KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Saturday, April 13, 2013

AMRI IBRAHIM, MKONGWE WA SOKA ANAYEWASIKITIKIA VIONGOZI WA SASA WA MCHEZO HUO




WIKI iliyopita, mwanasoka mkongwe nchini, Amri Ibrahim alielezea mambo mbalimbali yanayomkera katika uendeshaji wa mchezo huo hivi sasa hapa nchini na kupendekeza hatua mbalimbali zinazofaa kuchukuliwa na kuinua kiwango cha soka. Katika sehemu hii ya pili na ya mwisho, mkongwe huyo anaelezea historia yake na matukio mbalimbali anayoyakumbuka.


Amri alisema kama klabu inaye mfadhili, anapaswa kuheshimu nafasi za viongozi na makocha, vivyo hivyo vongozi, ambao alisema nao wanapaswa kuheshimu nafasi za wafadhili na makocha.

Aliipongeza TFF kwa hatua, ambazo imekuwa ikichukua kukomesha vitendo vya vurugu kwenye viwanja vya soka kwa kuwaadhibu wachezaji, waamuzi na viongozi wanaohusika kuchochea vitendo hivyo.

"Nidhamu ni muhimu sana katika soka, na ilikuwa imeshuka sana katika miaka ya nyuma. Mashabiki walifikia hatua ya kuweka mikojo kwenye chupa za maji na kuwarushi waamuzi na wachezaji uwanjani. Huu ulikuwa uhuni," alisema kiungo huyo wa zamani wa Pamba na Simba.

Aliitaka TFF kuweka wazi programu zake za kuendesha soka nchini ili wadau wa mchezo huo waweze kuzisoma, kuzielewa na kuchangia mawazo yao. Alisema ni vyema programu hizo ziwe zikisambazwa katika vyama vya soka vya wilaya ya mikoa yote nchini.

Amri alizaliwa 1959 kijiji cha Gungu kilichopo Kigoma Mjini. Alisoma elimu ya msingi mkoani Kigoma na katika mikoa ya Mwanza na Mara.

Alianza kucheza soka tangu alipokuwa mdogo kwa kutumia chandimu. Alichezea timu za mitaani na za shule alizosoma kabla ya kujiunga na Gungu Heroes na baadaye Lake Stars.

Alianza kupata umaarufu kisoka 1973 alipokuwa akichezea Lake Stars katika michuano ya kuwania ubingwa wa wilaya na mkoa. Timu hiyo ilifanikiwa kucheza fainali ya ubingwa wa Taifa na kufungwa mabao 2-0 na Simba.

Amri alijiunga na Pamba ya Shinyanga 1975 na kuichezea kwa muda mfupi kabla ya kuhamishiwa Pamba ya Mwanza. Aliichezea Pamba ya Mwanza kwa mara ya kwanza ilipomenyana na Luo Union ya Kenya katika mechi ya kirafiki iliyochezwa kwenye uwanja wa Nyamagana na kuibuka na ushindi wa bao 1-0.

Katika mechi hiyo, Amri aliingizwa uwanjani kipindi cha pili na kutoa pasi kwa Ibrahim Posi, aliyefunga bao hilo na pekee na la ushindi kwa kichwa.

Wakati Amri alipojiunga na Pamba ya Mwanza, kikosi cha timu hiyo kilikuwa kinaundwa na baadhi ya wachezaji waliokuwa nyota wakati huo kama vile Joram Mwakatika, Tabu Mwakatika, Titus Bandawe, Khalid Bitebo, Hamisi Bilali, James Ng'ong'a na Makinga Shabani.

Mechi ya pili ya kimataifa kwa Amri kuichezea Pamba ilikuwa dhidi ya Galacia ya Brazil. Mechi hiyo pia ilichezwa kwenye uwanja wa Nyamagana na Pamba ilichapwa mabao 2-1.

Amri amemwelezea mwenyekiti wa zamani wa Pamba, marehemu Shabani Mwakayugwa kuwa alichangia kwa kiasi kikubwa kuinua maendeleo ya soka mkoani Mwanza kutokana na kuzialika timu mbalimbali za kigeni kucheza na Pamba.

Amri alihamishiwa mkoa wa Mara kikazi 1976, ambako alijiunga na Mara Stars. Timu hiyo ilikuwa ikiongozwa na Suleiman Kigera.

Mwaka uliofuata, alirejeshwa Mwanza na kuitwa katika timu ya Taifa, Taifa Stars ilipokuwa ikijiandaa kwenda Malawi kucheza na timu ya taifa ya nchi hiyo katika mechi ya michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Afrika.

Hata hivyo, Amri hakuweza kusafiri na timu hiyo kwenda Malawi kutokana na kuumia mguu. Alisikitika kwa kupoteza nafasi hiyo, ambayo alisema kwa kawaida huwa ni ndoto ya kila mwanasoka katika maisha yake.

Baada ya kuzidi kung'ara katika kikosi cha Pamba, hatimaye Amri alinaswa na klabu ya Simba 1980. Binafsi anakiri kwamba, alikuwa na mapenzi na klabu hiyo tangu akiwa mdogo, hivyo ilipomuhitaji, hakujiuliza mara mbili.

"Viongozi wa Simba waliniona nina uwezo, maana wakati huo nilikuwa natisha katika namba zote mbili za kiungo na ushambuliaji. Nilikuwa na uwezo wa kucheza namba sita, nane, saba hadi 11,"alisema Amri, ambaye kwa kawaida ni mcheshi.

Mechi ya kwanza kuichezea Simba ilikuwa ya kirafiki dhidi ya Power Dynamos ya Russia. Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Simba ilichapwa mabao 3-2.

Wakati alipojiunga na Simba, kikosi cha timu hiyo kilikuwa kikiundwa na wachezaji tishio kama vile marehemu Jumanne Hassan 'Masimenti', marehemu Adam Sabu, Thuweni Ally, marehemu Athumani Mambosasa, George Kulagwa, Rahim Rumelezi, Nico Njohole, Abbas Kuka.

Amri alikuwa mmoja wa wachezaji walioiwezesha Simba kutwaa ubingwa wa Bra 1984. Alisema katika kipindi cha miaka saba alichoichezea Simba, mwaka huo pekee ndio ambao hakukuwepo migogoro ya uongozi.

"Niliichezea Simba katika kipindi ambacho ilikuwa ikikabiliwa na migogoro mingi. Mgogoro wa kwanza mkubwa ulizuka 1980 wakati huo, mwenyekiti alikuwa, marehemu Alfred Sanga. Baadaye akaingia David Ngonya. Mgogoro mkubwa zaidi ulizuka 1985 na kusababisha timu isambaratike,"alisema.

Anaikumba zaidi mechi ya ligi kati ya Simba na Yana iliyochezwa 1985 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ambapo timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1. Kinachomfanya aikumbuke mechi hiyo ni wachezaji wa timu zote mbili kucheza kwa kukamiana.

Kwa mujibu wa Amri, katika mechi hiyo, kipa Hamisi Kinye wa Yanga aliwachezea rafu mbaya washambuliaji Zamoyoni Mogella na Zuberi Magowa wa Simba na kuwasababishia maumivu makubwa.

Amri aliwahi kuwa kocha wa timu ya daraja la tatu ya Rhino ya Morogoro, ambayo aliiwezesha kufuzu kucheza ligi daraja la pili ngazi ya kanda.

Hata hivyo, aliamua kuacha kuifundisha timu hiyo kwa kile alichodai kuwa, kukatishwa tamaa na mfumo mpya wa ligi uliotangazwa na TFF, ambapo ligi za soka zitaanza kuchezwa katika ngazi ya wilaya, mkoa na Taifa.

"Nilikata tamaa. Niliiwezesha Rhino kupanda hadi daraja la pili ngazi ya taifa, lakini baada ya kutangazwa kwa mfumo huo, nimeona jitihada zangu ni sawa na kazi ya bure,"alisema.

"Unajua klabu zetu nyingi ni za mitaani, hazina vyanzo vya uhakika vya mapato, zinategemea michango ya wanachama, sasa sisi tulishalipa ada ya kucheza ligi daraja la pili, leo hii TFF inasema ligi zote zimefutwa. Nani angeturejeshea fedha zetu za ada ya ligi." alihoji.

1 comment:

  1. Hello, Je, unahitaji mkopo kutoka kampuni kuaminiwa zaidi na ya kuaminika
    katika dunia? kama ndiyo basi wasiliana nasi sasa kwa sisi kutoa mkopo kwa wote
    makundi ya watu wanaotafuta kuwa ni makampuni au kwa ajili ya matumizi ya wafanyakazi. Tunatoa
    mkopo kwa kiwango 3% riba, Wasiliana nasi kupitia barua pepe:
    jonsonlanld@gmail.com

    (1) Jina kamili
    (2) Full mitaani
    (3) Nchi
    (4) Umri
    (5) Kazi
    (6) Mwambie namba ya simu
    (7) Jinsia:
    (8) Loan Kiasi inahitajika:
    (9) Loan Duration

    Email yetu katika: jonsonlanld@gmail.com

    ReplyDelete