KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, April 25, 2013

SIMBA, RUVU SHOOTING KAZI IPO LEO


TIMU kongwe ya soka ya Simba inatarajiwa kushuka dimbani leo kumenyana na Ruvu Shooting katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Pambano hilo lina umuhimu mkubwa kwa Simba kwa vile iwapo itashinda, itajiweka katika nafasi nzuri ya kumaliza ligi ikiwa nafasi ya tatu.

Simba inashika nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi 36 baada ya kucheza mechi 22, sawa na Mtibwa Sugar, lakini zinatofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa.

Yanga yenye matumaini makubwa ya kutwaa ubingwa wa ligi hiyo, bado inaongoza ikiwa na pointi 56 baada ya kucheza mechi 24, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 47 na Kagera Sugar yenye pointi 40.

Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Simba, Joseph Itangale, maarufu kwa jina la Kinesi, alisema jana kuwa, timu hiyo imeshaingia kambini kwa ajili ya kujiandaa kwa pambano hilo.

Kinesi alisema lengo kubwa walilonalo ni kushinda mechi zote nne zilizosalia ili waweze kumaliza ligi wakiwa kwenye nafasi ya tatu.

Baada ya mechi ya leo, Simba inatarajiwa kushuka tena dimbani Aprili 28 kumenyana na Polisi Moro kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya kuvaana na Mgambo JKT Mei 8 mwaka huu kwenye uwanja huo.

Mabingwa hao wa mwaka jana wa ligi hiyo, watahitimisha mechi zao za ligi Mei 18 mwaka huu kwa kumenyana na watani wao wa jadi, Yanga.

Kwa mujibu wa Kinesi, katika mechi zote hizo, Simba itaendelea kuwatumia wachezaji wake wa kikosi cha pili, ambao wameonyesha kiwango cha juu.

No comments:

Post a Comment