KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Tuesday, January 24, 2012

Ni Simba na Coastal kesho Dar, viingilio vyatajwa



Mzunguko wa 14 wa Ligi Kuu ya Vodacom unamalizika kesho (Januari 25 mwaka huu) kwa mechi mbili zitakazochezwa kwenye viwanja tofauti jijini Dar es Salaam.
Simba itakuwa mwenyeji wa Coastal Union kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Viingilio vitakuwa sh. 3,000 kwa viti vya bluu na kijani, sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, sh. 10,000 kwa VIP B na C, sh. 15,000 kwa VIP A.

Nayo Azam itakuwa mgeni wa African Lyon katika mechi namba 97 itakayochezwa Uwanja wa Chamazi. Viingilio katika mechi hiyo ni sh. 10,000 kwa Jukwaa Kuu na sh. 3,000 mzunguko.
Wakati huo huo, kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imefanya marekebisho madogo kwenye ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom kutokana na Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kutumika kwa sherehe za kitaifa za kuzaliwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mechi namba 111 kati ya Toto Africans na African Lyon ambayo kwa mujibu wa ratiba ilikuwa ichezwe Februari 5 mwaka huu Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza sasa itachezwa Aprili 18 mwaka huu.
Mabadiliko hayo yamefanyika baada ya wamiliki wa Uwanja wa CCM Kirumba, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kueleza kuwa watautumia kwa sherehe za kuzaliwa chama chao, hivyo hautakuwa na nafasi kwa Februari 4, 5 na 6 mwaka huu.
Uamuzi huo umesababisha pia mabadiliko kwa mechi nyingine mbili. Mechi namba 168 kati ya Villa Squad na African Lyon iliyokuwa ichezwe Aprili 18 mwaka huu Uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaam, sasa itachezwa Aprili 22 mwaka huu.
Pia mechi namba 170 kati ya Azam na Toto Africans iliyokuwa ichezwe Aprili 29 mwaka huu jijini Dar es Salaam sasa imerudishwa nyuma hadi Aprili 26 mwaka huu ambayo ni Sikukuu ya Muungano.

No comments:

Post a Comment