KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, April 17, 2013

NGASA AITABIRIA MAKUBWA SIMBA MSIMU UJAO


MSHAMBULIAJI Mrisho Ngasa wa Simba amesema wachezaji chipukizi wa timu hiyo ni wazuri, lakini bado wanahitaji muda zaidi ili kuzoea mikikimikiki ya ligi kuu ya Tanzania Bara.

Akizungumza mjini Dar es Salaam wiki hii, Ngasa alisema chipukizi hao wanacheza soka ya kiwango cha juu na ya kuvutia, lakini kutokana na kukosa uzoefu, wamekuwa wakifanya makosa ya kizembe.

Akitoa mfano, Ngasa alisema katika mechi yao dhidi ya Azam iliyochezwa Jumapili iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, chipukizi hao walionyesha kiwango cha juu kuliko wapinzani wao.

"Tatizo lililosababisha wapinzani wetu wasawazishe ni makosa madogo madogo yaliyofanywa na vijana wetu. Vinginevyo, Simba itakuwa na timu nzuri sana mwakani,"alisema.

Ngasa amewataka mashabiki na wanachama wa Simba wawe na subira kwa sababu vijana hao wanahitaji muda zaidi ili waweze kuzoea mikikimikiki ya ligi hiyo.

Katika mechi hiyo, Simba na Azam zilishindwa kutambiana baada ya kutoka sare ya mabao 2-2. Simba ilikuwa ya kwanza kupata mabao kupitia kwa mshambuliaji wake chipukizi, Ramadhani Singano, aliyetengenezwa vyumba safi na Ngasa.

Azam ilisawazisha kwa bao la penalti lililofungwa na Kipre Tchetche baada ya beki Miraji Juma kumchezea vibaya Khamis Mcha ndani ya eneo la hatari. Bao la kusawazisha lilifungwa na Humphrey Mieno.

Tayari Simba imeshavuliwa ubingwa wa ligi hiyo na kupoteza mwelekeo wa kushika nafasi ya pili baada ya kuvurunda katika mechi zake za hivi karibuni, ikiwa ni pamoja na kuchapwa bao 1-0 na Kagera Sugar na kulazimishwa sare ya mabao 2-2 na Toto African.

No comments:

Post a Comment