'
Monday, April 8, 2013
TFF YAMKALIA KOONI NSA JOB
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limemtaka mshambuliaji Nsa Job wa Coastal Union kuwasilisha maelezo yake juu ya madai kuwa alipewa rushwa ya sh. milioni mbili ili asiifunge moja ya timu vigogo vya soka nchini.
Job alikaririwa Aprili 3 mwaka huu na kituo cha redio cha Clouds FM katika kipindi cha Amplifier kuwa alipewa kiasi hicho cha fedha na kiongozi wa timu husika ili asiifunge katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom, lakini alipokea fedha hizo na kuifunga timu hiyo.
Baadaye kiongozi huyo alikuwa akimtaka arejeshe fedha hizo. Pia TFF imekiandikia kituo hicho cha redio kutaka nakala ya kipindi hicho ili pamoja na maelezo ya mshambuliaji huyo vipelekwe katika Kamati ya Nidhamu kwa ajili ya hatua za kinidhamu.
TFF itachukua hatua kali dhidi ya Job iwapo hatawasilisha maelezo yake kuhusiana na suala hilo, na imetaka wadau kutoa ushirikiano ili iweze kupambana kikamilifu na vitendo vya rushwa kwenye mpira wa miguu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment