KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, April 21, 2013

TASWA YAAHIDIWA MAKUBWA NA AIPS




CHAMA cha Kimataifa cha Waandishi wa Habari za Michezo (AIPS),
kimeahidi kusaidia masuala mbalimbali yahusiyo mafunzo kwa
waandishi wa habari za michezo wa Tanzania.

Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi za Michezo Tanzania (TASWA), Juma
Pinto amesema kwamba rais wa AIPS, Gianni Merlo raia wa Italia
aliwapa fursa viongozi wa vyama vya waandishi wa habari za michezo
wa Afrika kuwasilisha changamoto mbalimbali zinazovikabili vyama
vyao, lakini kati ya hizo changamoto waitaje moja ambayo wanataka
AIPS isaidie kuwapa msaada.

Pinto amesema anashukuru Merlo kwanza alivutiwa sana na namna TASWA
inavyofanya kazi zake na ushiriki wake wa mikutano ya Dunia mara
kwa mara, hali ambayo aliahidi yeye binafsi kusaidia chama chetu
kuboresha masuala ya kimsingi.

Amesema kubwa ambalo AIPS baada ya kuelezwa imesema italipangia
utaratibu ni suala la mafunzo kwa waandishi wa habari chipukizi na
wanawake kwani hayo ni baadhi ya mambo ambayo wenyewe wanayatilia
mkazo na hasa baada ya kujulishwa kuwa kuna wanahabari zaidi ya 50
wanawake hapa nchini wanaofanya kazi kwenye masuala ya michezo.

Hata hivyo, Pinto amesema ingawa TASWA iliomba isaidiwe mafunzo kwa
wanachama wake wote kwa kupatiwa wataalamu hasa wakati huu ambao
kuna changamoto kubwa ya teknolojia ya habari na mawasiliano,
lakini AIPS imesema kwa mwaka huu uwezo wake ni kwa waandishi wa
habari za michezo chipukizi kupitia programu inayoandaliwa na AIPS.

Lakini Rais wa AIPS aliutaka ujumbe wa Tanzania utakapokuwa umerudi
nyumbani umuandalie mikakati hiyo kwa mafunzo ya wanawake ili
ikiwekezekana yafanyike kwa awamu katika kipindi cha miezi 18
kutegemea na idadi ya wahusika na pia gharama zenyewe.

Nchi wanachama 103 duniani zikiwemo nchi 24 za Afrika zilihudhuria
mkutano huo uliomalizika juzi Sochi, Urusi, ambapo pia ulifanyika
uchaguzi wa viongozi wa AIPS watakaokuwa madarakani kwa miaka minne
ijayo, ambapo Merlo alipita bila kupingwa.

Mkutano Mkuu wa AIPS ambao ni wa 76 ulimalizika juzi, ambapo
kulikuwa na kikao cha makatibu wakuu wa kila nchi kilichoendeshwa
na Katibu Mkuu wa AIPS, Roslyn Morris ambapo Tanzania iliwakilishwa
na Katibu Mkuu wa TASWA, Amir Mhando na huko pia suala la tuzo
mbalimbali zinazotolewa na wanahabari zilizungumzwa kwa kina.

Pia kulifanyika kikao cha marais wa AIPS wa mabara na baadhi ya
viongozi wa vyama vya wanahabari wa michezo wa Afrika kilichokuwa
chini ya Merlo, ambapo Mwenyekiti wa TASWA, Pinto alidhuria na
ajenda kubwa ilikuwa suala la rushwa kwenye michezo na mambo ya
upangaji wa matokeo wa mechi mbalimbali.

Baada ya mkutano huo, wakati ujumbe wa Tanzania ukiwa njiani
kurejea nyumbani ulipitia jijini Moscow, Urusi na kuzungumza
masuala mbalimbali na Balozi wa Tanzania nchini Urusi, Jaka Mwambi.

“Kwa ujumla mkutano ulikuwa na manufaa makubwa kwa Tanzania na
Afrika kwa ujumla, ambapo masuala mengine mengi yaliyojitokeza
kwenye mkutano huo ikiwemo namna ya mafunzo hayo yatakavyofanyika
tutayazungumza Jumatano ijayo kwenye mkutano na wanahabari
utakaofanyika ukumbi wa City Sports Lounge, Dar es Salaam saa tano
asubuhi,”alisema Pinto.

TASWA ni mwanachama hai wa AIPS yenye makao yake makuu Lausanne,
Uswisi, ndiyo sababu kila mwaka tumekuwa tukishiriki mikutano hiyo
tangu tulipoingia madarakani mwaka 2010.

Mwaka 2011 tulishiriki Mkutano Mkuu wa AIPS uliofanyika Seoul
Korea, Korea Kusini na tuliwakilishwa na Makamu Mwenyekiti, Maulid
Kitenge na Katibu Msaidizi, George John. Pia ilishiriki Mkutano Mkuu wa AIPS uliofanyika Innsbruck, Austria Januari mwaka jana, ambako Katibu Mkuu, Amir Mhando alihudhuria.

No comments:

Post a Comment