KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, April 4, 2013

EXTRA BONGO, JAHAZI KUNOGESHA BONANZA LA TASWA


Juma Pinto Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa habari za michezo TASWA akitangaza bendi ya muziki itakayotumbuiza kwenye bonanza la waandishi wa habari litakalofanyika Aprili 6 Jumamosi kwenye viwanja vya Leaders jijini Dar es salaam, kulia ni Katibu Mkuu wa TASWA Amiri Mhando na kulia ni Doris Malulu Ofisa Uhusiano TBL
BENDI ya muziki wa dansi ya Extra Bongo na kundi la taarabu la Jahazi Modern ndiyo burudani zitakazonogesha tamasha la vyombo vya habari litakalofanyika Dar es Salaam kesho (Jumamosi).

Akizungumza Dar es Salaam jana, wakati wa kutambulisha burudani hizo, Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kinachoandaa bonanza hilo, Juma Pinto alisema maandalizi kuhusiana na tamasha hilo linalojulikana kama Media Day Bonanza yamekamilika.

Alisema wameichukua Extra Bongo inayoongozwa na Ally Choki na Jahazi Modern inayoongozwa na Mzee Yusuph kutokana na makundi hayo kuwa juu hivi sasa katika muziki kwa maeneo yao.

“Tunaamini watakaokuja kwenye tamasha watakuwa na furaha ya aina yake na tumejiandaa vya kutosha,” alisema Pinto na kueleza kuwa bonanza hilo litafanyika viwanja vya Sigara Chang’ombe, Dar es Salaam na mgeni rasmi atakuwa Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe.

Pia Pinto alisema bendi ya Msondo Ngoma Music itapiga kwenye viwanja hivyo kuanzia saa moja usiku baada ya bendi za Extra Bongo na Jahazi kumaliza kutumbuiza Media Day na kwamba imetoa ofa kwa wanahabari watakaotaka kubaki kuendelea kupata burudani mpaka usiku wa manane.

“Msondo wana bonanza lao kila Jumamosi, sasa wamekubali kwamba wanahabari watakaotaka kubaki baada ya bonanza kumalizika jioni wabaki wajiunge na Msondo Ngoma,” alisema Pinto.

Bonanza hilo la TASWA linadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) likiwa na lengo la kuwaweka pamoja waandishi wote wa habari bila kujali ni wa siasa, michezo, uchumi, afya na mambo mengine pamoja na wafanyakazi wa vyombo mbalimbali vya habari ili kubadilishana mawazo na kufurahi pamoja.

Kwa upande wake Ofisa Uhusiano wa TBL, Doris Malulu alisema wamejipanga vya kutosha na kwamba wadau wafike kwa wingi kuhakikisha mambo yanaenda kama yalivyopangwa.

“TBL ni mdau mkubwa wa wanahabari, tumewaandalia mambo mazuri, naomba msikose,” alisema Malulu na kuongeza kuwa wanaamini wadau 1,500 kutoka vyombo mbalimbali vya habari wanaotarajiwa kushiriki bonanza hilo watafurahi vya kutosha siku hiyo.

Naye Choki akizungumza kwenye mkutano huo, alisema vijana wake wamejipanga vya kutosha kushambulia na kuwa dhamira yao ni kuona wana habari wanafurahi vya kutosha na kuwa mambo waliyowaandalia kila mtu atafurahi kuiona Extra Bongo.

No comments:

Post a Comment