KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, April 4, 2013

WOLPER AMTUNGIA FILAMU KANUMBA


MSANII nyota wa filamu nchini, Jacqueline Wolper ameandaa filamu maalumu kwa ajili ya kumuenzi marehemu Steven Kanumba.

Wolper alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, filamu hiyo inatarajiwa kuzinduliwa Jumapili kwenye viwanja vya Leaders, Kinondoni, Dar es Salaam.

Hata hivyo, Wolper hakuwa tayari kutaja jina la filamu hiyo. Alisema litajulikana siku ya uzinduzi, lakini alisisitiza ni maalumu kwa ajili ya kumuenzi Kanumba.

"Kanumba ni kila kitu kwetu katika tasnia ya filamu, ndio maana tunamkumbuka na tutazidi kumuenzi,"alisema Wolper.

Kwa mujibu wa Wolper, siku hiyo pia utafanyika uzinduzi wa filamu ya mwisho ya marehemu Kanumba, inayojulikana kwa jina la Love & Power.

Kanumba aliandaa filamu hiyo siku chache kabla ya kifo chake kilichotokea Aprili 7 mwaka jana, nyumbani kwake, Sinza, Dar es Salaam.

Maudhui ya filamu hiyo hayana tofauti na mazingira ya kifo chake, ambacho kilipokelewa kwa simanzi kubwa na mashabiki wa fani hiyo nchini.

Wakati huo huo, mdogo wa marehemu Kanumba, Seth Bosco amesema wameandaa misa ya kumuombea ndugu yao itakayofanyika Jumapili kwenye kanisa la Kimara, Dar es Salaam.

Bosco alisema juzi kuwa, baada ya misa hiyo kukamilika, mambo yote yatahamia kwenye viwanja vya Leaders, ambako utafanyika uzinduzi wa filamu ya mwisho ya marehemu Kanumba.

"Itakuwa ni siku, ambayo tutatimiza mwaka mmoja baada ya mpendwa wetu Kanumba kufariki dunia,"alisema.

No comments:

Post a Comment