KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, June 9, 2011

IRENE UWOYA: Hakuna kitu kizuri kama kuitwa mama







MCHEZA filamu nyota wa kike nchini, Irene Uwoya amesema hakuna kitu kizuri kwa mwanamke kama kuwa na mtoto na kuitwa mama.
Akihojiwa katika kipindi cha Take One kilichorushwa hewani na kituo cha televisheni cha Clouds hivi karibuni, Irene alisema amekuwa mtu mwenye furaha kubwa tangu alipojifungua kiasi kwamba wakati mwingine huchanganyikiwa.
“Kwa kweli najisikia furaha sana. Sikutarajia iwapo siku moja nitakuwa mama. Nilikuwa naogopa siku ya kujifungua. Nilisikia watu wanasema leba shughuli yake ni nzito,”alisema.
Irene, ambaye ni mke wa mchezaji wa zamani wa Yanga, Hamad Ndikumana na mama wa mtoto Krish alisema, alitamani ajifungue kwa njia ya kawaida, lakini daktari alisema isingewezekana kwa sababu mtoto alikuwa mkubwa.
Mcheza filamu huyo alisema alipatwa na woga mkubwa siku ya kujifungua, hasa baada ya kuambiwa kwamba atafanyiwa operesheni.
“Uchungu niliusikia, lakini haikuwa sana. Nilisikia maumivu ya kawaida,”alisema mwanamama huyo mwenye sura na umbo lenye mvuto.
Irene alisema kabla hajaondoka nchini kwenda Burundi, tayari alishakuwa na uja uzito wa mumewe na wakati alipocheza filamu ya Senior Bachelor ya Jacob Steven (JB), alikuwa na uja uzito wa miezi minne.
Alisema katika kipindi chote cha uja uzito, hakuwahi kupatwa na matatizo na kwamba alijiona akiwa katika hali ya kawaida. Alisema hakuwahi kutapika wala kujisikia vibaya kama inavyotokea kwa wanawake wengine.
“Nilikuwa nafanya kila kitu. Nilikuwa nakula kila kitu na hata disco nilikuwa nakwenda,”alisema.
Irene alisema siku ya kujifungua ilipofika, alikwenda hospitali kama kawaida na kupangiwa muda wa kufanyiwa operesheni, lakini daktari alitaka athibitishe iwapo muda wake wa kujifungua ulishafika.
Alisema baada ya kufanyiwa vipimo, akawa anajiandaa kurudi nyumbani, lakini daktari alimzuia kuondoka na kumtaka aelekee chumba cha upasuaji muda huo huo.
Kwa mujibu wa Irene, baada ya kuingia kwenye chumba hicho, alisali na kumuomba Mungu ajifungue salama. Alisema aliweza kushuhudia kwa macho kila kilichokuwa kikitendeka kwa sababu mwili ulikuwa na ganzi kidogo.
“Niliona kila kilichokuwa kikifanyika kwa sababu sikuwa na ganzi mwili mzima. Kuna wakati walikuwa wananiongelesha. Mpaka mtoto alipokuwa anatoka, niliweza kumuona. Sikuogopa kwa sababu nilikuwa na hamu ya kuona wanachofanya,”alisema.
Irene alisema ameamua kumpa mtoto wake jina ka Krish kutokana na kuvutiwa na mwigizaji mmoja wa Kihindi. Mwigizaji huyo mtoto alicheza filamu hiyo kwa kutumia jina la Krish.
Alisema licha ya kuwa bado mdogo, mtoto wake huyo ameshaanza kuonyesha tabia za kisanii kwa kufanya vitendo vya kiuigizaji kila anapombeba ama kuwa naye karibu.
“Nikimweka chini, anaamka, nikimbeba anajidai amelala, akiniona naondoka, analia. Usiku mzima huwa halali, anakesha akilia,”alisema.
Irene alisema bado hajaona tofauti kubwa ya maisha baada ya kujifungua kwa sababu ni mapema mno. Alisema alichokibaini kwa sasa ni kutingwa na majukumu mengi ya kifamilia.
“Kwa kweli nina furaha hadi nachanganyikiwa. Hakuna kitu kizuri kama kuwa na mtoto na kuitwa mama,”alisema mcheza filamu huyo aliyeng’ara katika filamu ya Offside.
“Natoa mwito kwa wanawake wenzangu, wasiogope kubeba uja uzito. Baadhi ya wanawake wanadhani baada ya kujifungua miili yao itaharibika, hii si kweli hata kidogo,”aliongeza.
Mwanamama huyo alisema ameshakamilisha uandaaji wa filamu yake ya kwanza, inayojulikana kwa jina la Eagle Eyes, ambayo inatarajiwa kutoka hivi karibuni.
Alisema amecheza filamu hiyo kwa kushirikiana na waigizaji mbalimbali nyota nchini kama vile JB, Johari, Jackline Wolper, Dude, Tino na Steve.

No comments:

Post a Comment