KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, June 23, 2011

SERENA AMWAGA CHOZI


LONDON, England
MCHEZA tennis nyota duniani, Serena William wa Marekani juzi aliangua kilio baada ya kumbwaga Aravane Rezai wa Ufaransa katika mechi ya michuano ya tennis ya Wimbledon.
Katika mechi hiyo, iliyokuwa na ushindani mkali, Serena alimbwaga Aravane kwa seti 2-1 na kufanikiwa kusonga raundi ya pili.
Akihojiwa na waandishi wa habari baada ya mchezo huo, Serena alisema alishindwa kujizuia kutokwa na machozi kutokana na kushinda mchezo huo.
Serena alisema kutokana na kuumia mguu na kushindwa kushiriki michuano yoyote kwa mwaka mmoja, hakuwa na matarajio ya kurejea katika kiwango chake cha kawaida.
Binti huyo wa Kimarekani aliendelea kutokwa na machozi hata alipokuwa akiondoka kwenye viwanja vya Arena, ambako michuano hiyo inafanyika.
Serena alionekana mara kwa mara akipunga mkono mwa mashabiki wake huku akipangusa uso kufuta machozi yaliyokuwa yakimtoka.
“Kwa kawaida, huwa silii. Sielewi kwa nini imenitokea hivi,”alisema Serena.
“Imekuwa vigumu, kamwe sikuamini iwapo ningerejea uwanjani. Ulikuwa mwaka mgumu kwangi na sikutarajia iwapo ningecheza tena ama kufanya chochote. Nilitaka kushinda mechi angalau moja tu katika michuano hii ya Wimbledon,”aliongeza.

No comments:

Post a Comment