'
Thursday, April 25, 2013
YANGA: UBINGWA HAUNA RAHA BILA KUMUUA MNYAMA
MAKAMU Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, Clement Sanga amesema japokuwa timu yake inayo nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya Tanzania Bara msimu huu, hautakuwa na raha bila kuwafunga watani wao wa jadi Simba.
Akizungumza mjini Dar es Salaam wiki hii, Sanga alisema watakuwa na raha ya kuwa mabingwa wa Bara iwapo wataifunga Simba katika mechi yao ya mwisho.
Simba na Yanga zinatarajiwa kushuka dimbani Mei 18 mwaka huu katika moja ya mechi saba za mwisho za ligi hiyo itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika mechi ya kwanza iliyochezwa Oktoba 3 mwaka jana kwenye uwanja huo, timu hizo zilishindwa kutambiana baada ya kutoka sare ya bao 1-1.
Yanga huenda ikatawazwa kuwa mabingwa wapya wa ligi iwapo itaishinda Coastal Union katika mechi itakayopigwa Mei Mosi mwaka huu.
Yanga inaongoza ligi hiyo kwa kuwa na pointi 56 baada ya kucheza mechi 24, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 47 na Kagera Sugar yenye pointi 40.
Iwapo Yanga itatoka sare ama kuishinda Coastal, itatwaa ubingwa kabla ya ligi kumalizika na pambano lake dhidi ya Simba litakuwa la kukamilisha ratiba.
"Ni kweli nafasi ya Yanga kutwaa ubingwa ni kubwa kwa vile tunahitaji pointi moja tu katika mechi yetu na Coastal Union. Ni kama vile tumeshatwaa ubingwa,"alisema Sanga.
"Lakini sintakuwana na raha hadi pale tutakapotoa kipigo kwa wapinzani wetu Simba. Lazima tuwafunge, tena kwa idadi kubwa ya mabao,"aliongeza.
Sanga alisema wamejipanga vyema kuhakikisha kuwa, wanashinda mechi zote mbili zilizosalia ili kuufanya ubingwa huo uwe na ladha iliyokamilika.
Kwa mujibu wa Sanga, wamepania kuishinda Simba kwa idadi kubwa ya mabao kwa lengo la kulipa kisasi cha kufungwa mabao 5-0 katika ligi ya msimu wa 2011/2012.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment