KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, June 23, 2011

LUKA MODRIC ANAVYOIPASUA KICHWA TOTTENHAM


LONDON, England
WAKATI klabu ya Tottenham ya England ikihaha kumbakisha kiungo wake, Luka Modric msimu ujao, mchezaji huyo amesisitiza kuwa, anataka kuondoka na kujiunga na Chelsea.
Modric (25) alielezea msimamo wake huo wiki hii huku klabu ya Chelsea ikiwa inajiandaa kuwasilisha maombo ya kumsajili mchezaji huyo wa kimataifa wa Croatia kwa mara ya pili.
Kiungo huyo alisema anataka kujiunga na Chelsea kwa vile moja ya malengo yake makubwa ni kushinda taji la ligi kuu ya England na mengineyo.
Akihojiwa na gazeti la Daily Mail la Uingereza akiwa mapumzikoni, mchezaji huyo alisema: “Nataka kuondoka Tottenham kama rafiki. Nimefurahia kuwepo kwangu hapa, lakini sasa ni wakati mwafaka kwangu kutafuta klabu nyingine.”
“Nilikuwa na makubaliano na mwenyekiti. Wakati nilipotia saini mkataba wangu mpya, alisema kwamba, kama klabu nyingine itatokea na kutaka kunisajili, wataifikiria ofa yao,”aliongeza.
Awali, Chelsea iliwasilisha maombi kwa Tottenham ya kutaka kumsajili kiungo huyo kwa pauni milioni 22 za Uingereza, lakini yalikataliwa. Kwa sasa, klabu hiyo inajiandaa kuongeza dau lingine na kufika pauni milioni 30.
Mbali na dau hilo, Chelsea inataka kumsajili Modric kwa kubadilishana na kiungo wake, Michael Essien.
“Chelsea ni klabu kubwa na mmiliki wake ni mtu mwenye mvuto. Wanao wachezaji wazuri na malengo yao ni kupigania mataji na kutwaa ubingwa wa ligi ya Ulaya.
“Nataka kubaki London. Nafurahia kuwepo hapa kama ilivyo kwa familia yangu. Naupenda mji huu,”alisema kiungo huyo.
Kauli ya Modric kwamba anapenda kubaki London, imezivutia klabu za Manchester United na Manchester City, lakini hazijasema lolote ama kuwasilisha maombi ya kumsajili.
“Sitaki kuwa na mabishano na Tottenham,”alisema Modric. “Mashabiki wamekuwa wazuri sana kwangu na nimeufurahia muda wote niliochezea klabu hii, lakini ni kwa sababu ya soka, wachezaji wanahama kutoka klabu moja hadi nyingine. Imewahi kutokea hivyo kwa Tottenham huko nyuma. Ni jambo la kawaida kwa mchezaji kuwa na ndoto ya kuchezea klabu kubwa.”
Modric anatarajiwa kuzungumza na Mwenyekiti wa Tottenham, Daniel Levy kuhusu mipango ya uhamisho, lakini alisisitiza kuwa, uamuzi wake wa kuhama hauhusiani na masuala ya pesa.
“Kama atakuja mtu klabuni na ofa ni nzuri kwangu na wanaikubali, bila shaka nitahama. Ni jambo zuri kwa malengo yangu ya baadaye. Nahitaji kuchezea klabu inayotwaa mataji na kucheza katika ligi ya mabingwa wa Ulaya,”alisema.
“Hii haihusu mambo ya pesa, inahusu malengo. Wakati nilipokuja England, nilikuwa na ndoto ya kutwaa mataji. Hivyo ndivyo ilivyo hadi sasa,”alisema.
“Tottenham ni klabu kubwa, ikiwa na wachezaji wazuri na kocha mzuri, lakini nataka kupigania ubingwa. Siku zote Tottenham itakuwa na nafasi moyoni mwangu. Uzoefu wangu katika ligi ya mabingwa umeniacha niwe na kiu ya mafanikio makubwa zaidi,” aliongeza kiungo huyo.
Alipoulizwa nini kitafuata kutokana na msimamo wake huo, Modric alisema: “Nahitaji kuzungumza na mwenyekiti. Siwezi kumuuliza kuhusu uhamisho, hapana. Natumaini wanaweza kufikia makubaliano. Nipo mapumziko, lakini nahitaji kuzungumza na kuona kama naweza kupata suluhisho.”
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Tottenham, Daniel Levy amesisitiza msimamo wake wa awali kuwa, kiungo Luka Modric hatauzwa kwa gharama yoyote.
Levy alisema wiki hii kuwa, klabu yake haijajiandaa kumuuza kiungo huyo kwa Chelsea ama klabu nyingine yoyote.
“Tumeeleza wazi msimamo wetu kuhusu jambo hilo kwa kuiandikia Chelsea,”alisema Levy. “Walikataa kuutambua msimamo wetu huo na kutangaza ofa yao hadharani.”
Tottenham imeelezea msimamo wake huo baada ya Modric kulieleza gazeti la Daily Mail kwamba anataka kuhama. Hata hivyo, Modric hajawasilisha maombi binafsi ya kutaka kuhama.
Levy alisema kwa sasa, Tottenham inajenga timu imara kwa ajili ya baadaye ili iweze kucheza kwa kiwango cha juu na kusisitiza kuwa, hakuna mchezaji yeyote mingoni mwa wachezaji nyota atakayeuzwa msimu huu.
Msimamo huo wa Tottenham imekuja siku chache baada ya Kocha Mkuu wa timu hiyo, Harry Redknapp kukaririwa akisema kuwa, ofa iliyotolewa na Chelsea kwa kiungo huyo haikubaliki.
Redknapp alisema wapo wachezaji wanaoweza kuuzwa kwa kiwango hicho cha pesa, lakini si kwa mchezaji kama Modric, ambaye alikiri wazi kwamba pengo lake haliwezi kuzibika.
Alisema iwapo Tottenham inataka kupata maendeleo zaidi, haipaswi kumuuza Modric kwa vile ni miongoni mwa wachezaji muhimu katika klabu hiyo.
Kocha huyo alisema wanapaswa kufanya kila wanaloweza kumshawishi kiungo huyo abaki White Hart Lane.
Beki wa kulia wa Tottenham, ambaye pia anachezea timu ya taifa ya vijana wa chini ya miaka 21 ya England, Kyle Walker alisema litakuwa pigo kubwa kwa klabu hiyo iwapo Modric atauzwa.
“Huwa ni vigumu kumpokonya mpira wakati wa mazoezi, ni mzuri kucheza naye, mzuri kutoa pasi na ni mchezaji wa aina yake,”alisema Kyle.
Modric, ambaye alijiunga na Tottenham mwaka 2008 akitokea Dinamo Zagreb ya Croatia, ameifungia timu hiyo mabao 12 katika mechi 120. Usajili wake uliigharimu Tottenham pauni milioni 16.6.
Katika msimu wake wa pili ndani ya klabu hiyo, alikuwa mmoja wa wachezaji waliochangia kuiwezesha timu hiyo kufuzu kucheza ligi ya mabingwa wa Ulaya kwa mara ya kwanza.
Mwaka jana, Modric alitia saini mkataba mpya wa kuichezea timu hiyo kwa miaka sita.
Hata hivyo, akihojiwa na gazeti la Jutarnji List la Croatia mwezi uliopita, Modric alisema iwapo itakuja ofa nzuri kwake na Tottenham, uwezekano wa kuhama ni mkubwa.
WASIFU WA LUKA MODRIC
Alizaliwa Septemba 9, 1985

Anacheza nafasi ya kiungo

Ni mchezaji wa Tottenham

Mechi yake ya kwanza ilikuwa dhidi ya Norwich City 2008

Ameifungia timu hiyo mabao 12

Ameichezea mechi 120

Klabu alizochezea awali ni Dinamo Zagreb, Zrinjski Mostar (mkopo), Inter Zapresic (mkopo)

No comments:

Post a Comment