SWALI: Timu yako imeanza vizuri mechi za mzunguko wa pili wa ligi kuu kwa kuifunga JKT Ruvu. Nini siri ya mafanikio hayo?
JIBU: Ninachoweza kusema ni kwamba, siri ya mafanikio haya ni kuwepo kwa umoja kati ya viongozi, wapenzi na wachezaji kwa jumla, ambapo kila moja anatimiza majukumu yake.
Lakini jambo la msingi ni kwamba, Polisi Dodoma imebadilika na kila mchezaji ana hamu kubwa ya kutaka kuona timu yake inashika mojawapo ya nafasi za juu katika ligi kuu msimu huu.
Kwa upande mwingine, naweza pia kusema kuwa mafanikio haya yametokana na wachezaji wote kuwa fiti, hakuna wachezaji majeruhi hadi sasa, kitu ambacho kwa kweli kinanipa faraja sana.
SWALI: Unadhani ni kwa nini timu yako haikufanya vizuri katika mechi za mzunguko wa kwanza?
JIBU: Kulikuwepo na matatizo madogo ya kiufundi, ambayo tayari viongozi wa jeshi la polisi mkoa wa Dodoma wameshayafanyiakazi.
Unajua miongoni mwa sera za jeshi hilo ni kuhakikisha polisi wanashiriki kikamilifu katika michezo na hii imesaidia sana kuifanya timu yetu na zinginezo za jeshi hili kuwa na mafanikio makubwa katika ngazi zilizopo.
SWALI: Nini matarajio yako katika mechi zijazo baada ya kuibuka na ushindi dhidi ya JKT Ruvu? Unapenda kuwaahidi nini mashabiki wenu?
JIBU: Lengo letu ni kushinda mechi zetu zote za mzunguko wa pili wa ligi. Tumejipanga kuendeleza wimbi la ushindi katika mechi yetu ijayo dhidi ya African Lyon na zile zitakazofuata. Lengo ni kuhakikisha tunachukua tena pointi tatu.
Sina hofu na mchezo huo na mingineyo kwa sababu bado naendelea na kazi ya kuisuka timu yangu ili kuhakikisha tunafanya vizuri kwenye michezo yote ya ligi kuu mzunguko wa pili.
SWALI: Timu yako imekuwa ikipata ushirikiano wowote kutoka kwa viongozi wa soka mkoani Dodoma na polisi makao makuu?
JIBU: Tangu nimejiunga na Polisi, nimegundua kwamba baadhi ya wadau wa soka mkoani Dodoma wanatoa ushirikiano wa hali ya juu kwa timu yetu.
Lakini kupitia gazeti lako, nawaomba wakazi wa mkoa huu kujitokeza kwa wingi kutusaidia vitu mbalimbali na pia kuishangilia kila inapocheza kwa sababu hii ni timu ya mkoa wao, ikishuka daraja, hawatapata nafasi ya kushuhudia mechi za ligi.
Ningependa kuwaona wadau wa soka katika mkoa wa Dodoma wakiipa sapoti timu yao, hata pale itakapokuwa ikicheza na timu kubwa za Simba na Yanga, waishangilie kwa hamasa zote ili kuwaongezea ari wachezaji.
SWALI: Katika miaka ya nyuma uliwahi kuichezea timu ya Yanga, ambayo mwaka huu inashiriki katika michuano ya klabu bingwa Afrika wakati wapinzani wao wa jadi, Simba watashiriki michuano ya Kombe la Shirikisho. Una maoni gani kuhusu ushiriki wa timu hizo kongwe katika michuano hiyo?
JIBU: Napenda kuwashauri viongozi wa klabu hizo wawe makini katika maandalizi ya timu zao ili ziweze kufanya vizuri na kupeperusha vyema bendera ya taifa.
Viongozi wa klabu hizo wanapaswa kusikiliza na kupokea ushauri wa kitaalam kutoka kwa makocha wao kwa sababu wanakuwa wameshaandaa programu zao, ambazo zinapaswa kutekelezwa.
Ukweli ni kwamba, iwapo viongozi wa Simba na Yanga watashindwa kutekeleza programu za makocha wao, haitakuwa rahisi kwa timu hizo kupata mafanikio.
Timu zinapaswa kukaa kambini mapema na kwa muda mrefu ili kuwafanya wachezaji waweze kucheza kwa uelewano na kushika mafunzo ya makocha wao.
Pia ni muhimu kwa viongozi kuhakikisha kuwa, wachezaji wanalipwa haki zao zote na kwa wakati ili kuepuka kuwepo na malalamiko ama manung’uniko. Hii itasaidia kuzifanya akili za wachezaji ziwe kwenye mchezo muda wote badala ya kufikiria vitu vingine.
SWALI: Yanga wanacheza mechi yao ya kwanza dhidi ya Zamalek ya Misri. Unauzungumziaje mchezo huu? Unadhani Yanga wana uwezo wa kuitoa Zamalek?
JIBU: Hakuna kisichowezekana katika soka. Jambo la msingi ni kwa kila mmoja kutimiza wajibu wake. Ushauri wangu kwa Kocha Kostadin Papic ni kuimarisha zaidi safu zake za ulinzi na ushambuliaji. Nilivyoiona Yanga hadi sasa, tatizo lake kubwa lipo kwenye safu ya ulinzi. Haichezi kwa uelewano mkubwa.
Kasoro nyingine ipo kwenye ufungaji wa mabao. Tatizo hili linapaswa kufanyiwa kazi mapema ili washambuliaji wa timu hiyo wawe na uwezo wa kufunga mabao mengi katika mechi moja.
Ni kweli kwamba Zamalek ni moja ya timu ngumu na tishio nchini Misri na barani Afrika, lakini iwapo viongozi, makocha na wachezaji wa Yanga watajipanga vizuri, wanaweza kuitoa kwenye mashindano.
Moja ya mbinu zinazotumiwa sana na timu za Misri ni kutafuta ushindi mkubwa nyumbani na kulazimisha sare ugenini, hasa inapokutana na timu ngumu. Hivyo Yanga nayo inapaswa kuhakikisha wanashinda mechi ya nyumbani.
Kwa upande wa Simba, naona kidogo wao wapo makini kutokana na kuiweka timu kambini mapema, ingawa nimesikia kocha wao, Milovan Cirkovic ameamua kuifumua timu hiyo.
Uzuri wa Simba ni kwamba walianza kambi kabla ya kwenda Zanzibar kushiriki mashindano ya Kombe la Mapinduzi, waliporejea wakaendelea na kambi na kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Tusker ya Kenya.
Jambo la msingi kwa benchi la ufundi la Simba ni kurekebisha dosari zote zilizojitokeza kwa timu hiyo katika mechi zake za hivi karibuni. Naamini kocha wao ameziona na ndio sababu ameamua kuisuka upya timu yake.
SWALI: Unauonaje mwenendo wa michuano ya ligi kuu hadi sasa? Unadhani ligi inaendeshwa kwa kufuata kanuni na kwa mfumo mzuri?
JIBU: Kwa maoni yangu, nadhani kuna umuhimu wa kufanya mabadiliko kidogo katika uendeshaji wa ligi kuu ili iweze kuwa na ushindani mkali zaidi.
Ilivyo sasa, baadhi ya timu, hasa zile kubwa na zenye uwezo kipesa, zimekuwa zikishinda mechi zake kimizengwe. Baadhi ya timu zimekuwa zikishinda kwa kutumia mbinu chafu za nje ya uwanja. Nina hakika kuwa, bingwa wa ligi hiyo msimu huu atapatikana kwa kazi ngumu.
Kasoro nyingine niliyoiona kwenye ligi ni uchache wa timu. Haipendezi kuona bingwa wa ligi kuu anapatikana baada ya kucheza mechi 26. Anapaswa kucheza mechi nyingi zaidi. Hivyo ligi yetu inapaswa kuwa na timu nyingi zaidi ili iwe ndefu na bingwa apatikane baada ya kucheza mechi nyingi.
Vilevile ningependa kulishauri Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) liboreshe zaidi mkataba wake na wadhamini, Kampuni ya Simu za Mkononi ya Vodacom, ili timu ziweze kupata maslahi bora zaidi.
Kama itawezekana, nadhani ni vyema TFF itafute wadhamini wengine zaidi kwa ajili ya kudhamini ligi hiyo ili maslahi kwa timu na wachezaji yawe bora. Tuachane na ukiritimba wa sasa wa ligi kudhaminiwa na kampuni moja pekee.
Ilivyo sasa, timu zinazonufaika zaidi kutokana na udhamini ni Simba na Yanga kwa sababu mbali ya kupata udhamini wa Vodacom, pia zinadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).
SWALI: Unapenda kutoa mwito gani kwa serikali kuhusu michezo?
JIBU: Naishauri serikali iendelee kuhimiza michezo yote ichezwe kuanzia katika shule za msingi, sekondari, vyuo na taasisi mbalimbali kwa sababu huko ndiko wanakoweza kupatikana wanamichezo wengi zaidi.
Vilevile naishauri serikali iendelee kuwachukulia hatua kali viongozi wa manispaa, ambao watabainika kuuza viwanja vya michezo. Tatizo hili limekuwa sugu na kusababisha watoto wengi wakose mahali pa kuchezea na hivyo kushindwa kuonyesha vipaji vyao.