KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, April 25, 2013

DEO MUNISHI 'DIDA': INAUMA SANA



UONGOZI wa timu ya soka ya Azam hivi karibuni uliamua kuwarejesha kikosini wachezaji wake wanne, akiwemo kipa Deo Munishi 'Dida', waliokuwa wakikabiliwa na tuhuma za kupokea rushwa kutoka kwa timu pinzani. Katika makala hii ya ana kwa ana iliyoandikwa na Mwandishi Wetu ATHANAS KAZIGE, kipa huyo anasimulia mkasa huo na masuala mengine kuhusu maisha yake kisoka.

SWALI: Ulijisikiaje wakati uongozi wa Azam ulipotangaza kukusimamisha wewe na wachezaji wenzako watatu kwa tuhuma za kupokea rushwa kutoka kwa timu pinzani baada ya timu yako kufungwa mabao 3-1 na Simba katika mechi ya ligi?

JIBU: Kwanza kabisa ninapenda kumshukuru Mungu baada ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kutusafisha kwa vile hali ilikuwa mbaya sana. Haya mambo omba yatokee kwa mtu mwingine, lakini yanapotokea kwako, utajuta.

Tuhuma hizo zilitunyima raha na kutufanya tukose amani. Kila tulipokuwa tukikatiza, tulionekana kama vile watu wa ajabu mbele ya jamii.

Binafsi tuhuma hizi zilinikera sana kwa sababu hazikuwa na ukweli wowote. Ndio sababu siku niliposikia TAKUKURU ikitoa taarifa ya kutusafisha, nilifurahi sana na kujiona kama vile nimekuwa mtu huru baada ya kutoka kifungoni.

SWALI: Ni kitu gani hasa kilichokuwa kikikufanya ukose raha?

JIBU: Kila nilipokuwa nikipita kwenye mkusanyiko wa watu wengi, baadhi yao walikuwa wakinong'onezana na wengine kunisema vibaya. Nilikuwa naonekana kama vile ni mhalifu.

Unajua inapofika hatua hata watoto wadogo wanajua nini kimetokea na kukushangaa wakati kitu chenyewe sio cha kweli, inauma sana. Nashukuru kwamba mambo haya yamemalizika salama na nimeamua kumshtakia Mungu.

Napenda kuweka wazi kwamba, kamwe sijawahi kupokea rushwa katika maisha yangu kutoka kwa kiongozi wa timu yoyote. Mimi ni muumini mzuri wa kanisa katoliki na kila Jumapili nasali kwenye kanisa la Chang'ombe.

SWALI: Familia yako, ndugu zako na rafiki zao alizipokeaje taarifa za wewe kusimamishwa Azam kwa tuhuma za kupokea rushwa?

JIBU: Familia yangu ilishangazwa sana na taarifa hizi kwa vile inanifahamu vyema. Baadhi ya ndugu zangu walinishauri niwaache viongozi wa Azam wajiridhishe wakiamini kwamba ipo siku ukweli utadhihirika na kweli hilo limefanyika.

SWALI: Je, umepanga kuchukua hatua zozote kwa uongozi wa Azam kutokana na kukupakazia tuhuma hizo?

JIBU: Kwa kweli sitarajii kufanya lolote kwa uongozi wa Azam kwa sababu umeshatangaza kuturejesha kwenye timu na tumeshaanza mazoezi na wenzetu. Waswahili wanasema, yaliyopita si ndwele, tugange yajayo. Kwangu hayo sasa yameshapita, najipanga upya kutafuta namba kwenye kikosi cha kwanza.

SWALI: Athari zipi nyingine ulizozipata kutokana na kusimamishwa na uongozi wa Azam?

JIBU: Athari zipo nyingi tu. Nyingine zilikuwa ni kutosajiliwa katika michuano ya Kombe la Shirikisho na hivyo kukosa pesa nyingi za posho za safari.

Michuano hii ilikuwa sehemu nzuri kwetu kuonyesha uwezo na vipaji vyetu na pengine kupata nafasi ya kucheza soka ya kulipwa nje. Nilijikuta nikigeuka kuwa mtazamaji wa Azam katika mechi za michuano hiyo badala ya mchezaji.

Ninachopenda kusisitiza ni kwamba, sina kinyongo na mtu yeyote, nimeamua kumuachia Mungu. Ninaendelea na kazi yangu ya kuichezea Azam bila ya kuwa na hofu yoyote. Nawaomba viongozi wa Azam waendelee kuniamini kwa vile kucheza soka ndio kazi yangu.

SWALI: Unauelezeaje ushindani wa namba kwenye kikosi cha Azam kwa sasa, hasa ya ukipa?

JIBU: Ninachoweza kusema ni kwamba, Azam imebahatika kuwa na makipa wazuri. Yupo Mwadini Ally na Aishi Manura, wote ni wazuri na wapo kwenye kiwango cha juu. Nitakachokifanya ni kupambana nao kuwania namba. Mwamuzi wa mwisho ni kocha Stewart Hall.

Lakini nitakuwa na kazi ngumu kwa sababu nimekuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu. Nitalazimika kufanya mazoezi kwa bidii ili niwe fiti. Naamini mazoezi binafsi niliyokuwa nikiyafanya wakati tumesimamishwa, yatanisaidia kuwa fiti.

SWALI: Nini matarajio yako kwenye kikosi cha Taifa Stars?

JIBU: Hakuna kitu ambacho nimekuwa nikikipa kipaumbele kama kuichezea Taifa Stars. Nitafanya kila ninaloweza ili niitwe kwenye kikosi hicho.

SWALI: Umejifunza nini katika maisha yako ya soka hadi sasa?

JIBU: Nashukuru kwa swali lako zuri. Nimejifunza mambo mengi katika maisha yangu, lakini kubwa ni kwamba usimuamini kila mtu kwenye ulimwengu huu kwa vile unaweza kuzuliwa jambo, likakuangamiza ama kukuletea matatizo.

Kuanzia sasa nitakuwa makini sana na watu wangu wa karibu. Sitakuwa karibu na watu wenye tabia za majungu kwa sababu wanaweza kunizulia mambo mengine nikapata matatizo. Waliyonifanyia yanatosha. Nimepoteza vitu vingi sana.

Funzo lililonipata litaendelea kudumu ndani ya moyo wangu. Lakini daima nitabaki kuwa mtu mwenye nidhamu na upendo kwa wenzangu. Nataka kuishi maisha ya amani.

No comments:

Post a Comment