KWA mashabiki wanaofuatilia tamthilia ya Mara Clara, inayoonyeshwa na kituo cha televisheni cha Star TV kila siku za Jumanne, Ijumaa, Jumamosi na Jumapili usiku, jina la Mara si geni kwao. Ni mmoja wa wasanii walioinadhifisha tamthilia hiyo kutokana na uigizaji wake mzuri na wa kuvutia.
Mara Clara ni tamthilia ya Kifilipino, ambayo ilionyeshwa kwa mara ya kwanza na kituo cha ABS-CBN kuanzia Agosti 17, 1992 hadi Februari 14, 1997. Ni tamthilia inayotokana na kitabu cha Mara Clara kilichoandikwa na Emil Cruz Jr.
Katika tamthilia hiyo, Mara ambaye jina lake halisi ni Kathryn Bernardo, ameigiza na Julia Montes, anayetumia jina la Clara.
Mabinti hawa wawili walibadilishwa na Karlo mara baada ya kuzaliwa bila ya wazazi wao kujijua. Mara aliishi maisha ya kimaskini akiwa na wanandoa, Susan na Gary wakati binti yao halisi, Clara aliishi katika familia ya matajiri ya Amante na Alvira del Valle.
Lengo la Karlo kuwabadilisha watoto hao wawili baada ya kulizaliwa, lilikuwa kumwezesha Clara kuishi maisha ya kifahari na kupata elimu nzuri kwa vile baba yake halisi, Gary alikuwa jela.
Karlo, ambaye alikuwa mtumishi wa hospitali na ndugu wa Gary, aliamua kuandika kumbukumbu ya tukio hilo kwenye kitabu chake maalumu na ndicho kilichowezesha ukweli kubainika hata baada ya kufa kwake.
Kuna wakati, familia ya Del Valle ilimchukulia Mara kama mtumishi wa ndani na kuamua kumgharamia kimasomo bila kujua ndiye mtoto wao halisi. Clara, ambaye ni mtoto halisi wa Gary, alisababisha maisha ya Mara yawe magumu.
Hasira za Clara kwa Mara zilitokasana na sababu nyingi. Ya kwanza ilikuwa Mara alimzidi Clara kimasomo. Ya pili ilikuwa uhusiano wa karibu aliokuwa nao Mara kwa Cristian, ambaye Clara alikuwa akimpenda.
Hata hivyo, kadri maisha yalivyosonga mbele, ukweli ukaja kubainika kwamba Mara ndiye mtoto halisi wa familia ya Del Valle wakati Clara ni mtoto halisi wa familia ya Gary.
Unazuka uhasama mkubwa kati ya familia hizo mbili, ambapo Gary analazimika kufanya kila linalowezekana kumfanya Clara amkubali kwamba ndiye baba yake halisi, ikiwa ni pamoja na kumteka Mara na Clara kwa lengo la kuishinikiza familia ya Del Valle ilipe pesa kwa ajili ya kuwagomboa.
Licha ya Gary kufanikiwa kupata mamilioni ya pesa kutoka kwa familia ya Del Valle, anaandaa mpango wa kumuangamiza Mara kwa milipuko ya mabomu huku Clara akifanikiwa kujiokoa. Kifo cha Mara kinawasikitisha wazazi wake, ambao wanaapa lazima wawapate wauaji na kuwafikisha kwenye vyombo vya dola.
Hata hivyo, inakuja kubainika baadaye kwamba, Mara hakuwa amekufa kwenye mlipuko uliotokea kwenye jumba alimofungiwa na Clara. Aliokolewa na mmoja wa vikaragosi wa Gary kabla ya kupelekwa mafichoni na Cristian.
Mama yake Gary ndiye anayefanikiwa kufichua mpango mzima wa mauaji ya kupanga ya Mara baada ya kukuta mamilioni ya pesa chumbani kwa mtoto wake huyo na pia kumfuatilia na kumuona akiingia kwenye nyumba alimomuhifadhi Cristine, ambaye alikuwa akitafutwa na polisi.
Hatimaye Gary na Cristine wanatiwa mbaroni na polisi na wakati huo huo, Mara anaibuka kutoka mafichoni na kuibua furaha kwa familia yake.
Mara alizaliwa Machi 26, 1996 katika mji wa Cabanatuan , Philippines. Ni mmoja wa waigizaji wa kike wenye mvuto nchini humo, akiwa amejipatia umaarufu mkubwa baada ya kucheza filamu ya Mara Clara.
Kwa sasa, Mara ni msanii mwenye mkataba na vituo vya televisheni vya Star Magic na ABS-CBN na hivi karibuni alishiriki kuigiza tamthilia ya Way Back Home akiwa anatumia jina la Ana Bartolome. Tamthilia hiyo iliandaliwa 2011.
Binti huyo mwenye sura jamali, pia amecheza tamthilia ya Princess and I akiwa anatumia jina la Mikay. Mara ni swahiba mkubwa wa Clara na mara nyingi hupenda kutembea pamoja.
Mara ni mwanafunzi wa chuo cha Angelicum na amewahi kushinda tuzo mbalimbali kutokana na tamthilia ya Mara Clara.
Mara alianza kucheza filamu tangu 2004 alipoigiza filamu ya Gagamboy, lakini alianza kupata umaarufu baada ya kucheza filamu ya Way Back Home akishirikiana na Julia Montes.
Filamu hiyo iliongozwa kwa kutazamwa na watu milioni 18 katika wiki yake ya kwanza na kuzipiku filamu za kizungu zilizokuwa zikionyeshwa nchini humo katika wiki hiyo kama vile The Smurfs na Conan the Barnarian.
Mbali na kucheza filamu na tamthilia, Mara pia ni mwanamitindo na amekuwa akitumika kutangaza bidhaa mbalimbali kama vile Bench and Coca-Cola. Pia ni mwanamuziki na mwaka jana alirekodi kibao cha Mula Noon Hanggang Ngayon.
No comments:
Post a Comment