KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, June 15, 2011

Jim Iyke azushiwa kifo


LAGOS, Nigeria
MCHEZA filamu machachari wa Nigeria, Jim Iyke ameibuka na kukanusha uvumi uliokuwa umezagaa kwamba amefariki katika ajali ya gari iliyotokea hivi karibuni katika barabara ya Benin mjini Lagos.
Katika taarifa yake aliyoituma kwa vyombo vya habari, Iyke alisema amestushwa na taarifa hizo kwa sababu hazikuwa za kweli na kwamba yeye ni mzima wa afya njema.
Mbali na kuvumishiwa kifo, baadhi ya vyombo vya habari hivi karibuni viliripoti kuwa, Iyke ametekwa nyara na watu wasiojulikana na hajulikani mahali alipo.
“Hizi ni habari za uzushi mtupu. Mnaweza kuelewa ni kwa kiasi gani mama na familia yangu walipatwa na mshtuko kusikia taarifa hizi?” Alisema na kuhoji mwigizaji huyo.
“Familia yangu nzima ilichanganyikiwa kutokana na taarifa hizi za uzushi na hii si mara ya kwanza, nilizipuuza taarifa za awali, lakini kwa hizi za wakati huu siwezi kukaa kimya,”aliongeza.
Taarifa hiyo aliyoitoa Juni 6 mwaka huu ilieleza kuwa, anachukiwa na baadhi ya waandishi wa habari, wamiliki wa blogu na baadhi ya waigizaji wenzake ndio sababu amekuwa akizushiwa mambo ya uongo mara kwa mara.
Iyke alisema kuna wakati aliwahi kuzushiwa kwamba anajihusisha na utumiaji na biashara ya dawa za kulevya na haelewi taarifa hizi huwa zinatoka wapi na kwa nani.
“Mimi ni mlengwa mkuu wa taarifa hizi za uzushi, ambazo zimekuwa zikiwaathiri kwa kiasi kikubwa familia yangu na watu wanaonipenda,”alisema.
“Wamekuwa wakipanga kuniangamiza na kuniangusha, lakini wanashindwa kuelewa kwamba mimi si nyota. Siwezi kuangushwa na watu wenye malengo mabaya juu yangu. Mimi ni zao la madhehebu ya Jehovah. Nang’ara kama jua. Mungu atawalaani wote wanaonitakia mabaya,”aliongeza.

No comments:

Post a Comment