KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, June 2, 2011

Kado alamba mamilioni Yanga



KIPA wa timu ya soka ya Mtibwa Sugar, Shaaban Kado amekubali kutia saini mkataba wa miaka miwili wa kuichezea Yanga wenye thamani ya sh. milioni 13.
Taarifa za uhakika zilizopatikana jana kutoka ndani ya Kamati ya Usajili ya Yanga zimeeleza kuwa, Kado alitia saini mkataba huo wiki iliyopita.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, uongozi wa Mtibwa Sugar umeshafikia makubaliano na Yanga kuhusu usajili wa kipa huyo.
Kado, ambaye pia yumo kwenye kikosi cha timu ya Taifa, Taifa Stars anakuwa kipa wa tatu kusajiliwa na Yanga kwa ajili ya msimu ujao. Wengine ni Yaw Berko kutoka Ghana na Mohamed Saidi kutoka Majimaji.
Mabingwa hao wa soka wa Tanzania Bara, wameamua kumsajili Kado kwa lengo la kukiongezea nguvu kikosi hicho, ambacho mwakani kitashiriki michuano ya klabu bingwa Afrika.
Tayari Yanga imeshatangaza kuwaacha wachezaji wake kadhaa, wakiwemo makipa Ivan Knezevic kutoka Serbia na Onesmo Kimathi, ambaye kuna habari kuwa, huenda akauzwa kwa mkopo.
Ivan ameichezea Yanga msimu mmoja tu na kudaka mechi chache za ligi baada ya kuonekana kiwango chake kipo chini. Kipa huyo alisajiliwa na kocha wa zamani wa timu hiyo, Kostadin Papic. Makamu Mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Yanga, Seif Ahmed hakuwa tayari kuthibitisha ama kukataa kuhusu kusajiliwa kwa Kado. Hata hivyo, alisema wakati utakapowadia, watatoa taarifa kwa vyombo vya habari.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mtibwa Sugar, Jamal Bayser ameutaka uongozi wa Yanga kwenda kumalizana nao ili mchezaji huyo aweze kupata uhamisho.
Usajili wa wachezaji kwa ajili ya msimu ujao ulianza rasmi jana, ambapo timu kadhaa zitakazoshiriki ligi kuu msimu ujao zimeshaanza kusajili nyota wapya.

Wakati huo huo, Kado, aliyeichezea Mtibwa Sugar katika ligi kuu ya Tanzania Bara msimu uliopita, amesema hakulazimishwa kujiunga na klabu ya Yanga.
Kado alisema mjini Dar es Salaam juzi kuwa, uamuzi wake wa kujiunga na mabingwa hao wa Tanzania Bara ulitokana na mapenzi yake mwenyewe.
“Mimi ni mtu mzima na nina uwezo wa kuamua mambo yangu mwenyewe. Hakuna mtu aliyenishinikiza kuondoka Mtibwa na kujiunga na Yanga,”alisema.
Kipa huyo, ambaye pia yumo kwenye kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars alisema lengo lake kubwa ni kukuza kipaji chake kwa kucheza michuano ya kimataifa.
Kado atakuwa kipa wa tatu kusajiliwa na Yanga kwa ajili ya msimu ujao. Wengine ni Yaw Berko kutoka Ghana na Mohamed Saidi, aliyesajiliwa kutoka Majimaji.
Kwa mujibu wa Kado, anapenda kupigania namba kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga kwa sababu kufanya hivyo kutamwezesha kuwa fiti zaidi kiuchezaji.
“Najua kwamba nakwenda kupambana na makipa wenzangu wawili kusaka namba. Hii ni changamoto kubwa sana kwangu,”alisema.
Alimsifu Berko kuwa ni kipa mzuri na alitoa msaada mkubwa ulioiwezesha Yanga kutwaa ubingwa wa ligi kuu msimu huu kwa tofauti ya magoli kati yake na Simba.

No comments:

Post a Comment