KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, June 23, 2011

Sista P aburuzwa kortini

MSANII nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Happy Thadfi 'Sister P' amepandishwa kizimbani kujibu shitaka la kujeruhi kwa kutumia chupa.
Happy (26), mkazi wa Mwananyamala kwa Kopa, Dar es Salaam, alipandishwa kizimbani jana katika Mahakama ya Mwanzo Kinondoni.
Mbele ya Hakimu wa Mahakama hiyo, Hanifa Mwingira, karani wa mahakama, Shani Idi alidai kuwa, mshitakiwa alitenda kosa hilo Juni 21, mwaka huu, saa 3.00 usiku, maeneo ya Mwananyamala.
Shani, alidai kuwa, msanii huyo alimpiga kwa chupa Jackson Tenga kichwani na kumsababishia majeraha katika sehemu mbalimbali za mwili wake.
Mshtakiwa alikana shitaka hilo na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuomba upangiwe tarehe nyingine ya kutajwa kwa kesi hiyo.
Hakimu Hanifa alisema haki ya dhamana kwa mshitakiwa ipo wazi na kumtaka awe na wadhamini wawili wanaotambulika kisheria.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Julai 7 mwaka huu, itakapotajwa tena na mshitakiwa yuko nje kwa dhamana.
Happy, ambaye ni maarufu zaidi kwa jina la Sista P, aliwahi kutamba kimuziki kutokana na vibao vyake mbalimbali, kikiwemo ‘Wanachonga sana juu yangu’. Kwa sasa, msanii huyo anatamba kwa kibao cha ‘Nani mkali’, alichomshirikisha Ney wa Mitego.
Akizungumza akiwa nje ya mahakama, Happy ambaye alionekana kuchoka na kuwa kama mtu aliyeshikwa na usingizi alisema, alikuwa kimya kwa muda mrefu kwa vile yupo kwenye maandalizi ya kurekodi wimbo mpya.
Msanii huyo mwenye makeke aliutaja wimbo wake mpya kuwa ni ‘Wapotezee’, ambao amemshirikisha Dully Sykes.
Baadhi ya watu waliokuwepo mahakamani hapo walionekana kumshangaa msanii huyo kutokana na mabadiliko makubwa aliyokuwa nayo, hasa mwili wake kupungua.

No comments:

Post a Comment