KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, June 2, 2011

NELLY KAMWELU: Nitawasaidia wanawake wenye saratani ya matiti

NELLY Kamwelu (katikati) akiwa na mshindi wa pili, Neema Kilango (kushoto) na mshindi wa tatu, Yacoba Assenga mara baada ya kutangazwa kwa matokeo ya shindano la Miss Universe 2011 wiki iliyopita.

NELLY akiwa katika picha ya pamoja na mrembo wa mwaka jana, Hellen Dausen.


MSHINDI wa taji la Miss Universe 2011, Nelly Kamwelu amesema atajikita zaidi katika kuwasaidia wanawake wanaosumbuliwa na ugonjwa wa kansa ya matiti.
Mbali na kuwasaidia wanawake wanaosumbuliwa na ugonjwa huo, Nelly amesema atalitumia taji lake na muda wake mwingi kutetea haki za wanyama.
Nelly (18) alisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita alipokuwa akihojiwa na kituo cha televisheni cha TBC 1 kuhusu malengo yake baada ya kushinda taji hilo.
Mrembo huyo mwenye rangi na sura yenye mvuto, alishinda taji hilo wiki iliyopita baada ya kuwabwaga washiriki wenzake 18 katika shindano lililofanyika kwenye ukumbi wa Golden Tulip mjini Dar es Salaam.
Katika shindano hilo lililodhaminiwa na Kampuni ya Simu za Mkononi ya Vodacom, mshindi wa pili alikuwa Neema Kilango wakati nafasi ya tatu ilinyakuliwa na Yacoba Assenga.
Kwa ushindi huo, Nelly ataiwakilisha Tanzania katika shindano la dunia la Miss Universe litakalofanyika baadaye mwaka huu mjini Sao Paulo nchini Brazil.
Ushindi huo pia ulimwezesha Nelly kuzawadiwa kitita cha sh. milioni tatu, kozi ya masomo ya mawasiliano ya umma na utengenezaji wa filamu katika Chuo cha New York Film Academy cha Marekani na tiketi tatu za ndege kwa ajili ya safari za kazi za jamii kutoka Kampuni ya Precision Air.
Zawadi zingine zilizotolewa kwa mrembo huyo kupitia wadhamini mbalimbali ni pamoja na simu aina ya Blackberry, vipodozi vyenye thamani ya sh 350,000.
Kwa kushika nafasi ya pili, Neema alizawadiwa sh. milioni moja na tiketi ya kushiriki katika shindano la Miss Earth wakati Yacoba alizawadiwa sh. 500,000 na tiketi ya kushiriki shindano la Miss International.
Nelly amekuwa mrembo wa nne kushinda taji la Miss Universe Tanzania, tangu mashindano hayo yalipoanzishwa mwaka 2007. Wa kwanza alikuwa Flaviana Matata, aliyefuatiwa na Amanda Sululu (2008), Illuminata James (2009), Hellen Dausen (2011).
“Kwa kweli nilijisikia furaha kubwa sana kushinda taji hili,”alisema Nelly. “Sikuwa nategemea kushinda. Furaha yangu ilizidi pale nilipomuona mama akilia. Hakuwa akitegemea. Alinigusa sana.”
Mrembo huyo mantashau alisema, kulikuwa na changamoto nyingi wakati wakiwa kambini kwa sababu washiriki karibu wote walikuwa na mvuto na sifa zinazofanana.
“Sijasema mimi sio mzuri, lakini nilikuwa na presha kwa sababu warembo wote walikuwa wazuri na wenye akili,”alisema.
Nelly, ambaye ni mchanganyiko wa makabila ya Kimanyema na Kifipa alisema, amepania kufuta aibu ya kuvurunda katika mashindano ya dunia kwa kuanza maandalizi mapema.
Alisema anategemea kupata msaada mkubwa wa maandalizi kutoka kwa wazazi wake, waandaaji wa mashindano hayo nchini pamoja na wadau mbalimbali.
Mrembo huyo alisema hatarajii kufanya maajabu katika shindano la dunia, lakini lengo lake kubwa ni kufika hatua za mbali. Flaviana ndiye mrembo pekee aliyefika hatua ya 10 bora mwaka 2007.
“Vitendo huzungumza zaidi kuliko maneno. Nitajitahidi kadri ninavyoweza kufanya vizuri katika shindano la dunia,”alisema.
Alipoulizwa kuhusu malengo yake katika kuisaidia jamii, mrembo huyo alisema atajikita zaidi katika kuwasaidia wanawake wanaosumbuliwa na ugonjwa wa kansa ya matiti na pia kutetea haki za wanyama.
“Hii ni ndoto yangu tangu nilipokuwa mdogo. Nilikuwa nimejiwekea lengo hilo kwa sababu shangazi yangu alikufa kwa ugonjwa huu. Iliniuma sana,”alisema mrembo huyo, ambaye alishika nafasi ya pili katika mashindano ya Miss Dar City Centre na Miss Ilala mwaka 2008.
Kwa upande wake, mratibu wa mashindano hayo hapa nchini, Maria Sarungi alisema wameridhishwa na ushindi wa Nelly kwa sababu anakidhi vigezo vyote vinavyotakiwa.
Alisema kabla ya shindano hilo, washiriki waliulizwa maswali na majaji kuhusu mambo mbalimbali kwa lengo la kupimwa ufahamu wao, hasa ikizingatiwa kuwa, hatua inayofuata na kwenda kushiriki mashindano ya kimataifa.
Maria alisema hadi sasa anafurahia mafanikio waliyoyapata baadhi ya washindi wa mashindano hayo miaka iliyopita na kuongeza kuwa, baadhi yao wamekuwa mfano wa kuigwa na jamii.
Alitoa mfano wa Flaviana, ambaye alisema kwa sasa anafanya vizuri katika fani ya mitindo ya mavazi nchini Marekani na picha zake zimekuwa zikitumika kupamba majarida mbalimbali ya nchi hiyo.
“Flaviana ana malengo mengi mazuri, anataka kuanzisha taasisi yake mwenyewe. Kwa sasa anafanyakazi chini ya mashirika mbalimbali,”alisema.
Alimtaja mrembo mwingine kuwa ni Miriam Odemba, ambaye kwa sasa ana mtoto mmoja. Alisema mrembo huyo anatarajia kurejea kwenye fani ya uanamitindo hivi karibuni.

No comments:

Post a Comment