KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, April 17, 2013

MOO KUONGOZA KAMATI YA TAIFA STARS



Kama mnavyofahamu, hivi sasa Timu ya Taifa ya mpira wa Miguu kwa Wanaume (Taifa Stars) ipo kwenye michuano ya kufuzu kushiriki Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika nchini Brazil mwaka 2014.

Katika Afrika, Tanzania (Taifa Stars) imepangwa kundi C kati ya makundi 10. Kundi C linajumuisha timu za Ivory Coast, Morocco, Gambia na Tanzania.

Kwa sasa katika kundi C, Taifa Stars inashika nafasi ya pili ikiwa na alama sita (6), nyuma ya Ivory Coast yenye alama saba (7), Morocco ina alama mbili (2) na Gambia ina alama moja(1).

Kwa mara nyingine Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo inapenda kuwapongeza Taifa Stars, kwa kazi nzuri ambayo wameishaifanya ikiwemo ushindi wa Bao Tatu kwa Moja dhidi ya Morocco. Watanzania wote na Wadau wa Soka nchini wamefurahishwa sana na mafanikio yaliyofikiwa na Taifa Stars na yenye kutupa matumaini katika kuitayarisha Taifa Stars kufuzu kucheza Fainali za Kombe la Dunia kwa mwaka 2014 nchini Brazil.

Kwa hali ilivyo hivi sasa, Taifa Stars ipo katika nafasi nzuri ya kufuzu. Ili Tanzania tuweze kufuzu, Taifa Stars inatakiwa ishinde mechi zote tatu (3) na kuongoza kundi C na baadae iingie katika Timu kumi (10) bora na kisha zipatikane Timu tano (5) kutoka Afrika ambazo zitakuwa zimefuzu kwenda Brazil katika Fainali za Kombe la Dunia kwa mwaka 2014. Tunaamini hili linawezekana.

Sasa kwa kuzingatia uzito wa jukumu lililo mbele yetu na kwa Taifa Stars kwa ujumla; Serikali imeunda Kamati ya Ushindi ya Taifa Stars.

Jukumu la msingi la Kamati tunayoiunda ni kuhakikisha Taifa Stars inawezeshwa na kuandaliwa ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuunda kikundi cha kuishangilia timu ya Taifa ndani na nje ya nchi. Wajumbe wa Kamati ya Taifa Stars Stars itakayoongozwa na Mhe. Mohamed Dewji ni hawa wafuatao:-

1. Mhe Mohamed Dewji - Mbunge
2. Bi. Teddy Mapunda - Montage
3. Dkt. Ramadhani Dau - Mkurugenzi Mtendaji NSSF
4. Bw. Dioniz Malinzi - Mwenyekiti BMT
5. Bw. Abji Shabir - New Africa Hotel
6. Bw. George Kavishe - TBL
7. Mhe. Mohamed Raza - Zanzibar
8. Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
9. Bw. Joseph Kusaga - Clouds
10. Mhe. Kapt. John Komba - Mbunge
11. Mhe. Zitto Kabwe - Mbunge

Kamati hii iliyoteuliwa leo, naomba ianze kazi mara moja. Hadidu za rejea zitakazowaongoza kutekeleza majukumu yao chini ya Kamati hii watazipata kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo. Kamati itashirikisha wadau mbalimbali kadri itakavyoona inafaa.

Serikali inaahidi kutoa ushirikiano utakaohitajika katika kuhakikisha Kamati hii inafanya kazi vizuri ili kuiwezesha Taifa Stars kushinda Mechi zote zilizombele yetu.

Aidha nichukue fursa hii kutoa wito kwa Watanzania wote, kuiunga mkono Taifa Stars na Kamati ya Ushindi ya Taifa Stars kwa hali na mali katika kuhakikisha timu yetu inafuzu kucheza Fainali za Kombe la Dunia.

Kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri Mkuu naomba niwasilishe salaam zao za kuwapongeza Vijana wetu wa Taifa Stars, pamoja na benchi la ufundi likiongozwa na Kocha Mkuu Kim Poulsen. Kwa pamoja wanaomba Taifa Stars iendelee kujipanga kwa mechi zijazo. Nawahakikishia kuwa Serikali, Watanzania na wadau wa Soka nchini wapo nyuma yao.

Mungu Ibariki Taifa Stars. Mungu Ibariki Tanzania.

Dkt. Fenella Mukangara (Mb)
WAZIRI WA HABARI, VIJANA, UTAMADUNI NA MICHEZO
16 Aprili, 2013

No comments:

Post a Comment