KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, June 2, 2011

MAPOKEZI YA SAMATTA CONGO USIPIME!


MSHAMBULIAJI mpya wa klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Mbwana Samatta wiki iliyopita alitambulishwa rasmi kwa viongozi na mashabiki wa klabu hiyo katika hafla maalumu iliyofanyika kwenye uwanja mpya wa timu hiyo uliopo mjini Lubumbashi.
Samatta alitambulishwa kwa mashabiki hao na Rais wa klabu hiyo, Moise Katumbi na kuamsha shangwe, hoi hoi na nderemo.
Mara baada ya kutambulishwa, mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba alipewa nafasi ya kuzungumza na mashabiki wa klabu hiyo.
Samatta aliushukuru uongozi wa TP Mazembe kwa kumsajili na kuahidi kufanya kila analoweza kutoa mchango mkubwa kwa timu hiyo. Pia aliushukuru uongozi kwa mapokezi mazuri uliyompa alipowasili katika Jiji la Lubumbashi.
TP Mazembe imemsajili Samatta kwa kitita cha sh. milioni 150 baada ya kuvutiwa na uchezaji wake wakati timu hiyo ilipomenyana na Simba katika mechi ya raundi ya pili ya michuano ya klabu bingwa Afrika.
Simba ilitolewa na TP Mazembe kwa jumla ya mabao 6-3. Ilichapwa mabao 3-1 mjini Lubumbashi kabla ya kuchapwa mabao 3-2 mjini Dar es Salaam.
Mbali na Samatta, TP Mazembe pia imemsajili kiungo Patrick Ochan kutoka Simba kwa kitita hicho cha pesa.
Hata hivyo, TP Mazembe ilimzuia Samatta kuichezea Simba ilipomenyana na Wydad Casablanca ya Morocco katika mechi ya klabu bingwa Afrika, iliyochezwa wiki iliyopita mjini Cairo, Misri. Simba ilichapwa mabao 3-0.
Kwa sasa, Samatta yupo kwenye kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars kinachojiandaa kumenyana na Jamhuri ya Afrika ya Kati katika mechi ya michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Afrika za mwaka 2012.

No comments:

Post a Comment