KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, June 2, 2011

Simba, Yanga kuvaana Agosti 13

WATANI wa jadi wa soka nchini, Simba na Yanga wanatarajiwa kumenyana Agosti 13 mwaka huu katika mechi ya kuwania Ngao ya Hisani.
Mechi hiyo, ambayo huchezwa kila mwaka, ni maalumu kwa ajili ya ufunguzi wa michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara, ambayo inatarajiwa kuanza Agosti 20 mwaka huu.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, mechi hiyo itapigwa kwenye Uwanja wa Taifa.
Wambura alisema tayari shirikisho lake limeshaandaa kalenda yake ya matukio kwa mwaka 2011/2012, ambapo kipindi cha kwanza cha matayarisho ya msimu kinaanza Juni Mosi (jana) hadi Agosti 13 mwaka huu.
Ofisa huyo alisema kipindi cha kwanza cha uhamisho kinaanza Juni Mosi hadi Julai 15, ambapo usajili wa kwanza utakuwa Juni Mosi hadi Julai 20. Aliongeza kuwa, kutangaza wachezaji wa kuachwa na kusitisha mikataba ni kuanzia Juni Mosi hadi 21 mwaka huu wakati kupitia majina na kutangaza pingamizi ni kati ya Julai 21-31 mwaka huu. Kwa mujibu wa Wambura, kipindi cha pili cha uhamisho kitaanza Novemba Mosi hadi 20 mwaka huu wakati usajili utaanza Novemba Mosi hadi 30 mwaka huu.
Aliongeza kuwa, ratiba ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara inatarajiwa kutoka Julai 20 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment