KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, June 27, 2010

Ghana yaiua Marekani na kutinga robo fainali

ASAMOAH Gyan (kushoto) akishangilia na mchezaji mwenzake baada ya timu hiyo kuichapa Marekani mabao 2-1 jana katika mechi ya raundi ya pili ya michuano ya fainali za Kombe la Dunia.
MCHEZAJI Ayew wa Ghana (chini) akishangilia ushindi wa timu hiyo na mchezaji mwenzake baada ya timu hiyo kuishinda Marekani mabao 2-1.MASHABIKI wa Ghana wakiserebuka katika mji wa Kumasi kushangilia ushindi wa timu hiyo jana dhidi ya Marekani.BEKI John Mensah (kulia) wa Ghana akiwania mpira hewani na mshambuliaji wa Marekani, Deschamps timu hizo zilipomenyana jana katika mechi ya raundi ya pili ya michuano ya Kombe la Dunia. Ghana ilishinda mabao 2-1 na kufuzu kucheza robo fainali.

JOHANNESBURG, Afrika Kusini
GHANA juzi ilifuzu kucheza robo fainali ya michuano ya soka ya fainali za Kombe la Dunia baada ya kuichapa Marekani mabao 2-1 katika mechi ya raundi ya pili iliyochezwa mjini hapa.
Mshambuliaji Asamoah Gyan ndiye aliyeibuka shujaa wa Ghana baada ya kuifungia baoa la pili dakika ya tatu ya muda wa nyongeza wa dakika 30 baada ya timu hizo kumaliza dakika 90 zikiwa sare ya bao 1-1.
Kipigo hicho kinamaanisha kwamba, safari ya Marekani katika fainali hizo imefikia ukingoni na itabidi isubiri hadi miaka minne iweze kujaribu tena bahati yake katika michuano hiyo mikubwa duniani.

Kevin-Prince Boateng aliifungia Ghana bao la kuongoza dakika ya 50 baada ya kupokea pasi kutoka kwa Ricardo Clark na kufumua shuti lililompita kipa Tim Howard wa Marekani.
Landon Donovan aliisawazishia Marekani kwa mkwaju wa penalti dakika ya 62 baada ya beki Jonathan Mensah wa Ghana kumwangusha Clint Dempsey ndani ya eneo la hatari.
Katika mechi nyingine ya michuano hiyo iliyochezwa juzi, Uruguay nayo ilifuzu kucheza robo fainali baada ya kuichapa Korea Kusini mabao 2-1.

Friday, June 25, 2010

Ghana yafungwa, lakini yasonga mbele

JOHANNESBURG, Afrika Kusini
GHANA imekuwa timu ya kwanza ya Afrika kufuzu kucheza raundi ya pili ya michuano ya soka ya Kombe la Dunia, licha ya kuchapwa bao 1-0 na Ujerumani katika mechi ya kundi D iliyochezwa juzi kwenye uwanja wa Soccer City mjini hapa.
Bao pekee na la ushindi la Ujerumani lilipatikana katika kipindi cha pili kupitia kwa mshambuliaji Mesut Ozil. Alifunga bao hilo baada ya kupokea pasi kutoka kwa Cacau, ambaye alikuwa mwiba kwa mabeki wa Ghana.
Ushindi huo uliiwezesha Ujerumani kumaliza mechi za kundi hilo ikiwa ya kwanza kwa kuwa na pointi sita baada ya kucheza mechi tatu, ikifuatiwa na Ghana na Australia, ambazo zilipata pointi nne kila moja, lakini zinatofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa.
Kwa matokeo hayo, Ghana sasa itacheza raundi ya pili kwa kuvaana na Marekani katika mechi itakayochezwa kesho kwenye uwanja wa Rustenburg wakati Ujerumani itavaana na England siku inayofuata mjini Bloemfontein.
Wakati huo huo, Australia juzi iliichapa Serbia mabao 2-1 katika mechi ya mwisho ya kundi D iliyochezwa mjini Nelspruit.
Pamoja na kuibuka na ushindi huo, Australia imeshindwa kusonga mbele kutokana na kuzidiwa na Ghana kwa uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Mabao ya Australia yalifungwa na Tim Cahil na Brett Holman wakati bao la kujifariji la Serbia lilifungwa na Marko Pamtelie.
Ratiba ya mechi zingine za raundi ya pili inaonyesha kuwa, Uruguay itavaana na Korea Kusini kesho mjini Port Elizabeth wakati Argentina itavaana na Mexico keshokutwa mjini Johannesburg.

Simba yapata mrithi wa Kaduguda


Malinzi sasa mlezi wa klabuL Rage kuwania ubunge Tabora

KLABU ya Simba imemtangaza Evodius Mtawala kuwa Katibu Mkuu mpya wa klabu hiyo, akichukua nafasi ya Mwina Kaduguda.
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage aliwaambia waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana kuwa, Mtawala atafanya kazi chini ya uangalizi kwa kipindi cha miezi mitatu akiwa ofisa utawala kabla ya kuendelea na majukumu yake.
Rage alisema lengo la kufanya hivyo ni kupima uwezo wake kikazi na kutambua kama atamudu majukumu yake kwa sababu ni mgeni katika uongozi wa soka.
Alisema kamati ya utendaji iliyokutana wiki hii iliamua kumteua Mtawala kushika wadhifa huo baada ya kuridhishwa na sifa zake kielimu.
Kwa mujibu wa Rage, Mtawala alizaliwa Agosti 1984 na kupata elimu ya msingi na sekondari katika mikoa ya Bukoba na Morogoro. Kwa sasa, Mtawala ana taaluma ya sheria aliyoipata katika Chuo Kikuu cha Cambrige cha Uingereza.
Mbali ya kufanya uteuzi huo, Rage alisema kamati hiyo pia imemuidhinisha Dioniz Malinzi kuwa mlezi wa klabu ya Simba na kuwapitisha wajumbe wanne kuunda bodi ya udhamini.
Aliwataja wajumbe hao kuwa ni Ramesh Patel, Hamis Kilomoni, Abbas Sykes na Abdulwahab. Alisema mhasibu na ofisa habari wa klabu hiyo watatangazwa baadae.
Wakati huo huo, Rage ametangaza nia ya kuwania ubunge katika jimbo la Tabora Mjini kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.
Rage alisema jana kuwa, amemua kuwania nafasi hiyo ili kutekeleza demokrasia ndani ya chama kwa vile uongozi ni suala la kupokezana kama mbio za vijiti.
Rage aliwania nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 na kushinda kura za maoni, lakini alienguliwa na nafasi yake kuchukuliwa na Siraji Kaboyonga.

BARNABAS: Mama haupendi wimbo wa Wrong Number


MSANII machachari wa muziki wa kizazi kipya nchini, Elias Barnabas amekiri kuwa, mama yake mzazi haupendi wimbo wake wa ‘Wrong Number’.
Barnabas alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, wakati mama yake anauchukia wimbo huo, hali ni tofauti kwa baba yake, ambaye anaufagilia ile mbaya.
"Mama hataki kabisa kuusikia huu wimbo, lakini baba hana tatizo lolote," anasema Barnabas, akimaanisha kwamba ni vigumu wimbo huo kusikika redioni nyumbani kwao wakati mama yake akiwepo.
Msanii huyo kutoka kundi la Tanzania House of Talent (THT) alisema, anahisi mama yake haupendi wimbo huo kwa sababu unasimulia kisa cha kweli kuhusu baba yake, ambacho kilimtokea huku mama yake akishuhudia.
Kibao hicho, ambacho kimekuwa kikipendwa na mashabiki wengi wa muziki wa kizazi kipya, kinazungumzia udanganyifi wa kimapenzi kwa wawili waliotengana.
Mashabiki wengi wa muziki huo wamekuwa wakijiuliza, ni vipi Barnabas, kijana mwembamba na mwenye urefu wa wastani, alipata wazo la kutunga kibao hicho?
Msanii huyo ameieleza Burudani kuwa, tukio alilosimulia kwenye kibao hicho ni la kweli na kwamba lilimtokea baba yake mzazi. Alisema alichokifanya ni kulielezea tukio hilo kimafumbo.
Msanii huyo, ambaye ana uwezo mkubwa wa kuimba na kupiga gita alisema, alishuhudia kisa hicho kati ya baba na mama yake, ambacho kilisababishwa na ujumbe mfupi wa simu ya mkononi.
Barnabas anasema ugomvi huo ulitokea siku za hivi karibuni saa nane usiku, nyumbani kwao Kigogo Makuburi, Dar es Salaam na chanzo kilikuwa ujumbe uliokutwa na mama yake kwenye simu ya baba yake, ukielezea masuala ya mapenzi ndipo mama yake akahisi amesalitiwa.
"Siku hiyo nikiwa nimelala, mara baba na mama wakaanza kugombana, nilisikia mama akimtuhumu baba kuwa ametumiwa ujumbe wa mapenzi na alitaka kufahamu ulitokea wapi," anasema Barnabas.
"Mama alipofanya uchunguzi, aligundua kwamba ujumbe huo ulitumwa na mwanamke mmoja anayeishi mtaani kwetu, ambaye alikuwa akimtaka baba kimapenzi,”aliongeza.
"Unajua baba ameokoka na anasali kanisa la Jangwani Makuburi, mama ni mkatoliki. Baba ni mcheshi wakati wote kanisani na nyumbani, jambo hilo huwavutia wasichana, ambao baadhi humtaka kimapenzi," alisema Barnabas.
Barnabas, ambaye aliwahi kutamba na wimbo wa 'Njia Panda' aliomshirikisha Dorine 'Pipi' anasema, ucheshi wa baba yake ulikaribia kumponza kwani mwanamke huyo wa mtaani alianza kumzoea kwa kasi, lakini Mungu alimuepusha kwani baba hakuwa na nia mbaya," alisema Barnabas akimtetea baba yake.
Wanamuziki hao ambao pia walikuwemo katika kinyang'anyiro cha kuwania Tuzo za Muziki za Kili na kutoka mikono mitupu wanasema hilo haliwapi presha kwani wanaamini wakati wao bado haujafika ingawa wanakiri kuwa wapo juu.
Akizungumzia kushindwa kwake kutwaa tuzo ya Kilimanjaro mwaka huu, Baranabas alisema hilo ni jambo la kawaida kwa msanii na ni lazima akubali matokeo.
"Nawapongeza waliochukua tuzo kwani ndio walionekana wanastahili, mimi nasubiri wakati wangu haujafika, ukifika nami naweza kuwa mshindi,”alisema Barnabas.
Alisema kitendo cha kuwemo katika kinyang'anyiro bado ni faraja kubwa kwake na amewataka wasanii walioshinda tuzo mbalimbali, wasibweteke na kujisahau kwani wanaweza kuanguka.
"Ukiingia kwenye kuwania tuzo, ujue wewe ni mkali, naamimi mimi ni mkali, lakini asiyekubali kushindwa si mshindani, ila ninachowaambia waliochukua tuzo hizo, wasilale ili wasianguke halafu ikawa balaa,”alisema.
Barnabas alikiri kuwa, washindi wa mwaka huu walipatikana kihalali kwa sababu mashabiki ndio walioamua baada ya kuwaona wanastahili.
Msanii huyo amekiri kuwa, heshima na uvumilivu ni miongoni mwa vitu vilivyomwezesha kufikia mafanikio aliyonayo sasa kimuziki, kiasi cha kualikwa kurekodi na mwanamuziki Fally Ipupa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo. Hivi karibuni, Barnabas alishirikiana na msanii Amini Mwinyimkuu kurekodi albamu ya pamoja, itakayokuwa na nyimbo 14. Wamerekodi baadhi ya nyimbo zilizomo kwenye albamu hiyo kwa kushirikiana na wasanii wa kundi la THT na Nyota Ndogo kutoka Kenya.
Baadhi ya nyimbo zilizomo kwenye albamu hiyo ni 'Njia Panda', 'Muongo', 'Nimelimisi, Mbalamwezi', 'Mama Vanesa', 'Robo Saa', 'Wrong Number' na ‘So so’.
Barnabas alizaliwa miaka 19 iliyopita katika jiji la Dar es Salaam.Wazazi wake ni wenyeji wa mkoa wa Morogoro na kabila lao ni Wapogoro.
Elias, ambaye ni mtoto wa kwanza katika familia yao, alipata bahati ya kumaliza elimu ya msingi na baada ya hapo alijiunga na sekondari ya Mikoji, lakini aliacha shule alipofika kidato cha pili na kuamua kujikita katika fani ya muziki.
Uamuzi wake huo ulipingwa vikali na wazazi wake, ambao walitegemea angejikita zaidi kwenye elimu kwa kuwa waliamini ndio msingi wa maisha.
Licha ya kuonekana kuwa na kipaji cha hali ya juu cha muziki, Barnabas hakuweza kujua apite wapi ili afike kileleni. Ni baada ya kujiunga na kundi la THT mwaka 2007 ndipo Mungu alipoanza kumuonyesha njia.
Jukumu la kwanza la THT lilikuwa kumsaidia kimawazo na kumpa elimu ya muziki, ambayo hivi sasa anamini ndio sababu kubwa ya mafanikio yake.

MAICON DOUGLAS SISENANDOSikutarajia kama ningeweza kutembea tena
Aligongwa na gari na kuvunjika miguu yote miwili
JOHANNESBURG, Afrika Kusini
HAKUNA jambo lililomfurahisha beki Maicon Douglas Sisenando wa Brazil kama kuitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya nchi hiyo, kinachoshiriki katika michuano ya fainali za Kombe la Dunia, inayoendelea nchini Afrika Kusini.
Beki huyo wa kimataifa wa Brazil nusura apoteze miguu yake yote miwili wakati alipokuwa na umri wa miaka 10 baada ya kupatwa na ajali ya kugongwa na gari.
Maicon (26) alikumbana na ajali hiyo wakati alipokuwa akienda kwenye baa ya jirani na nyumbani kwao kwa lengo la kumkabidhi funguo za nyumba baba yake.
Kufuatia ajali hiyo, Maicon hakuweza kutembea kwa miezi kadhaa. Alikuwa akifanya kila kitu kwa msaada wa baba yake, ikiwa ni pamoja na kubebwa na kulazwa kitandani.
Waswahili wanasema Mungu si Athumani. Baada ya takriban mwaka mmoja, Maicon aliweza kupona kabisa, japokuwa alishakuwa na mawazo kwamba asingeweza kutembea tena.
Kuwepo kwake nchini Afrika Kusini ndiko kulikomfanya akumbukie tukio hilo lililotokea miaka kadhaa iliyopita. Bado anakumbuka jinsi alivyokuwa akitembea kwa tabu kutoka kwenye sofa kwenda mahali ilipokuwa televisheni nyumbani kwao Novo Hamburgo.
Miaka minane baada ya kupatwa na ajali hiyo, Maicon aliweza kujumuika tena na vijana wenzake kucheza soka. Ni beki aliyerithi mikoba ya Carlos Alberto, Josimar na Cafu, akiwa ameichezea Brazil mechi 59 za kimataifa na kutwaa ubingwa wa Ulaya akiwa na klabu ya Inter Milan ya Italia.
Maicon ni miongoni mwa wachezaji wa Brazil waliong’ara wakati timu hiyo ilipoichapa Korea Kaskazini mabao 2-1 katika mechi ya ufunguzi ya kundi G. Alifunga moja ya mabao hayo mawili ya Brazil kwa shuti kali la mbali.
“Nalikumbuka vizuri tukio zima la ajali ile,”alisema Maicon alipozungumza na gazeti la News of The World.
“Nilikuwa nikikimbia na kuanguka katikati ya mtaa na nikagongwa na gali. Mama yangu aliona kila kitu na alichanganyikiwa,”aliongeza.
“Baba yangu alipatwa na ghadhabu kwa sababu alishanieleza kwamba sipaswi kukimbia ninapokatiza mtaani. Wazazi wangu walipatwa na wasiwasi mkubwa kuhusu mimi,”alisema Maicon.
“Walishampoteza mtoto wa kiume, aliyeitwa Elton Luis katika ajali ya gari kabla mimi sijazaliwa. Alikuwa na umri wa miaka minane na alikuwa akiendesha baiskeli wakati alipogongwa na gari,”alisema beki huyo wa klabu ya Inter Milan. “Hivyo wazazi wangu hawakuwa tayari kupoteza mtoto mwingine. Nakumbuka nilikuwa nimelala barabarani na baba yangu alikuwa akilia na kuniuliza ‘Upo hai, upo hai?’” Alisema.
“Nilijaribu kumjibu kwa kumwambia ‘Nipo salama, hakuna kibaya kilichotokea’, lakini hakuwa akinisikiliza. Kwa wakati huo, niligundua ni jinsi gani kifo cha kaka yangu kilivyowaumiza mioyo yao na jinsi gani walivyokuwa na uchungu.
“Sikuweza kutembea wala kujiinua baada ya ajali ile. Nilipoteza nguvu za miguu yangu. Baada ya kutibiwa na kurejea nyumbani, nakumbuka nilitumia muda mwingi bila kutembea kwa miguu yangu,”alisema.
“Kwa mfano, sikuweza kutembea kutoka kwenye sofa nilipotaka kutazama TV, hivyo baba yangu alipaswa kunibeba. Na nilipotaka kulala, baba yangu alinibeba kunipeleka kitandani. Sikuweza kutembea kwa miguu yangu na sikuweza kuelewa nini kilitokea kwangu. Nilikuwa na wasiwasi kwamba nisingeweza kutembea tena,”aliongeza.
Baba wa mchezaji huyo, Manoel alikuwa beki wa kati wa klabu ya Novo Hamburgo na wakati alipokuwa kocha wa timu ya Criciuma, aliamua kumchukua Maicon na kuanza kumfundisha soka. Ndiye aliyembadili Maicon kucheza kutoka nafasi ya kiungo kwenda beki. Baadaye, Maicon alijiunga na klabu ya Cruzeiro ya Brazil kabla ya kujiunga na Monaco ya Ufaransa mwaka 2004. Miaka minne baadaye, Maicon alijiunga na Inter Milan ilipokuwa chini ya Kocha Roberto Mancini.
“Nilikuwa mnyonge na mwenye masikitiko makubwa kwa sababu sikutaka kuiangusha familia yangu. Nakumbuka kuna siku nilirudi nyumbani nikilia kwa sababu nilitaka kuchezea klabu ya Gremio,”alisema.
“Wakati huo, baba yangu alikuwa na mawasiliano na klabu ya Criciuma, hivyo nikaenda kule. Miezi michache baadaye, baba aliajiriwa kama kocha. Siku moja, beki wetu wa kulia hakuweza kupatikana. Hivyo baba yangu aliniambia, ‘unapaswa kucheza nafasi hiyo kwa sababu huchezi vizuri nafasi ya kiungo.’
“Alikuwa na mawazo kwamba sikuwa na kasi ya kucheza nafasi ya kiungo na ningeweza kucheza vizuri nikiwa beki wa kulia. Alikuwa sahihi,”alisema Maicon.
Maicon alizaliwa Julai 26, 1981 katika kitongoji cha Cricium kilichopo mji wa Santa Catarina. Aliitwa kwa mara ya kwanza kwenye kikosi cha Brazil mwaka 2004 baada ya kujiunga na klabu ya Monaco.

SIKINDE KUTAMBULISHA MBILI MPYA

KIONGOZI wa bendi ya Mlimani Park Orchestra, Habibu Abbas Jeff akimkabidhi zawadi Amina Michael baada ya kuibuka mshindi wa kucheza miondoko ya Sikinde. Shindano hilo lilifanyika kwenye ukumbi wa DDC Kariakoo, Dar es Salaam.
MASHABIKI wa Mlimani Park Orchestra wakijimwayamwaya kwenye ukumbi wa DDC Kariakoo, Dar es Salaam.

WAPULIZA Tarumbeta, Mbaraka Othman (kushoto) na Hamisi Milambo wakifanya vitu vyao.


WAIMBAJI Abdalla Hemba (kushoto) na Hassan Bitchuka wa Mlimani Park Orchestra wakiwajibika jukwaani.

BENDI ya muziki wa dansi ya Mlimani Park Orchestra ‘Sikinde’ imeibuka na vibao viwili vipya, vinavyotarajiwa kutambulishwa rasmi kwa mashabiki mwishoni mwa wiki hii.
Msemaji Msaidizi wa bendi hiyo, Emmanuel Ndege alisema mjini Dar es Salaam juzi kuwa, vibao hivyo vimetungwa na mwimbaji mkongwe, Shaaban Dede.
Alivitaja vibao hivyo kuwa ni ‘Mapenzi kitu cha ajabu’ na ‘Mwanamke kumwezesha’.
Kwa mujibu wa Ndege, vibao hivyo vitapigwa kwa mara ya kwanza katika onyesho litakalofanyika Jumapili kwenye ukumbi wa DDC, Kariakoo, Dar es Salaam.
Alisema kutungwa kwa vibao hivyo ni maandalizi ya utambulisho wa albamu mpya ya bendi hiyo, inayotarajiwa kukamilika hivi karibuni.
Mbali na kutambulisha vibao hivyo, Ndege alisema bendi hiyo imeanzisha utaratibu wa kuwapa zawadi mashabiki wake kupitia mashindano ya kucheza miondoko ya Sikinde na kuimba.
“Kuanzia wiki iliyopita, tulianzisha shindano la kucheza miondoko ya Sikinde na washindi wawili wa kwanza walipata zawadi zilizotolewa na wanachama wetu wa kundi la Sikinde Family,”alisema.
Aliwataja washindi hao kuwa ni Amina Michael kwa upande wa wanawake na Sirikali Msumali aliyeibuka mshindi kwa wanaume. Hata hivyo, hakutaja zawadi zilizotolewa kwa washindi hao.
“Hiyo ni siri yao, tunachokifanya ni kuwakabidhi zawadi hizo pale pale ukumbini zikiwa zimefungwa kwenye mifuko maalumu. Lengo letu ni kuwashangaza na kuwaonyesha kwamba tunawapenda na kuwathamini,”alisema.

JABIR: Nimeondoka Simba kutafuta maslahi bora zaidi

JABIR Azizi akipachika bao pekee la Taifa Stars ilipomenyana na Brazil kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Katika mechi hiyo, Stars ilichapwa mabao 5-1.

JABIR Azizi (kulia) akiwa na wachezaji wenzake wa timu ya taifa, Taifa Stars. Kutoka kushoto ni Mrisho Ngasa, Mussa Hassan Mgosi na Jerryson Tegete.
WANACHAMA na mashabiki wa klabu ya Simba hivi karibuni walipigwa na butwaa baada ya kupata taarifa kuwa, mshambuliaji Jabir Azizi ameitosa timu hiyo na kujiunga na Azam FC. Katika makala hii iliyoandikwa na Mwandishi Wetu Athanas Kazige, mchezaji huyo anaelezea kuhusu uamuzi wake huo na mipango yake ya baadaye.
SWALI: Kipi kilichokufanya ufikie uamuzi wa kuondoka Simba na kujiunga na Azam FC kwa ajili ya msimu ujao wa ligi?
JIBU: Kwa kweli nimeamua kuondoka Simba kwa lengo la kutafuta maslahi bora zaidi, ambayo nimeahidiwa na viongozi wa Azam. Sikugombana na mtu Simba, isipokuwa viongozi wa Azam walinifuata na kuniomba nijiunge na timu yao kwa ahadi mbalimbali, ambazo kwangu naziona ni nzuri na zitaboresha maisha yangu.
SWALI: Unataka kusema kwamba maslahi uliyokuwa ukiyapata Simba ni madogo ikilinganishwa na yale uliyoahidiwa na viongozi wa Azam au kuna tatizo jingine?
JIBU: Azam wameahidi kunipa maslahi mazuri, ambayo hakuna timu yoyote hapa Tanzania inayoweza kumpa mchezaji wake. Licha ya jambo hilo, mimi sijawahi kugombana na kiongozi yeyote wa Simba, wachezaji wenzangu au wanachama. Nimekaa Simba vizuri na nimeondoka bila ya kukwaruzana na mtu yeyote.Lakini jambo la msingi ni kwamba, nimefanikiwa kutimiza malengo yangu ya kupata maslahi bora na nina imani nitacheza soka kwa nguvu zote.
SWALI: Huoni kama kuondoka kwako Simba kutawaumiza viongozi, wanachama na wachezaji wenzako wa klabu hiyo?
JIBU:Kwa kweli inawabidi wanielewe kwani nimefuata maendeleo kwa vile soka ndio sehemu ya maisha yangu ya kila siku.
SWALI: Ni mafanikio gani uliyoyapata Simba na ambayo unaweza kujivunia nayo? Na ni kipi ulichojifunza ulipokuwa katika klabu hiyo?
JIBU: Nimejifunza mambo mengi sana, ambayo mengine siwezi kuyaelezea kwa vile yapo mazuri na mabaya, lakini kwa ujumla nimenifunza mengi sana kuhusu soka.
SWALI: Jambo gani baya ulilowahi kukumbana nalo ndani ya Simba baada ya kujiunga na klabu hiyo ukitokea Ashanti?
JIBU: Ninachoweza kusema ni kwamba yapo machache mabaya, ambayo nimeyaona, lakini sipendi kuyaanika na kuyapa nafasi kwenye vyombo vya habari. Binafsi ninapasha kuishukuru Simba na wanachama wake na wachezaji wote niliokutana nao pale.
SWALI: Katika kipindi chote ulichoichezea klabu ya Simba, kipi kilikufurahisha zaidi?
JIBU: Nilifurahishwa na kitendo cha kuwepo ushindani wa namba kwenye kikosi cha kwanza miongoni mwa wachezaji. Hiyo ndiyo siri kubwa ya Simba kupata mafanikio msimu uliopita.
SWALI: Mara nyingi ulikuwa unashindwa kuitumikia Simba katika michuano mbalimbali kutokana na kuwa majeruhi kwa muda mrefu. Unazungumza nini kuhusu hilo? JIBU: Ni kweli nilishindwa kucheza mechi nyingi msimu uliopita kutokana na kuwa majeruhi kwa muda mrefu, lakini kila nilipopata nafasi ya kucheza, nilijitahidi kuhakikisha kwamba nafanya kweli kwa kuonyesha uwezo mkubwa ndani ya dimba.
SWALI: Unapenda kuwaahidi nini viongozi, mashabiki na wachezaji wenzako wa Azam msimu ujao? Nini wakitegemee kutoka kwako?
JIBU: Nimekuwa nikijifua kwa nguvu ili kuhakikisha ninakuwa fiti kwa lengo la kukabiliana na changamoto ya kuwania namba kwenye kikosi cha kwanza. Najua ndani ya Azam wapo wachezaji wengi wakali, lakini nitahakikisha ninapambana nao ili lengo langu liweze kutimia.
SWALI: Una maoni gani kuhusu kuondoka kwa Kocha Mkuu wa timu ya Taifa, Taifa Stars, Marcio Maximo, ambaye anamaliza mkataba wa kuinoa timu hiyo mwezi ujao?
JIBU: Kwa kweli mimi binafsi nasikitika sana kwa kuondoka kwake kwa sababu ameweza kuleta maendeleo na mageuzi makubwa katika soka ya Tanzania na pia kufufua mapenzi ya Watanzania kwa timu ya Taifa Stars.
Ni kweli kwamba yapo baadhi ya mapungufu aliyokuwa nayo kama kocha, lakini lazima tukiri kwamba mimi na wachezaji wenzangu wengi wa Taifa Stars tutamkumbuka kocha huyo kwa kipindi kirefu.
Kupitia kwake, nimeweza kujifunza mambo mengi, ikiwa ni pamoja na uchezaji soka makini, nidhamu na bidii ndani na nje ya uwanja. Hivyo ni miongoni mwa vitu, ambavyo Maximo alikuwa akivisisitiza sana kwetu.
SWALI: Kitu gani ulichokipata kutoka kwa kocha huyo na ambacho unajivunia hivi sasa katika maisha yako kisoka?
JIBU: Nimepata vitu vingi. Kama si yeye kuniita katika timu ya Taifa Stars, nisingeweza kupata nafasi ya kucheza na wachezaji bora ulimwenguni. Na kwa bahati nzuri, Mungu alinisaidia nikafunga bao la kufuta machozi kwa nchi yangu katika mechi dhidi ya Brazil.
SWALI: Ulijisikiaje baada ya kufunga bao hilo mara baada ya mchezo huo kumalizika, hasa ikizingatiwa kwamba ulikuwa umetokea benchi kuchukua nafasi ya Abdulrahim Humoud?
JIBU: Mechi hiyo ni kumbukumbu kubwa katika maisha yangu yote. Sikutegemea hata siku moja kukutana na wachezaji nyota kama Kaka, Lucio na wengine na hata kufunga bao katika mechi dhidi ya Brazil.
Lakini bado nina imani kwamba Tanzania tunavyo vipaji vingi vya soka, ambavyo vikipata malezi bora, ipo siku tutacheza hata fainali zijazo za Kombe la Dunia.
SWALI: Je una matarajio gani kuhusu kocha mpya wa Taifa Stars, Jan Borge Poulsen, ambaye ataanza kazi hivi karibuni ya kuinoa timu hiyo?
JIBU: Nina imani kubwa kwamba ujio wake utaendeleza mafanikio tuliyoyapata kutoka kwa Maximo. Tunachohitaji kukifanya ni kumpa ushirikiano wa kutosha ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
SWALI: Una maoni gani kuhusu mchakato wa kuwapata wachezaji wa Taifa Stars? Au nini kifanyike ili wapatikane wachezaji wenye vipaji?
JIBU: Ninachoweza kushauri ni kwamba, mara atakapokuja kocha huyo na kuanza kazi, apewe nafasi ya kuzunguka mikoa yote nchini kwa lengo la kusaka vipaji. Asichaguliwe wachezaji. Tunayo mashindano mengi hivi sasa, naamini akipata nafasi ya kuyashuhudia, ataweza kupata wachezaji wengi wazuri.
SWALI: Serikali imekuwa inawekeza zaidi katika soka, ni mapungufu gani uliyoweza kuyabaini, ambayo ni kikwazo kwa maendeleo ya mchezo huo nchini?
JIBU: Napenda kumpongeza sana Rais Jakaya Kikwete kwani ameleta changamoto kubwa na kuchangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya soka hapa nchini. Hii ni kwa sababu alikubali kumlipa mshahara Kocha Marcio Maximo na kufanikisha ujio wa timu za Brazil na Ivory Coast, ambazo tulicheza nazo mechi za kirafiki.
Mbali na Rais Kikwete, ninampongeza sana Rais wa awamu ya pili, Benjamin Mkapa kwa kufanikisha ujenzi wa Uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam. Uwanja huo umesaidia watu wengi kujitokeza kwenda kushuhudia mechi za kimataifa kwa sababu wana uhakika watakaa kwa raha uwanjani.

Sunday, June 20, 2010

CHUJI: Nitachezea timu yoyote, ninachozingatia maslahi


MSHAMBULIAJI Athumani Iddi ‘Chuji’ wa Yanga hivi karibuni alikaririwa akisema kuwa, huenda akarejea katika klabu yake ya zamani ya Simba baada ya viongozi wa timu hiyo kuonyesha nia ya kumsajili. Katika makala hii ya ana kwa ana, Chuji anaelezea mambo mbalimbali kuhusu maisha yake kisoka na mipango yake ya baadaye.

SWALI: Hivi karibuni ulikaririwa na gazeti hili ukisema kuwa, upo katika mazungumzo na viongozi wa klabu ya Simba kwa ajili ya usajili wa msimu ujao wa ligi. Je, mazungumzo yako na viongozi wa Simba yamefikia wapi hadi sasa?
JIBU: Ni kweli nilikutana na viongozi wa Simba hivi karibuni na katika mazungumzo yetu, walionyesha nia ya kutaka kunirejesha katika klabu hiyo msimu ujao, lakini bado hatujafikia mwafaka, tunaendelea na mazungumzo.
SWALI: Kwa nini hujafikia mwafaka na Simba wakati umeonyesha wazi kwamba hutaki kuendelea kuichezea Yanga msimu ujao kutokana na sababu mbalimbali?
JIBU:Ni kweli, awali niliwahi kusema hivyo, lakini tofauti kati yangu na Simba zimemalika na ndio maana hata mama yangu mzazi alipokuwa anaumwa, walinisaidia sana, kwa kweli nawashukuru kwa jambo hilo.
SWALI: Huoni kama utakuwa umekula matapishi yako na pengine wapenzi wa soka watashindwa kukuelewa?
JIBU: Soka ni sehemu ya maisha yangu ya kila siku, napenda kutengeneza maisha yangu ya baadae kupitia soka,hivyo ninaangalia zaidi maslahi bora kwanza na mapenzi ya klabu baadae.
SWALI: Una mpango wowote wa kuongeza mkataba wa kuichezea Yanga msimu ujao?
JIBU: Nilishafanya mazungumzo na uongozi wa Yanga kuhusu jambo hilo, lakini mfadhili wetu Yusuf Manji alitoa pesa kidogo kwa wachezaji wote. Hadi sasa bado sijakaa chini na viongozi wa Yanga kuzungumzia suala la mkataba.
SWALI: Huoni kama kuna hatari ya wewe kuingia kwenye matatizo iwapo utatia saini fomu za usajili za klabu mbili?
JIBU: Siwezi kufanya hivyo kwa sababu najua sheria zinavyosema kuhusu jambo hilo. Nipo makini kukwepa matatizo ya aina hiyo. Nikifungiwa, maana yake ni kwamba ninahatarisha ajira yangu, ambayo ni kucheza soka.
SWALI: Iwapo klabu ya Yanga itakupa pesa kwa ajili ya kuongeza mkataba, utakuwa tayari kufanya hivyo? Na ni kiasi gani cha pesa, ambacho utataka ulipwe ili kumwaga wino Yanga?
JIBU: Kwa kweli siwezi kutaja kiwango cha fedha ninachotaka kulipwa na klabu yoyote, sio Yanga tu. Hiyo ni siri yangu. Lakini nitakuwa tayari kuendelea kuichezea Yanga iwapo watanilipa fedha ninazozihitaji, si vinginevyo.
SWALI: Kwa muda mrefu sasa umeondolewa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kwa tuhuma za utovu wa nidhamu. Umejifunza nini kutokana na tatizo hilo?
JIBU: Nimejifunza mambo mengi na kujua jinsi watu walivyo. Lakini jambo la msingi ni kwamba, bado nahitaji kulitumikia taifa langu muda wowote nitakapotakiwa kujiunga na timu hiyo.
SWALI: Una maoni gani kuhusu kumalizika kwa mkataba wa Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Marcio Maximo?
JIBU: Waswahili wanasema mnyonge mnyongeni, lakini haki yake mpeni. Japokuwa sikuwa nikielewana na Maximo, lakini ametupa mafanikio makubwa, licha ya kuwepo kwa kasoro ndogo ndogo, ambazo mimi binafsi naziona ni za kibinadamu.
SWALI: Je, kuondoka kwa Maximo kunaweza kufungua milango kwako kurejea kwenye kikosi cha Taifa Stars?
JIBU: Hilo siwezi kulijibu kwa sababu mwamuzi wa kurejea kwangu kwenye kikosi hicho ni kocha mpya, aliyetangazwa hivi karibuni na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
SWALI: Je, una mipango yoyote ya kwenda kucheza soka ya kulipwa nje ya Tanzania?
JIBU: Ni kweli ni nina mpango wa kwenda Sweden. Nimepata timu huko, lakini bado kuna mambo madogo ninayaweka sawa, ikiwa ni pamoja na usajili na kujua hali ya wazazi wangu kwanza. Pia natarajia kukutana na Manji ili kujua hatma yangu msimu ujao.

Khadija: Sina ugomvi na Mzee Yussuf


MWIMBAJI nyota wa muziki wa taarab nchini, Khadija Yussuf ameanika hadharani sababu za kuondoka kwake katika kundi la Jahazi Modern Taarab, linaloongozwa na kaka yake, Mzee Yussuf.
Akizungumza mjini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita, Khadija alisema alijiengua katika kundi hilo kwa sababu ya maslahi duni si vinginevyo.
Khadija alisema si kweli kwamba aliondoka katika kundi hilo kutokana na kushindwa kuelewana na Mzee, hasa katika mambo ya maslahi.
Mwanamama huyo tipwatipwa alijiengua katika kundi la Jahazi mwaka mwishoni mwa mwaka jana na kujiunga na kundi jipya la Five Stars Modern Taarab.
"Sina ugomvi wowote na Mzee, yeye ni kaka yangu, tunaheshimiana sana na tunaelewana sana, lakini nilihama katika kundi lake kutokana na uchache wa maslahi," alisema.
Mwimbaji huyo anayependwa na mashabiki wengi kutokana na sauti yake maridhawa alisema, yupo tayari kufanya maonyesho na kaka yake iwapo atatakiwa kufanya hivyo.
Alisema tangu ajiunge na kundi la Five Stars, linaloongozwa na Ally Jay, mambo yake yamekuwa mazuri na hana matatizo kama alivyokuwa Jahazi.
"Hivi sasa mambo yangu yanakwenda vizuri, tofauti na nilipokuwa Jahazi, namshuruku Mungu malengo yangu yametimia," alisema.
Khadija aliwahi kutamba kwa vibao vyake vitamu kama vile Mkuki kwa Nguruwe, Zilipendwa, Hayanifiki, Hamchoki kusema, Riziki mwanzo wa chuki.
Alikiri kwamba kibao kilichompandisha chati na kumpatia umaarufu mkubwa ni Mkodombwe, alichokiimba wakati akiwa katika kundi la East African Melody.
Khadija alisema kwa sasa anajipanga upya kabla ya kuibuka na kibao chake kipya kitakachojulikana kwa jina la Ukisema cha nini.
"Ninawaahidi mashabiki wangu wakae mkao wa kula kwani niko mbioni kuachia tungo yangu mpya, ambayo bila shaka itakuwa gumzo hapa nchini," alisema.

Siamini, najihisi nipo ndotoni-AT

SIKU chache baada ya kupokea tuzo ya Kilimanjaro ya wimbo bora wa korabo, msanii Ali Ramadhani, maarufu kwa jina la AT amesema, haamini mafanikio aliyoyapata hadi sasa.
AT, ambaye amekuwa akitamba kwa kibao chake cha Nipigie, alichomshirikisha mkongwe Stara Thomas, amesema hadi sasa bado anajihisi kama yupo ndotoni.
Msanii huyo anayetamba kwenye vituo mbalimbali vya radio na televisheni hapa nchini, alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, kamwe hakuwahi kufikiria katika maisha yake iwapo anaweza kuwapagawisha mashabiki kwa singo yake moja.
"Mafanikio ya singo hiyo yamenifanya niwe na kiburi, najiona ninaweza muziki na ndoto zangu za kuwa mmoja wa watawala katika fani hii zipo mbioni kutimia,"alisema.
"Hivi sasa napata shoo za kufa mtu mpaka zingine nazikataa, yaani naringa, najaa kiburi kutokana na wimbo huo," aliongeza.
Msanii huyo mwenye asili ya Pemba alisema, hatua aliyofikia sasa ni kubwa na kwamba ameanza kuwatetemesha wakali wengine wa muziki huo na wenye majina makubwa.
"Wakati nilipoanza muziki, wengi hawakuamini kama ningefanya vema, sasa wengi wanakubali sikuwa nikifanya utani," alisema na kuongeza kuwa, matunda ya wimbo huo yamemfanya atunze wazazi wake waliopo Zanzibar na vilevile anaishi vema pamoja na mchumba wake (hakutaka kumtaja jina).
"Nimetoka kwenye familia ya kimasikini, hilo silikatai, nalikubali tena kwa moyo mmoja, ninapopata mafanikio, anajiona mwenye amani zaidi," alisema.
"Japokuwa siwasaidii wazazi wangu kwa kila kitu, lakini nawapa kile kidogo ninachokipata kutokana na muziki, hasa wimbo wa Nipigie," alisema AT.
Alisema ingawa yeye ni mtu wa watu, wimbo huo umemfanya atembee mabega juu zaidi. "Kuna maringo ya kujisikia na ya kujiamini, mimi nina maringo ya kujiamini, ndiyo maana ni mtu wa watu, napenda kukaa uswahilini, kujichanganya na watu kwa sababu hao ndiyo wanaonifanya niwe juu,"alisema. AT alisema anaamini amepata tuzo ya muziki ya Kilimanjaro kutokana na ushirikiano alioupata kutoka kwa watu wa mitaani.
Msanii huyo anatarajia kuzindua albamu yake, iliyobeba jina la 'Nipigie' yenye nyimbo 14 hivi karibuni. Albamu hiyo ina vionjo vya sauti za wasanii Nyota Ndogo, Nameless, Ngoni, Shircom, Stara Thomas,Tina, Khadija Kopa na Joti.

Thursday, June 10, 2010

Bwagamoyo Sound yazaliwa upyaMWIMBAJI na kiongozi wa bendi ya muziki wa dansi ya Bwagamoyo Sound, Mwinjuma Muumin akiwaongoza wacheza shoo wake kufanya vitu vyao katika onyesho la uzinduzi wa bendi hiyo lililofanyika hivi karibuni kwenye ukumbi wa Vatican City, Sinza, Dar es Salaam.

JK ALIPOIALIKA TWIGA STARS IKULU

RAIS Jakaya Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na wachezaji wa timu ya soka ya taifa ya wanawake, Twiga Stars leo asubuhi Ikulu, Dar es Salaam. JK aliipa heshima hiyo Twiga Stars kutokana na kuweka rekodi ya kufuzu kwa mara ya kwanza kucheza fainali za Mataifa ya Afrika zinazotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu nchini Afrika Kusini. Twiga ilifuzu hatua hiyo baada ya kuitoa Ethiopia kwa jumla ya mabao 4-2 kabla ya kuibwaga Eritrea kwa jumla ya mabao 11-4.
(Picha na Bashir Nkoromo)

Radio, TV sasa kulipia kazi zote za wasanii

SERIKALI imesema kuanzia sasa vyombo vyote vya habari nchini, hasa vituo vya televisheni na radio, vitalazimika kuwalipa wasanii kila vitakapokuwa vikitumia kazi zao.
Msimamo huo wa serikali ulitolewa mwishoni mwa wiki iliyopita na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Hakimiliki Tanzania (COSOTA), Yustus Mkinga alipokuwa akizungumza kwenye kipindi cha Kipima Joto, kilichorushwa hewani na kituo cha televisheni cha ITV.
Mkinga alisema tayari wameshafanya mazungumzo na wamiliki wa vyombo hivyo vya habari ili waanze kulipia kazi za wasanii, badala ya utaratibu uliopo sasa, ambapo hakuna malipo yoyote yanayotolewa kwa wasanii.
“Hii ni sheria, haikwepeki. Ni kweli kwamba kwa sasa vyombo hivyo vinatumia kazi za wasanii bila kuwalipa, hili ni kosa kisheria,”alisema.
Akichangia mada hiyo, kiongozi wa bendi ya muziki wa dansi ya The Kilimanjaro, Waziri Ally alisema, si kweli kwamba vyombo vya habari vimekuwa vikiwapromoti wasanii kwa kutumia kazi zao.
“Hiyo si kweli hata kidogo, vinapaswa kutulipa. Wasanii na vyombo vya habari tunafanyakazi kwa kutegemeana,” alisema Waziri, mmoja wa wanamuziki wakongwe nchini, aliyewahi kupigia bendi ya Msondo Ngoma miaka ya 1970.
Waziri alisema wanamuziki wengi wakongwe nchini wamekuwa wakiifanyiakazi serikali tangu miaka ya 1950, lakini hakuna faida yoyote waliyoipata na wengi wao wamekufa wakiwa maskini.
“Umefika wakati sasa tuviambie vyombo hivi vya habari kwamba hapana, wakati wetu umepita hatukunufaika lolote, lakini sasa lazima tuwatengenezee mazingira mazuri vizazi vijavyo,”alisema.
Mmoja wa wasambazaji maarufu wa kazi za wasanii nchini, Ignas Kambarage alisema, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), haitekelezi majukumu yake ipasavyo kutokana na kuruhusu biashara hiyo ifanyike holela.
Ignas alisema kazi nyingi feki za wasanii zimekuwa zikiingizwa nchini kutoka nchini jirani ya Kenya na China, lakini TRA imekuwa haichukui hatua zozote kuwashughulikia wahusika.
Alihoji iwapo ni kweli CD za filamu na muziki mchanganyiko zinazouzwa nchini, wasanii husika wanafahamu kuwepo kwake na pia iwapo wamelipwa chochote.

PATRICK MTILIGA, Mtanzania atakayecheza fainali za Kombe la Dunia


SOKA ya Tanzania inatarajiwa kuingia kwenye historia mpya, kutokana na kuwa na mwakilishi katika fainali za mwaka huu za Kombe la Dunia, zinazotarajiwa kuanza kesho nchini Afrika Kusini.
Katika fainali hizo, mchezaji Patrick Mtiliga, anayecheza soka ya kulipwa katika klabu ya Malaga ya Hispania, anatarajiwa kuwa Mtanzania wa kwanza kupeperusha bendera ya Tanzania.
Hata hivyo, Mtiliga atacheza fainali hizo akiwa mchezaji wa timu ya taifa ya Denmark, ambako ndiko alikozaliwa. Baba wa mchezaji huyo ni mtanzania wakati mama yake ni raia wa Denmark.
Mtiliga alizaliwa Januari 28, 1981 katika mji wa Copenhagen. Ni mchezaji anayecheza nafasi ya beki wa kushoto. Ameichezea timu ya taifa ya Denmark katika mechi tatu za kimataifa.
Alianza kucheza soka katika timu ya vijana ya Boldklubben ya Copenhagen mwaka 1993. Alikuwa akicheza nafasi ya kiungo mshambuliaji.
Alianza kuichezea timu ya wakubwa ya klabu hiyo mwaka 1998 hadi 1999. Baada ya kuichezea klabu hiyo mechi 13 za ligi, aliihama na kujiunga na Feyenoord Rotterdam ya Uholanzi.
Klabu ya Feyenoord ilimuuza Mtiliga kwa mkopo kwa klabu ya vijana ya Excelsior Rotterdam kwa kipindi, ambacho hakikuweza kufahamika. Alianza kuichezea timu ya wakubwa katika mwaka wake wa kwanza ndani ya klabu hiyo.
Aliichezea timu hiyo kwa misimu miwili na nusu, akiwa miongoni mwa wachezaji walioiwezesha kupanda daraja msimu wa 2001-02. Timu hiyo ilishuka daraja msimu uliofuata.
Msimu wa 2003-04, Mtiliga alijihakikishia namba ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo na kuichezea mechi 23 kabla ya kurejeshwa kwenye klabu ya Feyenoord.
Januari 2005, Mtiliga alikumbwa na balaa baada ya kuumia msuli wa paja, baada ya kuichezea Feyenoord mechi 11 za ligi. Baada ya kupona Januari 2006, Feyenoord iliamua kumuuza tena kwa mkopo, lakini Mtiliga aligoma na kuamua kusugua benchi hadi mkataba wake ulipomalizika.
Agosti 2006, Mtiliga alijiunga na klabu ya NAC Breda kwa mkataba wa mwaka mmoja, ukiwa na kipengele kinachoruhusu kuongezwa iwapo atafanya vizuri.
Baada ya kuonyesha kiwango cha juu, ilipofika Januari 2007, aliamua kuongeza mkataba wake na kuwa wa miaka miwili na nusu. Aliichezea timu hiyo katika mechi 34 na kumaliza msimu wa 2007-08 ikiwa ya tatu kwenye ligi.
Mkataba wake ulipomalizika mwaka 2009, Mtiliga alianza kuwaniwa na klabu mbalimbali za Ulaya kabla ya kuamua kujifunga kitanzi katika klabu ya Malaga ya Hispania
Mtanzania huyo mwenye uraia wa Denmark alikumbwa na balaa la kuumia katika mechi yake ya kwanza akiwa na Malaga na kuwa nje ya uwanja kwa kipindi kirefu.
Baada ya kupona, Kocha Juan Ramon Lopez wa Malaga alimshauri abadili namba na kucheza nafasi ya ushambuliaji na muda si mrefu uliofuata, akaanza kujihakikishia namba kwenye kikosi cha kwanza.
Januari 24 mwaka huu, Mtiliga alikumbwa na balaa lingine la kuumia baada ya kuvunjika pua, kufuatia kupigwa kwa kiwiko cha mkono na mshambuliaji Cristiano Ronaldo wa Real Madrid. Ronaldo alionyeshwa kadi nyekundu kwa kosa hilo na Mtiliga alikaa nje ya uwanja kwa wiki tatu.
Mtiliga alianza kucheza soka ya kimataifa mwaka 1997 katika timu ya taifa ya vijana wa chini ya miaka 17 ya Denmark. Amecheza mechi 28 katika timu tofauti za vijana za nchi hiyo na kufunga mabao manne.
Wakati akiwa klabu ya Feyenoord, Kocha Ruud Gullit alimwelezea mchezaji huyo kwamba, atakuwa tegemeo kubwa la Denmark katika miaka ijayo.
Alianza kuichezea timu ya wakubwa ya Denmark, Novemba 2008 baada ya kuitwa na kocha Morten Olsen. Aliichezea kwa mara ya kwanza ilipocheza na Wales kabla ya kutemwa.
Aliitwa tena kwenye kikosi hicho Mei mwaka huu kwa ajili ya fainali za Kombe la Dunia.

Huyu ndiye kocha mpya Taifa Stars


SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limemtangaza Jan Borge Poulsen kuwa kocha mkuu mpya wa timu ya Taifa, Taifa Stars.
Poulsen (64) anatarajiwa kuanza kibarua hicho Agosti Mosi mwaka huu, akichukua nafasi ya kocha wa sasa, Marcio Maximo anayemaliza mkataba wake Julai 31 mwaka huu.
Katibu Mkuu wa TFF, Fredrick Mwakalebela aliwaambia waandishi wa habari mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, Poulsen anatarajiwa kutia saini mkataba wa miaka miwili wa kuifundisha timu hiyo.
Uamuzi wa kumteua Poulsen kuwa kocha mkuu wa Taifa Stars ulifikiwa katika kikao cha kamati ya utendaji ya TFF kilichofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita.
Poulsen, ambaye ni kocha mkuu wa zamani wa timu ya taifa ya Denmark, aliwabwaga makocha wengine wanne kutoka nchi za Bulgaria, Poland, Serbia na Ureno.
Awali, jumla ya makocha 59 kutoka nchi mbalimbali duniani, wakiwemo wanne kutoka Tanzania, walituma maombi ya kazi hiyo kabla ya kuchujwa na kubaki watano.
Mwakalebela alimwelezea Poulsen kuwa ni kocha mwenye kiwango cha juu na pia mkufunzi wa makocha, anayetambuliwa na Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA).
Poulsen alizaliwa Machi 23, 1964. Alianza kucheza soka katika klabu ya vijana ya Store Heddinge BK kabla ya kujiunga na Ronne IK. Alianza kucheza soka ya wakubwa katika klabu ya Boldklubben Frem.
Mwanzoni mwa miaka ya 1980, aliteuliwa kuwa kocha wa klabu ya Boldklubben Frem na baadaye Koge Boldklub kabla ya kuteuliwa kuwa kocha msaidizi wa timu ya taifa ya Denmark, ambayo ilitwaa ubingwa wa Ulaya mwaka 1992.
Baada ya kushinda taji la Ulaya, aliteuliwa kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya vijana wa chini ya miaka 21. Aliifanyakazi hiyo hadi mwaka 1999, alipoteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Michezo wa timu ya taifa ya Singapore.
Wakati kocha Vincent Subramaniam wa Singapore alipotimuliwa mwaka 2001 kutokana na matokeo mabaya, Poulsen aliteuliwa kushika nafasi yake.
Hata hivyo, hakuweza kuiletea Singapore mafanikio yoyote. Naye alitimuliwa mwaka uliofuata na kurejea Denmark, ambako na kuendelea na kazi hiyo katika klabu mbalimbali.
Mwaka 2006, alifikia makubaliano na klabu ya Greve Fodbold ya kuwa kocha mpya wa timu hiyo, lakini wakati huo huo, akapata ofa ya kuwa kocha wa timu ya vijana wa chini ya miaka 20 na Jordan. Aliikubali ofa ya Jordam.
Januari mwaka 2008, Poulsen aliteuliwa kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Armenia. Machi 30 mwaka jana, alitemeshwa kibarua hicho na Shirikisho la Soka la Armenia.

Kaka: Brazil bado kiwango


JOHANNESBURG, Afrika Kusini
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Brazil, Ricardo Kaka amekiri kuwa, bado kikosi chao hakijakamilika kwa ajili ya fainali za Kombe la Dunia zinazotarajiwa kuanza kesho nchini Afrika Kusini.
Kaka alisema hayo alipokuwa akihojiwa na waandishi wa habari waliofuatana na timu hiyo nchini kwa ajili ya pambano la kimataifa la kirafiki dhidi ya timu ya Tanzania, Taifa Stars.
Katika pambano hilo lililochezwa mwanzoni mwa wiki hii kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Brazil iliicharaza Taifa Stars mabao 5-1.
“Bado kuna kitu kinachokosekana. Lakini bado tuna wiki moja kabla ya mechi yetu ya ufunguzi na tutalazimika kufanyakazi ya ziada ili tuwe katika hali nzuri,”alisema Kaka, ambaye alifunga moja kati ya mabao matano ya Brazil katika mechi hiyo.
Japokuwa hakufafanua kuhusu kauli yake hiyo, wadau wengi wa soka nchini Brazil wamelalamikia kitendo cha Kocha Carlos Dunga kumwacha kwenye kikosi hicho kiungo Ronaldinho Gaucho.
Katika mechi hiyo, mshambuliaji Robinho de Souza alifunga mabao mawili, kama ilivyokuwa kwa Ramirez, aliyeingia kipindi cha pili, yakiwa mabao yake ya kwanza kwa timu hiyo. Bao la Taifa Stars lilifungwa na Jabir Azizi.
Ilikuwa mara ya kwanza kwa Brazil kufungwa bao katika mechi tano. Kwa mara ya mwisho, ilifungwa bao Oktoba mwaka jana, ilipofungwa mabao 2-1 na Bolivia katika mechi ya kuwania kufuzu kucheza fainali hizo, iliyopigwa mjini La Paz.
Brazil imepangwa kundi C pamoja na timu za Korea Kaskazini, Ivory Coast na Ureno. Itacheza mechi yake ya kwanza Juni 15 kwa kupambana na Korea Kaskazini.
Katika hatua nyingine, mshambuliaji Ramires wa Brazil mwanzoni mwa wiki hii alimpigia simu mama yake, akimjulisha kuhusu mabao mawili aliyoifungia timu hiyo dhidi ya Taifa Stars.
Ilikuwa mara ya kwanza kwa Ramires, ambaye ni mchezaji wa akiba, kuifungia mabao Brazil katika mechi za kimataifa.
Mara baada ya pambano hilo kumalizika, Ramires alimtwangia simu mama yake mzazi, Judith kumwelezea furaha aliyokuwa nayo kwa kutimiza ndoto yake,
Akihojiwa na mtandao wa Yahoo mara baada ya timu hiyo kurejea Afrika Kusini juzi, Ramires alisema alitaka kusherehekea pamoja mabao hayo na mama yake, anayeishi kwenye kitongoji cha Barra do Pirai kilichopo mjini Rio de Janeiro.
“Pia nilizungumza na kaka zangu. Wote walikuwa wakisherehekea mabao yangu na inawezekana bado wanashangilia,”alisema mchezaji huyo wa klabu ya Benfica ya Ureno.
Ramires (23), ambaye aliingia uwanjani kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Felipe Melo alisema, lilikuwa jambo la kufurahisha kwake kwa sababu lengo lake lilikuwa angalau kufunga bao moja, lakini akapata mawili.
Mshambuliaji huyo alisema yupo tayari kucheza nafasi yoyote, lakini hawezi kulalamika kwa kutopata namba kwenye kikosi cha kwanza wakati wa fainali za Kombe la Dunia.
“Kuwemo kwangu kwenye kikosi hiki pekee hunijaza furaha. Hupata zawadi kila wakati ninapoingia uwanjani na kuisaidia timu,”alisema Ramires, ambaye ameichezea Brazil mechi 14 za kimataifa.

Narudi Simba-Chuji


KIUNGO Athumani Idd wa klabu ya Yanga amesema huenda akarejea katika klabu yake ya zamani ya Simba iwapo viongozi wake watashindwa kumalizana naye haraka.
Akizungumza na Burudani kwa njia ya simu jana, Chuji alisema amekuwa akifanya mawasiliano mara kwa mara na viongozi wa Simba ili arejee klabu hiyo msimu ujao wa ligi.
Chuji alisema amefikia uamuzi huo baada ya kumaliza mkataba wake wa miaka miwili wa kuichezea Yanga na kwamba kwa sasa yupo huru.
"Soka ndiyo ajira yangu, naona Yanga wapo kimya hadi sasa kuhusu mkataba mpya, lakini Simba wananisumbua mara kwa mara, kama watanipa dau kubwa, nitarudi,"alisema kiungo huyo wa zamani wa timu ya taifa, Taifa Stars.
Wakati Chuji akielezea msimamo wake huo, Mfadhili mkuu wa Yanga, Yusuf Manji mwishoni mwa wiki iliyopita alitoa orodha ya wachezaji wenye mkataba na klabu hiyo. Wachezaji hao ni Nurdin Bakari, Athumani Idd, Shamte Ally, Jerson Tegete, Idd Mbaga na Ally Msigwa.
Manji alikaririwa akisema kuwa, ametenga kitita cha sh. milioni 108 kwa ajili ya kuwalipa wachezaji wa ndani na nje ili waweze kuichezea timu hiyo msimu ujao.
Wachezaji, ambao mfadhili huyo atalazimika kuwalipa fedha zingine ili waendelee kuichezea timu hiyo ni kipa Yaw Berko kutoka Ghana, Fred Mbuna, Steven Marashi na beki Wisdom Ndhlovu kutoka Malawi.
Wengine ni Bakari Mbegu, Shadrack Nsajigwa, Godfrey Bonny, Kigi Makasi, John Njoroge, Nadir 'Cannavaro' Haroub na Abdi Kassim.
Wakati huo huo, Chuji amesema kipigo ilichokipata Taifa Stars katika mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Brazil kilichangiwa na wachezaji kuchoka.
Chuji alisema kutokana na kukabiliwa na mechi mbili ndani ya saa 24, wachezaji wengi walichoka na kushindwa kucheza katika kiwango chao cha kawaida.
“Timu yoyote, ambayo ingekutana na Brazil katika mazingira kama hayo, lazima ingekumbana na kipigo kama hicho,”alisema mchezaji huyo aliyetemwa kwenye kikosi hicho na Kocha Marcio Maximo kwa tuhuma za utovu wa nidhamu.
Kabla ya kucheza na Brazil, Stars ilipambana na Rwanda na kufungwa bao 1-0 katika mechi ya marudiano ya raundi ya pili ya michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN).

Witness awashangaa wanaonenepesha makalioMSANII machachari wa muziki wa kizazi kipya nchini, Witness Maliwigi ameeleza kukerwa na tabia za baadhi ya wanawake nchini kuongeza makalio yao kwa kutumia dawa za kichina.
Witness alielezea dukuduku lake hilo mwishoni mwa wiki iliyopita alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha Friday Nite Live kilichorushwa hewani na kituo cha televisheni cha East Africa.
Alisema haelewi kwa nini wanawake hao wanapenda kuwa na makalio makubwa kinyume na maumbile aliyowaumba nayo Mwenyezi Mungu.
Witness alisema inashangaza kuona kuwa, Wachina wanatengeneza dawa za kunenepesha makalio na maumbile mengine ya mwanadamu, lakini wao hawazitumii.
“Ni vizuri kwa mwanamke kubaki kama ulivyoumbwa na Mungu, uwe mbantu halisi. Kwa mfano, nilivyo mimi hapa si mbaya, huu uafrika halisi, si wa Kichina,” alisema mwanadada huyo aliyejazia vyema kimwili akiwa na makalio ya asili.
“Hii ni orijono prodakti kutoka Mbeya, kilikuwepo kabla ya Wachina kuanza kuuza dawa zao. Hatuhitaji kujibadilisha, kaka zetu ndio wanaopenda haya mambo,”aliongeza.
Witness alisema pia kuwa, siku zote katika maisha yake amekuwa akipendelea kuvaa mavazi anayoyapenda na kusisitiza kuwa, mwonekane wake si rahisi kuwaridhisha watu wengi.
Alisema siku zote anaamini kuwa, ukipendwa na wengi, lazima utakuwa na matatizo, tofauti na wakikuchukia kwa sababu itakusaidia kujua kasoro zako na kujirekebisha.
Msanii huyo alisema si rahisi kwa binadamu kuishi kwa lengo la kuwaridhisha watu fulani na kusisitiza matatizo yapo siku zote, hayawezi kukwepeka.

Banza achengua mashabiki Dar

MWIMBAJI mahiri wa muziki wa dansi nchini, Ramadhani Masanja 'Banza Stone' mwishoni mwa wiki iliyopita aliwateka mamia ya wapenzi wa burudani baada ya kupanda jukwaani na kuimba kwa dakika tatu wimbo wake wa 'Mtu pesa'.
Banza, ambaye amekuwa kimya kwa muda mrefu kutokana na kusumbuliwa na maradhi, aliibuka ghafla kwenye ukumbi wa Vatican City, Sinza, Dar es Salaam, wakati wa uzinduzi wa bendi ya Bwagamoyo Sound International.
Mwimbaji huyo aliyepata umaarufu mkubwa alipokuwa bendi ya Twanga Pepeta kutokana na kipaji chake cha uimbaji, aliingia ukumbini saa sita usiku na kushangiliwa na mamia ya wapenzi waliohudhuria uzinduzi huo.
Baada ya kuingia ukumbini hapo, Mkurugenzi wa bendi ya Bwagamoyo, Mwinjuma Muumini alimtambulisha kwa wapenzi waliokuwa na shauku ya kutaka kumuona akipanda jukwaani na kuimba japo kwa dakika moja.
Banza, ambaye hadi sasa anasifika kutokana na uwezo mkubwa wa kutawala jukwaa na tungo zake nzuri, alilazimika kupanda jukwaani na kuimba beti mbili za wimbo huo, ambao uliteka hisia za wapenzi wa muziki waliohudhuria onyesho hilo.
Kupanda jukwaani kwa Banza kuliwafanya mashabiki hao kumsogelea kwa karibu zaidi huku wengine wakitaka kushikana naye mikono kwa lengo la kumpongeza.
"Huyu jamaa ni noma kweli, hakuna mwimbaji anayeweza kumfikia, tunamuombea kwa Mungu apate nafuu haraka arudi kwenye gemu," alisikika akisema mmoja wa wapenzi hao, aliyekuwepo ukumbini hapo.
Akizungumza wakati wa onyesho hilo, Banza alisema hali yake kwa sasa inaendelea vizuri na kwamba yupo mbioni kuzindua bendi yake itakayoitwa Sony Sound.
"Niko poa kwa sasa, tayari nimetunga wimbo wangu unaofahamika kwa jina la 'Falsafa', ambao umekamilika, ninawaomba mashabiki na wapenzi wangu wajiandae," alisema huku akiwa na tabasamu kubwa.

Mzee Yusuph haninyimi usingizi-Leila

MWIMBAJI mahiri wa kikundi cha taarab cha Jahazi, 'Wana wa Nakshinakshi', Leila Rashid ametoa ya moyoni kwa kutamka kuwa, tabia ya mume wake, Mzee Yusuph kuoa mara kwa mara haimsumbui.
Leila, ambaye aliolewa na Mzee miaka minne iliyopita alisema, ameizoea tabia hiyo ya mumewe na kusisitiza kuwa, hana presha na jambo hilo.
"Sipati tabu hata kidogo ninaposikia Mzee ameoa, kwani najua dini yetu imeruhusu mwanaume kuoa wake hata wanne, sasa nitashaangaa nini?” Alihoji mwimbaji huyo.
Leila, mmoja wa waimbaji waliojaaliwa kuwa na mvuto wa hali ya juu na sauti murua alisema, wanaheshimiana na kupendana na mumewe,tofauti na wanavyofikiria watu wa nje.
Mwanamama huyo, anayetamba na wimbo wa 'Ubinadamu Kazi', alisema mume wake anapotaka kufunga ndoa, anamshirikisha kabla ya kumpa ruksa.
"Tangu aliponiona, mume wangu hafanyi jambo bila kunishirikisha. Anapotaka kufunga ndoa, hunitaarifu na mimi humpa ruksa, najua ni hiari kwa kila muislamu kuoa mke zaidi ya mmoja kama ana uwezo," alisema mwimbaji huyo.
Leila alisema pia kuwa, haoni tatizo kufanyakazi kikundi kimoja na mumewe, ambaye ndiye mkurugenzi wa Jahazi Modern Taarab. Alijiunga na kikundi hicho akitokea East African Melody.
Akizungumzia kibao chake cha kwanza kinachokwenda kwa jina la ‘Maneno ya mkosaji’, Leila alikiri kwamba ndicho kilichompandisha chati na kumfanya we kwenye matawi ya juu.

Madega bado kiongozi halali Yanga


‘Madega out Yanga’, ‘Madega ang’olewa’, ‘Uchaguzi Yanga Juni 27’, ‘Jaji Mkwawa kuiongoza Yanga hadi uchaguzi’, ‘Katiba Yanga yapitishwa’.
Hivyo ni baadhi tu ya vichwa vya habari vilivyopamba magazeti mbalimbali yaliyochapishwa Juni 7 mwaka huu, ikiwa ni siku moja baada ya klabu ya Yanga kufanya mkutano mkuu maalumu wa kupitisha katiba.
Mkutano huo uliohudhuriwa na wanachama wapatao 4,000 na kuendeshwa na Mwenyekiti wa Yanga, Imani Madega, ulifanyika kwenye ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa Polisi, Oysterbay, Dar es Salaam.
Karibu kila gazeti liliandika taarifa za mkutano huo kivyake. Yapo yaliyoandika kuwa, uongozi wa Madega umeondolewa madarakani na mengine yaliripoti kuwa, umesimamishwa. Vyombo vingine vilikwenda mbali zaidi kwa kuripoti kuwa, katika mkutano huo, wanachama walimteua Jaji Mkwawa, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Yanga, kuchukua nafasi ya Madega hadi uchaguzi mkuu utakapofanyika.
Hali hii ilisababisha wananchi wengi kushindwa kutambua ni kipi hasa kilichotokea kwenye mkutano huo. Je, ni kweli kwamba uongozi wa Madega uliondolewa madarakani? Kwa kigezo na taratibu zipi?
Wengine walishindwa kutambua lengo hasa la mkutano huo lilikuwa lipi? Je, marekebisho ya katiba yalipitishwa? Na kama mkutano huo ulikuwa wa kujadili katiba, kwa nini wanachama walichukua uamuzi wa kumuondoa madarakani Madega?
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na uongozi wa Yanga kabla ya mkutano huo, lengo lilikuwa kujadili na kupitisha marekebisho ya katiba, vikiwemo vipengele kadhaa vilivyopendekezwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Na hivyo ndivyo ilivyofanyika. Baada ya Madega kuwauliza wanachama mara tatu, iwapo wameyakubali marekebisho hayo yaliyotolewa na TFF na kumjibu ndio, aliamua kufunga mkutano na kutangaza kuwa, uchaguzi mkuu utafanyika Julai 4 mwaka huu.Alifanya hivyo kwa sababu ajenda ya mkutano huo ilishamalizika.
Karibu vipengele vyote vipya vya katiba ya Yanga vilivyowasilishwa kwenye mkutano huo, vilitokana na ushauri wa TFF, isipokuwa kipengele kinachohusu Baraza la Wadhamini, ambacho ndicho kilichozua utata.
Katika mapendekezo yaliyowasilishwa na uongozi, Baraza la Wadhamini lilitakiwa kuwajibika kwa kamati ya utendaji, lakini wanachama walipinga na kutaka liwajibike kwenye mkutano mkuu wa wanachama. Katika hali ya kushangaza, mara baada ya Madega kutangaza kufunga mkutano, wanachama walianza kumzomea Madega wakidai kuwa, wamemchoka.
Ilibidi Jaji Mkwawa aingilie kati na kuokoa jahazi kwa kuamuru mkutano uendelee ili wanachama waweze kupanga tarehe ya uchaguzi. Na kwa kauli moja, wanachama walikubali uchaguzi ufanyike Juni 27 mwaka huu.
Katika maelekezo yake kwa wanachama, Jaji Mkwawa alisema, kisheria, uongozi wa Madega ulimaliza muda wake tangu Mei 29 mwaka huu na kama bado wapo madarakani, ukomo wao ni siku 40, hivyo upo uwezekano wa uchaguzi mkuu kufanyika Juni 27 au siku zingine ndani ya hizo.
Kwa mantiki hiyo, si sahihi kwa sasa kusema kuwa Madega ameondolewa madarakani. Madega bado ni mwenyekiti halali wa Yanga hadi uchaguzi utakapofanyika.
Uhalali wa Madega kuendelea kuwa mwenyekiti wa Yanga pia unatokana na ukweli kwamba, hakukuwa na hoja iliyowasilishwa kwa wanachama ya kutaka kumuondoa.
Ikumbukwe kuwa, mwenyekiti wa Yanga ndiye mwendeshaji na msimamizi wa mikutano yote ya wanachama wa klabu hiyo. Hivyo hakukuwa na uhalali kwa wanachama kumteua Jaji Mkwawa kuendesha mkutano huo kwa sababu hayo si majukumu yake.
Kwa mujibu wa katiba ya Yanga, Jaji Mkwawa ni mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi, hivyo majukumu yake ni kusimamia zoezi la uchukuaji fomu, kuwahoji wagombea na kuendesha uchaguzi.
Pia haiingii akilini ni vipi Makamu wa Kwanza wa Rais wa TFF, Athumani Nyamlani na Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria na Hadhi kwa Wachezaji ya TFF, Alex Mgongolwa walihudhuria mkutano huo na kuwahutubia wanachama.
Je, ni kweli kwamba TFF inapaswa kuwatuma viongozi ama wajumbe wake kuhudhuria mikutano ya klabu zilizo wanachama wake? Kama si kweli, Nyamlani na Mgongolwa walihudhuria mkutano huo kwa mwaliko wa nani? Kama walihudhuria kama wanachama wa Yanga, kwa nini walipewa nafasi ya kuzungumza?
Kauli iliyotolewa na Nyamlani wakati wa mkutano huo pia inashangaza. Makamu huyo wa kwanza wa rais wa TFF alisema, muda wa kiongozi kuwepo madarakani unapomalizika, lazima mkutano mkuu uridhie kumwongezea muda zaidi, hata kama ni siku moja.
Lakini Nyamlani amesahau kwamba anahodhi vyeo vitatu katika vyama tofauti. Mbali na kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais TFF, pia bado ni Katibu wa Chama cha Soka mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) na Katibu wa Chama cha Soka wilaya ya Temeke (TEFA) wakati muda wa uongozi wake katika vyama hivyo umeshamalizika.
Sasa hapa ni nani anayehodhi madaraka kati ya Madega na Nyamlani?
Ikumbukwe pia kwamba, Madega na Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako ndio wanaopaswa kutia saini marakebisho ya katiba ya Yanga baada ya kupitishwa na TFF. Hakuna wengine wanaoweza kufanya hivyo zaidi yao.
Sasa iweje wanachama waseme wamemuondoa Madega madarakani? Hiyo katiba itatiwa saini na nani kabla ya kupelekwa kwa Msajili wa Vyama na Klabu za Michezo nchini ili isajiliwe?
Aidha, kama Madega ameondolewa madarakani, ni nani atakayeitisha mkutano wa uchaguzi mkuu hiyo Juni 27? Na je, uongozi mpya utakaoingia madarakani hiyo siku utakabidhiwa madaraka vipi na nani?
Jambo jingine linaloshangaza kuhusu mkutano huo wa marekebisho ya katiba ni kitendo cha baadhi ya viongozi wa TFF kuwasilisha mapendekezo mapya ya marekebisho ya katiba kwa Yanga usiku wa kuamkia mkutano huo wa Jumapili.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa, Jumamosi usiku, mmoja wa viongozi wa TFF aliwasilisha kwa Katibu Mkuu wa Yanga maelekezo mengine ya shirikisho hilo kuhusu marekebisho ya ibara za 22 (2); 29 (4); na 61 (9) kinyume na maelekezo yao ya awali kuhusu ibara 22 (2) na 29 (4) katika barua ya TFF kumb. Na. TFF/TECH/LEP.09/04 ya Desemba 18, 2009.
Maelekezo hayo mapya ya TFF ni kuhusu muda wa mwisho wa uongozi kwa mujibu wa katiba ya 2007, ambapo awali shirikisho hilo lilitaka ibara hiyo iondolewe; pia akidi ya mkutano wa dharura, ambayo sasa itakuwa ni ½ ya wajumbe waliohudhuria badala ya maelekezo ya awali ya 2/3 ya wajumbe.
Katika maelekezo hayo mapya ya TFF ya Jumamosi usiku, mdhamini wa Yanga sasa atawajibika kwa mkutano mkuu badala ya kamati ya utendaji.
Ni kwanini TFF iliwasilisha maelekezo hayo mapya usiku wa kuamkia mkutano huo wa marekebisho ya katiba?Kama walifanya hivyo kwa shinikizo, basi ni TFF wenyewe ndio wanaofahamu na yule aliyewapa shinikizo hilo.
Kilichotokea katika mkutano huo linapaswa kuwa funzo kubwa kwa wanachama wa Yanga kwamba wasikubali ‘kupelekeshwa’ na watu wachache wenye lengo la kuweka mbele zaidi maslahi yao binafsi badala ya klabu. Wanapaswa kukumbuka msemo wa Kiswahili unaosema, ‘Majuto mjukuu’.
Ni dhahiri kwamba wanachama wa Yanga waliingia kwenye mkutano huo wakiwa tayari wameshaandaliwa kutenda waliyoagizwa na ‘watu’ wao. Hili ni jambo la hatari kwa mustakabali wa Yanga na endapo hawatakuwa makini, watakuja kujuta baadaye.
Inawezekana ni kweli Madega ana matatizo yake, lakini ukweli unabaki palepale kwamba, taratibu zilizotumika kumwondoa madarakani katika mkutano huo hazikuwa halali na hakuna kipengele chochote kwenye katiba ya Yanga kinachozungumzia kuwepo kwa uongozi wa muda.
Hivi kwa namna ile alivyozomewa Madega, ni mtu gani na heshima zake atakubali kugombea nafasi mojawapo ya uongozi wa Yanga? Tusubiri, tuone.


MSHAMBULIAJI Robinho de Souza (kulia) wa Brazil akitia saini mpira wa mchezaji, Uhuru Selemani wa timu ya taifa, Taifa Stars mara baada ya kumalizika kwa pambano kati ya timu hizo lililofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Brazil ilishinda mabao 5-1.

Wachezaji Stars watoboa siri nzito

WACHEZAJI wa timu ya soka ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars wamelionya Shirikisho la Soka nchini (TFF), kuacha tabia ya kuingilia masuala ya ufundi yanayoihusu timu hiyo.
Walitoa onyo hilo mwishoni mwa wiki iliyopita mara baada ya Taifa Stars kuchapwa mabao 5-1 na Brazil katika mechi ya kirafiki ya kimataifa, iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Wakizungumza kwa masharti ya kutotajwa majina yao, wachezaji hao walisema tabia hiyo imekuwa ikichangia kuleta madhara makubwa kwenye timu hiyo.
Kauli ya wachezaji hao imekuja siku chache baada ya TFF kumtangaza Jan Borge Poulsen kutoka Denmark kuwa kocha mkuu mpya wa timu hiyo, akichukua nafasi ya Marcio Maximo, anayetarajiwa kumaliza mkataba wake Julai 31 mwaka huu.
“Ukweli ni kwamba kocha wetu wa sasa Maximo amekuwa akitupiwa lawama nyingi kutokana na timu kufanya vibaya katika michuano mbalimbali, lakini kuna baadhi ya mambo alikuwa akikwamishwa na viongozi wa TFF,” alisema mmoja wa wachezaji hao.
Mbali na kukwamishwa kwa Maximo, wachezaji hao walisema kwa kipindi kirefu sasa wamekuwa wakicheleweshewa malipo yao, hali inayochangia kumvunja moyo kocha huyo katika kutekeleza majukumu yake.
Wachezaji hao walisema pia kuwa, Maximo amekuwa akikwamishwa kwenda kuzichunguza timu pinzani kabla ya kupambana na Taifa Stars na hivyo kushindwa kujua mbinu zao.
“Wapo baadhi ya viongozi walikuwa wakijaribu kuingilia mambo ya kiufundi, ikiwemo kutaka baadhi ya wachezaji waitwe ama watemwe kwenye kikosi cha Taifa Stars kwa matakwa yao,” alisema mchezaji mwingine.
Walionya kuwa, iwapo tabia hiyo itaendelea, itakuwa vigumu kwa kocha mpya, Poulsen kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi kama ilivyokuwa kwa Maximo.

VUMILIA: Nina mtoto, ndoa bado kidogo


MSANII nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Vumilia amekiri kuwa ni kweli kwamba anaye mtoto, aliyezaa na mpenzi wake, lakini bado hawajafunga ndoa.
Vumilia alibainisha hayo mwishoni mwa wiki iliyopita alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha Friday Nite Live kilichorushwa hewani na kituo cha televisheni cha East Africa.
Alisema mtoto wake huyo anaitwa Mariam, lakini haishi pamoja na baba yake na kusisitiza kuwa, mipango ya ndoa bado haijatimia.
Vumilia, ambaye ni mmoja wa waasisi wa kundi la Tanzania House of Talent (THT), amekuwa akitamba kwa kibao chake kipya kinachojulikana kwa jina la ‘Tatizo ni umaskini’.
Alisema alikitunga kibao hicho yeye mwenyewe kutokana na wazo la kubuni na kukanusha madai kuwa, ni tukio lililowahi kumtokea katika maisha yake.
“Unajua watu wengi wamekuwa wakitunga nyimbo za kuelezea matukio mbalimbali, lakini hakuna aliyewahi kuzungumzia jambo hili,”alisema.
“Hivyo kuna siku nilikaa nyumbani na kuwaza sana kuhusu sababu zinazowafanya wazazi kuwakatalia watoto wao wasioe ama kuolewa na watu wanaowapenda ndipo nikapata wimbo huu,” aliongeza.
Vumilia amesema amekuwa akipata nguvu ya kimuziki kutokana na binti yake, ambaye kila anapomuona ameamka salama, hujisikia vizuri. Alimzaa mtoto huyo mwaka juzi.
Mwanadada huyo mwenye sura na umbo la kuvutia alisema, alimzaa mtoto wake huyo kwa kukusudia na si kwa bahati mbaya kama baadhi ya watu walivyokuwa wakimvumishia.
“Wenzangu walidhani nisingeweza tena kuendelea na muziki baada ya kujifungua. Walidhani ningefilisika. Jambo hilo lilinihuzunisha sana. Lakini Mungu alikuwa upande wangu na nikafanikiwa zaidi,”alisema.
Vumilia alisema kwa sasa anafanyakazi ya muziki kwa mafanikio zaidi na anaishi vizuri na baba wa mtoto wake, japokuwa hawaishi pamoja, lakini wanaheshimiana kama mtu na mzazi mwenzake. Mwadada huyo amewataka wasanii wenzake wa kike wanapopata uja uzito, wawe wamedhamiria kwa dhati kuwa na watoto na kufanya hivyo si kosa la jinai.
Mwanadada huyo amesema hadi sasa hajawahi kupata tatizo lolote kimuziki kwa sababu mashabiki wamekuwa wakimpokea vizuri na humshangilia kila anapopanda na kushuka stejini.
Vumilia alijiunga na kundi la THT mwaka 2006 akiwa mmoja wa waanzilishi wake. Wakati akijiunga na kundi hilo, alikuwa na kipaji cha kuimba, lakini alilazimika kujifunza upya.
Akizungumzia wimbo wake wa 'Utanikumbuka', Vumilia alisema umemwezesha kupata mafanikio zaidi kifedha na kimaisha na pia ameweza kuisaidia familia yake.
Alisema alitunga wimbo huo kutokana na matatizo aliyowahi kuyapata dada yake kutoka kwa mume wake, ambapo kila alipokuwa akienda kumtembelea, alimkuta akiwa na majonzi.
Kutokana na kukithiri kwa mates ohayo, Vumilia alisema dada yake alilazimika kuondoka kwa mumewe na kurejea kwa wazazi wake huku akimuapiza mumewe kwamba ipo siku atamkumbuka.
Vumilia alisema anachoshukuru ni kuona kwamba, kibao hicho kimemsaidia dada yake kurejea kwa mumewe kutokana na ukweli kwamba, alianza kumkumbuka kimapenzi.
Mwanadada huyo alisema wapo wasichana wengi wanaopenda kujitosa kwenye fani ya muziki, lakini wanakatishwa tamaa kutokana na kutojitokeza watu wa kuwaunga mkono.
Alisema baadhi yao baada ya kujitokeza, wamekuwa wakikumbwa na tamaa za kimapenzi kwa mapromota, madj na mameneja wao na kusahau majukumu yao.
Kwa sasa, Vumilia ameamua kujifunza upigaji wa vyombo vya muziki likiwemo gita na anatarajia kuzindua albamu yake mpya yenye nyimbo kumi hivi karibuni.
Baadhi ya nyimbo zinazotarajiwa kuwemo kwenye albamu hiyo ni pamoja na ‘Utanikumbuka’, 'Tatizo Umaskini', 'Nenda', 'Akupe Raha', 'Penzi la Kinafiki' na 'Telephone'.
Mbali na kupiga muziki, Vumilia anapendelea kusoma vitabu, kukutana na watu tofauti ili kujua maisha yao na shida zao kwa lengo la kupata matukio ama visa vya kuvitungia nyimbo.
Anavutiwa na uimbaji wa mwanamuziki Pauline Zongo, Juliana wa Rwanda na Nyota Ndogo wa Kenya. Kwa wanamuziki wa kimataifa, anavutiwa na Monica Seka.
Anamshukuru mwalimu mkuu wa kundi la THT, Richard Mangustino kuwa ndiye aliyemfundisha muziki na kumwezesha kufika alipo sasa.

Monday, June 7, 2010

Wabrazil watua Dar

KIKOSI cha timu ya soka ya taifa ya Brazil kiliwasili nchini jana usiku kwa ajili ya pambano lake la kimataifa la kirafiki dhidi ya Tanzania litakalochezwa leo. Timu hiyo iliwekewa ulinzi mkali baada ya kuwasili na waandishi wa habari na wapiga picha wa vyombo vya habari vya Tanzania hawakuruhusiwa kuwasogelea. Waliofanikiwa kuwapiga picha ni waandishi kutoka Brazil. Kivutio kikubwa katika msafara huo, alikuwa mshambuliaji Ricardo Kaka.

Sunday, June 6, 2010

Kanu aionya Argentina

JOHANNESBURG, Afrika Kusini
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Nigeria, Nwankwo Kanu ameionya Argentina kwamba isiwadharau na kutarajia kushinda kirahisi mechi kati yao.
Nigeria na Argentina zinatarajiwa kukutana Juni 12 mwaka huu katika mechi ya ufunguzi ya kundi G ya michuano ya fainali za Kombe la Dunia, itakayochezwa mjini Johannesburg.
Nahodha huyo wa Nigeria alisisitiza kuwa, timu yao inao uwezo wa kufanya maajabu dhidi ya miamba hiyo ya dunia kutoka bara la Amerika ya Kusini.
Nchi hizo mbili zimepangwa kundi moja, sanjari na timu za Ugiriki na Korea Kusini.
Nigeria, inayofundishwa na Kocha Lars Lagerback, iliwasili Afrika Kusini mapema wiki hii, ikiwa na kikosi cha wachezaji 23 tayari kwa maandalizi ya mwisho ya fainali hizo.
Mabingwa hao wa zamani wa Afrika, maarufu kwa jina la Super Eagles, wanatarajiwa kucheza mechi ya mwisho ya kujipima nguvu leo dhidi ya Korea Kaskazini.
“Swali sio ni jinsi gani tutapona kwa Argentina, bali ni jinsi gani wao watapona kwetu,”alisema nahodha huyo wa Nigeria kwenye kambi ya timu hiyo iliyopo mjini Durban.
“Hakuna anayeweza kufahamu nini kitatokea siku ya mchezo, lakini kila timu inayo nafasi ya kushinda. Tumejiandaa vyema na tupo tayari kukabiliana nao,”aliongeza mshambuliaji huyo, anayechezea klabu ya Portsmouth ya England.
Nigeria haijashinda mechi zake mbili ilizocheza ikiwa chini ya Kocha Lars, lakini hilo halimpi hofu mshambuliaji huyo, ambaye amejigamba kuwa, wamepania kuonyesha maajabu katika mechi ya ufunguzi.
Kikosi cha Nigeria kinaundwa na makipa: Dele Aiyenugba (Bnei Yehuda), Austin Ejide (Hapoel Petah Tikvah), Vincent Enyeama (Hapoel Tel Aviv).
Mabeki ni Dele Adeleye (Sparta Rotterdam), Rabiu Afolabi (Red Bull Salzburg), Elderson Echiejile (Stade Rennes), Chidi Odiah (CSKA Moscow), Danny Shittu (Bolton Wanderers), Taye Taiwo (Olympique Marseille), Joseph Yobo (Everton).
Viungo ni Yusuf Ayila (Dynamo Kiev), Dickson Etuhu (Fulham), Sani Kaita (Alania Vladikavhaz), Nwankwo Kanu (Portsmouth), Haruna Lukman (Monaco), John Obi Mikel (Chelsea), Kalu Uche (Almeria), John Utaka (Portsmouth).
Washambuliaji ni Yakubu Aiyegbeni (Everton), Obafemi Martins (VfL Wolfsburg), Obinna Nsofor (Malaga), Chinedu Obasi (Hoffenheim), Peter Odemwingie (Lokomotiv Moscow).
Wakati Nigeria ikijigamba kushinda mechi hiyo, Kocha Mkuu wa Argentina, Diego Maradona amesema wiki hii kuwa, bado hana hakika na kikosi chake cha kwanza kitakachocheza fainali za mwaka huu za Kombe la Dunia.
Kauli hiyo ya Maradona ilikuja siku 11 kabla ya Argentina kushuka dimbani kucheza mechi yake ya kwanza ya michuano hiyo dhidi ya Nigeria.
Maradona aliitisha mkutano wake wa kwanza na waandishi wa habari wiki hii mjini Johannesburg na kusema hatatangaza kikosi hicho hadi siku chache kabla ya kucheza na Nigeria.
Kocha huyo alisema kwa sasa bado anawatafutia nafasi kwenye kikosi hicho wachezaji wake wote nyota, wakiwemo Lionel Messi, Carlos Tevez, Gonzalo Higuain na Diego Milito.
“Itakuwa siku chache kabla ya mchezo wetu wa ufunguzi, nitaelewa nini la kufanya,”alisema Maradona. “Nina wachezaji 23 ambao wote uwezo wao ni mkubwa uwanjani.”
Maradona alisema kikosi chake cha sasa ni kizuri kuliko cha mwaka 1986, alichokiongoza kutwaa kombe hilo.
“Mwaka 1986 kulikuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu kikosi chetu. Lakini wachezaji tulionao sasa wapo kwenye kiwango cha juu kuliko wa mwaka 86 na wanaelewa mambo vizuri kuliko sisi tulivyokuwa,”alisema.
Kocha huyo alisema pia kuwa, ushindani wa wachezaji wakati wa mazoezi ni mkubwa kwa vile kila mchezaji anafanya kila analoweza ili apewe nafasi kwenye kikosi cha kwanza.
Naye mshambuliaji Carlos Tevez wa Argentina amesema, ameamua kupunguza uzito kwa kula zaidi matunda na mboga za majani kwa lengo la kujiweka.
“Nataka kufurahia fainali hizi za Kombe la Dunia,” alisema mshambuliaji huyo wa klabu ya Manchester City ya England.
Teves alisema amekodisha mtaalamu wa lishe kutokana na tatizo lake la kuongezeka uzito, ambalo hataki litokee wakati wa michuano hiyo.
“Napenda niwe mwanasoka halisi wa kulipwa katika fainali hizi, napaswa kuwajibika,”aliongeza.
“Nataka kucheza katika mechi ya kwanza dhidi ya Nigeria, lakini Lionel Messi na Higuan wapo kwenye kiwango cha juu. Tunao washambuliaji wazuri duniani, lakini tunapaswa kuonyesha hilo katika fainali za Kombe la Dunia,”alisema.

Kaka na Dada wanaotamba katika taarab


TANGU muziki wa taarab ulipoanza kupigwa hapa nchini, hasa katika visiwa vya Zanzibar, imewahi kutokea kwa baadhi ya vikundi kuwa na wasanii wa familia moja.
Imewahi kutokea kwa baadhi ya vikundi kama vile TOT mama kuimba na mwanawe, kama ilivyokuwa kwa Khadija Kopa na marehemu Omar Kopa.
Pia imetokea kwa mwimbaji Eshe Mashauzi wa Jahazi Modern Taarab kurekodi albamu kwa kushirikiana na mama yake, Rukia Juma, ambaye aliwahi kuimbia kundi la TOT.
Kiongozi wa Jahazi, Mzee Yusuph naye amewahi kuimba kundi moja na dada yake, Khadija Yussuf wakiwa East African Melody na Jahazi kabla ya kutengana na kila mmoja kuamua kuwa kivyakevyake.
Na sasa wapo waimbaji ndugu wawili, Omar Tego na Maua Tego, ambao ni waanzilishi na wamiliki wa kundi la Coast Modern Taarab, ambalo limetokea kuteka hisia za mashabiki wengi wa muziki huo kutokana na nyimbo zake nzuri.
Kundi la Coast lilianzishwa mwaka 1998. Wakati lilipoanzishwa, kundi hilo halikuweza kupata umaarufu kutokana na kutokuwa na waimbaji mahiri na wenye mvuto. Lilipiga muziki wake kwenye kumbi za vichochoroni.
Lakini hivi sasa, kundi hilo limepata umaarufu mkubwa kutokana na vibao vyake vitamu vinavyoimbwa na Maua na kaka yake, Omar. Vibao hivyo vimekuwa vikipigwa mara kwa mara kwenye vituo vya radio na televisheni hapa nchini.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti mjini Dar es Salaam hivi karibuni, ndugu hao walikiri kuwa, muziki huo umewawezesha kupata mafanikio makubwa.
Wakati kundi hilo lilipoanzishwa, Maua alianza kung’ara kwa vibao vyake vya ‘Kayaona mambo’ na ‘Full kujiachia’. Vibao hivyo ndivyo vilivyomsafishia nyota na kumfanya afahamike kwa mashabiki. Hata hivyo, Maua alikihama kikundi hicho siku miezi michache baadaye na kuhamia Zanzibar Stars. Alisema sababu kubwa iliyomfanya ahame ni kutafuta maslahi mazuri zaidi.
Pamoja na kujiunga na kundi hilo, hakufanikiwa kurekodi nalo wimbo wowote. Lakini anakiri kwamba, lilimwezesha kuongeza ujuzi zaidi wa muziki huo kutokana na kuundwa na wanamuziki kadhaa wakongwe.
Alirejea Coast mwaka 2004 akiwa ameiva kiusanii. Alitaja baadhi ya sababu zilizomfanya aondoke Zanzibar Stars kuwa ni pamoja na kukithiri kwa majungu na maslahi madogo.
"Ukubwa wa pua sio wingi wa makamasi. Ni kweli Zanzibar Stars ni kundi kubwa, lakini kwangu halikuwa na maslahi, nilinyimwa nafasi ya kurekodi nyimbo zangu ndio sababu nikaachana nalo,”alisema.
Mara baada ya kurejea Coast, aliibuka na kibao cha ‘Kuvuja kwa pakacha, nafuu ya mchukuzi’, ambacho kililiweka kundi hilo kwenye chati ya juu na kumfanya azidi kufahamika kwa mashabiki.
Kwa sasa, Maua anajiandaa kuachia kibao cha ‘Damu nzito’, ambacho atakiimba kwa kushirikiana na kaka yake, Omar. Pia anatarajia kuibuka na kibao kingine cha ‘Gubu la mawifi’.
Maua alisema yeye na kaka yake, Omar wanapenda na hawajawahi kugombana na ndio sababu wamemudu kufanyakazi pamoja kwa muda mrefu.
Mwanamama huyo mwenye watoto wawili, anavutiwa na waimbaji Mwanahawa Ally na Omar, ambaye pia ni maarufu kwa jina la Special One.
Naye Omar, ambaye ana uwezo wa kuimba, kupiga kinanda, gita la solo na kutunga nyimbo amesema albamu ya ‘I’m Crazy for you’, waliyeirekodi mwanzoni mwa mwaka 2004 ndiyo iliyowapa umaarufu zaidi.
"Kwa kweli baada ya kuachia albamu hiyo, mashabiki wengi walinikubali sana na ndio ilikuwa mwanzo wa jina langu kusikika kwenye masikio ya mashabiki wa muziki huu," anasema.
Hivi karibuni, aliachia albamu yake ya pili inayojulikana kwa jina la ‘Chongeni furniture, ambayo hadi sasa ipo kwenye chati ya juu katika muziki huo.
Mwanamuziki huyo, ambaye ni kipenzi cha mashabiki wengi, anasema amepiga hatua kubwa kupitia muziki huo na anaamini ataendelea ‘kutesa’ kwa kipindi kirefu.
Omar amekiri kuwa, muziki huo umemwezesha kujulikana sana hapa nchini na pia kunufaika kimaisha, tofauti na wakati alipoanza muziki huo miaka ya 1990. Kwa sasa, Omar amejenga nyumba na anamiliki gari la kutembelea.
“Nimetokea mbali sana, awali nilikuwa nikipiga muziki kule Temeke tu, lakini hivi sasa nafahamika karibu mikoa yote Tanzania na nina wapenzi wengi," anasema mwanamuziki huyo mwenye umbo la kuvutia.
Omar anavutiwa zaidi na uimbaji wa Eshe Mashauzi na Khadija Kopa.
0000

KAKA: Nipo tayari kuiongoza Brazil

JOHANNESBURG, Afrika Kusini
MSHAMBULIAJI Ricardo Kaka wa Brazil amesema, hana wasiwasi kuhusu afya yake na kusisitiza kuwa, yupo tayari kuchukua jukumu la kuwa kiongozi wa timu hiyo katika fainali za mwaka huu za Kombe la Dunia.
Kaka atashiriki katika fainali hizo akiwa mchezaji pekee nyota wa Brazil, lakini amekuwa akikabiliwa na maumivu ya mara kwa mara yanayotishia kiwango chake katika fainali hizo.
Hata hivyo, mshambuliaji huyo wa klabu ya Real Madrid ya Hispania anaamini kuwa, atakuwa katika hali nzuri wakati fainali za Kombe la Dunia zitakapoanza.
“Afya yangu inaimarika kila siku. Maumivu hayanisumbui tena. Nimekuwa nikifanya kila kitu kilichopangwa hadi sasa na hadi itakapofika siku ya mechi yetu ya ufunguzi, nitakuwa katika hali nzuri zaidi,”alisema. Maumivu, ambayo yamekuwa yakimkumba Kaka mara kwa mara, yalisababisha ashindwe kuonyesha kiwango chake katika klabu ya Real Madrid msimu huu.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa AC Milan ya Italia, alikuwa akikabiliwa na maumivu ya kifundo cha mguu na misuli, ambayo yalisababisha awe benchi kwa siku 45.
Madaktari wa Brazil wamesema, maumivu ya kifundo cha mguu kwa sasa si tatizo tena kwa mchezaji huyo na kwamba maumivu ya paja hayawezi kumfanya kumfanya asiwemo kwenye kikosi cha kwanza katika mechi ya ufunguzi dhidi ya Korea Kaskazini, itakayochezwa Juni 15 mwaka huu.
Kaka amekuwa akifanya mazoezi ya pamoja na wachezaji wenzake wa Brazil tangu timu hiyo ilipowasili Afrika Kusini, Mei 27 mwaka huu, lakini amekuwa akiendelea kupatiwa matibabu wakati wachezaji wenzake wanapokuwa mapumziko.
Mchezaji huyo alicheza kwa dakika 45 siku Brazil ilipoichapa Zimbabwe mabao 3-0 katika mechi ya kirafiki ya kimataifa iliyochezwa Jumatano iliyopita.
Kutokuwemo kwa wachezaji Ronaldinho Gaucho, Ronaldo de Lima, Roberto Carlos na Adriano kunayafanya macho yote ya Wabrazil yawe kwa Kaka.

Wamarekani wampania Rooney


LOS ANGELES, Marekani
BEKI wa zamani wa kimataifa wa Marekani, Alexi Lalas amewataka wachezaji wa timu hiyo kuhakikisha wanammaliza mapema mshambuliaji Wayne Rooney wa England katika mechi ya ufunguzi ya Kombe la Dunia kati yao, itakayochezwa Juni 12 mwaka huu.
Alexi alisema juzi mjini hapa kuwa, wanapaswa kuhakikisha Rooney anaonyeshwa kadi nyekundu katika mechi hiyo ili kufifisha matumaini ya England katika fainali hizo.
Beki huyo wa zamani wa Marekani alisema, anaamini hasira za Rooney zinaweza kuigharimu England katika fainali hizo.
“Hakuna ubaya kutumia udhaifu wa mchezaji kumsababishia matatizo uwanjani,”alisema mkongwe huyo, aliyekuwemo kwenye kikosi cha Marekani kilichoifunga England mwaka 1993.
“Ni mwepesi wa kupandwa na hasira, ningependa kumuona akifanya vitendo uwanjani kama mtoto mdogo,”alisema.
Alexi aliiponda England kwa kujiona kuwa ni timu bora kuliko zingine zilizopangwa kwenye kundi C.
“Nafikiri wanayo timu nzuri, lakini inawezekana si timu nzuri kama wanavyofikiria wao,”alisema.
Wakati huo huo, mshambuliaji nyota wa Argentina, Lionel Messi amekiri kuwa, Wayne Rooney ndiye tegemeo kubwa la England katika fainali za Kombe la Dunia.
Messi alilieleza gazeti la The Sun juzi kuwa, kwa kushirikiana na Steven Gerrard na Frank Lampard, Rooney anaweza kuiongoza England kufanya maajabu katika fainali hizo.
“Nafikiri Rooney ni mchezaji mzuri, si tu kwa yale aliyoyafanya mwaka huu,”alisema.
“Kwa miaka mingi sasa, amekuwa akionyesha kwamba ni mmoja wa wachezaji nyota wa kizazi chake na kadri miaka inavyosonga mbele, kiwango chake kimekuwa kikizidi kupanda,”aliongeza.
Messi alisema Rooney ni mchezaji aliyekamilika, ana uwezo mkubwa wa kukaa na mpira miguuni, ana nguvu na uwezo wa kufunga mabao.

Babu Chuchu afariki

ALIYEKUWA mmiliki wa bendi ya muziki wa dansi ya Chuchu Sound, Yusuf Ahmed Alley, maarufu kwa jina la ‘Babu Chuchu’ amefariki dunia.
Habari zilizopatikana mjini Dar es Salaam jana zilisema kuwa, Babu Chuchu alifia mjini Nairobi, Kenya nyakati za asubuhi, ambako alikwenda kikazi.
Kwa mujibu wa habari hizo, mwili wa marehemu ulirejeshwa Zanzibar jana na mazishi yalifanyika jana kwenye makaburi ya Mwanakwerekwe.
Hata hivyo, hakuna taarifa zilizotolewa kuhusu sababu za kifo chake, ambacho kimepokelewa kwa mshtuko mkubwa na mashabiki wa muziki nchini.
Taarifa za kifo cha Babu Chuchu zilianza kutangazwa jana asubuhi kupitia kwenye vituo mbalimbali vya radio.
Babu Chuchu atakumbukwa kwa uhodari wake katika muziki, ulioiwezesha bendi yake ya Chuchu Sound kupata umaarufu mkubwa kabla ya kusambaratika.
Umaarufu wa Babu Chuchu ulitokana na chombezo zake kwenye nyimbo za bendi hiyo, hapa alipokuwa akijibizana maneno na mwimbaji Omari Mkali.
Babu Chuchu pia alikuwa mmoja wa wajumbe wa bodi ya tamasha la kila mwaka la Sauti za Busara. Pia alikuwa akimiliki studio yake binafsi ya kurekodi muziki na kituo cha radio.

Yanga sasa vurugu tupu

WAKATI mkutano mkuu wa wanachama wa klabu ya Yanga wa kujadili marekebisho ya katiba unafanyika leo, hali ndani ya klabu hiyo si shwari.
Hilo lilidhihirika jana baada ya Mwenyekiti wa klabu hiyo, Iman Madega na mfadhili mkuu, Yusuf Manji kutoa taarifa zinazopingana kuhusu mkutano huo na mustakabali wa Yanga.
Mkutano huo umepangwa kufanyika leo kwenye ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa Polisi uliopo Oysterbay mjini Dar es Salaam.
Katika taarifa yake aliyoitoa kwa wanachama wa Yanga kuhusu mkutano huo, Manji ameutaka uongozi uliopo madarakani kukabidhi madaraka yake kwa Baraza la Wadhamini mara baada ya kufanyika kwa marekebisho hayo.
Mfadhili huyo alisema kamati ya utendaji ya Yanga, iliyo chini ya uenyekiti wa Madega, haina uhalali wa kusimamia mkutano huo kwa vile ilishamaliza muda wake tangu Mei 30 mwaka huu na hakuna ridhaa ya wanachama inayoiruhusu kuendelea kuwepo madarakani.
Manji alisema ni vyema kamati hiyo ijiuzulu na kukabidhi madaraka yake kwa Baraza la Wadhamini, ambalo ndilo linalopaswa kuitisha na kusimamia uchaguzi mkuu wa klabu hiyo. Baraza hilo linaundwa na Mama Fatuma Karume na Manji.
“Kwa mujibu wa katiba iliyorekebishwa mwaka 2008, muundo mpya wa uongozi kwa maana ya kamati ya utendaji na sekretarieti wenye kipindi cha miaka minne, utaanza mara tu baada ya uongozi uliopo, ambao uliingia madarakani kwa katiba ya mwaka 2007 kumaliza kipindi chake. Kipindi cha kamati ya Madega na miaka mitatu na si minne,” amesema.
Manji ameutaka uongozi wa Madega kutangaza tarehe ya uchaguzi kabla ya kuingia kwenye mkutano wa leo na ameshauri uchaguzi huo ufanyike Juni 27 mwaka huu.
Mfadhili huyo pia amewataka wanachama wa Yanga kuvifanyia marekebisho vipengele vyote vya katiba vinavyoonekana kuwa na utata badala ya vile vilivyoelekezwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Manji alisema amebaini kuwepo kwa mbinu za kijanja za kupenyeza marekebisho ya katiba yenye mwelekeo wa kuwanufaisha watu wachache ndani ya Yanga, jambo ambalo alidai kuwa ni la hatari.
Alivitaja baadhi ya vipengele alivyodai kuwa, vimefanyiwa marekebisho kinyemela kuwa ni pamoja na ibara ya 22 (2), ili idadi ya wanachama inayohitajika kuitisha mkutano wa dharula iongezeke kutoka nusu hadi theluthi mbili.
Alikitaja kipengele kingine, alichodai kimenyofolewa kwa makusudi kuwa ni ibara ya 29 (4), ambacho madhara yake ni kuruhusu uongozi uliomaliza muda wake uendelee kuwa madarakani kwa mwaka mmoja zaidi hadi 2011.
Vipengele vingine, ambavyo Manji amedai vilifanyiwa marekebisho kinyemela ni ibara ya 57 (5) inayohusu majukumu ya kampuni ya umma na ibara ya 62 (h), inayohusu wajibu wa Baraza la Wadhamini.
“Narudia kushauri kwamba,marekebisho yale tu, ambayo ni lazima kwa mujibu wa maelekezo ya TFF ndio yafanyike Jumapili na mengine yasubiri mpaka Yanga itakapofanya uchaguzi na viongozi wapya kuingia madarakani,” ameeleza.
Manji pia ameutaka uongozi wa Madega kuiachia Kamati ya Uchaguzi chini ya Jaji Mkwawa, jukumu la kusimamia uchaguzi mkuu bila kuiingilia ili iweze kufanyakazi yake kwa uhuru na haki.
Hata hivyo, uchunguzi wa MZALENDO umebaini kuwa, marekebisho ya vipengele hivyo yalitolewa na TFF katika barua yake ya Desemba 18, 2009 iliyotumwa kwa uongozi wa Yanga.
Katika barua hiyo yenye kumbukumbu namba TFF/TECH/LEP 09/045, shirikisho hilo liliutaka uongozi wa Yanga kuvifanyia marekebisho vifungu 24 vya katiba yake vilivyobainika kuwa na mapungufu.
Barua hiyo pia iliutaka uongozi wa Yanga kuweka kwenye katiba yake muda wa uongozi wa kipindi cha miaka minne, sifa za wagombea na viongozi watatu wa kuajiriwa.
Akizungumzia taarifa hiyo ya Manji kwa waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, Madega alimshutumu mfadhili huyo na kumwelezea kuwa ni mchochezi, anayetaka kuleta vurugu ndani ya Yanga.
Madega alisema amegundua Manji amekuwa akichochea kuwepo kwa hali ya vurugu ndani ya klabu hiyo, kutokana na kutoa taarifa katika vyombo vya habari Juni 4, mwaka huu.
Ameonya kuwa, endapo zitatokea vurugu wakati wa mkutano huo, Manji anapaswa kuwa muhusika mkuu na kusisitiza kuwa, si kweli kwamba uongozi wake unang’ang’ania kuwepo madarakani kwa vile walishapendekeza uchaguzi mkuu ufanyike Januari 3 mwaka huu kabla ya kusimamishwa na TFF.
Mwenyekiti huyo amewaomba wanachama wa Yanga kujitokeza kwa wingi kwenye mkutano huo ili wapate nafasi ya kuijadili na kuipitisha katiba mpya ya klabu hiyo kabla haijasajiliwa na Msajili wa Vyama na Klabu za Michezo nchini.
Alipoulizwa sababu za kutokuelewana kwake na Manji, Mwenyekiti huyo alisema, ni kutokana na mfadhili huyo kuweka mbele zaidi maslahi yake binafsi kuliko ya klabu.
Akito mfano, alisema haoni kwa nini mfadhili huyo anashinikiza kamati ya utendaji ya Yanga iwe na wajumbe sana na ipewe madaraka ya kumchagua mwenyekiti wa klabu badala ya jukumu hilo kufanywa na mkutano mkuu.
Madega alisema pia kuwa, Manji anataka kipengele kinachohusu utaratibu wa kumchagua mwenyekiti na makamu wake kifutwe kwenye katiba, jambo ambalo alisema haliwezekani kutokana na mfumo wa TFF na Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA).
“Nina imani wanachama wa Yanga watakuwa watulivu wakati wa mkutano huo na sisi kama viongozi, tumechukua hatua zote kuhakikisha usalama unakuwepo,”alisema.
Wakati huo huo, Manji amesema ametoa pesa kwa ajili ya kuwalipia ada ya uanachama wanachama wote 7,155 wa Yanga kwa kipindi cha miaka miwili.
Manji alisema jana kuwa, wanachama hao ni wale waliokuwa hai kuanzia Juni Mosi mwaka huu, siku ambayo alitangaza kuwalipia tiketi wanachama wa Yanga kwa ajili ya kushuhudia pambano la kirafiki la kimataifa kati ya timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars na Brazil, litakalochezwa kesho.

Thursday, June 3, 2010

Chuji, Tegete, Kigi kuondoka Yanga

WACHEZAJI watatu nyota wa klabu ya Yanga wamepata nafasi ya kwenda kucheza soka ya kulipwa nje ya nchi.
Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako alithibitisha jana kuhitajiwa kwa wachezaji hao nchini Sweden na Afrika Kusini.
Aliwataja wachezaji hao kuwa ni kiungo Athumani Iddi ‘Chuji’ na washambuliaji Jerryson Tegete na Kigi Makasi.
Kwa mujibu wa Mwalusako, Tegete na Chuji wanatakiwa na klabu moja ya Sweden wakati Kigi
anatakiwa na klabu ya Afrika Kusini. Hakuzitaja klabu hizo.
Tegete aliwahi kwenda kufanya majaribio ya kucheza soka ya kulipwa katika klabu ya FK Dalkurd ya Sweden na kufuzu, lakini alishindwa kuingia nayo mkataba kutokana na kuwekewa ngumu na uongozi wa Yanga.
Katika hatua nyingine, klabu za Simba na Azam zimeanza kupigana vikumbo kumwania mshambuliaji wa timu ya mkoa wa Ilala, Marcel Kaeza.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 18, aliwavutia viongozi wa klabu hizo wakati wa michuano ya Kombe la Taifa, iliyomalizika mwishoni mwa wiki iliyopita mjini Dar es Salaam.
Ilala ilikuwa ikinolewa na Kocha Jamhuri Kihwelo, maarufu kwa jina la Julio, ambaye naye imedaiwa anamfanyia mipango mchezaji huyo kwenda kucheza soka ya kulipwa Qatar.