KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, June 15, 2011

CHIOMA: Sijawahi kukumbwa na kashfa

LAGOS, Nigeria

MCHEZA filamu Chioma Chukwuka wa Nollywood amesema anamshukuru Mungu kwa kumuepusha na kashfa na matukio ya kufedhehesha kama yanayowakuta wasanii wengine maarufu nchini humo.
Chioma, ambaye hivi karibuni alifunga ndoa na mpenzi wake wa siku nyingi, Franklin Akpotu alisema wiki hii kuwa, licha ya kuwepo kwenye fani hiyo kwa miaka tisa, hajawahi kukumbwa na kashfa yoyote.
Mcheza filamu huyo alisema, amekuwa akijitahidi kwa kadri ya uwezo wake kujiepusha na matukio ya kashfa kwa lengo la kulinda hadhi yake na familia yake.
Chioma, ambaye pia ni mwanamuziki wa Injili, hivi karibuni aliibuka na albamu yake mpya ya muziki huyo, ambayo kwa sasa ipo sokoni na inafanya vizuri.
Mwigizaji huyo alisema anayafurahia maisha yake ya ndoa na kusisitiza kuwa, hayajaathiri kazi zake kwa sababu yeye na mumewe wanapendana na kuelewana.
“Ndoa ni uhusiano mzuri kati ya wawili wapendanao. Ni kitu ambacho huwezi kukiota, unatakiwa kukielewa vyema,”alisema.
Chioma alisema siku ya kwanza alipokutana na mumewe huyo, kila mmoja alitokea kumpenda mwenzake na hivyo ndivyo uhusiano wao ulivyoanza na kufikia hatua ya kufunga ndoa.
Mwanamama huyo mwenye watoto wawili alisema, hana sehemu maalumu katika mwili wake, inayowavutia zaidi wanaume kwa sababu anaamini yeye ni mrembo kuanzia kichwani hadi unyayoni.

No comments:

Post a Comment