KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, April 4, 2013

NURU THE LIGHT, SHOMBESHOMBE WA KIBONGO ANAYETAMBA KIMUZIKI

WAKATI aliporekodi kibao chake cha kwanza kinachojulikana kwa jina la Walimwengu, mwanadada Nuru Mohamed, maarufu kwa jina la Nuru the Light, hakuwa akijulikana sana miongoni mwa mashabiki wa muziki wa kizazi kipya nchini.

Ni kwa sababu hakuwa akiishi hapa nchini, japokuwa alikuwa akifika Dar es Salaam mara kwa mara kwa ajili ya kuwatembelea ndugu zake. Nuru alizaliwa na kukulia nchini Sweden, ambako ndiko wazazi wake wanakoishi.

Kilichomfanya Nuru ajitose kwenye fani ya muziki ni baada ya kuvutiwa na mwanamuziki wa kitanzania aliyekuwa akiishi Sweden wakati huo, marehemu Mtoto wa Dandu.

Mbali na kuvutiwa na mwanamuziki huyo, Nuru pia alishangaa kuona kuwa, wakati alipofika Tanzania kwa mara ya kwanza, msanii pekee wa kike aliyekuwa akitamba wakati huo alikuwa Judith Wambura 'Lady JayDee'.

"Nikawa najiuliza kwa nini hakuna wanamuziki wa kike wenye vipaji kama Lady JayDee? Nilichogundua ni kwamba wasichama wa Kitanzania hatujiamini, tuna woga wa kufanya vitu ndio sababu tunachukiana bila sababu,"alisema.

"Ukiona mwenzako amefanikiwa katika sekta fulani, unatishika. Badala ya kujitahidi ufike pale alipo, unajaribu kumjenga chuki ili arudi nyuma," aliongeza msanii huyo mwenye haiba yenye mvuto.

Nuru alisema baada ya kurudi Sweden, alimtafuta prodyuza, ambaye licha ya kutofahamu lugha ya kiswahili, aliweza kutengeneza naye wimbo wa Walimwengu, ambao anakiri kwamba ndio uliomtoa kimuziki.

Katika wimbo huo, Nuru amezungumzia matatizo mbalimbali yaliyowahi kumkuta katika maisha yake, kila alipokuwa akija nchini kuwatembelea ndugu zake, ambapo watu wengi walikuwa wakimfikiria kwamba ni binti wa kitajiri.

Baada ya muda si mrefu, Nuru aliibuka na kibao kingine kinachokwenda kwa jina la Msela, ambacho kilizua gumzo kwa mashabiki kutokana na maudhui yake.

"Nilipotoa wimbo huu, mashabiki wengi hawakunielewa. Wakawa wanajiuliza, iweje msichana huyu mrembo anawapenda wasela. Kwangu neno msela ni tofauti na inavyoeleweka kwa watu wengine. Msela ni mtu anayependa kuchapakazi hata kama amevaa suti,"alisema Nuru.

"Usimuhukumu mtu kwa mwonekano wake, lazima umchunguze ili upate ukweli," alisisitiza mwanadada huyo, ambaye kwa kawaida ni mcheshi na mzungumzaji mno, akiwa anapenda kujichanganya na watu wa aina tofauti.

Licha ya kuajiriwa nchini Sweden na pia kujihusisha na biashara, Nuru alisema hafanyi muziki kwa ajili ya kujifurahisha kwa vile ni fani anayoipenda na kuvutiwa nayo.

Nuru anavutiwa zaidi na wasanii Juma Kassim 'Nature' na Joseph Haule 'Profesa Jay', ambao amewaelezea kuwa wana vipaji vya asili na kuimba nyimbo zenye mvuto.

"Navutiwa na Nature kutokana na staili ya maisha yake. Wakati mwingine huwa anaimba vitu nisivyovielewa, lakini navipenda,"alisema.

"Navutiwa na Profesa Jay kwa sababu ni msanii asiyekuwa na maringo wala kujikweza. Yupo kama alivyo. Kwa msanii wa aina yake, angekuwa na maringo mno,"aliongeza.

Kwa upande wa wasanii wa kike, Nuru alisema anapenda kufanya kolabo na Grace Matata na Nakaaya Sumari kwa vile wana vitu, ambavyo havifanani, lakini vikichanganywa pamoja vinakuwa bomba.

Mbali na kuwa msanii wa muziki wa kizazi kipya, Nuru pia ni prodyuza. Ndiye aliyetengeneza vibao vyake vya Walimwengu na Msela.

Ili kwenda na wakati kimuziki, Nuru alisema utaratibu wake ni kurekodi CD na Audio za nyimbo zake kwa pamoja. Alisema lengo ni kuwawezesha mashabiki wake kupata burudani ya nyimbo zake kwa wakati mmoja.

"Sipendi kutoa kitu kimoja kimoja, mtu mwingine akisikia wimbo kwenye CD, hawezi kuelewa mpaka aone video yake. Kuna wengine hawajui kiswahili, lakini akiona video, anaelewa,"alisema.

Nuru hajaolewa na kwa mujibu wa maelezo yake, hahitaji rafiki wa kiume kwa wakati huu. Alisema anachotaka ni kutimiza malengo aliyojiwekea.

Msanii huyo hafurahishwi na maonyesho ya baadhi ya wasanii wa Tanzania waliyowahi kuyafanya katika nchi za Ulaya. Alisema maonyesho mengi aliyowahi kuyashuhudia Sweden, yaliyowahusisha Naseeb Abdul 'Diamond' na Jay More yalikuwa feki.

"Nafurahi kuona wasanii wa Tanzania wanapata nafasi ya kufanya maonyesho Ulaya, lakini mengi yanakuwa hayana hadhi kwa sababu wanapelekwa katika kumbi ndogo mno na mashabiki wanaohudhuria wanakuwa wachache,"alisema.

Nuru alisema moja ya malengo yake katika siku zijazo ni kupigania haki za wasanii wa Tanzania, hasa katika suala la usambazaji wa kazi zao, ambao ameuelezea kuwa kwa sasa ni duni.

Alisema amejifunza mengi kutokana na vifo vya wasanii Steven Kanumba na Sharo Milionea, ambao familia zao hazinufaiki lolote kutokana na kazi zao.

Nuru alisema binafsi amekuwa akisajili nyimbo zake katika chama cha hakimiliki cha Sweden, hivyo hata kama atafariki, familia yake itaweza kunufaika kutokana na kazi zake.

Ametoa mwito kwa wasanii kuungana na kuacha kujengeana chuki bila sababu za msingi. "Hii habari ya mimi napiga hip hop, mimi napiga bongo fleva, haiwezi kutufikisha popote. Usimcheke mwenzako, tuwe na utaratibu wa kusaidiana,"alisema.

Amemfagilia Adam Juma kwa kuwa mshauri wake mzuri kimuziki baada ya kumuona amekata tamaa kutokana na maprodyuza wengi kumtongoza na kumtaka kimapenzi. Adam ni mtaalamu wa kutengeneza video za muziki.

"Hivi sasa nina msimamo. Prodyuza akinitongoza, namtukana papo hapo na sifanyi naye kazi,"alisema Nuru, ambaye ni mtoto pekee wa kike katika familia yake, akiwa na kaka zake watatu.

No comments:

Post a Comment