KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, January 12, 2012

Chipolopolo kuwaenzi wanasoka wake waliokufa 1993

Kalusha Bwalya

LUSAKA, Zambia
CHAMA cha Soka cha Zambia (FAZ) kimesema kitahakikisha timu ya taifa ya nchi hiyo (Chipolopolo) inafika hatua za juu zaidi katika fainali za mwaka huu za Kombe la Mataifa ya Afrika.
Rais wa FAZ, Kalusha Bwalya alisema juzi mjini hapa kuwa, lengo lao ni kuwaenzi wanasoka 23 wa Zambia waliofariki katika ajali ya ndege iliyotokea mwaka 1993 nchini Gabon.
Bwalya alikuwa miongoni mwa wachezaji waliokuwemo kwenye kikosi cha timu hiyo wakati huo, lakini hakusafiri nacho kwenye ndege moja.
Abiria wote 25 waliokuwemo kwenye ndege hiyo, wakiwemo wafanyakazi watano, ambao walikuwa wakisafiri kwenda Dakar, Senegal walifariki dunia.
Zambia ilikuwa ikienda Senegal kucheza na timu ya taifa ya nchi hiyo katika mechi ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia za mwaka 1994.
Timu ya wakati huo ya Zambia, inaelezewa kuwa ndiyo iliyokuwa bora zaidi kuliko zote zilizowahi kuundwa nchini humo.
Bwalya alisema akili zote za Wazambia zitakuwa zikikumbuka ajali hiyo mbaya wakati timu hiyo itakapokuwa ikishiriki kwenye fainali za Afrika zinazotarajiwa kuanza Januari 21 mwaka huu nchini Gabon na Equatorial Guinea.
“Kikosi chetu kimepania kuienzi timu ya Zambia ya mwaka 1993 kwa kufika hatua za juu katika fainali za mwaka huu nah ii itanisaidia kupunguza machungu ya kuwapoteza wachezaji wenzangu,”alisema. “Lengo ni kufika mbali zaidi ya hatua ya robo fainali. Hatutakwenda Gabon kwa matembezi, bali kuifanya nchi yetu ione fahari,”alisema rais huyo wa FAZ na nahodha wa zamani wa Zambia.
Kiungo Isaac Chansa alisema kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika kikosi chao, ikilinganishwa na kile kilichocheza fainali hizo mwaka 2010 nchini Angola.
“Wachezaji wamepata uzoefu mkubwa zaidi, hasa baada ya kucheza mechi nyingi za kimataifa. Lengo letu ni kuvuka hatua ya nusu fainali,”alisema.
“Tunataka kuipa heshima timu iliyopata ajali Gabon kwa kufanya vizuri katika michuano hii,”aliongeza kiungo huyo.
Zambia imepangwa kundi A pamoja na timu za Equatorial Guinea, Libya na Senegal na itacheza mechi yake ya kwanza Januari 21 kwa kumenyana na Senegal.
Wakati huo huo, mshambuliaji Given Singuluma wa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, ametemwa kwenye kikosi cha Zambia kitakachoshiriki kwenye fainali za Afrika.
Wachezaji wengine waliotemwa kwenye kikosi hicho ni Thomas Nyirenda, ambaye ni majeruhi na Justin Zulu.

1 comment: