'
Thursday, April 18, 2013
SIMBA: HATUIBEBI YANGA NG'O
UONGOZI wa klabu ya Simba umesema kamwe hauna mpango wa kuwabeba watani wao wa jadi Yanga katika mechi yao ya mwisho ya ligi kuu ya Tanzania Bara, itakayochezwa Mei 18 mwaka huu mjini Dar es Salaam.
Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema mjini Dar es Salaam juzi kuwa, habari hizo zinazosambazwa kwa kutumia meseji kupitia simu za mkononi hazina ukweli wowote.
"Kuna ujumbe mfupi wa maneno umeenezwa kwenye baadhi ya simu za mkononi za wapenzi wa Simba ukidai kwamba washabiki wa Yanga waliokuwa wakiishangilia timu yetu tulipocheza na Azam walifanya hivyo kwa sababu klabu hizi mbili zimeingia katika mahusiano," alisema Kamwaga.
"Ujumbe huo ukadai kwamba lengo la mahusiano hayo mapya baina ya Simba na Yanga ni kuhakikisha kwamba Simba inafungwa kwa idadi kubwa ya mabao kwenye mechi ya watani wa jadi Mei 18 mwaka huu.
Ujumbe huo ukaenda mbali zaidi kwa kudai kwamba hata kambi ya Simba ya Bamba Beach imefadhiliwa na Yanga. Ujumbe huo wa simu ni wa kuchekesha sana,"aliongeza.
"Uongozi wa Simba unakana kuwepo kwa mahusiano yoyote ya kuhujumu timu baina ya viongozi wa klabu na Yanga. Kitendo cha kushangiliwa kwa timu pinzani si kigeni kwani kimewahi pia kutokea katika nchi kadhaa duniani.
"Ikumbukwe kwamba kimsingi, sio kosa la jinai au mwiko kwa shabiki wa Yanga kuishangilia Simba. Kama washabiki wa wapinzani wetu wa jadi walivutiwa na kiwango chetu na kuamua kutushangilia, hiyo haikuwa dhambi.
"Uongozi unapenda kuwaomba wanachama wa Simba kuwa na imani na uongozi wao na kufahamu kwamba unafanya kila unaloweza kulinda na kuhifadhi hadhi na heshima ya klabu,"alisisitiza Kamwaga.
Wakati huo huo, Kamwaga alisema kikosi cha timu hiyo kilianza mazoezi jana kwa ajili ya maandalizi ya mechi zake zijazo za ligi kuu.
Kamwaga alisema wachezaji wa timu hiyo walikuwa wamepewa mapumziko ya siku mbili baada ya kucheza mechi yao dhidi ya Azam mwishoni mwa wiki iliyopita na kutoka nayo sare ya mabao 2-2.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment