KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, June 15, 2011

Cannavaro azua balaa Yanga


WAKATI kikosi cha timu ya soka ya Yanga kikiwa kimeshaanza mazoezi rasmi kwa ajili ya michuano ijayo ya ligi kuu ya Tanzania Bara, beki Nadir Haroub 'Canavaro' amegoma kuanza mazoezi.
Habari za uhakika zilizopatikana jana kutoka ndani ya Yanga zimeeleza kuwa, Canavaro amegoma kuanza mazoezi kutokana na kutokamilishiwa malipo yake ya mkataba mpya na ule wa zamani.
Kwa mujibu wa habari hizo, Canavaro ameapa kutohudhuria mazoezi hadi atakapokamilishiwa malipo yake. Hata hivyo, haikuweza kujulikana mara moja kiasi cha pesa, ambacho mchezaji huyo anaidai Yanga.
Uchunguzi wa Burudani umebaini kuwa, kwa sasa Canavaro yupo nyumbani kwao visiwani Zanzibar, ambako alikwenda kwa mapumziko baada ya kurejea nchini kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Kuna habari kuwa, Canavaro hakumaliziwa malipo yake ya mkataba wa zamani na pia hajalipwa pesa zote za mkataba wake mpya.
Mmoja wa wachezaji, aliye karibu na Canavaro, ambaye hakupenda jina lake litajwe gazetini, alithibitisha jana kuhusu uamuzi wa mchezaji huyo kugomea mazoezi hadi atakapokamilishiwa malipo yake.
Mbali na nyota huyo, kuna habari pia kuwa, wachezaji wengine kadhaa wa Yanga nao wamepanga kugomea mazoezi iwapo hawatamaliziwa pesa zao za mikataba mipya.
Wachezaji hao wamepanga kuendesha mgomo huo kabla ya kuanza kwa michuano ya Kombe la Kagame, iliyopangwa kuanza Juni 25 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Hii itakuwa mara ya pili kwa wachezaji wa Yanga kupanga kugoma kwa lengo la kushinikiza walipwe malipo yao. Waliwahi kufanya hivyo mwanzoni mwa mwaka huu kabla ya ligi kuu ya msimu uliopita kumalizika.
Mgomo huo ulisababisha mfadhili mkuu wa klabu hiyo, Yusuph Manji kuitisha mikataba yao ili kujua madeni yote ya wachezaji, ambapo ilibainika kuwa, wachezaji wengi walisajiliwa kwa malipo kiduchu.
Hata hivyo, viongozi wa Yanga hawakuwa tayari kuzungumzia suala la Canavaro, lakini mmoja wa viongozi hao alisema, anachotambua ni kwamba beki huyo alitakiwa kuripoti mazoezi na wenzake Jumatatu iliyopita.
Wachezaji wa Yanga walianza mazoezi wakiwa chini ya kocha msaidizi wa timu hiyo, Fred Felix Minziro. Mazoezi hayo yanafanyika kwenye uwanja wa Kaunda, Dar es Salaam.
Wakati huo huo, Yanga inatarajiwa kushuka dimbani Jumamosi kucheza na kombaini ya Dar es Salaam katika mechi ya kirafiki itakayopigwa kwenye uwanja wa Kaunda.

No comments:

Post a Comment