KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, April 17, 2013

YANGA CHUPUCHUPU KWA MGAMBO JKT


Na Sophia Wakati, Tanga

BAO lililofungwa na mshambuliaji Simon Msuva jana liliinusuru Yanga isiadhirike kwa Mgambo JKT baada ya timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini hapa.

Msuva alifunga bao hilo dakika tano kabla ya mchezo kumalizika, baada ya kutokea piga nikupige kwenye lango la Mgambo JKT na mabeki wa Maafande hao kujichanganya.

Mgambo JKT ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 43 lililofungwa na Issa Kandulu baada ya kumalizia pasi kati yake, Nassoro Gumbo na Sammy Mlima.

Sare hiyo imepunguza kasi ya Yanga kutangaza ubingwa wa ligi hiyo mapema, lakini bado inaendelea kuongoza ikiwa na pointi 53 baada ya kucheza mechi 23, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 47. Timu hizo zinatofautiana kwa pointi sita.

Mgambo JKT ililianza pambano hilo kwa kasi na kupata nafasi mbili nzuri za kufunga mabao dakika za mwanzo, lakini umaliziaji mbovu wa washambuliaji wake, Nassoro Gumbo na Sammy Mlima ulikuwa kikwazo.

Yanga ilijibu mashambulizi hayo dakika ya 10 na 15, lakini washambuliaji wake, Simon Msuva na Hamisi Kiiza walikosa umakini na kupoteza nafasi za kufunga mabao.

Pambano hilo liliingia doa dakika ya 44 baada ya Simon Msuva kuangushwa ndani ya eneo la hatari na beki Bakari Mtama wa Mgambo JKT , lakini mwamuzi Athumani Lazi kutoka Morogoro aliamua kupeta.

Kufuatia mwamuzi kutotoa adhabu yoyote, mashabiki wa Yanga waliamua kurusha chupa ndani ya uwanja, lakini hakuna mchezaji aliyejeruhiwa. Ilibidi pambano lisimame kwa dakika mbili kabla ya kuendelea. Timu hizo zilikwenda mapumziko Mgambo ikiwa mbele kwa bao 1-0.

Pambano hilo liliingia tena doa dakika ya 56 baada ya mashabiki wa Yanga kurusha chupa uwanjani, wakipinga kitendo cha mwamuzi kumwonyesha kadi ya njano Nadir Haroub 'Cannavaro' aliyemlalamikia baada ya Kevin Yondan kupigwa kiwiko na mchezaji mmoja wa Mgambo JKT.

Katika kipindi cha pili, Yanga iliwapumzisha Hamisi Kiiza na Frank Dumayo, ambao nafasi zao zilichukuliwa na Saidi Bahanuzi na Nurdin Bakari.

Pamoja na kufanya mabadiliko hayo, Yanga ilishindwa kusawazisha kutokana na washambuliaji wake kukosa umakini kila walipofika kwenye lango la Mgambo JKT.

No comments:

Post a Comment