KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, April 8, 2013

AZAM, BARRACK ZAINGIZA MIL 44

MECHI ya marudiano ya raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho kati ya Azam ya Tanzania na Barrack Young Controllers II ya Liberia iliyochezwa jana (Aprili 6 mwaka huu) imeingiza sh. 44,229,000.

Fedha hizo katika mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa timu hizo kutoka suluhu zimetokana na watazamaji 17,128 waliokata tiketi.

Viingilio vilikuwa sh. 2,000, sh. 5,000, sh. 10,000 na sh. 20,000 ambacho kilikuwa kiingilio cha juu kwa jukwaa la VIP A. Kiingilio cha sh. 2,000 ndicho kilichovutia watazamaji wengi ambapo walikuwa 15,212.

Mgawo ulikuwa kama ifuatavyo; gharama za tiketi sh. 5,575,500, asilimia 15 ya uwanja sh. 5,798,025, asilimia 10 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) sh. 3,865,350 na asilimia 75 iliyokwenda kwa klabu ya Azam ni sh. 28,990,500.

Mechi iliyopita ya raundi ya awali ya mashindano hayo kati ya Azam na El Nasir ya Sudan Kusini iliyochezwa kwenye uwanja huo huo Februari 16 mwaka huu iliingiza sh. 34,046,000 kwa viingilio hivyo hivyo huku ikishuhudiwa na watazamaji 13,431.

No comments:

Post a Comment