LICHA ya serikali kuanza kutoza kodi kazi za wasanii kwa lengo la kudhibiti wizi wa sanaa, msanii Joseph Haule amesema bado haijaweza kuwakwamua kimaendeleo.
Haule, ambaye ni maarufu zaidi kwa jina la Profesa Jay, alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, bado kilio cha wasanii wa Tanzania ni kuibwa kwa kazi zao na kwamba serikali haijachukua hatua madhubuti kupambana na tatizo hilo.
"Serikali ingejaribu kuangalia jinsi gani ya kuwasaidia wasanii wa Tanzania katika kazi zao, kama vile milio ya simu na katika sheria, jinsi gani msanii anaweza kunufaika na kazi zake anazozifanya,"alisema.
"Hivi sasa kuna stika za TRA, lakini haziwezi kusaidia kitu, stika zitakuwepo, lakini tatizo sugu tumeliacha, tatizo ni wizi wa kazi za wasanii," aliongeza msanii huyo mkongwe.
Mbali na kuilaumu serikali, Profesa Jay pia aliwaponda baadhi ya wasanii wa muziki wa kizazi kipya nchini kwa kukosa ubunifu na kuimba nyimbo zisizoeleweka na kudumu kwa muda mrefu.
Profesa Jay alisema wakati umefika kwa wasanii wa Tanzania kuamka na kutazama wapi wanakopaswa kwenda na pia kutumia vyema fursa ya lugha ya kiswahili kuwa ya kimataifa.
"Hivi sasa kila mmoja anamtupia lawama mwenzake. Jambo la muhimu ni kwamba tukae kama wasanii tunaotaka kuupeleka muziki wetu mahali fulani,"alisisitiza.
Msanii huyo mkongwe alisema muziki wa Tanzania unaharibiwa na wasanii wenyewe kutokana na kuandika mashairi yasiyoeleweka na pia kufanya maonyesho yasiyo na mvuto.
Profesa Jay pia alivilaumu vyombo vya habari nchini, hasa redio na televisheni kwa kupiga nyimbo zinazokiuka maadili na hivyo kutosaidia katika kuutangaza muziki wa Tanzania kimataifa.
No comments:
Post a Comment