdul

Isha Mashauzi

Baadhi ya waimbaji wa Mashauzi Classic


KIKUNDI cha taarab cha Mashauzi Classic kimeanza kumong’onyoka baada ya waimbaji wake watatu wa kike kuamua kujivua gamba.
Waimbaji hao, ambao ni ndugu wa familia moja, walitangaza kujiondoa Mashauzi Classic mwishoni mwa wiki iliyopita kwa madai ya kuchoshwa na kero za bosi wao, Isha Ramadhani ‘Mashauzi’.
Mmoja wa waimbaji hao, Rahma Machupa alikieleza kituo cha redio cha Clouds wiki hii kuwa, binafsi amefikia uamuzi huo kutokana na Isha kumtuhumu kwamba ana uhusiano wa kimapenzi na mpiga kinanda Thabiti Abdul.
Rahma na waimbaji wenzake hao wawili, ndio walioshiriki kuimba nyimbo zilizomo kwenye albamu binafsi ya Isha inayojulikana kwa jina la Mama nipe radhi na baadaye kushiriki katika kuanzisha kundi hilo.
Mwanadada huyo alisema, awali Isha alikuwa na tabia ya kumsema kimafumbo kila walipokuwa wakifanya maonyesho katika kumbi mbalimbali za Dar es Salaam kabla ya kumshushia tuhuma hizo ‘laivu’.
Alisema baadaye, Isha aliamua kumsimamisha kazi kwa mwezi mmoja kwa tuhuma za utovu wa nidhamu, lakini alibadili uamuzi huo na kumrejesha kundini.
“Kuna siku alikuja nyumbani, akazungumza na mama yangu na kuniomba nirudi, nikakubali, lakini matatizo hayakumalizika,”alisema mwimbaji huyo mwenye umbo lenye mvuto.
Rahma alisema kilichomsikitisha zaidi ni kuona kuwa, aliyekuwa akitoa tuhuma hizo nzito kwake ni kiongozi wa kikundi, hivyo alishindwa kuvumilia na kuamua kujiengua.
“Afadhali ugomvi huo ungekuwa kati yetu sisi wasanii, hapo mtu unaweza kuelewa, lakini unamuhusisha kiongozi wa kikundi? Halafu anakutolea mafumbo stejini? Nimeshindwa kuelewa,”alisema Rahma.
Hata hivyo, Rahma alikanusha madai hayo ya Isha na kusema kuwa, anamuheshimu Thabiti kama kiongozi wake ndani ya kikundi hicho.
Kwa sasa, Rahma ameamua kujiunga na kikundi cha Jahazi Modern Taarab na amekuwa akiimba baadhi ya nyimbo za msanii nyota wa kundi hilo, Khadija Yusuph.
Kwa upande wake, Thabiti alithibitisha kuondoka kwa Rahma, lakini alikanusha madai kuwa alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwimbaji huyo.
“Ni kweli alinipigia simu na kunieleza kwamba yeye na ndugu zake wameamua kujitoa kwenye kundi letu na sisi hatuna kinyongo,”alisema Thabiti.
“Nilichomweleza ni kumtakia kila la heri huko aendako kwa sababu cha msingi ni kufanya kazi, mafanikio yanapatikana kwa kufanya kazi,”aliongeza.
Thabiti alimtetea Isha kwa madai kuwa, ana uwezo wa kumchukulia hatua msanii yeyote kwa sababu ndiye kiongozi mkuu wa kikundi.
“Sidhani kama Isha alifanya makosa kumsimamisha Rahma kwa sababu anayo mamlaka hayo anapoona msanii anakwenda kinyume na kikundi,” alisisitiza.
Alipoulizwa iwapo ana uhusiano wa kimapenzi na Isha na ndio sababu iliyomfanya kiongozi huyo wa Mashauzi Classic awe mkali kwa Rahma, mpapasa kinanda huyo alikanusha katakata.
“Mimi sina uhusiano wowote wa kimapenzi na Isha na wala sikuwa na uhusiano wowote na Rahma, hizo taarifa sio za kweli hata kidogo,”alisema.
Rahma alianza kupata umaarufu kwenye kundi la Mashauzi Classic kutokana na uimbaji wake kufanana na ule wa Isha.
Hata hivyo, baadhi ya wadau wa taarab hawakuwa wakivutiwa na uimbaji huo na kumshauri awe na uimbaji wa peke yake kwa lengo la kuwapa mashabiki ladha tofauti.
Juhudi za kumtafuta Isha ili azungumzie suala hilo hazikuweza kufanikiwa kwa vile simu yake ya mkononi ilikuwa haipatikani.

No comments:

Post a Comment