KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, April 14, 2013

MBAGA, MSAIDIZI WAKE WAIBEBA AZAM KWA BAO LA MKONO, CHIPUKIZI WA SIMBA USIPIME



MWAMUZI Oden Mbaga leo alionekana dhahiri kuibeba Azam baada ya kuruhusu bao lake la kusawazisha lililofungwa na Humphrey Mieno baada ya kuushika mpira kwa mkono kwa makusudi.

Mieno alifunga bao hilo katika kipindi cha pili baada ya mpira wa krosi uliopigwa na Khamis Mcha kutoka pembeni kidogo ya uwanja.

Awali, mwamuzi msaidizi namba mbili alinyoosha kibendera hewani kuashiria kwamba kuna mashambi yalitendeka, lakini baada ya kumuona Mbaga akielekea kati, aliamua kukishusha mara moja na kuungana naye.

Kipa Abbel Dhaira wa Simba hakuwa amefanya jitihada yoyote ya kuokoa mpira uliopigwa na Mieno kwa sababu aliushika mpira kwa mkono mbele yake na pia alimuona mwamuzi msaidizi akinyoosha kibendera hewani.

Kutokana na utata huo, wachezaji wa Simba walimzonga Mbaga na msaidizi wake, wakilalamikia bao hilo, lakini hakuna aliyebadili msimamo.

Baadhi ya mashabiki waliohudhuria pambano hilo, wamekielezea kitendo hicho cha Mbaga kuwa ni cha fedheha kwa mwamuzi mwenye beji ya Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA), anayetakiwa kuchezesha mechi za michuano ya kimataifa.

Katika pambano hilo, Simba ambayo ilichezesha wachezaji wengi chipukizi, ilionyesha kiwango cha juu na kuwafanya mashabiki wake wawashangilie kwa furaha kubwa. Pia mashabiki wa Yanga leo walikuwa wakiishangilia Simba ili iifunge Azam.

Kwa matokeo hayo, Simba imeendelea kushika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi 36 wakati Azam ni ya pili ikiwa na pointi 47.

Mshambuliaji Ramadhani Singano aliibuka shujaa wa Simba baada ya kuifungia mabao yote mawili dakika ya 10 na 14 baada ya kupokea pasi kutoka kwa Mrisho Ngasa.

Azam ilipata bao lake la kwanza kwa njia ya penalti kupitia kwa Kipre Tchetche baada ya beki wa pembeni, Miraji Juma kumkwatua ndani ya eneo la hatari kabla ya Mieno kufunga bao la utata.

Simba: Abbel Dhaira, Nassor Masoud ‘Chollo’, Miraj Adam, Mussa Mudde, Shomary Kapombe, Amri Kiemba, Haroun Chanongo/Edward Christopher, Abdallah Seseme, William Lucian/Mwinyi Kazimoto, Ramadhani Singano na Mrisho Ngassa/Fliex Sunzu.

Azam :Mwadini Ally, Himid Mao, Waziri Salum, David Mwantika, Joackins Atudo, Kipre Balou, Luckson Kakolaki/Khamis Mcha ‘Vialli’ dk, Salum Abubakar, John Bocco/Abdi Kassim, Humphrey Mieno/Jabir Aziz na Kipre Tchetche

No comments:

Post a Comment