KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, June 9, 2011

LLYOD NCHUNGA: Nitahakikisha Yanga inajiendesha kibiashara


SWALI: Hongera sana mwenyekiti kwa kuiongoza Yanga kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya Tanzania Bara msimu huu.
JIBU: Asante sana ndugu yangu, nashukuru. Lakini nadhani pongezi hizi zinawastahili zaidi wachezaji, viongozi wenzangu, wanachama pamoja na mashabiki kwa kuiunga mkono timu yao muda wote wa ligi.
SWALI: Nini matarajio yenu katika michuano ijayo ya ligi kuu na ile ya klabu bingwa barani Afrika?
JIBU: Kwanza kabisa tumepanga kufanya usajili kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha tunaendelea kufanya vizuri katika michuano ijayo ya ligi kuu.
Uongozi wangu umeunda kamati mbalimbali kwa ajili ya kusimamia shughuli za klabu. Kamati ya usajili ipo chini ya Salum Rupia na Seif Mohamed.
Kutokana na kamati hiyo kuundwa na watu makini, utaona kuwa, tumeweza kusajili wachezaji kadhaa wazuri kutoka ndani na nje ya nchi. Lengo ni kukiboresha zaidi kikosi chetu si kusajili timu mpya.
Tunatarajia kazi hii itakamilika Juni 22 mwaka huu kabla ya Kocha Sam Timbe kukabidhiwa orodha ya wachezaji waliosajiliwa kwa ajili ya msimu ujao. Wachezaji hao ni wale, ambao yeye mwenyewe aliwapendekeza.
SWALI: Pamoja na maelezo yako mazuri, katika siku za hivi karibuni kumekuwepo na taarifa kwamba, kuna baadhi ya wachezaji mmeshindwa kumalizana nao kutokana na matatizo ya pesa. Je, taarifa hizi ni za kweli?
JIBU: Unajua sisi tunafanyakazi zetu kwa umakini. Kila mtu anapaswa kuhakikisha kwamba ametimiza majukumu yake. Kamati ya usajili ndiyo yenye jukumu la kuhakikisha kuwa, kazi hiyo inakamilika kwa muda uliopangwa na inafanyika kwa ufanisi mkubwa. Hivyo si kweli kwamba tumeshindwa kutimiza kazi hiyo.
Ninachoweza kukuhakikishia ni kwamba kazi hiyo inakwenda vizuri na wapo baadhi ya wadau wa Yanga, ambao wamekuwa wakijitolea kwa hali na mali kuifanikisha. Na hivi karibuni tuliitisha harambee ya wanachama kwa ajili ya kuichangia timu pale hoteli ya Regency na nashukuru kwamba mambo yalikwenda vizuri.
SWALI: Mbona kuna taarifa kwamba wajumbe wengi waliopewa mwaliko hawakufika?
JIBU: Siyo kweli hata kidogo. Napenda nikueleze kwamba watu wanaendelea kuchangia pesa za usajili na kazi hiyo inaendelea bila matatizo. Subiri uone, itakapofika Juni 22, kikosi chetu kitakuwa tayari kimekamilika. Kitakuwa kikosi cha mauaji.
SWALI: Vipi suala la uhamisho wa Haruna Niyonzima kutoka APR ya Rwanda?
JIBU: Taarifa ambazo ninazo hadi sasa kutoka kamati yetu ya usajili zinaeleza kwamba, usajili wa mchezaji huyo unaendelea vizuri na tunasubiri ligi kuu ya Rwanda imalizike ili aje nchini kukamilisha taratibu za kujiunga na Yanga.
Nina imani na kamati yetu kwamba itaweza kufanikisha ujio wa mchezaji huyo kutokana na kuwepo watu makini na wenye uwezo wa kazi hiyo.
SWALI: Unazungumziaje kuhusu taratibu za usajili wa wachezaji watano kutoka nje ya nchi badala ya 10 kama ilivyokuwa msimu uliopita?
JIBU: Kwa kweli hapo bado kuna tatizo kidogo, lakini kwa vile utaratibu umeshapangwa, sina cha kusema kwa sababu sheria ni msumeno.
SWALI: Hivi karibuni tulisikia habari kwamba ulikuwa nchini Ghana kwa ajili ya kusaka wafadhili wa kuisaidia Yanga. Hebu tueleze ukweli wa habari hizo?
JIBU: Ni kweli nilikuwa nchini Ghana na niliweza kupata nafasi ya kuhudhuria tamasha la maendeleo ya soka barani Afrika. Huko nilikutana na baadhi ya viongozi wa taasisi nyingi za soka, ambao nitaendelea kuwasiliana nao ili kupata wadhamini wa kuisaidia klabu yangu.
Baadhi ya viongozi hao wameonyesha nia ya kuisaidia klabu yetu pamoja na soka la Tanzania. Tamasha hilo lilifanyika Mei 26 na 27 mjini Accra na pia lilihudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).
Pia walikuwepo watu mashuhuri kama vile Cyril Loisel, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Kombe la Dunia 2010 kule nchini Afrika Kusini.
Mwingine ni Danny Jordan, wajumbe kutoka Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na mashirika yasiyo ya kiserikali, ambayo baadhi ya viongozi wake niliweza kuzungumza nao.
Lakini jambo la kufurahisha ni kwamba, mkurugenzi anayesimamia Ligi ya Bundesliga ya Ujerumani, Jog Daubitzer ameahidi kuwa atafanya juhudi za kuanzisha uhusiano wa karibu kati ya klabu hizi mbili kuitangaaza nchini kwao.
Pia Mkurugenzi wa Masoko wa Super Sport, Gary Rathbone aliniahidi kuwa, watafanya jitihada za kurusha matangazo kuhusu Yanga.Haya yote ni miongoni mwa mambo, ambayo tumepania kuyafanya ndani ya mwaka huu ili Yanga iweze kuepuka kuwa tegemezi.
Chini ya uongozi wangu, tumepania kuhakikisha kuwa, mali za klabu zinatumika ipasavyo ili kuiletea maendeleo Yanga na wanachama wake kwa ujumla.
SWALI: Vipi kuhusu mpango wako wa kuanzisha Saccos ya wanachama ndani ya klabu ya Yanga?
JIBU: Kwa upande wa kiuchumi, naweza kusema kuwa, bado naendelea kutumia elimu yangu ili kujenga uhusiano mzuri na taasisi kubwa ili kuanzisha SACCOS na baadaye benki ya Yanga.
Kazi hii inafanywa na wanachama, ambao wapo kwenye kamati ya uchumi. Hao wana watu wenye kujua mambo hayo kwa undani na mchakato bado unaendelea vizuri.
SWALI: Vipi kuhusu hatima ya adhabu mliyopewa na CECAFA?
JIBU: Mambo yanakwenda vizuri na hakuna wasiwasi kwamba tutamalizana nao ili kuhakikisha Yanga inaendelea kuwa na ushirikiano mzuri na CECAFA.
Tunasubiri taarifa ya kikao kati ya viongozi wa CECAFA na Yanga, ambacho kinatarajiwa kufanyika hivi karibuni. Lengo ni kumaliza tofauti zilizojitokeza kati yetu wakati wa mashindano ya Kombe la Kagame mwaka 2008.

No comments:

Post a Comment