KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, April 4, 2013

AMRI IBRAHIM, MKONGWE WA SOKA ANAYEWASIKITIKIA VIONGOZI WA MCHEZO HUO

UTAKAPOKUTANA na Amri Ibrahim njiani, siyo rahisi kuamini kwamba ndiye yule kiungo na mshambuliaji aliyeng'ara katika timu za Pamba ya Mwanza, timu ya mkoa huo, Mwanza Heroes na Simba.

Kwa sasa ni mtu mzima. Umri wake ni miaka 57. Mwili wake ni mwembamba na wakati mwingine anapotembea, anaonekana kama vile anapepesuka. Uvaaji wake ni wa kawaida. Anapenda zaidi kuvaa nguo za michezo.

Kinachofurahisha ni kwamba, Amri ni mcheshi kwa mtu yeyote anayeonyesha dalili za kumfahamu. Si mtu wa kujikweza na kupenda kujionyesha, hata kama hoja inayozungumzwa na kujadiliwa mbele yake anaifahamu au inamuhusu.

Kumtafuta Amri katika mji wa Morogoro haikuwa kazi ngumu. Anapatikana zaidi kwenye ofisi za Chama cha Soka cha mkoa wa Morogoro (MRFA). Hapo ndipo kilipo kijiwe cha wanasoka wa zamani wa timu za mji huo uliozungukwa na milima mingi ya mawe.

Siku nilipokutana naye na kumweleza madhumuni ya safari yangu katika mji wa Morogoro, hakuonekana kushtuka. Tukakubaliana tukutane siku inayofuata kwenye mgahawa mmoja uliopo nje ya Uwanja wa Jamhuri wa Morogoro.

Nilichoweza kugundua ni kwamba, bado Amri anaendelea kujihusisha na mchezo wa soka, akiwa kocha. Awali, alipendelea zaidi kuwafundisha vijana wadogo wa mkoa huo, lakini baadaye aliamua kuifundisha timu ya Rhino FC ya Lindi kabla ya kujiuzulu baada ya timu hiyo kuvurunda katika michuano ya ligi daraja la kwanza Tanzania Bara msimu huu.

Kama ilivyo kwa wanasoka wengi wa zamani, Amri hafurahishwi na mwenendo wa soka ulivyo hivi sasa hapa nchini. Kwa mtazamo wake, soka ya Tanzania ni sawa na mtoto aliyesimama dede. Yaani anaweza kuinuka na kusimama, lakini hawezi kutembea.

"Miaka ya nyuma, kiwango chetu cha soka kilikuwa kikubwa. Timu yetu ya taifa (Taifa Stars), ilifuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 1980 na tulitoa wachezaji wawili katika timu ya Afrika miaka ya 1970. Pia tulizitambia timu kutoka Ghana, Nigeria na Congo," alisema Amri.

Alizitaja baadhi ya sababu za kushuka kwa kiwango cha soka nchini kuwa ni pamoja na klabu na vyama vya michezo kuongozwa na watu, ambao hawana taaluma ya michezo. Aliwaita watu hao kuwa ni wavamizi wa uongozi wa michezo.

"Mtu asiye na taaluma ya michezo, asiruhusiwe kugombea uongozi. Hawa wanaharibu michezo na wanachangia migogoro. Yule anayeujua vyema mchezo wa soka, ndiye anayepaswa kupewa uongozi na yule anayeupenda mchezo huo, abaki kuwa mpenzi," alisema mwanasoka huyo mkongwe.

"Kama mtu hawezi kutongoza mwanamke yeye mwenyewe, anamtuma mwenzake kumtongozea, hayo si mapenzi. Kwa hiyo, kama huna kauli nzuri kwa wachezaji ya kuwashawishi wacheze vizuri, huwezi kufanya hivyo,"aliongeza.

Amri aliishutumu tabia ya baadhi ya viongozi wa klabu za soka na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutowashirikisha wanasoka wa zamani katika kutoa mchango wa mawazo yanayoweza kusaidia kuinua kiwango cha mchezo huo nchini.

Alisema iwapo wanasoka wa zamani, hasa waliowahi kuichezea Taifa Stars watakutanishwa mara kwa mara na kuombwa kuchangia mawazo juu ya kuinua kiwango cha mchezo huo, upo uwezekano mkubwa wa kupatikana kwa kiini cha matatizo yaliyopo sasa na hatua zinazopaswa kuchukuliwa.

Kiungo huyo wa zamani wa Pamba na Simba alilitaja tatizo lingine linalochangia kudidimia kwa maendeleo ya mchezo huo kuwa ni kutokuwepo kwa utaratibu wa kuwaandaa vijana kucheza soka tangu wakiwa wadogo.

Hata hivyo, aliipongeza TFF kwa kuanzisha michuano ya Copa Coca Cola, inayozishirikisha timu za mikoa za vijana wa umri wa chini ya miaka 17 na ile ya Kombe la Uhai, ambayo inazishirikisha timu za vijana wa chini ya umri wa miaka 20.

Aliitaja sababu nyingine ya kudidimia kwa maendeleo ya soka nchini kuwa ni kuzuka kwa migogoro ya mara kwa mara katika klabu kongwe, hasa Simba na Yanga. Alisema chanzo kikubwa cha migogoro hiyo ni ulaji wa pesa kwa vile wanachama wengi wanaopata nafasi ya kuziongoza, wamekuwa wakiweka mbele zaidi maslahi yao binafsi.

"Nadhani wakati umefika kwa serikali kutengeneza sera, iende Bungeni ili iidhinishwe na kuifanya soka ya Tanzania iwe ya kulipwa. Sera hiyo ikipitishwa, nina hakika Simba na Yanga zitakoma. Kama serikali inaweza kutunga sheria kuhusu mambo mengine, sioni kwa nini isitunge sheria ya kuigeuza soka yetu kuwa ya kulipwa,"alisema.

Amri pia aliilaumu tabia ya makocha wenye taaluma ya kufundisha soka kuwadharau wanasoka wa zamani, waliojitolea kutoa mafunzo kwa vijana kwa lengo la kuwaendeleza.

"Kuna tabia kwa baadhi ya makocha waliosomea fani hiyo, kuwadharau wale, ambao hawakusoma, lakini wanasahau kwamba, ndio waliovumbua vipaji vya vijana na kuwaendeleza,"alisema.

"Hawa wenzetu waliosomea ukocha wa soka, wanasubiri kuitwa kufundisha timu za Simba, Yanga na Taifa Stars, hawataki kuja chini. Huku ndiko kugumu. Wanawadharau wale wanaojitolea kufundisha vijana wakati wao wanashindwa kutumia taaluma yao kufanya hivyo. Kisingizio chao siku zote ni kwamba wanazo kazi nyingi. Lakini wanapoitwa kuzifundisha Simba na Yanga, wanapata muda wa kufanyakazi hiyo,"alisema.

Amri alisema Tanzania inayo hazina ya makocha wazuri wenye uwezo wa kufundisha soka, lakini wanakosa nyenzo na pia wamekuwa wakidharauliwa, badala yake makocha wa kigeni ndio wamekuwa wakiaminiwa zaidi na kuthaminiwa.

"Wanachokosa makocha wetu wa kizalendo ni nyenzo.Leo hii akija kocha wa kigeni na kusema anataka mipira 30 na jozi 30 za raba na jozi 30 za viatu vya kuchezea soka, ataletewa mara moja. Lakini kocha mzalendo akiomba apatiwe vifaa hivyo, ataonekana kama vile chizi,"alisema kocha huyo.

"Lakini akija kocha wa nje na kutaka alipwe mshahara wa shilingi milioni tatu kwa mwezi, atapatiwa mara moja. Kocha mzalendo akiomba alipwe mshahara wa shilingi laki tatu kwa mwezi, atanyimwa na kama kulipwa, atalipwa kwa mafungu,"alisema.

Amri alisema kazi ya kufundisha soka ni ngumu, hivyo makocha wanapaswa kuthaminiwa na kuheshimiwa ili waweze kutimiza vyema majukumu yao.

Mwanasoka huyo mkongwe pia alitoa ushauri wa kuwepo na utaratibu wa pande muhimu katika uongozi wa klabu, kuheshimu nafasi za wenzao.

Itaendelea Alhamisi ijayo

No comments:

Post a Comment