KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, March 31, 2014

KOMBE LA NSSF LAANZA KWA KISHINDO



 Mgeni rasmi, Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudencia Kabaka akisalimiana na wachezaji wa Azam TV
 Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudencia Kabaka akirusha mpira kimiani wakati alipokuwa akifungua michuano ya netiboli.
 Waziri Kabaka akisalimiana na mwamuzi, Hassan Isihaka aliyechezesha mechi ya soka kati ya Habari Zanzibar na New Habari
Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudencia Kabaka akisalimiana na wachezaji wa Habari Zanzibar
HABARI Zanzibar jana ilianza vyema michuano ya soka ya Kombe la Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), baada ya kuibugiza New Habari mabao 4-1 katika mechi iliyochezwa kwenye uwanja wa klabu ya Sigara, Chang'ombe, Dar es Salaam.

Mabao ya Habari Zanzibar yalifungwa na Yussuf Chuma aliyefunga matatu bna Amir Suleiman wakati bao la kujifariji la New Habari lilifungwa na Florian Masinde.

Katika netiboli, Jambo Leo ilianza michuano hiyo kwa kishindo baada ya kuibugiza Wizara ya Habari mabao 60-8 wakati Azam TV iliicharaza TSN mabao 18-13.

Michuano hiyo ilifunguliwa na Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudencia Kabaka, ambaye alivitaka vyombo vya habari kuitumia kujenga ushirikiano na kuimarisha umoja miongoni mwao.

Waziri Kabaka pia alivitaka vyombo hivyo vya habari kuepuka kuwatumia wachezaji wasio waajiriwa kwa sababu kufanya hivyo ni kuondosha maana ya mashindano hayo.

SIMBA, YANGA ZACHEZEA VICHAPO LIGI KUU



MABINGWA watetezi wa ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara, Yanga na watani wao wa jadi, Simba jana walichezea vichapo kutoka kwa timu za Mgambo JKT na Azam.


Wakati Yanga ilichapwa mabao 2-1 na Mgambo kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga, watani wao Simba walichezea kichapo hicho kutoka kwa Azam kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Matokeo hayo yaliiwezesha Azam kuzidi kujichimbia kileleni mwa ligi hiyo, ikiwa na pointi 53 baada ya kucheza mechi 22 wakati Yanga inaendelea kushika nafasi ya pili ikiwa na pointi 46.

Mabao ya Azam yalifungwa na Khamis Mcha na John Bocco dakika ya 16 na 56 wakati bao la Simba lilifungwa na Uhuru Selemani dakika ya 45.

Kwa upande wa Yanga, kipigo ilichokipata kimefifisha matumaini ya timu hiyo kutetea taji hilo msimu huu.

Iliwachukua Mgambo dakika moja kuhesabu bao la kwanza lililofungwa na Full Maganga kwa shuti la mbali lililomshinda kipa Juma Kaseja.

Bao la kusawazisha la Yanga lilifungwa kwa njia ya penalti na nahodha Nadir Haroub 'Cannavaro dakika ya 52 baada ya beki mmoja wa Mgambo kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari.

Mgambo iliongeza bao la pili dakika ya 63 lililofungwa na Malima Busungu kwa njia ya penalti baada ya kukwatuliwa na beki mmoja wa Yanga ndani ya eneo la hatari.

Thursday, March 27, 2014

YANGA YAUA, AZAM YASONGA MBELE


MABINGWA watetezi wa ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara, Yanga jana waliendelea kuitimulia vumbi Azam baada ya kuichapa Prisons mabao 5-0 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Ushindi huo mnono uliiwezesha Yanga kuendelea kushika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi 46 baada ya kucheza mechi 21 huku ikiwa na mchezo mmoja mkononi.

Azam, ambayo jana iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mgambo JKT kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, bado inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 50 baada ya kucheza mechi 22.

Yanga ilihesabu bao la kwanza dakika ya 21 lililofungwa na Emmanuel Okwi kwa mpira wa adhabu ya moja kwa moja, ambao kipa Beno Kakolanya wa Prisons hakuweza kuuona.

Prisons ilipata nafasi nzuri ya kusawazisha dakika ya 43 baada ya beki Oscar Joshua wa Yanga kumwangusha Frank Hau ndani ya eneo la hatari na mwamuzi Andrew Shamba kutoka Pwani kuamuru ipigwe penalti. Hata hivyo, shuti la Lugano Mwangama lilitoka nje ya lango.

Dakika tano baadaye, Mrisho Ngasa aliiongezea Yanga bao la pili baada ya kuunganisha wavuni krosi maridhawa kutoka kwa Hussein Javu, aliyeingia kuchukua nafasi ya Jerry Tegete.

Katika dakika ya 44, lango la Prisons lilikuwa kwenye msukosuko mkali baada ya Yanga kufanya shambulizi zito, lakini shuti la Javu liligonga mwamba wa goli na mpira uliporudi uwanjani, uliokolewa na beki mmoja wa Prisons, ukamkuta Ngasa, ambaye shuti lake lilitolewa nje na kuwa kona.

Timu hizo zilikwenda mapumziko Yanga ikiwa mbele kwa mabao 2-0.

Bao la tatu la Yanga lilifungwa na Hamisi Kiiza dakika ya 67 baada ya kuuwahi mpira uliotemwa na kipa Beno wa Prisons, aliyepangua kiki kali ya Simon Msuva ambaye aligongeana vizuri na Hassan Dilunga.

Beki Nadir Haroub 'Cannavaro' aliiongezea Yanga bao la nne dakika ya 78 kwa

njia ya penalti, iliyotokana na Javu kuangushwa ndani ya eneo la hatari. Kiiza alihitimisha karamu ya mabao kwa kufunga bao la tano dakika ya 88 baada ya kupokea pasi kutoka kwa Javu.

Katika kipindi hicho cha pili, Prisons ilionekana kuzidiwa kila idara na kushindwa kufanya mashambulizi kama ilivyokuwa kipindi cha kwanza wakati Javu aliongeza kasi ya mashambulizi kwa Yanga na kushangiliwa na mashabiki kila alipogusa mpira.

Yanga: Juma Kaseja, Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub 'Cannavaro', Kelvin Yondan, Frank Domayo, Simon Msuva, Hassan Dilunga, Jerry Tegete/Hussein Javu, Mrisho Ngasa/Haruna Niyonzima, Emmanuel Okwi/Hamisi Kiiza.

Prisons: Beno Kakolanya, Salum Kimenya, Laurian Mpalile, Lugano Mwagama, Nurdin Chona, Jumanne Fadhil, Godfrey Mageta, Fred Chudu, Peter Michael, Frank Hau/Bryson Mponzi na Ibrahim Mamba/ Six Mwakasega.

Mwandishi Wetu ameripoti kutoka Tanga kuwa, Azam iliendelea kujikita kileleni mwa ligi hiyo baada ya kuichapa Mgambo JKT bao 1-0 kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.

Bao la kwanza la Azam lilifungwa na mshambuliaji John Bocco dakika ya 60 kabla ya Brian Umony kuongeza la pili dakika ya 82.

OKWI AUZIMIA MUZIKI WA MBEYA CITY


Na Emmanuel Ndege
MSHAMBULIAJI nyota wa klabu ya Yanga, Emmanuel Okwi, amesema anakunwa na kiwango cha juu cha soka kinachoonyeshwa na timu ya Mbeya City katika michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara.

Akizungumza na Burudani makao makuu ya klabu hiyo, mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam juzi, Okwi alisema Mbeya City imeleta changamoto mpya katika ligi kuu msimu huu.

Okwi alisema timu hiyo yenye makao makuu yake mjini Mbeya, haijayumba kisoka tangu ligi kuu ilipoanza na wachezaji wake wanacheza kwa kujiamini na bila kukata tamaa.

"Iwapo wataendelea hivi msimu ujao, haitakuwa ajabu kwa Mbeya City kutwaa ubingwa,"alisema mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Uganda.

Okwi amekiri kuwa, ligi ya msimu huu ni ngumu na yenye ushindani mkali na hakuna timu yenye uwezo wa kutangaza ubingwa mapema.

"Nimeichezea Simba kwa miaka zaidi ya miwili. Huko nyuma timu zilikuwa na uwezo wa kutangaza ubingwa zikiwa zimesalia mechi mbili au tatu, lakini msimu huu ni vigumu,"alisema Okwi.

"Yanga, Azam na Mbeya City kila moja ina uwezo wa kutwaa ubingwa, hali hii imesababisha kuwepo kwa ushindani mkali. Ni vigumu kutabiri bingwa mapema,"aliongeza.

Hata hivyo, Okwi alisema licha ya kuzidiwa kwa pointi na Azam, Yanga bado inayo nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa ligi hiyo, iwapo wachezaji wake wataendelea kucheza kwa kujituma.

Alisema atahakikisha anasaidiana vyema na wachezaji wenzake kuiwakilisha vizuri timu hiyo ili itwae ubingwa na kupata nafasi nyingine ya kushiriki michuano ya klabu bingwa Afrika mwakani.

Akizungumzia jinamizi lililoikumba timu hiyo hivi karibuni la kupoteza penalti katika mechi muhimu, Okwi alisema, adhabu hiyo haina ufundi na kwamba mchezaji yeyote anaweza kupoteza.

"Penalti ni sawa na mchezo wa bahati nasibu, unaweza kupata au kukosa, hazina ufundi,"alisisitiza nyota huyo wa zamani wa Simba.

Wakati huo huo, klabu ya Yanga imesema, itakata rufani kwenye Mahakama ya Rufani Tanzania kupinga hukumu ya Makahama Kuu Divisheni ya Kazi ya kuitaka timu hiyo iwalipe wachezaji Wisdom Ndlovu na Stephen Marashi sh. milioni 106.

Katibu Mkuu wa Yanga, Ben Njovu, alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, wamepokea nakala ya hukumu ya kesi hiyo iliyofungiwa na wachezaji hao ya kupinga kukatishiwa mikataba yao.

KUMBE ZACK ORJI NI MWANAMUZIKI




LAGOS, Nigeria
WATU wengi wanamtambua Zack Amaefula Orjioke, kuwa ni mmoja wa wacheza filamu nyota na wakongwe nchini Nigeria.

Mkongwe huyo, ambaye ni maarufu zaidi kwa jina la Zack Orji, amecheza filamu nyingi na kujipatia sifa na umaarufu mkubwa kwa mashabiki wa fani hiyo nchini Nigeria.

Kumbe Zack anacho kipaji kingine cha ziada. Nacho ni muziki. Amepanga kuingia studio hivi karibuni na kurekodi wimbo wake wa kwanza.

Akihojiwa na gazeti la Sun la Nigeria wiki hii, Zack alisema ameamua kujitosa kwenye fani hiyo kwa vile anacho kipaji kingine cha ziada.

Kwa mujibu w a Zack, kibao chake hicho kinajulikana kwa jina la Cradles of Greatness, ambacho kinaelezea mambo mbalimbali kuhusu nchi yake ya Nigeria.

Katika moja ya beti za wimbo huo, Zack ameandika maneno yafuatayo:

"Oh Nigeria, nchi ya asili ya mababu zetu, tunajivunia asili yetu, tunakupenda. Japokuwa tunatofautiana katika makabila na lugha, bado tuko pamoja. Tunajivunia nchi ya asili yetu. Nchi yenye ndoto na nafasi nyingi. Alama ya umoja wetu. Nchi ya uhuru wetu."

EMEKA IKE AKANA KUTENGANA NA MKEWE




LAGOS, Nigeria
KATIKA siku za hivi karibuni, kumekuwepo na uvumi kwamba, mwigizaji Emeka Ike na mkewe, wamekuwa katika msuguano mkali uliosababisha watengane.

Kwa mujibu wa habari hizo, mke wa Emeka alidai talaka kutoka kwa mumewe kutokana na kuchoshwa na tabia za mwigizaji huyo.

Habari hizo ziliendelea kueleza kuwa, kutokana na ndoa ya wawili hao kuvunjika, Emeka aliamua kuwachukua watoto wao wawili na kwenda nao Abuja, akimuacha mkewe akibaki na watoto wengine wawili mjini Lagos.

Hata hivyo, Emeka amekanusha vikali habari hizo na kuziita kuwa ni za uzushi.

Emeka ameandika kwenye mtandao wa facebook wiki hii: " Huu ni uzushi."

Mbali na kuandika maneno hayo, Emeka aliweka picha aliyopiga pamoja na mkewe na watoto wao wanne.

DESMOND: SIWEZI KUACHA UIGIZAJI

LAGOS, Nigeria
KUMEKUWEPO na uvumi kwamba, mwigizaji na mtayarishaji mahiri wa filamu wa Nigeria, Desmond Elliot, anataka kuachana na fani hiyo ili ajitose kwenye siasa.

Baadhi ya mitandao ya kijamii na magazeti ya Nigeria, yaliripoti hivi karibuni kuwa, Elliot anataka kuipa kisogo fani hiyo ili aweze kupata muda wa kutosha katika masuala ya siasa.

Hata hivyo, mwigizaji huyo mwenye mvuto na mshindi wa tuzo za AMVCA, amekanusha taarifa hizo kwa kusema si sahihi.

Eliiot alisema wiki hii mjini hapa kuwa, ni kweli anataka kuwania nafasi ya kisiasa katika uchaguzi mkuu wa 2015, lakini hawezi kuacha uigizaji.

Msanii huyo, ambaye amekuwepo kwenye fani ya uigizaji kwa karibu miaka 12 sasa, alisema: "Siwezi kuacha uigizaji. Kama wamesema hivyo, siyo kweli. Sielewi wameyapata wapi maneno hayo."

Wednesday, March 26, 2014

STELLA AFUNGA AKAUNTI ZAKE ZOTE ZA FACEBOOK


LAGOS, Nigeria
MCHEZA filamu mwenye mvuto nchini Nigeria, Stella Damasus, ameamua kufunga akaunti zake za facebook kutokana na kuingiliwa na baadhi ya watu wenye dhamira mbaya.
Stella alisema wiki hii mjini hapa kuwa, baadhi ya watu wamekuwa wakitumia akaunti zake hizo kuwalaghai mashabiki wake na kujipatia pesa kwa njia ya udanganyifu.
Uamuzi huo wa Stella, umekuja siku chache baada ya mcheza filamu mwingine nyota wa Ghana, Yvonne Nelson, kuwataka wamiliki wa mtandao wa Twitter kuwadhibiti watu wanaoingilia akaunti yake.
"Napenda kuwafahamisha kwamba, kuanzia leo nafunga akaunti zangu zote za facebok. Ninamaanisha hivyo. Tafadhali sambaza ujumbe huu na kuwaeleza marafiki kwamba, baada ya leo, yeyote atakayejiita Stella Damasus kwenye facebook, siye mimi.
"Nataka kujilinda na kujiweka kwenye mtazamo bora, hasa baada ya baadhi ya matapeli kuanza kutumia akaunti zangu kukusanya pesa kutoka kwa watu wasiokuwa na hatia, ambao wanataka kujitosa kwenye fani ya uigizaji. Ni bora nipoteze akaunti zangu za facebook kuliko kuwaacha watu wafikirie kwamba naweza kufanya kitu kama hicho. Nawapenda na Mungu awabariki," ameeleza Stella.

SIJUTII KUWA NILIVYO-AKI



LAGOS, Nigeria
MARA nyingi watu wenye maumbo madogo na wafupi huwa wakikumbana na misukosuko mingi katika jamii, ikiwa ni pamoja na kutaniwa ama kudhihakiwa.

Lakini hali ni tofauti kwa mcheza filamu machachari wa Nigeria, Chinedu Ikedieze 'Aki', ambaye anaamini kuwa, umbile lake ni zawadi maalumu aliyobarikiwa na Mwenyezi Mungu ana anajivunia kuwa alivyo.

Akihojiwa na gazeti la YES la Nigeria hivi karibuni, Aki alisema anafurahia kupata tuzo za heshima kutokana na fani yake ya uigizaji, lakini hakuna faida yoyote kubwa anayoipata kutokana na tuzo hizo.

Aki alisema hakuna zawadi ya pesa ama nyingine yoyote kubwa anayoipata kama ilivyo kwa wasanii wanaoshinda tuzo hizo katika nchi za Ulaya Magharibi, lakini anafurahia kutambuliwa kwake na kuheshimiwa katika jamii.

"Ninaposafiri na kufika kwenye uwanja wa ndege, napata heshima maalumu na kutambuliwa. Mbali na hilo, hakuna kingine ninachokipata. Silipwi chochote, sipati faida yoyote.

"Sana sana napata heshima kama wanayoipata wanandugu wa ukoo wa kifalme wa Uingereza. Wao wanayo heshima wanayoipata katika jamii ya kimataifa na kutambulika, lakini vitu hivyo havipo hapa,"alisema msanii huyo, ambaye hivi karibuni alitunukiwa tuzo ya heshima ya MFR.

Alipoulizwa iwapo aliwahi kujishangaa kwa nini alizaliwa kama alivyo, mcheza filamu huyo alijibu: "Kwani mimi ndiye niliyejiumba? Kwa nini nijiulize swali kama hilo? Unaweza kujiuliza swali hilo iwapo utakuwa umechanganyikiwa kuhusu maisha ama umechoshwa na maisha."

"Lakini katika suala langu, sipo hivyo. Unapoamka asubuhi na kupata kitu fulani cha kula, unakuwa na watu wanaotabasamu kwa ajili yako na wewe kuwarejeshea tabasamu, unahitaji kitu gani kingine? Baadaye unakwenda kitandani, unalala na unapoumwa unakwenda hospitali, ni zawadi ipi nyingine muhimu kuliko hivyo?" Alihoji Aki.

Aki alisema kwa kadri anavyojitambua, umbo lake ni zawadi pekee aliyopewa na Mungu na kuongeza kuwa, wapo watu waliobarikiwa kuwa na pesa, magari, nyumba za fahari na kila wanachokihitaji, lakini ni wagonjwa.

"Hawazifurahii fedha walizonazo. Hivyo zawadi sahihi kwangu ni kuwa na afya nzuri,"alisisitiza mcheza filamu huyo machachari.

MLIMANI PARK ORCHESTRA 'SIKINDE' WAINGIZWA MJINI


 
WIMBI la wizi wa kazi za sanaa limezidi kushika kasi baada ya baadhi ya wafanyabiashara kuiingiza mjini bendi ya muziki wa dansi ya Mlimani Park Orchestra 'Sikinde' kwa kutengeneza DVD yenye albamu tatu za bendi hiyo.

DVD hiyo yenye nyimbo 20, ilianza kuuzwa wiki mbili zilizopita katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam huku viongozi wa bendi hiyo wakiwa hawana taarifa.

Uchunguzi uliofanywa na Burudani umebaini kuwa, DVD hiyo ni feki kwa vile haina nembo ya hakimiliki na ile ya Mamlaka ya Kodi ya Mapato (TRA), ambayo imepewa jukumu la kusimamia mauzo ya kazi za wasanii.

Nyimbo zilizomo kwenye DVD hiyo, ambayo gazeti hili linayo nakala yake, ni za tangu miaka ya 2000 wakati bendi hiyo ilipokuwa chini ya uongozi wa Bennovilla Anthony na Shabani Dede, ambao kwa sasa hawapo.

Wanamuziki wengine wa zamani wanaoonekana kwenye DVD hiyo ni pamoja na marehemu Tino Masinge, marehemu Charles John 'Ngosha' na marehemu Machaku Salum.

Kava la DVD hiyo limeandikwa East African Music- DDC Mlimani Park-Three Album na picha kubwa zinazoipamba ni ya wanamuziki Hassan Bitchuka na Abdalla Hemba. Picha ndogo ni za Dede na Hassan Kunyata wakiwa wamevaa fulana zenye nembo ya Konyagi.

Kinachodhihirisha kwamba toleo hilo ni la 'kufoji' ni kukosewa kwa majina ya baadhi ya nyimbo na wanamuziki. Kwa mfano, wimbo wa Huruma kwa wagonjwa, umeandikwa Huruma kwa wagonwa.

Jina la mwanamuziki Karama Regesu, ambaye ni mtunzi wa wimbo wa Supu Umeitia nazi, nalo limekosewa kwa kuandikwa Karama Resegu wakati jina la Bitchuka katika baadhi ya nyimbo limeandikwa Bitchika.

Nyuma ya DVD hiyo zinaonekana picha ndogo za Hussein Jumbe, Bennovilla, Bitchuka na Ramadhani Kinguti 'System' wakiwa wamevaa sare za zamani za bendi hiyo.

Nyimbo zilizomo kwenye albamu ya Huruma kwa wagonjwa kwenye DVD hiyo ni Teddy Mwana Zanzibar, Furaha, Mkataa pema (Bitchuka), Binamu na Amina (Dede).

Albamu ya Supu umeitia nazi inaundwa na nyimbo za King Fish, Fitina, Full Squad na Ni nani (Bitchuka), Heshima, Njiwa Manga (Hemba) na Upendo (Ramadhani Mapesa).

Nyimbo zilizomo kwenye albamu ya Maneno Maneno ni Tende Haluwa, Fumanizi (Dede), Kelele za Paka (Bitchuka), Mshenga (Ally Jamwaka) na SACCOS uliotungwa kwa pamoja na wanamuziki wote wa bendi hiyo.

Nyimbo nyingi zilizomo kwenye albamu hiyo zilirekodiwa chini ya usimamizi wa Kampuni ya GMC Wasanii Promoters yenye makao makuu yake mjini Dar es Salaam.

Alipoulizwa kuhusu uhalali wa DVD hiyo, Katibu wa Mlimani Park Orchestra, Hamisi Milambo, alisema wamepata taarifa hizo na wameshaanza kuzifanyia kazi.

Milambo alisema walifika katika moja ya maduka yanayouza DVD hizo kwa jumla, lililoko mtaa wa Magila, Kariakoo, Dar es Salaam na kuzikuta zikiuzwa bila idhini ya uongozi.

"Tumeshangazwa sana na mmiliki wa duka hilo kwa sababu hatuna mkataba naye wowote. Tutakachokifanya ni kuwasilisha malalamiko yetu katika Chama cha Hakimiliki Tanzania (COSOTA) ili achukuliwe hatua za kisheria,"alisema Milambo bila kutaja jina la mmiliki huyo.

Aliongeza kuwa, kisheria bendi ya Mlimani Park ndiyo yenye hakimiliki ya kazi zake zote, hivyo hairuhusiwi kwa mtu mwingine kutumia kazi hizo bila idhini ya uongozi.

Hata hivyo, mmoja wa wanamuziki waandamizi wa bendi hiyo, ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, aliutupia lawama uongozi kwa kushindwa kusimamia kazi zao.

"Mimi moja kwa moja nautupia lawama uongozi kwa sababu kila tunapokamilisha kurekodi nyimbo mpya, huwa tunawaambia tutengeneze albamu, lakini hawafanyi hivyo. Matokeo yake wajanja wachache wanazikusanya na kutengeneza albamu kinyemela,"alisema.

Kwa mujibu wa mwanamuziki huyo, bendi hiyo imekuwa ikishindwa kuendesha vyema mambo yake kutokana na kukosekana kwa meneja wa bendi na uongozi uliopo madarakani hautaki kuajiri mtu mwenye sifa hiyo.

"Sikinde ni kama vile inaendeshwa bora liende. Tunaingia gharama kubwa kurekodi nyimbo zetu studio, lakini mwisho wa siku nyimbo zinaibwa na kuuzwa bila bendi kunufaika,"alisema.

Aliongeza kuwa, kwa mara ya mwisho waliingia mkataba wa kurekodi video zao kupitia Kampuni ya GMC wakati bendi ilipokuwa chini ya Shirika la Uchumi mkoa wa Dar es Salaam (DDC) na ndiyo iliyosimamia mauzo ya albamu yao ya mwisho, inayojulikana kwa jina la Maneno Maneno.

"Sasa kama zipo nyimbo kwenye DVD hiyo tulizorekodi na GMC, ni wazi kwamba nayo huenda imehusika, lakini sina hakika. Lakini kwa vyovyote vile, wapo baadhi yetu ndani ya bendi wamehusika,"alisisitiza.

Akizungumza kwa njia ya simu jana, mmoja wa wamiliki wa GMC, ambayo pia hujulikana kwa majina ya Mwananchi, Mamuu Store na Wasanii Promoters, alikana kuhusika kwao na kazi hiyo.

"Ni kweli tuliwahi kuwa na mkataba na DDC Mlimani Park miaka ya nyuma, lakini ulishamalizika hivyo hatuhusiki kwa lolote na kazi hiyo,"alisema mtu huyo, ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini.

ZAWADI KOMBE LA NSSF ZAONGEZWA, BINGWA WA SOKA KUPATA MIL 4.5/- WA NETIBOLI MIL NNE

 Meneja Kiongozi wa Idara ya Uhusiano na Huduma za Wateja wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Eunice Chiume (kushoto) akikabidhi jezi kwa mwakilishi wa Uhuru Media, Rashid Zahor, katika hafla iliyofanyika leo makao makuu ya shirika hilo mjini Dar es Salaam.
Meneja Kiongozi wa Idara ya Uhusiano na Huduma za Wateja wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Eunice Chiume (kushoto), akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa hafla ya kutangaza zawadi za washindi wa mashindano ya Kombe la NSSF mwaka huu. Katikati ni Mwenyekiti wa kamati ya mashindano hayo, Rashid Zahor na kulia ni katibu, Modest Msangi. (Picha zote na Emmanuel Ndege).

SHIRIKA la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), limeamua kuongeza zawadi kwa washindi wa mwaka huu wa michuano ya soka na netiboli ya vyombo vya habari nchini.

Meneja Kiongozi wa Idara ya Uhusiano na Hudma za Wateja wa NSSF, Eunice Chiume, amesema mjini Dar es Salaam leo kuwa, bingwa wa soka atapata sh. milioni 4.5 wakati bingwa wa netiboli atazawadiwa sh. milioni nne.

Eunice alisema mshindi wa pili wa soka atazawadiwa sh. milioni 3.5 wakati mshindi wa tatu atapata sh. milioni mbili. Alisema katika netiboli, mshindi wa pili atapata sh. milioni 2.5 na wa tatu sh. milioni 1.5.

Zawadi zingine zitakazotolewa ni sh. 350,000 kwa wachezaji bora wa mashindano hayo kwa mpira wa miguu na netiboli.

Kwa mujibu wa Eunice, wameamua kuongeza zawadi kwa washindi kwa lengo la kuongeza ushindani kwa timu shiriki na pia kuyafanya mashindano hayo yawe na msisimko zaidi.

Alisema NSSF imepanga kutumia sh. milioni 19 kwa ajili ya zawadi kwa washindi wa michuano hiyo, ambayo imepangwa kuanza keshokutwa kwenye viwanja vya TCC na DUCE vilivyoko Chang'ombe, Dar es Salaam.

Katika mechi za ufunguzi, New Habari itamenyana na Habari Zanzibar katika soka wakati katika netiboli, Jambo Leo itamenyana na Wizara ya Habari na kufuatiwa na mchezo kati ya Azam na TSN. Michezo hiyo itaanza saa 1.30 asubuhi.

Eunice alisema mashindano hayo, yatakayozishirikisha timu 20 za soka na 18 za netiboli, yataendeshwa kwa njia ya mtoano na yatafikia kilele Aprili 12 mwaka huu. Alisema mgeni rasmi katika sherehe za ufunguzi anatarajiwa kuwa Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudencia Kabaka.

Mashindano ya Kombe la NSSF yametimiza miaka 11 tangu yalipoanzishwa na mwaka huu yatakwenda sambamba na sherehe za miaka 50 ya shirika hilo na miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

"Michuano hii kwa mwaka huu, itafanyika katika sherehe hizo kubwa mbili na ndiyo yenye idadi kubwa ya timu kuliko miaka mingine tangu ilipoanzishwa 2004,"alisema Eunice.

Timu zitakazoshiriki katika mashindano ya mwaka huu ni IPP, Jambo Leo, BTL, New Habari, Mwananchi, Uhuru Media, Changamoto, Habari Zanzibar, Tumaini Media, Star TV na TBC.

Zingine ni TSN, Mlimani TV, Redio Maria, Wizara ya Habari, Global Publishers, Free Media, Raia Mwema na Azam TV.

Tuesday, March 25, 2014

DIAMOND, JAYDEE KUWANIA TUZO LUKUKI ZA MUZIKI ZA KILIMANJARO



Wimbo bora wa mwaka;
1 Number one-Diamond,
2 Joto hasira-Lady Jaydee Ft Prof Jay,
3 I love u-Cassim Mganga,
4 Yahaya-Lady JayDee,
5 Kidela -Abdu Kiba Feat Ali Kiba 
6 Muziki gani-Ney ft Diamond.


Wimbo bora wenye vionjo vya asili ya Kitanzania;
1 Kwejaga nyangisha-Batarokota,
2 Nalonji-Kumpeneka,
3 Bora Mchawi-Dar Bongo massive,
4 Tumbo lamsokota-Ashimba,
5 Aliponji –Wanakijiji 
6 Agwemwana-Cocodo African music band.

Wimbo bora wa kiswahili –Bendi;
1 Ushamba mzigo-Mashujaa Band,
2 Shamba la Bibi -Victoria Sound,
3 Chuki ya nini -FM Academia,
4 Yarabi nafsi -Mapacha Watatu
5 Kiapo mara 3 -Talent Band.

Wimbo bora wa Reggae;
1 Niwe na wewe-Dabo,
2 Hakuna Matata-Lonka,
3 Tell Me-Dj Aron ft Fidempha,
4 Bado nahitaji-Chikaka ft Bless p & Lazzy B
5 Bongo Reggae-Warriors from the east.

Wimbo bora wa Afrika Mashashariki;
1 Tubonge-Jose Chamelleone,
2 Nakupenda Pia-Waire Ft Allain,
3 Badilisha-Jose Chamelleone,
4 Kipepeo-Jaguar
5 Kiboko Changu-Aman FT Weizal and Radio.

Wimbo bora wa Afro pop;
1 Number one-Diamond,
2 Joto hasira-Jay Dee,
3 Kidela-abdul kiba ft Ali Kiba,
4 I love you-Kassim,
5 Tupogo-Ommy Dimpoz Ft J Martins
6 Roho yangu-Rich Mavoko.

Wimbo bora wa Taarab;
1 Wasi wasi wako-Mzee Yusuf,
2 Asiyekujua Hakuthamini-Isha Ramadhani & Saida Ramadhani,
3 Nipe stara -Rahma Machupa,
4 Sitaki shari-Leyla Rashid,
5 Fahari ya Mwanamke-Khadija Kopa,
6 Mambo bado-Khadija Yusuf
7 Kila muomba Mungu -Mwanahawa Ali.

Wimbo bora wa Hip hop;
1 Bei ya mkaa-Weusi,
2 Nje ya box-Nick wa pili ft Joh Makini na Gnako,
3 Siri ya mchezo-Fid q ft Nature,
4 2030-Roma
5 Pesa-Mr Blue Ft Becka Title.

Wimbo bora wa R&B;
1 Listen-Belle 9,
2 Closer -Vanessa Mdee,
3 So crazy-Maua ft Fa,
4 kama huwezi-rama dee ft jay dee
5 Wa ubani-Ben Pol ft. Alice

Wimbo bora wa kushirikisha/kushirikiana;
1 Music Gani-Ney Mitego ft Diamond,
2 Joto Hasira-Lady JayDee ft. Prof Jay,
3 Kidela -Abdul Kiba ft. Ali Kiba,
4 Bila Kukunja Goti-Mwana FA na AY ft. Jay Martins
5 Tupogo-Ommy Dimpoz ft. Jay Martins.

Wimbo bora wa Ragga/Dancehall;
1 Nishai-Chibwa Ft Juru,
2 Sex girl-Dr Jahson,
3 My sweet-Jettyman Dizano,
4 Feel Alright-Lucky Stone,
5 Wine-Princess Delyla.

Wimbo bora wa Zouk /Rhumba;
1 Yahaya-Lady Jaydee,
2 Yamoto-Mkubwa na wanawe,
3 Msaliti-Christian Bella,
4 Nakuhitaji-Malaika Band
5 Narudi kazini-Beka.

Mwimbaji bora wa kike -kizazi kipya;
1 Vanessa Mdee,
2 Lady Jaydee,
3 Linah na 4 Maua

Mwimbaji bora wa kiume -kizazi kipya
1 Ben Pol,
2 Rich Mavoko,
3 Diamond,
4 Ommy Dimpoz
5 Cassim Mganga.

Mwimbaji bora wa kike –Taarab;
1 Khadija Kopa,
2 Isha Ramadhani,
3 Khadija Yusuf,
4 Mwanahawa Ali
5 Leyla Rashid,

Mwimbaji bora wa kiume –Taarab wanashindana
1 Mzee Yusuf,
2 Hashimu Saidi
3 Mohamedi Ali aka Mtoto Pori.

Mwimbaji bora wa kiume –Bendi;
1 Jose Mara,
2 Kalala Junior,
3 Charz Baba,
4 Khalid Chokoraa
5 Christian Bella,

Mwimbaji bora wa kike -Bendi
1 Luiza Mbutu,
2 Catherine (Cindy) 
3 Ciana.

Msanii bora wa -Hip hop;
1 FID Q,
2 Stamina,
3 Young killer (Msodoki),
4 Nick wa pili,
5 Gnako.

Msanii bora chipukizi anayeibukia;
1 Young Killer(Msodoki),
2 Walter Chilambo,
3 Y Tony,
4 Snura
5 Meninah,

Rapa bora wa mwaka –Bendi kuna
1 Kitokololo,
2 Chokoraa,
3 Furguson,
4 Canal Top
5 Totoo ze Bingwa.

Mtumbuizaji bora wa kike wa Muziki.
1 Khadija Kopa,
2 Vanessa Mdee,
3 Isha Ramadhani,
4 Luiza Mbutu
5 Catherine (Cindy)

Mtumbuizaji bora wa kiume wa Muziki
1 Diamond,
2 Christian Bella,
3 Rich Mavoko,
4 Ommy Dimpoz
5 Abdu Kiba.

Mtayarishaji bora wa nyimbo wa mwaka –Taarab;
1 Enrico,
2 Ababuu Mwana ZNZ
3 Bakunde

Mtayarishaji bora wa nyimbo wa mwaka -Kizazi kipya
1 Marco chali-Mj Records,
2 Man Water-Combination Sound,
3 Mazoo-Mazoo Records,
4 Sheddy Clever-Burnz Records
5 Nahreel -Home Town Record.

Mtayarishaji bora wa nyimbo wa mwaka –Bendi;
1 Allan Mapigo,
2 C9,
3 Enrico,
4 Amoroso
5 Ababuu Mwana ZNZ,

Mtunzi bora wa mwaka –Taarabu,
1 Mzee Yusuf,
2 El-Ahad Omary,
3 El-khatib Rajab,
4 Kapten Temba,
5 Sadiki Abdul
6 Nassoro Seif,

Mtunzi bora wa mwaka -kizazi kipya,
1 Belle 9,
2 Ben Pol,
3 Diamond,
4 Rama dee
5 Rich mavoko.

Mtunzi bora wa mwaka –Bendi
1 Christia Bella,
2 Jose Mara,
3 Chaz Baba,
4 Nyoshi Saadat
5 Kalala Junior

Mtunzi bora wa mwaka -Hip hop,
1 Nikki wa Pili,
2 Young Killer(Msodoki),
3 Roma,
4 FID Q
5 G- Nako.

Video bora ya muziki ya mwaka;
1 Number One-Diamond,
2 Yahaya-lady Jaydee,
3 Joto hasira-Lady Jaydee Ft Prof Jay,
4 Uswazi takeaway-Chege Ft Malaika,
5 Mama Yeyo-Gnako Ft Ben Pol.

Bendi bora ya mwaka;
1 FM Academia,
2 Mapacha Watatu,
3 African Stars ‘Twanga Pepeta’,
4 Akudo Impact,
5 Malaika Band,
6 Mashujaa Band,

Kikundi cha mwaka cha Taarab ni
1 Jahaz Modern Taarab,
2 Mashauzi Classic
3 Five Stars

Kikundi cha mwaka cha kizazi kipya;
1 Makomandoo
2 Navy kenzo,
3 Weusi
4 Mkubwa na wanawe

(CHANZO: www.saluti5.com).

KORTI YAIAGIZA TFF IKAMATE MILIONI 106 ZA YANGA KUWALIPA MALASHI NA NDLOVU, YAKATWA MIL 9.2 MECHI YA RHINO


Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) tumepokea amri ya Mahakama Kuu (Kitengo cha Kazi) kukamata sh. milioni 106 za klabu ya Yanga kutokana na mapato ya mlangoni kwenye mechi zake ili kuwalipa waliokuwa wachezaji wake Stephen Malashi na Wisdom Ndlovu.


Tayari tumeanza utekelezaji wa amri hiyo ambapo katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) dhidi ya Rhino Rangers iliyochezwa Machi 22 mwaka huu mjini Tabora tumezuia sh. 9,221,250 ambazo ndizo zilizokuwa mgawo wa Yanga katika mchezo huo ulioingiza jumla ya sh. 38,655,000.

Wachezaji hao walifungua kesi kortini kupinga mikataba yao na klabu hiyo kuvunjwa bila kulipwa haki zao za kimkataba. Malashi na Ndlovu walishinda kesi hiyo, hivyo korti kuwapa tuzo hiyo ya sh. milioni 106.

Tunawakumbusha wanachama wetu (klabu za Ligi Kuu, vyama vya mpira wa miguu vya mikoa na vyama shiriki) kuzingatia mikataba wanayoingia na watendaji wao wakiwemo wachezaji, makocha na maofisa wengine.

Iwapo wanataka kuvunja mikataba ya ajira wafuate taratibu kwa vile hakuna mkataba ambao hauelezi jinsi ya kuvunjwa iwapo upande mmoja unataka kufanya hivyo.

KAZI IPO KESHO, YANGA NA PRISONS DAR, AZAM NA MGAMBO JKT TANGA



Timu za Azam na Yanga ambazo zinachuana kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara zinashuka tena viwanjani kesho (Machi 26 mwaka huu) kuwania pointi tatu.

Azam yenye pointi 47 itakuwa mgeni wa Mgambo Shooting katika mechi itakayochezwa Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga. Mgambo Shooting ipo katika nafasi ya kumi na moja kwenye msimamo wa VPL ikiwa na pointi 19.

Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Yanga na Tanzania Prisons kuanzia saa 10.30 jioni. Yanga ipo nyuma ya Azam kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 47. Hata hivyo, timu hiyo ina mchezo mmoja mkononi.

Tanzania Prisons ambayo ipo chini ya Kocha David Mwamaja hivi sasa ina pointi 22 ikiwa katika nafasi ya kumi. Timu tatu za mwisho katika ligi hiyo itakayomalizika Aprili 19 mwaka huu zitashuka kurudi Ligi Daraja la Kwanza (FDL).

Ligi itaendelea tena Jumamosi (Machi 29 mwaka huu) kwa mechi kati ya Ashanti United na Oljoro JKT itakayofanyika Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam.

Jumapili (Machi 30 mwaka huu) kutakuwa na mechi kati ya Mbeya City na Tanzania Prisons (Uwanja wa Sokoine), Kagera Sugar na Ruvu Shooting (Uwanja wa Kaitaba), Mtibwa Sugar na Coastal Union (Uwanja wa Manungu), JKT Ruvu na Rhino Rangers (Uwanja wa Azam Complex), Azam na Simba (Uwanja wa Taifa) na Mgambo Shooting na Yanga (Uwanja wa Mkwakwani).

KAMATI YA SHERIA KUPITIA MAREKEBISHO YA KATIBA
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) inatarajia kukutana mwishoni mwa wiki kupitia taarifa ya utekelezaji wa agizo la wanachama kurekebisha katiba zao.

TFF tulitoa agizo kwa wanachama wetu kufanyia marekebisho katiba ikiwemo kuingiza Kamati ya Maadili. Mwisho wa utekelezaji wa agizo hilo ulikuwa Machi 20 mwaka huu.

Hivyo, Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji itapokea taarifa ya utekelezaji wa agizo hilo kutoka kwa Sekretarieti, na baadaye kutoa mwongozo wa hatua inayofuata.

TIMU YA WATOTO WA MITAANI YAENDA BRAZIL


Timu ya Watoto wa Mitaani ya Tanzania kutoka Kituo cha Mwanza imeondoka leo (Machi 26 mwaka huu) kwenda Brazil kushiriki mashindano ya Kombe la Dunia kwa Watoto wa Mitaani.

John Kadutu ambaye ni mjumbe wa Bodi ya kituo hicho, na pia mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) akiwakilisha klabu za Mkoa wa Mwanza ndiye kiongozi wa msafara wa timu hiyo ya Tanzania.

Michuano hiyo ya siku 10 inayoshirikisha watoto wa mitaa (wavulana na wasichana) inaanza keshokutwa (Machi 28 mwaka huu). Nchi 19 zinashiriki michuano hiyo itakayofanyika katika Jiji la Rio de Janeiro.

Mbali ya Tanzania, nchi nyingine zinazoshiriki michuano hiyo kwa upande wa wavulana ni Argentina, Burundi, India, Kenya, Liberia, Marekani, Mauritius, Misri na Pakistan. Kwa wasichana ni Afrika Kusini, Brazil, El Salvador, Indonesia, Msumbiji, Nicaragua, Philippines, Uingereza na Zimbabwe.

Mwaka 2010 mashindano hayo yalifanyika Durban, Afrika Kusini ambapo pia Tanzania ilishiriki.

MABINGWA WA MIKOA MWISHO MACHI 30



Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linavikumbusha vyama vya mpira wa miguu vya mikoa kuwa vinatakiwa kuwasilisha majina ya mabingwa wao kufikia Machi 30 mwaka huu.

Majina ya mabingwa yanatakiwa kuwasilishwa pamoja na usajili wa wachezaji waliotumika kwenye ligi ya mkoa. Kila klabu inaruhusiwa kuongeza wachezaji watano kutoka ndani ya mkoa husika, ambapo unatakiwa uthibitisho wa usajili huo.

Mpaka sasa ni vyama viwili tu ndivyo vimeshawasilisha mabingwa wao. Vyama hivyo ni Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) ambapo bingwa wake ni Kiluvya United, na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Lindi (LIREFA) ambapo bingwa ni Kariakoo SC.

Monday, March 24, 2014

SIMBA PWAAA, YAPIGWA 1-0 NA COASTAL UNION, AZAM YAZIDI KUPAA





TIMU kongwe ya soka nchini, Simba jana ilipigwa mweleka wa bao 1-0 na Coastal Union katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kipigo hicho kimepoteza matumaini ya Simba kushika nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo baada ya kutokuwa na uwezo wa kushika nafasi mbili za kwanza.

Bao pekee na la ushindi la Coastal Union lilifungwa na mshambuliaji Hamad Juma dakika ya 44, kufuatia shambulizi kali lililofanywa kwenye lango la Simba.

Simba ilizinduka katika kipindi cha pili na kufanya mashambulizi kadhaa kwenye lango la Coastal Union, lakini juhudi za washambuliaji wake kusaka bao la kusawazisha hazikufanikiwa.

Kiungo Jonas Mkude ndiye aliyefanya majaribio mengi kwenye lango la Coastal Union kwa kupiga mashuti makali matano, lakini moja liligonga mwamba wa pembeni wa goli na mengine yalitoka nje.

Katika mechi zingine za ligi hiyo zilizochezwa juzi, Azam iliichapa JKT Oljoro bao 1-0 kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam wakati Ashanti ilipigwa mweleka wa mabao 2-0 na JKT Ruvu mkoani Pwani.

Sunday, March 23, 2014

YANGA YAIPUMULIA AZAM, LEO NI SIMBA NA COASTAL UNION



MABINGWA watetezi wa ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara, Yanga jana waliibuka na ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Rhino Rangers katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.


Ushindi huo umeiwezesha Yanga kuwa na pointi 43 baada ya kucheza mechi 20, ikiwa nyuma ya vinara, Azam kwa tofauti ya pointi moja. Azam inatarajiwa kushuka tena dimbani leo kuvaana na JKT Oljoro.

Mashujaa wa Yanga katika mechi hiyo walikuwa Jerry Tegete, aliyefunga bao la kwanza dakika ya 26, Simon Msuva, aliyefunga la pili dakika ya 67 ma Hussein Javu, aliyefunga dakika ya 90.

Wakati huo huo, Simba leo itakuwa na kibarua kigumu itakapomenyana na Coastal Union kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Friday, March 21, 2014

RWIZA, LIUNDI KUSIMAMIA MECHI ZA CAF

Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limewateua Watanzania Alfred Rwiza na Leslie Liunda kusimamia mechi zake za wikiendi hii na mwezi ujao.

Liunda ameteuliwa kuwa Kamishna wa mechi ya Kombe la Shirikisho (CC) kati ya How Mine ya Zimbabwe na Bayelsa United ya Nigeria itakayochezwa Jumamosi (Machi 22 mwaka huu) jijini Bulawayo.

Waamuzi wa mechi hiyo wanatoka Eritrea, na wanaongozwa na Maeruf Kherseed. Wasaidizi wake ni Angeson Ogbamariam, Berhe O’Michael na Luelseghed Ghebremichael.

Naye Rwiza atasimamia mechi ya michuano ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 kati ya Lesotho na Swaziland itakayochezwa kati ya Aprili 25-27 mwaka huu jijini Maseru.

Mechi hiyo ya marudiano itachezwa na waamuzi Duncan Lengani, Innocent Kaundula, Hendrix Maseko na Jones Makhuwira, wote kutoka nchini Malawi.

Wakati huo huo, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha mshabiki Deodatus Mwakyangula kilichotokea jana (Machi 19 mwaka huu) wakati ya mechi kati ya Yanga na Azam iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Msiba huo ni mkubwa kwa familia ya Mwakyangula na kwetu, kwani umetokea wakati akiwa uwanjani kushuhudia mechi hiyo ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1.

TFF tunatoa pole kwa familia ya marehemu Mwakyangula, na klabu ya Yanga na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.

Bwana alitoa, Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe. Amina

SIMBA, YANGA ZATOZWA FAINI SH. MIL 25



Klabu za Yanga na Simba zimeagizwa kulipa jumla ya sh. milioni 25 kutokana na uharibifu wa viti na vurugu zilizofanywa na washabiki wao kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Yanga na Al Ahly ya Misri iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Yanga italipa sh. milioni 15 ambayo ni gharama ya uharibifu wa viti uliofanywa na washabiki kwenye mechi hiyo. Pia imepigwa faini ya sh. milioni tano kutokana na vurugu za washabiki wake. Nayo Simba imepigwa faini ya sh. milioni tano kutokana na washabiki wake kuhusika katika vurugu hizo.

Uamuzi huo umefanywa na Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) katika kikao chake cha dharura kilichofanyika jana (Machi 19 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.

Tunatoa onyo kwa washabiki wa mpira wa miguu kujiepusha na vurugu viwanjani ikiwemo uharibifu wa miundombinu mbalimbali ya viwanja ikiwepo viti, na tutachukua hatua kali zaidi kwa klabu na washabiki wake iwapo vitendo hivyo vitajitokeza tena.

MADADI MKURUGENZI MPYA WA UFUNDI TFF


Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limemteua Salum Madadi kuwa Mkurugenzi wake mpya wa Ufundi.

Uteuzi huo umefanya na Kamati ya Utendaji katika kikao chake cha dharura kilichofanyika jana (Machi 19 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.

Kabla ya uteuzi, Madadi alikuwa akikaimu nafasi hiyo tangu Januari mwaka huu baada ya Mkurugenzi wa Ufundi aliyekuwepo kumaliza mkataba wake Desemba 31 mwaka jana.

Madadi mwenye leseni A ya ukocha ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) ni kocha mwenye uzoezi wa zaidi ya miaka 30 ambapo alianza kufundisha mpira wa miguu mwaka 1980 katika klabu ya Maji SC ya Lindi.

Ana elimu ya sekondari aliyoipata katika shule ya Chidya na diploma ya ukocha wa mpira wa miguu aliyoipata nchini Ujerumani. Pia ni Mkufunzi wa makocha wa CAF, na alijiunga na TFF mwaka 2006 akiwa Ofisa Maendeleo.

Alikuwa Kocha wa Taifa Stars mwaka 2000. Mbali ya Maji SC, amewahi kufundisha timu za Nyota Nyekundu, Ushirika ya Moshi, Simba, Shangani ya Zanzibar, Malindi ya Zanzibar, Cardif ya Mtwara na Kariakoo ya Lindi.

Pia amewahi kuwa mjumbe wa Kamati ya Ufundi ya Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).

Thursday, March 20, 2014

MZIMU WA PENALTI WAITESA YANGA




MABINGWA watetezi wa ligi kuu ya soka yaTanzania Bara, Yanga jana walizidi kupunguzwa kasi ya kuwania ubingwa huo msimu huu baada ya kulazimishwa kutoka sare ya bao 1-1 na Azam.

Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 14 lililofungwa na Didier Kavumbagu kabla ya Kelvin Friday kuisawazishia Azam dakika ya 84.

Kutokana na matokeo hayo, Azam inaendelea kuongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 44 baada ya kucheza mechi 20, ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 40 baada ya kucheza mechi 19.

Sare hiyo ilikuwa ya pili mfululizo kwa Yanga tangu ilipotolewa na Al Ahly ya Misri katika michuano ya klabu bingwa Afrika. Wiki iliyopita, mabingwa hao watetezi walilazimishwa kutoka suluhu na Mtibwa Sugar mjini Morogoro.

Kavumbagu aliifungia Yanga bao la kuongoza baada ya kumalizia mpira uliotemwa na kipa wa Azam, Aishi Manula, kufuatia krosi iliyopigwa na Simon Msuva kutoka pembeni ya uwanja.

Friday aliisawazishia Azam kwa shuti kali baada ya mabeki wa Yanga kuzembea kuondosha mpira kwenye lango lao. Jitihada za kipa Juma Kaseja kuokoa shuti hilo hazikuzaa matunda.

Yanga ililianza pambano hilo kwa kasi na kupata nafasi nzuri ya kuongeza bao dakika ya 15 wakati Simon Msuva alipopewa pasi akiwa ndani ya 18, lakini shuti lake lilitoka nje.

Mshambuliaji Kipre Tchetche wa Azam alikuwa mwiba mkali kwa mabeki wa Yanga kutokana na kuisumbua ngome yao mara kwa mara. Mshambuliaji huyo kutoka Ivory Coast nusura afunge bao dakika ya 22, lakini shuti lake liligonga mwamba na mpira kurudi uwanjani.

Kavumbagu nusura afunge bao lingine dakika ya 25 baada ya kusogezewa mpira nje kidogo ya eneo la hatari, lakini shuti lake lilidakwa kwa ustadi mkubwa na kipa Aishi Manula wa Azam.

Yanga ilifanya shambulizi lingine la nguvu dakika ya 30 wakati Emmanuel Okwi, alipoitoka ngome ya Azam na kupiga mkwaju mkali akiwa nje ya eneo la hatari, lakini mpira ulipanguliwa na kipa Manula. Timu hizo zilikwenda mapumziko Yanga ikiwa mbele kwa bao 1-0.

KIPINDI CHA PILI
Azam iliongeza kasi ya mchezo kipindi cha pili na nusura ipate bao dakika ya 50 wakati Kelvin Friday alipomalizia kazi nzuri iliyofanywa na Tchetche, lakini shuti lake lilitoka pembeni ya lango.

Yanga ilipata adhabu ya penalti dakika ya 69 iliyolewa na mwamuzi Hashim Abdalla baada ya beki mmoja wa Azam kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari, lakini shuti la Kiiza lilitoka nje.

Azam ilipata pigo dakika ya 73 baada ya mwamuzi Hashim kumtoa nje kwa kadi nyekundu beki Erasto Nyoni kwa kosa la kumtolea lucha chafu. Awali, Nyoni alilimwa kadi ya njano

REKODI
Mechi hiyo ilikuwa ya 12 kwa Yanga kukutana na Azam kwenye michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara. Katika mechi hizo, Yanga imeshinda mitano wakati Azam imeshinda minne huku mechi mbili wakitoka sare.

Nje ya ligi kuu, timu hizo zimekutana mara tano, Yanga imeshinda mara mbili (Ngao ya Hisani na Kombe la Kagame) wakati Azam imeshinda mara tatu (Kombe la Mapinduzi na mechi za kirafiki).

John Bocco ndiye mchezaji aliyefunga magoli mengi zaidi katika mechi kati ya Yanga na Azam wakati Nadir Haroub 'Canavaro' anashikilia rekodi ya kucheza mechi nyingi.

Yanga SC: Juma Kaseja, Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Frank Domayo, Simon Msuva, Hassan Dilunga, Didier Kavumbangu/Mrisho Ngasa, Hamisi Kiiza/Hussein Javu na Emmanuel Okwi.

Azam: Aishi Manula, Erasto Nyoni, Gabriel Michael, Saidi Mourad, David Mwantika, Kipre Balou, Himid Mao, Salum Abubakari, John Bocco, Kipre Tchetche na Khamisi Mcha/ Kelvin Friday.

YANGA KUONGEZEWA ENEO JANGWANI

Jopo la Madiwani wa Manispaa ya Ilala, Maofisa wa Mipango Miji na Mazingira katika Manispaa hiyo pamoja viongozi wa klabu ya Yanga, wakikagua maeneo mbalimbali yanayozunguka makao makuu ya klabu hiyo yaliyoko mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam ili kukagua eneo ambalo Yanga inataka kuongezewa kwa ajili ya ujenzi wa jengo la biashara na uwanja jana. (Picha na Jumanne Gude).

SERIKALI imesema ipo kwenye hatua za mwisho katika mchakato wa kuipatia klabu ya Yanga kibali cha nyongeza katika eneo la Jangwani kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa kisasa wa soka.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango Miji na Mazingira katika Manispaa ya Ilala, Sultan Salim, alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, wamelipa kipaumbele kikubwa ombi hilo la Yanga na kusisitiza kuwa, mambo yatakuwa mazuri.

Sultan alisema hayo baada ya jopo la madiwani na wajumbe wa kamati yake, kutembelea makao makuu ya klabu hiyo mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam na kukagua eneo, ambalo klabu hiyo inataka iongezwe kwa ajili ya ujenzi huo.

"Yanga wamekuwa wa kwanza kupewa kipaumbele kikubwa kuliko wote. Tulipokea maombi mengi, lakini hili la Yanga limepewa umuhimu mkubwa na mara baada ya ziara hii leo, tutakutana ili kutoa uamuzi kuhusu ombi lao,"alisema Sultan.

Alisema watalitolea uamuzi ombi hilo baada ya kutembelea eneo, ambalo Yanga wanalihitaji kwa ajili ya kupanua ujenzi wa uwanja wa kisasa pamoja na majengo mengine ya kibiashara.

Sultan alisema baada ya kamati yake kujadili ombi hilo, itatuma wataalamu wake kwenye eneo hilo kwa ajili ya ukaguzi wa mwisho kabla ya kutoa kibali cha kuiruhusu Yanga kuanza ujenzi huo.

Mjumbe wa Bodi ya Udhamini ya Yanga, Francis Kifukwe, alisema wanaishukuru Manispaa ya Ilala kwa kutuma ujumbe huo kwenda kukagua eneo wanalolihitaji kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wao.

"Sasa hivi tunavuta tu subira kwa sababu tunaamini mambo yatakuwa mazuri kwani kila kitu kuhusiana na ujenzi huo kimeshapangwa na tayari tunazo pesa za kuanzia ujenzi huo,"alisema Kifukwe.

Alisema endapo serikali itawapa kibali cha kuanza ujenzi huo, wanatarajia kuanza kazi hiyo ndani ya miezi sita.

Yanga inahitaji nyongeza ya eneo la hekta 11 kwa ajili ya ujenzi wa uwanja huo wa kisasa ambapo kwa sasa eneo linalomilikiwa na klabu hiyo ni hekta 3.5.

Januari mwaka jana, uongozi wa Yanga uliitangaza Kampuni ya Beinjing Cosntruction Engineering Group (BCEG) ya China, iliyojenga Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kuwa ingeanza ujenzi wa uwanja huo Mei mwaka jana.

Hata hivyo, ujenzi huo ulichelewa kuanza kutokana na Yanga kuhitaji eneo la ziada la hekta 11.5.

Uwanja huo, ambao utapewa jina la Jangwani City, utakuwa na uwezo wa kuchukua watazamaji 40,000 waliokaa kwenye viti, huku ukiwa na sehemu za maegesho ya magari, watu maarufu (VIP), hospitali, hoteli na hosteli.

D'BANJ: BABA HAKUTAKA NIWE MWANAMUZIKI




LAGOS, Nigeria
LICHA ya kupata mafanikio makubwa kimuziki, mwanamuziki nyota wa Nigeria, D'banj amefichua kuwa baba yake hafurahishwi na kazi yake hiyo.

"Baba yangu aliniasa tangu nikiwa mdogo kwamba nisijihusishe na mambo ya muziki,"alisema D'banj alipohojiwa na mtandao mmoja wa Nigeria.

"Hata hivi sasa, amekuwa akinieleza: 'Una hakika fani ya muziki ni sahihi kwako?'"Alisema mwanamuziki huyo.

D'banj amepata mafanikio makubwa kimuziki tangu alipoibuka na kibao cha Oliver Twist na ameuza nakala zaidi ya milioni 11 za albamu zake.

Alipoulizwa ni kazi ipi, ambayo baba yake angependa kumuona akiifanya, alisema: "Kazi nyingine yoyote mbali na muziki."

Kwa mujibu wa D'banj, baba yake amekuwa na wasiwasi kuwa, umaarufu alionao kutokana na muziki, huenda ukayaharibu maisha yake.

"Ana wasiwasi iwapo nitaendelea kupata mafanikio haya kwa muda mrefu,"alisema mwanamuziki huyo, ambaye amewahi kuhusishwa kimapenzi na wasanii mbalimbali maarufu wa Kinigeria.

"Amekuwa akiniambia: 'Nilipokuwa na umri kama wako, tayari nilishaoa na kukupata wewe. Ni lini utaweka mambo sawa na kufunga ndoa?'" Alisema D'banj.

Mwanamuziki huyo alisema moja ya malengo yake ni kushinda tuzo ya muziki ya Grammy kwanza, lakini iwapo malaika atampitia karibu, anaweza kubadili mpango wake huo.

MWANANGU ANANIFANYA NIONE FAHARI-CLARION




LAGOS, Nigeria
MCHEZA filamu mkongwe wa Nigeria, Clarion Chukwura, amesema anaona fahari kuwa mama wa muongozaji wa video za muziki nchini humo, Clarence Peter.

Clarion, amesema anaona fahari kwa kijana wake huyo kutokana na kuwa miongoni mwa watu waliochangia kuufanya muziki wa Nigeria upate sifa na umaarufu kimataifa.

Peter amechangia kuipaisha fani ya muziki wa Nigeria kutoka na ubunifu wake katika kutengeneza video zenye mvuto.

Kwa sasa, Peter anaheshimika kama mtayarishaji na muongozaji bora wa video za muziki kupitia lebo yake ya Capital Hill Records.

"Naona fahari kumzungumzia Peter popote ninapokwenda,"alisema Clarion, ambaye amecheza filamu zaidi ya 100 za Kinigeria na kujipatia umaarufu mkubwa.

Peter, hawafanyi wazazi wake pekee waone fahari ju yake, bali pia taifa zima la Nigeria. Ametayarisha na kuongoza video za muziki za wasanii mbalimbali wapya na wakongwe.

'WALIDHANI WANANOIIMALIZA, KUMBE WANANIPA UMAARUFU'


LAGOS, Nigeria
BAADA ya kukaa kimya kwa muda mrefu, mcheza filamu machachari wa Nigeria, Biola Ige, ameamua kufunguka na kuzungumzia picha zake zilizosambazwa kwenye mitandao.

Picha hizo zilizozua gumzo kubwa miongoni mwa mashabiki wa filamu wa Nollywood, zinamwonyesha Biola akiwa amekumbatiana na Muna Obiekwe huku mwanaume huyo akiwa ameweka mikono yake kwenye matiti ya binti huyo.

Katika taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari wiki hii, Biola ameamua kuweka mambo hadharani kwa kusema, picha hiyo alipigwa wakati wa kutayarisha filamu ya Pregnant Hawkers.

Biola amemponda mtu aliyeisambaza picha hiyo kwenye mitandao kwa malengo tofauti na kusema, alichokifanya ni kumtangaza na kumpa umaarufu.

"Picha inayozungumzwa na kuzua maswali, ilipigwa katika eneo tulilokuwa tukipiga picha za filamu ya Pregnant Hawkers, ambayo nilicheza kama mwanamke aliyekuwa katika hali ya mapenzi na mwanaume,"amesema Biola.

"Picha za filamu hii zilipigwa miaka miwili iliyopita. Picha iliyosambazwa kwenye mitandao kwa sasa ni picha iliyopigwa kwenye eneo tulilotumia kupiga picha za filamu hiyo, hakuna kingine,"aliongeza msanii huyo.

"Iwapo utatazama filamu hiyo, utaona kwamba hakuna kingine kilichojitokeza katika filamu hiyo zaidi ya ukweli kwamba, nilikuwa nikicheza nafasi niliyopangiwa,"alisema binti huyo katika taarifa yake hiyo.

"Nimepitia matatizo mengi mwaka huu, ikiwa ni pamoja na kumpoteza mama yake na kuugua kwa muda mfupi. Picha hiyo kutoka kwenye filamu niliyocheza miaka miwili iliyopita, haiwezi kunipa wasiwasi wowote,"alisisitiza binti huyo.

Biola amesema ataendelea kucheza filamu nyingi zaidi katika nafasi mbalimbali kwa lengo la kuwaburudisha mashabiki wake.

NEW HABARI, HABARI Z'BAR KUKATA UTEPE KOMBE LA NSSF


TIMU za soka za New Habari na Habari Zanzibar, zimepangwa kufungua dimba la michuano ya Kombe la Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) mwaka huu.

Ratiba ya michuano hiyo inaonyesha kuwa, mechi hiyo itachezwa Machi 29 mwaka huu kwenye uwanja wa klabu ya Sigara, Chang'ombe, Dar es Salaam.

Awali, mashindano hayo yanayozishirikisha timu za vyombo mbalimbali vya habari nchini, yalipangwa kuanza keshokutwa kwenye uwanja huo, lakini yamesogezwa mbele kwa wiki moja.

Mwenyekiti wa kamati ya mashindano hayo, Rashid Zahor, alisema mjini Dar es Salaam juzi kuwa, wameamua kuyazogeza mbele kutokana na maombi ya waandaaji, NSSF.

"Waandaaji wametuomba tuyasogeze mbele mashindano kwa wiki moja kwa sababu bado wanaendelea kukamilisha taratibu muhimu ikiwa ni pamoja na kununua vifaa vya michezo kwa timu zote 20,"alisema.

Kwa mujibu wa Zahor, mashindano ya mwaka huu yatazishirikisha timu 20 za soka na 18 za netiboli na kuongeza kuwa, kamati imeshapitisha usajili wa timu zote.

Alisema kikao cha kupitia usajili na kupanga ratiba ya mashindano hayo kilifanyika juzi kwenye ofisi za makao makuu ya NSSF zilizoko jengo la Benjamin Mkapa Towers, Dar es Salaam.

Zahor alisema ratiba kamili ya michuano hiyo inatarajiwa kutolewa kwa timu zote shiriki kabla ya keshokutwa.

Timu zingine zinazotarajiwa kushiriki kwenye mashindano hayo ni mabingwa watetezi Jambo Leo, Changamoto, TBC, IPP, Mwananchi, Tumaini Media, Uhuru SC, Business Times, Sahara Media, TSN na Mlimani TV.

Zingine ni Global Publishers, Free Media, Azam TV, Raia Mwema, Wizara ya Habari, Redio Maria na wenyeji NSSF.

AKI SASA AITWA BABA, AZUA GUMZO KWA KUVAA KIKE






LAGOS, Nigeria
MCHEZA filamu nyota wa Nigeria, Chinedu Ikedieze 'Aki', hivi karibuni aliamua kuweka hadharani picha za binti yake kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii.

Picha hizo zinamwonyesha Aki akiwa amempakata binti yake huyo mwenye umri wa miezi kadhaa, ikiwa ni miaka miwili baada ya kufunga ndoa na Nneoma.

Aki ameamua kuweka picha hizo hadharani kwa lengo la kuwafahamisha mashabiki wake kwamba, tayari anaitwa baba.

Mashabiki wengi wa filamu za Kinigeria walioziona picha hizo, wamempongeza Aki kwa uamuzi wake wa kuoa na hatimaye kuitwa baba.

Hivi karibuni, Aki na msanii mwenzake nyota wa fani hiyo, Osita Iheme 'Ukwa' walitawala vyombo vya habari baada ya kuibuka na filamu mpya inayokwenda kwa jina la The Return of Aki na PawPaw Sisters'.

Katika filamu hiyo, Aki na Ukwa wameigiza kama mabinti mapacha wanaoishi kijijini na kumpa usumbufu mkubwa baba yao kama ilivyokuwa katika filamu ya Aki na Ukwa.

Hata hivyo, filamu hiyo imezua gumzo mkubwa, huku baadhi ya mashabiki wakiipinga na wengine kuiunga mkono.

Baadhi ya mashabiki wanaoipinga wamesema, haikuwa sahihi kwa wacheza filamu hao kuigiza kama mabinti kwa kuvaa nguo za kike wakati wao ni vijana wa kiume.

Mtayarishaji wa filamu hiyo, Martin Onyemaobi na muongozaji wake, Amayo Uzo Philips, waliamua kubuni kisa kingine kinachofanana na kile cha kwenye filamu ya Aki na Ukwa, lakini kwa kuwatumia waigizaji wa kike.

Ukwa, alizaliwa Desemba 12, 1977 katika mji wa Bende ulioko kwenye Jimbo la Abia nchini Nigeria. Amejipatia umaarufu mkubwa kutokana na kucheza filamu nyingi akishirikiana na Ukwa.

Mcheza filamu huyo mwenye shahada ya mawasiliano ya umma, ameshinda tuzo nyingi, zikiwemo za mwigizaji bora wa Afrika.

Alianza kupata umaarufu kwa kucheza filamu ya Evil Men kabla ya kuibuka tena kwenye filamu ya The Last Burial. Baada ya hapo, alicheza filamu nyingi kwa kushirikiana na Ukwa, ambaye kwa sasa ndiye swahiba wake mkubwa.

Tuesday, March 18, 2014

YANGA, AZAM KIAMA TAIFA KESHO


Michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inaendelea kesho (Machi 19 mwaka huu) kwa mechi kati ya Yanga na Azam itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10.30 jioni.

Tiketi kwa ajili ya mechi hiyo zitaanza kuuzwa saa 2 asubuhi katika magari maalumu kwenye vituo vya Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Ubungo Terminal, mgahawa wa Steers uliopo Mtaa wa Samora/Ohio, OilCom Ubungo, Buguruni Shell, Dar Live- Mbagala, kituo cha daladala Mwenge na Uwanja wa Taifa.

Baada ya saa 6 mchana mauzo yote yatahamia Uwanja wa Taifa ambapo milango kwa ajili ya mechi itakuwa wazi kuanzia saa 7.30 mchana.

Viingilio katika mechi hiyo vitakuwa sh. 30,000 kwa VIP A, sh. 20,000 kwa VIP B na C wakati viti vya rangi ya chungwa, bluu na kijani kiingilio ni sh. 7,000.

Mechi hiyo itachezeshwa na mwamuzi Hashim Abdallah wa Dar es Salaam ambapo atasaidiwa na Anold Bugado (Singida), Florentina Zablon (Dodoma) na Lulu Mushi (Dar es Salaam). Kamishna wa mechi hiyo Emmanuel Kavenga kutoka Mbeya wakati mtathimini wa waamuzi ni Alfred Rwiza wa Mwanza.

31 KUUNDA NGORONGORO HEROES


Wachezaji 31 wameteuliwa kujiunga na timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes) kwa ajili ya michuano ya Afrika ambayo fainali zake zitafanyika mwakani nchini Senegal.

Ngorongoro Heroes itakayokuwa chini ya Kaimu Kocha John Simkoko akisaidiwa na Mohamed Ayoub inaingia kambini kesho (Machi 19 mwaka huu) jijini Dar es Salaam kujiandaa kwa mechi ya kwanza dhidi ya Kenya itakayochezwa kati ya Aprili 4-6 jijini Nairobi.

Kikosi kinachounda timu hiyo ambayo itarudiana na Kenya kati ya Aprili 25-27 mwaka huu jijini Dar es Salaam kinajumuisha pia baadhi ya wachezaji walioonekana katika mpango wa ung’amuzi wa vipaji kwa ajili ya maboresho ya Taifa Stars.

Wachezaji walioitwa ni makipa Aishi Manula (Azam), Hamad Juma Hamad (Scouting- Temeke), Manyika Peter Manyika (Scouting- Ilala) na Mwinyi Hassan Hamisi (Mtende, Zanzibar).

Mabeki wa pembeni ni Ayoub Semtawa (Coastal Union), Edward Charles (JKT Ruvu), Frank Linus Makungu (Scouting- Rukwa), Gabriel Gadiel Michael (Azam), Hussein Mkongo (Ashanti United) na Ibrahim Said Mohamed (Chuoni, Zanzibar). Mabeki wa kati ni Bashiru Ismail (Tanzania Prisons), Faki Rashid Hakika (Ashanti United) na Pato Ngonyani (Majimaji).

Viungo ni Ally Nassoro (Coastal Union), Bryson Raphael (Azam), Farid Musa (Azam), Hamid Mohamed (Mbeya City), Hassan Mbande (Mtibwa Sugar), Ibrahim Mohamed Ibrahim (Scouting- Ilala), Idd Seleman (Ashanti United), Mohamed Issa Juma (Acudu, Afrika Kusini), Muhsin Ally Muhsin (Scouting- Kinondoni), Seleman Magoma (Scouting- Ruvuma) na Tumaini John (Scouting- Mwanza).

Washambuliaji ni Ally Salum Kabunda (Ashanti United), Ibrahim Hamad Hilika (Zimamoto, Zanzibar), Jafari Mwambusi (Mbeya City), Kelvin Friday (Azam), Ramadhan Bilal (Mlale JKT), Salum Abdilah Mineli (Ndanda) na Sibiank Lambard (Tanzania Prisons).

VIPAJI 36 VYA KUBORESHA TAIFA STARS VYATAJWA



Jopo wa wang’amuzi vipaji limetangaza majina ya wachezaji 36 waliopataikana katika mchakato wa maboresho ya Taifa Stars ulioshirikisha mechi za mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Kaimu Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Salum Madadi amesema jopo hilo liling’amua vipaji 143 katika mchakato, lakini waliochukuliwa kwa sasa ni hao 36 tu.

Amewataja wachezaji waliochaguliwa katika mchakato huo kwa upande wa makipa ni Abdulaziz Khatib Haji (Mjini Magharibi), Abubakar Abbas Ibrahim (Tanga), Benedicto Tinoko Mlekwa (Mara) na Mtindi Kheri Ali (Kaskazini Unguja).

Kwa upande wa mabeki wa pembeni waliochaguliwa katika mchakato huo ambao upo chini ya udhamini wa Kilimanjaro Premium Lager ni Edward Peter Mayunga (Kaskazini Pemba), Hussein Moshi (Tabora), Omari Kindamba (Temeke) na Shiraz Abdallah (Ilala).

Mabeki wa kati ni Abbas Ali Haji (Kaskazini Unguja), Ancy Abdon (Kagera), Emma Namwamba (Temeke), Hussein Juma Akilimali (Njombe), Joram Nasson (Iringa), Kayombo Silvanus Henrico (Ilala), Miraji Maka (Mwanza), Ramadhan Ame Ramadhan (Kusini Unguja) na Said Juma Ali (Mjini Magharibi).

Viungo wapo Abubakar Mohamed Ally (Kusini Unguja), Hashim Ramadhan Magoma (Shinyanga), Juma Said Jega (Lindi), Mtenje Alban Juma (Tanga), Ryna Mgonyike (Temeke) na Yusuf Mpilipili (Temeke).

Washambuliaji ni Abdallah Kagumbwa (Temeke), Abrahman Othman Ally (Mjini Magharibi), Athanas Fabian Bayagala (Mbeya), Athanas Mdamu (Mwanza), Ayubu Hashim Lipati (Ilala), Chunga Said (Manyara), Mbwana Mshindo Mussa (Tanga), Michael David Mlekwa (Lindi), Mohamed Seif Said (Kusini Pemba), Omar Athuman Nyenje (Mtwara), Paul Michael Bundala (Ilala), Ramadhan Kapalamoto (Kinondoni) na Roman Nyapunda (Temeke).

Amesema wastani wa umri wa wachezaji hao ambao watafanyiwa vipimo vya afya Machi 19 na 20 mwaka huu kabla ya kambini Machi 21 mwaka huu, Tukuyu mkoani Mbeya ni miaka 21.

Timu hiyo itakuwa chini ya Madadi akisaidiwa na makocha Hafidh Badru, Salum Mayanga na Patrick Mwangata. Aprili 13 mwaka huu utafanyika mchujo ili kupata wachezaji wa mwisho watakaoungana na wale wa Taifa Stars watakaoingia kambini Aprili 22 mwaka huu.

Taifa Stars inatarajiwa kucheza mechi ya kirafiki mapema mwezi Mei mwaka huu ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mechi za mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika (AFCON) zitakazofanyika mwakani nchini Morocco.

Monday, March 17, 2014

MDOMO NUSURA UMPONZE RAGE, AWAITA WANACHAMA MBUMBUMBU



 
 
HATIMAYE klabu ya Simba jana ilifanya mkutano wa marekebisho ya katiba kwenye ukumbi wa bwalo la maofisa wa polisi, Oysterbay, Dar es Salaam.

Hata hivyo, mkutano huo nusura uvunjike baada ya Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage, kuwaita wanachama wa klabu hiyo mbumbumbu.

Rage alichafua hali ya hewa na kutaka kuzuka tafrani akidai kuwa, wanachama wa klabu hiyo hawana fedha.

"Nataka kila mmoja atambue kuwa, mimi ni Mwenyekiti wa Simba, ndiye naongoza mkutano huu, nyingi mbumbumbu msiokuwa na fedha mnapaswa kutulia,"alisema Rage.

Kauli yake hiyo iliwachefua wanachama hao, ambao walianza kurusha makombora ya maneno makali dhidi yake kabla ya kuwaomba radhi.

Baada ya Rage kuomba msamaha, mkutano uliendelea ambapo wanachama walijadili marekebisho ya katiba na kuyapitisha.

Baadhi ya vifungu vilivyofanyiwa marekebisho ni kupitishwa kwa suala la tawi kutokuwa na wanachama zaidi ya 25- au wasiopungua 50.

Pia wanachama walipitisha pendekezo la kutaka mkutano mkuu wa kawaida ufanyike mara mbili kwa mwaka badala ya mara moja kama ilivyokuwa awali.

Wanachama hao pia walipitisha ibara ya 26 fasili ya tano ya katiba, inayotamka kuwa, mgombea uongozi asiwe aliyewahi kutiwa hatiani kwa kosa la jinai.

JK AIPATIA SIMBA MIL 30



RAIS Jakaya Kikwete, ameipa klabu ya Simba sh. milioni 30 ili kupata hati ya kujenga uwanja wake wa soko ulioko Bunju, Dar es Salaam.

Akizungumza katika mkutano wa marekebisho ya katiba ya klabu hiyo jana, Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage alisema, Rais Kikwete, alitoa fedha hizo jana alipokutana naye Ikulu, Dar es Salaam.

Rage alisema Rais Kikwete alimwambia fedha hizo ametoa kama mwanamichez , anayependa kuona mchezo wa soka nchini unapata mafanikio kwa klabu kumiliki uwanja wake.

Alisema uzalendo wa Rais Kikwete, ni mfano bora wa kuigwa kwa kuwa amefanikisha jambo kubwa lililokuwa muhimu kwa ustawi wa Simba.

"Rais ameonyesha ni jinsi gani ana mapenzi na maendeleo ya michezo, hilo ni jambo kubwa,hivyo klabu ya Simba inamshukuru na tunaahidi kukamilisha ujenzi wa uwanja huo haraka iwezekanavyo,"alisema.

Mwenyekiti huyo wa Simba alisema, fedha hizo zitatumika kulipa hati ya uwanja na itakabidhiwa katika mkutano mkuu wa uchaguzi utakaofanyika Mei 4 mwaka huu.

Alisema ahadi ya ujenzi wa uwanja huo iko pale pale na utajengwa ndani ya siku 100 kama ilivyoahidiwa na maandalizi yanaendelea.

WACHEZAJI YANGA WANUSURIKA KATIKA AJALI


WACHEZAJI wa timu ya soka ya Yanga wamenusurika kifo baada ya basi walilokuwa wakisafiria kupata ajali walipokuwa njiani wakirejea Dar es Salaam kutoka Morogoro.

Ajali hiyo ilitokea jana saa tatu asubuhi katika eneo la Mikese, timu hiyo ilipokuwa ikitoka Morogoro kucheza mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Mtibwa Sugar.

Katika mechi hiyo iliyochezwa juzi kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, timu hizo zilishindwa kutambiana baada ya kutoka suluhu.

Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto, alisema kwa njia ya simu kutoka eneo la ajali kuwa, ajali hiyo ilitokea baada ya basi la klabuhiyo lenye namba za usajili T 916 CCS kuacha njia na kutumbukia kwenye mtaro.

Kizuguto alisema msafara wao ulinusurika kifo, baada ya basi hilo kukita katika eneo lenye majani nje kidogo ya barabara.

Alisema hakuna mchezaji au kiongozi aliyeumia kutokana na ajali hiyo na kwamba waliendelea na safari baada ya kupata basi lingine ya kampuni ya Abood.

Kwa mujibu wa Kizuguto, wachezaji na viongozi wa timu hiyo walilazimika kutokea madirishani kutokana na mlango wa basi kuegemea kwenye ardhi.