KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Tuesday, January 22, 2013

NAPATA TABU KUCHAGUA MWANAMKE WA KUOA-UKWA

LAGOS, Nigeria

MCHEZA filamu machachari wa Nigeria, Osita Iheme, maarufu zaidi kwa jina la Ukwa amesema anapata tabu kuchagua mwanamke wa kufunga naye ndoa.

Akihojiwa na mtandao wa Express Entertainment wiki iliyopita, Ukwa alisema ana marafiki wengi wa kike, lakini kila linapokuja suala la kuchagua mke, anashikwa na kigugumizi.

"Tatizo ni kwamba sielewi nani anayenifaa kumuoa. Ninao marafiki wengi wa kike na mashabiki, lakini nashindwa," alisema mcheza filamu huyo mwenye umbo fupi.

"Kumchagua mtu, ambaye nitaishi naye maisha yangu yote ndicho kinachonichelewesha kufunga ndoa. Mungu atanisaidia kuamua hivi karibuni kwa sababu kwake, kila kitu kinawezekana,"aliongeza.

Ukwa alianza kupata umaarufu mwaka 2002 baada ya kushirikiana na Chinedu Ikedieze 'Aki' kucheza filamu ya Aki na Ukwa na tangu wakati huo, wamekuwa marafiki wakubwa.

Hata hivyo, Aki aliamua kuachana na maisha ya ukapera mwaka juzi baada ya kufunga ndoa, hali inayomfanya Ukwa ajihisi kuwa mpweke.

Mapema mwaka jana, Ukwa alisema bado hajajua ni lini atafunga ndoa na atamuoa nani.

Ukwa alielezea msimamo wake huo, kufuatia ndugu, jamaa na marafiki kumuhoji mara kwa mara wakitaka kujua ni lini atafunga ndoa.

Ukwa alikiri kuwa, anajisikia vibaya kuona kuwa, swahiba wake huyo amefunga ndoa huku yeye akiwa bado anamsaka mchumba wa kumuoa.

"Sielewi lini nitafunga ndoa, lakini naelewa kwamba wakati utakapofika, kila mmoja atafahamu. Siwezi kueleza ni lini nitafanya hivyo," alisema Ukwa.

"Mungu ananitayarishia njia kwa ajili yangu nami naelekea katika njia hiyo. Nitakapofika, kila mmoja atafahamu."

"Siwezi kusema kama tayari ninaye mchumba ninayetarajia kufunga naye ndoa. Wapo wanawake wengi sehemu mbali mbali duniani. Ni jukumu langu kumsikiliza Mungu atakapozungumza nami na kunionyesha mwanamke sahihi. Wakati utakapofika, nitachagua mwanamke huyo,"alisema Ukwa.

OMOTOLA AANDAA ALBAMU MPYA, KUMSHIRIKISHA AKON

LAGOS, Nigeria

MWITE vyovyote upendavyo, iwe Omotola Jalade, Omo Sex au Omo Milionea, lakini ukweli ni kwamba mwanadada huyo ni sawa na samaki mkubwa ndani ya bahari kubwa.

Katika kudhihirisha ukweli huo, Omotola hivi sasa yupo katika maandalizi ya mwisho ya kurekodi albamu yake mpya ya muziki, kupitia Kampuni na Konvict Music, inayomilikiwa na mwanamuziki nyota wa Nigeria, Akon.

 Omotola ameamua kurekodi albamu hiyo baada ya kuwa kimya kwa kipindi kirefu, akiwa ameelekeza zaidi nguvu zake katika fani ya uigizaji filamu, ambayo imempatia mafanikio makubwa.

Mbali na kucheza filamu, mwanadada huyo, ambaye ni mke wa rubani Matthew Ekeinde na mwenye watoto wanne, pia ameanzisha kipindi maalumu cha televisheni kinachojulikana kwa jina la The Real Omosex.

"Kwa sasa nafanya maandalizi ya kurekodi albamu mpya kupitia kwa watayarishaji muziki Kendrick Dean na Verse Simmonds wa Kampuni ya Konvict Music na tunatarajia kumshirikisha mwanamuziki mmoja maarufu,"alisema Omotola.

Hata hivyo, Omotola hakuwa tayari kutaja jina la mwanamuziki huyo, lakini kuna habari kuwa amepanga kumshirikisha Akon.

Omotola alianza kujuhusisha na muziki mwaka 2006 baada ya kuibuka na albamu yake ya kwanza, inayojulikana kwa jina la Gba kabla ya kuachia albamu ya pili inayokwenda kwa jina la Feel Alright.

Mwanamama huyo alirekodi albamu yake ya pili kwa kushirikiana na mwimbaji na mpiga gita la solo, Harrisong, ambaye pia ni mwalimu wake wa sauti.

Wanamuziki wengine alioshirikiana nao kurekodi albamu hiyo ni prodyuza Del B na mwimbaji Paul PlayDairo. Nyimbo zilizomo kwenye albamu hiyo zimepigwa katika miondoko ya Pop na Rock.

"Nyimbo zilizomo kwenye albamu yangu ya pili hazikuweza kupata umaarufu kirahisi. Ni nyimbo zilizolenga kutoa ujumbe. Lengo halikuwa kuvutia watu,"alisema mwanadada huyo mwenye sura na umbo lenye mvuto.

Alipoulizwa ni nani anayemuandikia nyimbo zake, Omotola alisema:" Naziandika mimi mwenyewe, isipokuwa kwa zile, ambazo ninawashirikisha wanamuziki wengine."

Baadhi ya nyimbo zilizomo kwenye albamu ya Feel Alright ni Get Busy, Harmony, Through the Fire na Barren Land. Kibao cha Barren Land kinaelezea matatizo ya chakula duniani.

Omotola kwa sasa anashika nafasi ya kwanza kwa utajiri miongoni mwa wacheza filamu wa kike nchini Nigeria. Utajiri wake unakadiriwa kufikia Naira milioni 200 za Nigeria.

Mbali na kucheza filamu nyingi, Omotola amerekodi albamu zaidi ya mbili za muziki wa dansi. Kwa kiasi kikubwa, mapato yake yanatokana na filamu, muziki na matangazo ya biashara.

“Ninachokifanya ni kutekeleza majukumu yangu ya siku hadi siku. Ninayatambua na pia nakabiliana nayo kila yanapokuja mbele yangu. Hakuna nisichoweza kukifanya. Kusema kweli nimekuwa na bahati," alisema Omotola.

“Naishi maisha yangu. Naamini kile ninachokiamini. Siishi maisha yangu kwa lengo la kumridhisha mtu yeyote, hivi ndivyo nilivyo.

“Msemo wangu niupendao ni kwamba, kile unachokiona ndicho unachokipata. Kamwe siwezi kusema chochote nyuma yako, ambacho siwezi kukisema mbele yako. Hivi ndivyo nilivyo,”alisema mwanamama huyo mantashau.

YANGA YAMZAWADIA NSAJIGWA

MJUMBE wa kamati ya utendaji ya Yanga, Abdalla Bin Kleb akimkabidhi mchezaji Shadrack Nsajigwa bahasha yenye sh. milioni 1.5 kutokana na kuwa mchezaji aliyeitumikia klabu hiyo kwa miaka mingi na pia kuwa mfano wa kuigwa na wenzake. Makabidhiano hayo yalifanyika wakati wa mkutano mkuu wa klabu hiyo uliofanyika jana kwenye bwalo la maofisa wa polisi, Oysterbay, Dar es Salaam. (Picha na Emmanuel Ndege)

LULU AOMBA DHAMANA MAHAKAMA KUU, MAOMBI YAKE KUSIKILIZWA IJUMAA

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, imepokea maombi ya dhamana ya msanii wa maigizo nchini, Elizabeth Michael 'Lulu' na imepanga kuyasikiliza Ijumaa wiki hii.

 Taarifa zilizopatikana mahakamani hapo wiki iliyopita zimeeleza kuwa, maombi hayo yamepangwa kusikilizwa mbele ya Jaji Zainabu Mruke.

Lulu, ambaye anasota rumande katika gereza la Segerea, anakabiliwa na mashitaka ya kumuua bila kukusudia, aliyekuwa msanii mwenzake, Steven Kanumba kinyume cha kifungu cha 195 cha Kanuni za Adhabu.

Awali msanii huyo alikuwa akikabiliwa na shitaka la kuuwa kwa kukusudia katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, lakini baada ya upelelezi kukamilika, Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), alimbadilishia mashitaka na kuwa ya kuua bila kukusudia.

Upande wa Jamhuri katika kesi hiyo, ulimsomea mshitakiwa huyo maelezo ya mashahidi Desemba 21, mwaka 2012. Baada ya kusomewa maelezo hayo, kesi hiyo ilihamishiwa Mahakama Kuu, ambayo ndiyo yenye uwezo wa kusikiliza mashitaka yanayomkabili.

Shauri hilo la kuua bila kukusudia tayari limesajiliwa na kupewa namba 125/2012 katika Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam.

Lulu kwa kupitia jopo la mawakili wanaomtetea, Kennedy Fungamtama, Peter Kibatala na Fulgence Masawe, amewasilisha maombi ya dhamana Mahakama Kuu kwa kuwa kosa linalomkabili linaweza kumfanya apate dhamana.

Mawakili hao wamewasilisha maombi hayo chini ya hati ya dharura, wakiomba yasikilizwe na kuamriwa mapema kwa kuwa Lulu amekaa rumande kwa miezi saba na kosa lake linadhaminika.

Kwa mujibu wa hati ya maombi, iliyoambatanishwa na hati ya kiapo, Wakili Kibatala kwa niaba ya mshtakiwa huyo, wanaiomba Mahakama iamuru mshitakiwa apewe dhamana, akiwa au bila kuwa na wadhamini, au kwa amri na masharti mengineyo ambayo itaona yanafaa.

"Tunaiomba Mahakama hii tukufu impe dhamana mshitakiwa akiwa na au bila kuwa na wadhamini, wakati akisubiri usikilizwaji na uamuzi wa kesi yake ya msingi, shauri la jinai namba 125 la 2012, lililopo katika mahakama hii tukufu,” ilisema sehemu ya hati ya maombi.

Wakili Kibatala pia ameeleza kupitia hati hiyo kwamba, muombaji anao wadhamini wa kuaminika, ambao wako tayari kufika mahakamani kama wadhamini kwa niaba yake.

Katika hati hiyo, Wakili Kibatala pia amedai kuwa, iwapo mshitakiwa atakubaliwa dhamana, yuko tayari na ataweza kutimiza masharti yote ya dhamana yatakayotolewa na mahakama.

Wakili Kibatala amedai kuwa kwa muda ambao ameiendesha kesi hiyo, amepata fursa kubwa ya kufahamiana na muombaji pamoja na familia yake na kwamba kwa msingi huo, anajua kuwa muombaji huyo ana tabia nzuri na ni wa kuaminika.

Wakili huyo pia ameeleza kupitia kwenye hati hiyo kwamba, muombaji bado yuko chini ya uangalizi wa wazazi wake, ambao wako tayari kuhakikisha anatimiza masharti na anafika mahakamani wakati wowote kadri atakavyohitajika kwa ajili ya usikilizwaji wa shauri lake au kusudi lolote.

“Muombaji ni mtu maarufu na mkazi wa Dar es Salaam, hivyo kwa mazingira haya ni rahisi kumfuatilia katika utekelezaji wa masharti yoyote ya dhamana. Kama wakili wake (Kibatala) niko tayari, kutimiza wajibu wangu kuhakikisha muombaji anatimia masharti yote kikamilifu na kufika mahakamani kadri na wakati atakapohitajika," alidai Wakili huyo.

Lulu anadaiwa kumuua Kanumba bila kukusudia, April 7, 2012, nyumbani kwake (Kanumba), Sinza Vatican, Dar es Salaam.

Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Shadrack Kimaro, umedai kuwa utaita mashahidi tisa wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo.

Kimaro pia aliieleza mahakama kuwa, atawasilisha vielezo kadhaa vitakavyotumika kama sehemu ya ushahidi katika kesi hiyo, ikiwemo ramani ya eneo la tukio kwenye chumba alimofia Kanumba, ripoti ya uchunguzi wa kifo na maelezo ya onyo ya Lulu.

SENDEU, MWESIGWA WAMJIA JUU MANJI

SIKU moja baada ya uongozi wa klabu ya Yanga kutangaza kuwafuta uanachama, aliyekuwa katibu mkuu, Celestine Mwesigwa na ofisa habari, Louis Sendeu, viongozi hao wa zamani wamesema uongozi umekurupuka.

Wakizungumza na Uhuru kwa nyakati tofauti mjini Dar es Salaam jana, Mwesigwa na Sendeu walisema, uongozi wa Yanga ulikurupuka kuwasilisha ajenda hiyo kwa wanachama bila kufuata katiba ya klabu hiyo.

Mwesigwa na Sendeu walifukuzwa kazi Agosti mwaka jana kwa madai ya kushindwa kutekeleza vyema majukumu yao kabla ya kufutwa uanachama juzi kwa kosa la kuishitaki klabu hiyo mahakamani.

Akifafanua, Mwesigwa alisema haiwezekani kwa uongozi kumfuta uanachama mwanachama wake kwa sababu ya kudai haki yake ya msingi.

Alisema haki ya mtu na mapenzi kwa klabu ni vitu viwili tofauti na kwamba walikuwa na kila sababu ya kudai haki yao mahakamani baada ya uongozi kushindwa kuwalipa madai yao.

Mwesigwa alisema kwa hali ilivyo, klabu ya Yanga kwa sasa inaelekea pabaya kutokana na mtu mmoja kuamua kila jambo bila kuomba ushauri wa viongozi wenzake.

"Ndani ya miezi minne ya uongozi mpya, wanachama watatu tumefutwa uanachama! Je, ukifika mwaka mmoja hali itakuwaje? Hii itakuwa klabu au mali ya mtu binafsi?" Alihoji Mwesigwa.

Alisema anachotambua ni kwamba bado yeye ni mwanachama halali wa Yanga na kwamba maamuzi yaliyotolewa na wanachama katika mkutano wa juzi yalilenga kumfurahisha mtu mmoja.

"Klabu ya Yanga kwa sasa ipo mikononi mwa mtu mmoja, ambaye akiamka asubuhi, anakuwa na uwezo wa kuamua lolote analotaka hata kama halina maslahi kwa wanachama," alisema Mwesigwa.

Katibu mkuu huyo wa zamani wa Yanga alisema, ataendelea kudai haki yake mahakamni hadi uongozi utakapoamua kumlipa madai yake kwa vile haki ya mtu haiwezi kupotea bure.

Kwa upande wake, Sendeu alisema kitendo cha uongozi wa Yanga kuwasilisha ajenda ya kuwajadili mbele ya wanachama ni sawa na kuidharau mahakamani kwa vile suala hilo tayari lipo mahakamani.

Sendeu alisema pia kuwa, uongozi wa Yanga ulifanya makosa kuwahukumu kabla ya kuwaita kwa ajili ya kuwahoji na kusikiliza utetezi wao.

Msemaji huyo wa zamani wa Yanga alisema pia kuwa, mkutano wa wanachama ulioitishwa juzi ni batili kwa vile wanachama hawakupewa ajenda siku 21 kabla ya mkutano kama katiba inavyoelekeza, badala yake walipewa ndani ya ukumbi wa mkutano.

"Hii maana yake ni kwamba, wanachama hawakupata muda wa kuijadili ajenda hiyo na zinginezo kwa muda unaotakiwa ili waweze kuijadili na kibaya zaidi, uongozi uliingia mkutanoni ukiwa tayari na maamuzi,"alisema Sendeu.

Alidai kuwa upo uwezekano mkubwa kwa mkutano huo kuhudhuriwa na wanachama hai na wasiokuwa hai kutokana na utaratibu mbovu uliotumika kuuitisha na kutolipwa kwa ada za uanachama.

Alisisitiza kuwa, vyovyote itakavyokuwa, lazima uongozi wa Yanga umlipe madai yake kwa vile ni halali na kwamba hatakuwa tayari kuona haki yake ikidhulumiwa.

Akizungumza wakati wa mkutano huo, Manji alisema Mwesigwa na Sendeu wamefutwa uanachama kwa kosa la kuishitaki klabu hiyo mahakamani. Mwesigwa ameishitaki klabu hiyo kwa kuidai sh. 183,400,050 wakati Sendeu anaidai sh. 79,900.050.

Sunday, January 20, 2013

BILIONI 32 KUJENGA UWANJA WA KAUNDA

KLABU ya Yanga inatarajia kutumia sh. bilioni 32 kwa ajili ya kujenga uwanja wake mpya na wa kisasa katika makao makuu ya klabu hiyo mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa klabu hiyo, Yussuf Manji, aliwaambia wanachama wa klabu hiyo jana kuwa, ujenzi wa uwanja huo unatarajia kuanza Juni mwaka huu chini ya usimamizi wa kampumi ya Beijing Constructinon Engineering ya China.

Manji alisema uongozi wa Yanga unatarajia kufanya mazungumzo na Kampuni ya Unit Trust Fund Tanzania, ambayo ni wataalamu wa uchumi na kufanya mipango ya upatikanaji wa fedha za ujenzi wa uwanja huo.

Mwenyekiti huyo alisema, jukumu la kampuni hiyo litakuwa kutafuta benki au taasisi, ambayo itaikopesha Yanga fedha za kujenga uwanja huo na kuongeza kuwa, wanatarajia kufikia Mei mwaka huu, fedha hizo zitakuwa zimepatikana.

Alisema licha ya kutumia sh. bilioni 32 kwa ajili ya ujenzi wa uwanja, pia wanatarajia kutumia dola za Marekani milioni 21 kwa ajili ya kugharamia vifaa vya ujenzi huo.

Manji alisema pia kuwa, uongozi unatarajia kuwaomba wanachama wao 210,000 kuchangia sh. 250 kwa wiki ili kwa mwaka zipatikane sh. bilioni nane kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa uwanja huo.

Alisema mbali ya wanachama kuchangia, wanatarajia kuendesha harambee ya kukusanya fedha za ujenzi wa uwanja huo, itakayofanyika baadae mwaka huu.

KAMATI YA UTENDAJI YANGA KUFUMULIWA

KAMATI ya Utendaji ya klabu ya Yanga huenda ikavunjwa na kuundwa upya baada ya wanachama wa klabu hiyo kuwapa meno mwenyekiti na makamu mwenyekiti kufanya uteuzi wa wajumbe wanaowataka.

Uamuzi huo ulifikiwa jana katika mkutano mkuu wa wanachama wa klabu hiyo uliofanyika kwenye bwalo la maofisa wa Polisi, Oysterbay, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wanachama 1,114.

Uongozi wa Yanga uliamua kuwasilisha ombi hilo kwa wanachama ili mwenyekiti na makamu mwenyekiti wawe na uwezo wa kuteua wajumbe wa kamati hiyo na kuwatimua iwapo watashindwa kutekeleza vyema majukumu yao.

Akizungumza baada ya kupitishwa kwa azimio hilo, Manji alisema tayari mjumbe mmoja, ambaye hakumtaja jina ameshaenguliwa katika kamati hiyo kwa kosa la kuwatukana viongozi.

"Mwanachama yeyote atakayekwenda kinyume na muundo wa uendeshwaji wa klabu yetu tutamfukuza mara moja na lengo ni kujenga na si kubomoa," alisema Manji.

Hata hivyo, wanachama hao walikataa kupitisha ajenda ya kumpa nafasi mwenyekiti na makamu wake kupendekeza viongozi watakaochukua nafasi zao baada ya uongozi wao kumaliza muda wake.

Baada ya ajenda hiyo kukataliwa, Manji alisema utaratibu uliokuwepo awali utaendelea kutumika kama ilivyokuwa zamani na katiba haitabadilishwa.

Ajenda nyingine zote zilizosomwa katika mkutano huo zilipitishwa kwa kishindo na wanachama hao, ambao pia walipata nafasi ya kutoa ushauri kwa uongozi.

Katika hatua nyingine, wanachama wa Yanga wameridhia kuwaongezea muda wa miaka miwili, wadhamini wa bodi ya klabu hiyo, Mama Fatma Karume na Francis Kifukwe.

Mbali na kuwaongezea muda viongozi hao, wanachama wamekubali kuongezwa kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Utawala Bora, George Mkuchika kuwa mjumbe mwingine wa bodi hiyo.

Mkuchika ataungana na Kifukwe na Mama Karume na wadhamini wengine wawili, watakaoongezwa hapo baadaye na kuunda bodi itakayokuwa na wadhamini saba

MANJI AKUNJUA MAKUCHA YANGA, MWESIGWA, SENDEU WAFUTWA UANACHAMA

MKUTANO Mkuu wa wanachama wa klabu ya Yanga umewavua uanachama aliyekuwa katibu mkuu wa klabu hiyo, Celestine Mwesigwa na ofisa habari wa zamani, Louis Sendeu.

Uamuzi wa kuwavua uanachama Mwesigwa na Sendeu ulifikiwa katika mkutano mkuu wa klabu hiyo uliofanyika jana kwenye bwalo la maofisa wa Polisi, Oysterbay, Dar es Salaam.

Mkutano huo ulioongozwa na Mwenyekiti wa klabu hiyo, Yussuf Manji, ulihudhuriwa na wanachama 1,144.

Mwesigwa na Sendeu walifukuzwa kazi mwaka jana na uongozi wa klabu hiyo kwa tuhuma za utendaji mbovu wa kazi.

Akizungumza wakati wa mkutano huo, Manji alisema wameamua Sendeu na Mwesigwa wafutwe uanachama kutokana na kushindwa kuonyesha uzalendo kwa klabu yao.

Manji alisema licha ya wanachama hao wawili kuidai Yanga, walikwenda kinyume cha katiba kwa kuamua kufungua kesi ya madai mahakamani dhidi ya viongozi wa klabu hiyo.

Mwesigwa alifungua kesi akiidai klabu hiyo sh. 183,400,050 wakati Sendeu anadai sh. 79,900.050.

Manji alisema iwapo wanachama hao wangekuwa na mapenzi na klabu hiyo, wasingeishtaki Yanga mahakamani, badala yake wangekuwa wavumilifu kwa kusubiri malipo yao.

"Hawa ni wanachama wetu, lakini mwanachama aliye na mapenzi na klabu yake hawezi kukimbilia mahakamani kuishtaki," alisema Manji.

Mbali na Mwesigwa na Sendeu, Yanga pia imemfuta uanachama, mwanachama wake aliyetambulika kwa jina moja la Godwion, anayemiliki kampuni ya uwakili ya Auda &Company Advocates kutokana na kuidai klabu hiyo sh. 4,500,000.

Manji alisema, wakili huyo, ambaye alikuwa akisimamia kesi ya madai ya wachezaji Wisdom Ndlovu na Steven Marash, baada ya kumaliza kesi hiyo, aliamua kudai malipo hayo.

"Mwanachama huyu alifanyakazi kimaslahi binafsi na si kwa kutoa mchango kwa klabu yake,"alisema Manji.

ANGOLA, MOROCCO HAKUNA MBABE

JOHANNESBURG, Afrika Kusini

ANGOLA na Morocco juzi zilishindwa kutambiana baada ya kutoka suluhu katika mechi ya kundi A ya michuano ya soka ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika iliyochezwa kwenye uwanja wa FNB mjini hapa.

Katika mechi hiyo iliyokuwa na ushindani mkali, timu zote mbili zilipata nafasi kadhaa za kufunga mabao, lakini zilishindwa kuzitumia vyema.

Mshambuliaji, Younes Belhanda, aliyeingia kipindi cha pili, nusura aifungie bao Morocco katika kipindi cha pili baada ya kuitoka ngome ya Angola, lakini shuti lake lilitoka sentimita chache pembeni ya goli.

Angola nayo ingeweza kupata bao katika kipindi hicho wakati mshambuliaji wake, Guilherme Afonso alipoingia na mpira ndani ya eneo la hatari na kubaki na kipa Nadir Lamyaghri wa Morocco, lakini shuti lake lilitoka nje.

Kocha Rachid Taoussi wa Morocco aliamua kumweka benchi Belhanda katika kipindi cha kwanza kutokana na kuwa na wasiwasi na afya yake, lakini alilazimika kumuingiza kipindi cha pili kwa lengo la kuongeza kasi ya mashambulizi.

Angola ilikuwa ya kwanza kufanya mashambulizi kwenye lango la Morocco kipindi cha kwanza wakati Mingo Bille alipofumua kiki kali iliyopanguliwa na kipa Lamyaghri.

Morocco ilijibu mashambulizi wakati Abdelaziz Barranda na Oussama Assaidi walipokuwa wakiichachafya mara kwa mara ngome ya wapinzani wao na kusababisha mpira uchezwe ndani ya eneo la Angola.

Akizungumza baada ya pambano hilo, Kocha Rachid wa Morocco alisema walistahili kushinda mechi hiyo kutokana na kupata nafasi nyingi za kufunga mabao, lakini walishindwa kuzitumia.

Kocha Mkuu wa Angola,Gustavo Ferrin alisema sare hiyo imewapa faraja kubwa kwa vile timu yake haikuwa ikipewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri katika michuano hiyo.

BAFANA BAFANA ULIMI NJE KWA CAPE VERDE

JOHANNESBURG, Afrika Kusini

WENYEJI Afrika Kusini, maarufu kwa jina la Bafana Bafana juzi walianza vibaya michuano ya soka ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika baada ya kulazimishwa kutoka suluhu na Cape Verde.

Katika mechi hiyo ya kundi A, Bafana Bafana ilipata nafasi chache nzuri za kufunga mabao, lakini ilishindwa kuzitumia vyema.

Sare hiyo ilikuwa na faida kubwa kwa Cape Verde, ambayo ni mara yake ya kwanza kucheza fainali hizo, lakini ilionyesha soka ya kuvutia.

Cape Verde ilipata nafasi nzuri ya kufunga bao katika kipindi cha pili wakati mshambuliaji wake, Platini alipopewa pasi akiwa ndani ya 18, lakini shuti lake lilitoka nje.

Kocha Gordon Igesund wa Afrika Kusini, ambaye alikifanya kikosi chake cha kwanza kuwa siri, aliwashangaza mashabiki wengi wa nchi hiyo baada ya kumwanzisha Lehlohonolo Majoro katika safu ya ushambuliaji badala ya mchezaji mwenye uzoefu, Katlego Mphela.

Bafana Bafana haijawahi kushinda mechi za fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika tangu mwaka 2004. Timu hiyo haikushinda mechi hata moja katika fainali za 2006 na 2008 na ilishindwa kufuzu kucheza fainali za 2010 na 2012.

Kiungo Siphiwe Tshabalala angeweza kuifungia bao Bafana Bafana dakika za mwanzo za pambano hilo kwa mpira wa adhabu, lakini shuti lake lilikwenda moja kwa moja mikononi mwa kipa Vozhina wa Cape Verde.

Viungo Thuso Phala na Tshabalala walijitahidi kushirikiana vyema na washambuliaji Bernard Parker na Majoro, lakini tatizo kubwa lilikuwa umaliziaji mbovu.

Washambuliaji Heldon Ramos na Ryan Mendes wa Cape Verde walikuwa tishio katika safu ya ulinzi ya Bafana Bafana, lakini hawakuwa makini katika kuipenya.

Mabeki wa kati wa Cape Verde, Fernando Varela na Nando nao walikuwa makini kukabiliana na washambuliaji wa Bafana Bafana na hivyo kuufanya mpira uchezwe zaidi eneo la kati.

Phala alipata nafasi nzuri ya kuifungia bao Bafana Bafana kipindi cha pili baada ye kutengenezewa pasi na Tshabalala, lakini shuti lake lilitoka pembeni ya goli.

Mara baada ya pambano hilo kumalizika, wachezaji na maofisa wa benchi la ufundi la Cape Verde walionekana kuwa na furaha kubwa kwa kupata pointi ya kwanza katika fainali hizo, wakati wachezaji wa Afrika Kusini walikuwa na majonzi makubwa.

Kocha Mkuu wa Bafana Bafana, Igesund alisema hakufurahishwa na kiwango kilichoonyeshwa na vijana wake na kuongeza kuwa, kutokana na mchezo waliouonyesha, walistahili kupata sare.

Kocha Mkuu wa Cape Verde,Luico Antunes alisema amefurahishwa na kiwango kilichoonyeshwa na timu yake na kuongeza kuwa, sare hiyo itawafanya watu 500,000 wa nchi hiyo wawe na furaha.

YANGA YA UTURUKI WE ACHA TU

TIMU ya soka ya Yanga jana iliichapa Black Leopards ya Afrika Kusini mabao 3-2 katika mechi ya kirafiki ya kimataifa ya soka iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mechi hiyo ilikuwa ya kwanza kwa Yanga tangu iliporejea nchini kutoka Uturuki, ambako ilikwenda kuweka kambi ya wiki mbili kwa ajili ya kujiandaa na mzunguko wa pili wa ligi kuu ya Tanzania Bara.

Iliwachukua Yanga dakika 30 kuhesabu bao la kwanza lililofungwa kwa njia ya penalti na Jerry Tegete baada ya Haruna Niyonzima kuangushwa ndani ya eneo la hatari. Bao hilo lilidumu hadi mapumziko.

Black Leopards ilisawazishadakika ya 46 kwa bao lililofungwa na Humphrey Khoza baada ya kuunganisha wavuni kwa kichwa, kona iliyopigwa na Rodney Ramagalela.

Frank Domayo aliiongezea Yanga bao la pili dakika ya 70 kabla ya Tegete kuongeza la tatu kwa mkwaju mkali, uliotinga moja kwa moja wavuni.

Zikiwa zimesalia dakika mbili pambano hilo kumalizika, Leopards iliongeza bao la pili kupitia kwa Muganga Diunga kwa njia ya penalti baada ya Juma Abdul kumchezea vibaya Edgar ndani ya eneo la hatari.

Saturday, January 19, 2013

WASAUZI KUZIHUKUMU SIMBA NA LIBOLO

WAAMUZI kutoka Afrika Kusini wamepangwa kuchezesha mechi ya kwanza ya raundi ya awali ya michuano ya klabu bingwa Afrika kati ya Simba na Clube Recreation Libolo ya Angola.

Pambano hilo limepangwa kufanyika Februari 17 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya timu hizo kurudiana wiki mbili baadaye nchini Angola.

Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, mwamuzi wa kati atakuwa Daniel Volgraaff akisaidiwa na Enock Molefe, Lindikhaya Bolo na Lwandile Mfiki. Kamishna wa mechi hiyo atakuwa Emmanuel Lesita kutoka Lesotho.

Katika hatua nyingine, Shirikisho la Soka Afrika (CAF), limewateua waamuzi wanne wa Tanzania kuchezesha mechi ya marudiano ya michuano ya klabu bingwa Afrika kati ya URA ya Uganda na Cotton Sport ya Cameroon.

Wambura alisema jana kuwa, mchezo huo umepangwa kufanyika Machi 3 mwaka huu mjini Kampala, Uganda. Aliwataja waamuzi hao kuwa, Oden Mbaga, atakayekuwa mwamuzi wa kati, akisaidiwa na Jesse Erasmo na Hamis Chang’walu. Mwamuzi wa akiba atakuwa Israel Mujini wakati kamisaa ni Souleiman Waberi wa Djibouti.

Wakati huo huo, CAF imewateua waamuzi wastaafu, Leslie Liunda na Alfred Rwiza kuwa makamishna wa mechi za michuano ya klabu bingwa Afrika.

Wambura alisema Rwiza ameteuliwa kuwa kamishna wa mechi kati ya APR ya Rwanda na Vital’O ya Burundi itakayochezwa nchini Rwanda kati ya Februari 15 na 17 mwaka huu.

Aliongeza kuwa, Liunda ameteuliwa kuwa kamishna wa mechi ya marudiano kati ya Tusker ya Kenya na St. Michel United ya Seychelles itakayochezwa Kenya kati ya Machi 1 na 3 mwaka huu. Mechi zote ni za raundi ya awali.

BAFANA BAFANA KUKATA UTEPE NA CAPE VERDE FAINALI ZA AFRIKA LEO

JOHANNESBURG, Afrika Kusini

WENYEJI Afrika Kusini, maarufu kwa jina la Bafana Bafana, leo wanafungua dimbani la michuano ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa kumenyana na Cape Verde.

Pambano hilo la kundi A linalosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka barani Afrika, limepangwa kuanza saa 10 jioni (saa 11 kwa Tanzania) kwenye Uwanja wa City wa mjini hapa.

Afrika Kusini ilipewa uenyeji wa fainali hizo mwaka huu baada ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kuiengua Libya kutokana na kuzuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo mwaka 2011.

Fainali za mwaka huu zitachezwa kwenye viwanja vitano vilivyopo kwenye miji ya Port Elizabeth, Johannesburg, Nelspruit, Durban na Rustenburg, ambavyo pia vilitumika kwa fainali za Kombe la Dunia 2010.

Katika mechi nyingine ya kundi hilo itakayochezwa leo, Angola itamenyana na Morocco kuanzia saa moja usiku kwa saa za Afrika Kusini (saa mbili kwa saa za Tanzania).

Akizungumzia pambano hilo juzi, Kocha Mkuu wa Bafana Bafana, Gordon Igesund alisema wamejiandaa vyema kukabiliana na wapinzani wao na wana uhakika mkubwa wa ushindi.

Igesund alisema baada ya maandalizi ya muda mrefu, anaamini vijana wake watawazodoa wale, ambao wamekuwa wakiiponda timu hiyo kutokana na matokeo ya mechi mbili za kirafiki walizocheza.

Bafana Bafana ilicheza mechi mbili za kirafiki za kimataifa dhidi ya Norway na Algeria. Katika mechi ya kwanza, ilichapwa bao 1-0 na Norway kabla ya kulazimishwa kutoka suluhu na Algeria.

"Kama tutakuwa na bahati na kama tutaanza kufunga mabao, nafikiri tunaweza kufika mbali," Igesund aliwaambia waandishi wa habari.

"Natumaini mambo yatakwenda vizuri kwetu kwa sababu tunalo jukumu kubwa na tutakuwa tukiungwa mkono na mashabiki wapatao 90,000 nyuma yetu uwanjani,"alisema kocha huyo.

Hata hivyo, Igesund alikiri kwamba kazi iliyo mbele yao ni ngumu na wanapaswa kuziheshimu timu walizopangwa nazo kundi moja kwa sababu zipo baadhi ya timu, ambazo ni nzuri.

Cape Verde ilifuzu kucheza fainali za mwaka huu kwa matokeo yaliyowashangaza mashabiki wengi wa soka barani Afrika baada ya kuibanjua Cameroon mabao 4-0.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Lucio Antunes alisema juzi kuwa, kikosi chake kina uwezo wa kuvuka hatua ya makundi iwapo wachezaji wake watacheza kwa kufuata maelekezo yake.

Lucio alisema japokuwa ni mara yao ya kwanza kufuzu kucheza fainali hizo, vijana wake wana ari kubwa ya kuonyesha maajabu kwa kushinda mechi ya ufunguzi.

Alisema kama waliweza kuishinda Cameroon katika mechi ya kuwania kufuzu kucheza fainali za mwaka huu, haoni kwa nini washindwe kufanya hivyo kwa Bafana Bafana.

Pambano kati ya Angola na Morocco nalo linatarajiwa kuwa na ushindani mkali kutokana na timu zote mbili kuundwa na wachezaji mahiri, baadhi wakiwa wanacheza soka barani Ulaya.

HASSANOO, MOSHA WAINGIA VITANI TFF, KABURU AJITOA

MMILIKI wa klabu ya African Lyon, Rahim Kangenzi ‘Zamunda’ (katikati) akirejesha fomu ya kugombea uenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu kwa niaba ya Mwenyekiti wa Yanga, Yussuf Manji (kulia) katika ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ilala, Dar es Salaam jana. Anayepokea fomu hiyo kushoto ni Ofisa wa TFF, Jonathan Aloyce Kakwaya. (Picha kwa hisani ya blogu ya Bin Zubeiry).

Makamu Mwenyekiti wa zamani wa klabu ya Yanga, Davis Mosha na Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Pwani (COREFA), Hassan Othman Hassanol, wamechukua fomu za kuwania ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Mosha alichukuliwa fomu jana na Mwenyekiti wa Chama cha Soka mkoa Kilimanjaro, Godluck Moshi wakati Hassanoo alichukuliwa na Ofisa Habari wa COREFA, Masau Bwire.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumchukulia fomu Mosha, Godluck alisema imepita miaka zaidi ya 20 mkoa huo hauna mwakilishi ndani ya TFF hivyo wameona ni vyema wapate mwakilishi.

Godluck alisema Mosha anazo sifa zote za uongozi wa soka na anajua vizuri mambo ya utawala wa michezo hivyo wanaamini akipata nafasi hiyo, atakuwa mwakilishi mzuri wa kanda yao.

Mosha ni mmoja wa wafanyabiashara maarufu katika mkoa wa Dar es Salaam kama ilivyo kwa Hassanoo, ambaye kwa sasa yupo rumande kutokana na kukabiliwa na kesi mbili, moja ikiwa ya uhujumu uchumi.

Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema jana kuwa, kikatiba, Hassanoo anaruhusiwa kugombea uongozi kama watu wengine kwa vile bado hajapatikana na hatia ya kesi zinazomkabili.

Alisema wagombea wengine 11 walichukua fomu za kuwania nafasi mbalimbali za uongozi wa shirikisho hilo jana na hivyo kufanya idadi ya wagombea kufika 46. Jana ilikuwa siku ya mwisho kwa wagombea kuchukua na kurejesha fomu kwa ajili ya uchaguzi huo uliopangwa kufanyika Februari 24 mwaka huu mjini Dar es Salaam.

Waombaji wapya 11 waliojitokeza jana ni Richard Rukambura, anayeomba urais wakati Kaliro Samson, Jumbe Magati, Richard Rukambura, Omari Walii, Ahmed Mgoyi, John Kiteve, Stanley Lugenge, Francis Ndulane, Riziki Majara na Hassanoo wanawania ujumbe wa kamati ya utendaji.

Orodha kamili ya wagombea ni kama ifuatavyo: Wanaowania urais ni Athuman Nyamlani, Jamal Malinzi, Omari Nkwarulo na Richard Rukambura. Walioomba kuwania nafasi ya makamu wa rais ni Michael Wambura, Ramadhan Nassib na Wallace Karia.

Wanaowania ujumbe wa kamati ya utendaji ni Salum Chama na Kaliro Samson (Kagera na Geita), Jumbe Magati, Mugisha Galibona, Richard Rukambura, Samuel Nyalla, Titus Osoro na Vedastus Lufano (Mara na Mwanza), Epaphra Swai na Mbasha Matutu (Shinyanga na Simiyu), Charles Mugondo, Elly Mbise na Omari Walii (Arusha na Manyara), Ahmed Mgoyi na Yusuph Kitumbo (Kigoma na Tabora), Ayubu Nyaulingo, Blassy Kiondo, Nazarius Kilungeja na Selemani Kameya (Katavi na Rukwa) na James Mhagama na Stanley Lugenge (Njombe na Ruvuma).

Wengine ni Athuman Kambi, Francis Ndulane na Zafarani Damoder (Lindi na Mtwara), Hussein Mwamba na Stewart Masima (Dodoma na Singida), Farid Nahdi, Geofrey Nyange, Hassan Othman Hassanoo, Riziki Majara na Twahili Njoki (Morogoro na Pwani), Elias Mwanjala, Eliud Mvella na John Kiteve (Iringa na Mbeya), Khalid Mohamed (Kilimanjaro na Tanga) na Muhsin Balhabou, Omari Abdulkadir na Shaffih Dauda (Dar es Salaam).

Wakati huo huo, waombaji watatu wapya wamejitosa katika kinyang’anyiro cha kuwania uongozi wa Bodi ya Ligi Kuu (TPL Board) ambayo uchaguzi wake utafanyika Februari 22 mwaka huu.

Wambura aliwataja waliochukua fomu jana kuwa ni Hamad Yahya wa Kagera Sugar anayeomba uenyekiti wakati Christopher Peter wa Moro United na Kazimoto Miraji Muzo wa Pamba ya Mwanza wanaoomba ujumbe wa bodi kuwakilisha klabu za Ligi Daraja la Kwanza.

Orodha kamili ya waombaji uongozi wa Bodi ya Ligi Kuu ni Hamad Yahya wa Kagera Sugar na Yusuf Manji wa Yanga wanaoomba uenyekiti wakati Makamu Mwenyekiti aliyeomba ni Said Mohamed wa Azam.

Kwa upande wa wajumbe wawili kuwakilisha klabu za daraja la kwanza ni Christopher Peter Lunkombe wa Moro United ya Dar es Salaam na Kazimoto Miraji Muzo wa Pamba ya Mwanza.

YANGA, BLACK LEOPARDS HAPATOSHI TAIFA LEO

MABINGWA wa soka wa Kombe la Kagame, Yanga leo wanatarajiwa kushuka dimbani kumenyana na Black Leopards ya Afrika Kusini katika mechi ya kirafiki ya kimataifa, itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mechi hiyo itakuwa ya kwanza kwa Yanga tangu iliporejea nchini wiki iliyopita, ikitokea Uturuki, ambako ilikwenda kuweka kambi ya wiki mbili kwa ajili ya kujiandaa na mzunguko wa pili wa ligi kuu ya Tanzania Bara.

Black Leopards, ambayo inashika nafasi ya 12 katika msimamo wa ligi kuu ya Afrika Kusini yenye timu 16, iliwasili nchini jana asubuhi ikiwa na msafara wa wachezaji na viongozi 37.

Mwakilishi wa Kampuni ya Prime Time Promotions, iliyoandaa pambano hilo, Shaffih Dauda alisema jana kuwa, maandalizi yote muhimu kwa ajili ya pambano hilo yamekamilika.

Dauda alisema wanaamini mechi hiyo itakuwa kipimo kizuri kwa Yanga kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili wa ligi kuu, inayotarajiwa kutimua vumbi Januari 26 mwaka huu.

Amewataka mashabiki wa Yanga kujitokeza kwa wingi kushuhudia mechi hiyo ili kuwapa moyo wachezaji wa kufanya vizuri zaidi. Viingilio katika mechi hiyo ni Sh 30, 000 kwa VIP A, Sh 20, 000 kwa VIP B, Sh 15, 000 kwa VIP C, Sh 7, 000 kwa viti vya rangi ya chungwa na Sh 5, 000 kwa viti vya rangi ya bluu na kijani.

Wakati huo huo, uongozi wa klabu ya Yanga umewataka wanachama wake kuhakikisha kuwa wanalipia kadi zao za uanachama ili waweze kupata haki ya kuhudhuria mkutano mkuu.

Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, mwanachama atakayeshindwa kulipia kadi yake, hataruhusiwa kuhudhuria mkutano huo.

Mkutano mkuu wa Yanga umepangwa kufanyika kesho kwenye bwalo la maofisa wa Polisi, Oysterbay, Dar es Salaam.

Mwalusako alisema pamoja na mambo mengine, mkutano huo utajadili masuala mbalimbali yanayoihusu klabu hiyo, ikiweko ujenzi wa uwanja mpya na wa kisasa na ule wa jengo la kitega uchumi.

WALANGUZI WA TIKETI ZA MPIRA BYE BYE

ASILIMIA 80 ya maandalizi ya kutumika kwa mfumo mpya wa tiketi za elektroniki utakaoanza kutumika hivi karibuni katika michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara imekamilika.

Hayo yalisemwa mjini Dar es Salaam jana na Mkurugenzi wa Takwimu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Saad Kawemba alipokuwa akizungumzia maendeleo ya ufungwaji wa mashine mpya za kuuza tiketi hizo.

Kawemba alisema asilimia iliyobaki ni kwa ajili ya ufungwaji wa mashine hizo. Alisema ufungwaji wa mashine hizo utakamilika baada ya kuwasili kwake.

Ufungwaji wa mashine hizo unasimamiwa na Benki ya CRDB, ambayo ilishinda tenda ya kufanya kazi hiyo. Kawemba alisema mashine hizo zitafungwa katika viwanja vinane vinavyotumika katika mechi za ligi hiyo.

Alivitaja viwanja hivyo kuwa ni Kaitaba wa Kagera, CCM Kirumba wa Mwanza, Sheikh Amri Abeid wa Arusha, Mkwawani wa Tanga, Sokoine wa Mbeya, Jamhuri wa Dodoma na Taifa wa Dar es Salaam.

Alisema baada ya kufungwa kwa mashine hizo, hakutakuwa na mtu atakayenunua tiketi barabarani katika katika magari maalumu kama ilivyo sasa.

Kawemba alisema mfumo huo mpya utamuwezesha mtu atakayehitaji tiketi, kuzinunua kupitia katika ATM za benki ya CRDB, M-PESA, Tigopesa na Airtel Money.

Alisema baada ya kununua tiketi, mmiliki wake atakwenda kuichapicha katika mashine hizo, ambazo zitawekwa katika sehemu maalum na kisha kwenda nayo uwanjani, ambapo tiketi hiyo ndiyo itakayomfungulia mlango wa kuingia uwanjani.

POULSEN KUZIFANYIA UMAFIA IVORY COAST NA MOROCCO

KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars, Kim Poulsen, ameondoka nchini jana kwenda Afrika Kusini kuzifuatilia timu za Ivory Coast na Morocco.

Ivory Coast na Morocco ni miongoni mwa timu zinazoshiriki katika fainali za mwaka huu za Kombe la Mataifa ya Afrika na zimepangwa kundi moja na Taifa Stars katika fainali za kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia za 2014.

Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, Poulsen amepanga kutazama mechi za timu hizo ili kupima uwezo wake kabla ya kukabiliana na Taifa Stars.

Wambura alisema baada ya kutazama mechi hizo, kocha huyo kutoka Denmark atapata nafasi ya kupanga mbinu za kukabiliana nazo.

Alisema hiyo ni miongoni mwa mikakati iliyoandaliwa na TFF ili kuhakikisha Taifa Stars inafanya vizuri katika michuano hiyo na kufuzu kucheza fainali zitakazochezwa nchini Brazil.

Taifa Stars inayodhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia ya Kilimanjaro Premium Lager, inashika nafasi ya pili katika kundi lake. Itacheza na Morocco, Machi 24 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Wednesday, January 16, 2013

OKWI KUIAGA SIMBA JAN 26

KLABU ya Simba imesema mshambuliaji wake, Emmanuel Okwi atawaaga mashabiki wa klabu hiyo katika mchezo wa kirafiki dhidi ya African Lyon utakaofanyika Januari 26, mwaka huu.

Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, Okwi ameamua kuwaaga mashabiki wa timu hiyo kutokana na kumpa ushirikiano mkubwa.

Hata hivyo, Mtawala alisema watalazimika kuomba ruhusa ya kumtumia mchezaji huyo kutoka katika klabu yake ya sasa ya Etoile Du Sahel ya Tunisia.

Simba imemuuza Okwi kwa Etoile Du Sahel kwa kitita cha dola 300,000 za Marekani (sawa na sh. milioni 480,000) baada ya kufuzu majaribio aliyofanyiwa.

Kwa mujibu wa Mtawala, kikosi cha Simba, ambacho kwa sasa kipo kambini nchini Oman, kinatarajiwa kurejea nchini Januari 23 mwaka huu kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ya hatua ya pili ya ligi kuu ya Tanzania Bara.

Okwi ametia saini mkataba wa kuichezea Etoile Du Sahel kwa miaka miwili, ambapo atakuwa akilipwa mshahara wa dola 200,000 kwa mwaka. Pia amepewa nyumba ya kuishi na gari.

Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Uganda, alijiunga na Simba miaka mitatu iliyopita akitokea SC Villa ya Uganda na kuiwezesha kufanya vizuri katika michuano ya ligi na kimataifa.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspope amesema hawana haraka ya kutafuta mchezaji wa kuziba nafasi ya Okwi.

Hanspope alisema jana kuwa, watalazimika kufanyakazi hiyo kwa umakini mkubwa ili waweze kumpata mchezaji mwenye kiwango kinachoshabihiana na Okwi.

Okwi amekuwa mchezaji wa tatu wa Simba kuuzwa nje kwa bei mbaya. Awali, Simba iliwauza mshambuliaji Mbwana Samatta na kiungo Patrick Ochan wa Uganda kwa klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kwa kitita cha dola 200,000.

MANJI AWANIA UENYEKITI BODI YA LIGI

MWENYEKITI wa klabu ya Yanga, Yusuf Manji amechukua fomu ya kuwania nafasi ya mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu kwa niaba ya klabu za Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

Manji alichukuliwa fomu hiyo jana na Mwenyekiti wa klabu ya African Lyon, Rahim Kangezi 'Zamunda' kabla ya kuijaza na kuirejesha kwenye ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Alipoulizwa sababu za kumchukulia fomu hiyo Manji, Zamunda alisema amefanya hivyo kwa niaba ya klabu za ligi kuu, ambazo ndizo zimempendekeza.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kurejesha fomu hiyo, Manji alisema lengo lake ni kuziwezesha klabu za ligi kuu zijiendeshe kwa kujitegemea.

Manji alisema kwa kuwa klabu kwa sasa zimeundiwa bodi yao, atahakikisha anaisimamia vyema na kujenga misingi imara ya kuzifanya klabu zijitegemee.

Alisema atakuwa tayari kufanya kazi kwa bidii na kuzisaidia klabu ili ziweze kuwa katika hali nzuri kifedha kwa kuzijengea mfumo imara wa kuingiza mapato na kuwa na vyanzo vingine vya fedha.

Uchaguzi mkuu wa viongozi wa Bodi ya Ligi umepangwa kufanyika Februari 22, mwaka huu. Mgombea mwingine aliyejitokeza kuwania nafasi hiyo hadi sasa ni Said Mohamed, ambaye alichukua fomu Jumatatu iliyopita.

MALINZI, NYAMLANI WATAKA URAIS TFF

HARAKATI za kuwania urais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) sasa zimeanza kushika kasi baada ya wanamichezo wawili maarufu nchini kuchukua fomu za kuwania nafasi hiyo.

Wanamichezo hao, Makamu wa Kwanza wa Rais wa TFF, Athumani Nyamlani na Mwenyekiti wa Chama cha Soka mkoa wa Kagera, Jamal Malinzi walichukua fomu hizo jana.

Mgombea mwingine aliyechukua fomu jana kwa ajili ya kuwania nafasi hiyo ni Mwenyekiti wa Chama cha Soka mkoa wa Kigoma, Omari Mussa Nkwarulo.

Malinzi alichukua fomu ya kuwania nafasi hiyo kwa njia ya mtandao na kuirejesha jana, akiwa ameambatanisha ada ya sh. 500,000 wakati Nyamlani alichukua fomu hiyo katika ofisi za TFF na kuijaza papo hapo kabla ya kuirejesha.

Malinzi aliwahi kuwa katibu mkuu wa klabu ya Yanga mwishoni mwa miaka ya 1990 na pia aliwahi kuwania nafasi hiyo katika uchaguzi wa mwaka 2008, lakini alipigwa mweleka na rais wa sasa wa TFF, Leodegar Tenga.

Kwa upande wake, Nyamlani amewahi kuwa katibu wa Chama cha Soka wilaya ya Temeka (TEFA) na pia katibu wa Chama cha Soka mkoa wa Dar es Salaam (DRFA).

Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, alisema jana kuwa, hadi sasa jumla ya wagombea 30 wamechukua fomu za kuwania nafasi mbalimbali za uongozi wa shirikisho hilo.

Akizungumza baada ya kurejesha fomu yake, Malinzi alisema anampongeza Tenga kwa kufanya maamuzi magumu ya kutogombea tena nafasi hiyo.

Malinzi alisema hali hiyo inawafanya wapiga kura watakaoshiriki katika uchaguzi huo kufanya maamuzi sahihi kwa kumchagua kushika nafasi hiyo kwa vile ana uwezo wa kuliongoza shirikisho hilo.

"Naaamini kuwa wapiga kura watakuwa na imani na mimi kwani si mara yangu ya kwanza kuomba nafasi hii, niliomba mwaka 2008, lakini kura hazikutosha," alisema Malinzi.

Naye Nyamlani alisema ameamua kuwania nafasi hiyo kwa lengo la kuendeleza soka ya Tanzania, kazi iliyokuwa ikisimamiwa vyema na Tenga, ambaye yeye ni msaidizi wake mkuu.

"Nadhani mimi ndiye ninayefaa kuendeleza kazi hiyo na iwapo nitachaguliwa, nitaifanyakazi hiyo kwa umakini mkubwa na kutilia mkazo programu ya kuendeleza soka ya vijana,"alisema Nyamlani, ambaye alisindikizwa na kundi kubwa la wapambe.

Mgombea mwingine aliyechukua fomu jana ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mbeya (MREFA), Elias Mwanjala anayewania ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF kuwakilisha Kanda ya Iringa na Mbeya.

Orodha kamili ya wagombea waliochukua fomu ni Athumani Nyamlani, Jamal Malinzi na Omari Nkwarulo (urais), Michael Wambura, Ramadhan Nassib na Wallace Karia (umakamu wa rais).

Wanaowania ujumbe wa Kamati ya utendaji, kanda zao katika mabano ni Salum Chama (Kagera na Geita), Mugisha Galibona, Samuel Nyalla, Titus Osoro na Vedastus Lufano (Mara na Mwanza), Epaphra Swai na Mbasha Matutu (Shinyanga na Simiyu), Charles Mugondo na Elly Mbise (Arusha na Manyara), Yusuph Kitumbo (Kigoma na Tabora), Ayubu Nyaulingo, Nazarius Kilungeja na Selemani Kameya (Katavi na Rukwa).

Wengine ni James Mhagama (Njombe na Ruvuma), Athuman Kambi (Lindi na Mtwara), Hussein Mwamba na Stewart Masima (Dodoma na Singida), Farid Nahdi na Twahili Njoki (Morogoro na Pwani), Elias Mwanjala (Iringa na Mbeya), Khalid Mohamed (Kilimanjaro na Tanga) na Muhsin Balhabou, Shaffih Dauda na Zafarani Damoder (Dar es Salaam).

BRANDTS: YANGA IPO KAMILI GADO

KOCHA Mkuu wa Yanga, Ernest Brandts amesema, kukaa pamoja na wachezaji kwa muda wa wiki mbili wakati timu ilipokuwa kambini nhini Uturuki, kumemwezesha kupata muda wa kujenga kikosi imara.

Brandts alisema wakati alipoanza kuinoa timu hiyo mwishoni mwa mwaka jana, aliikuta ikishiriki kwenye mashindano ya ligi, hivyo hakupata muda wa kuijenga timu.

"Lakini kambi ya Uturuki imeniwezesha kufanikisha hilo kwa vile nimekaa na wachezaji kwa muda mrefu, kujua uwezo wao na kuwajenga kisoka,"alisema kocha huyo alipozungumza na waandishi wa habari makao makuu ya klabu hiyo mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam jana.

Kocha huyo kutoka Uholanzi alisema pia kuwa, kambi ya Uturuki imesaidia kuongeza kiwango cha wachezaji na kuwafanya wacheze kwa ushirikiano zaidi.

Alisema ana hakika mazoezi ya Uturuki yataiwezesha timu yake kufanya vizuri katika mzunguko wa pili wa ligi kuu ya Tanzania Bara, inayotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi huu.

Hata hivyo, Brandts alikiri kuwa, bado timu yake inahitaji mazoezi zaidi kwa lengo la kujiimarisha.

Yanga iliweka kambi katika mji wa Antalya nchini Uturuki ikiwa ni pamoja na kucheza mechi tatu za kirafiki kwa ajili ya kujiandaa na hatua ya pili ya ligi kuu.

Wakati huo huo, Kampuni ya Prime Time Promotions imesema  maandalizi ya mechi ya kirafiki ya kimataifa kati ya Yanga na Black Leopards ya Afrika Kusini yanakwenda vizuri.

Mwakilishi wa kampuni hiyo, Shaffih Dauda aliwaambia waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana kuwa, Black Leopards inatarajiwa kutua nchini kesho ikiwa na kikosi cha watu 37 wakiwemo wachezaji na viongozi.

"Tuanatarajia mchezo kati ya Yanga na Black Leopards utakuwa mzuri na Yanga itaweza kujipima vyema kwani itacheza na timu ambayo ipo katika kiwango kizuri," alisema Dauda.

Dauda alisema kutokana na Yanga kuwa kambini kwa wiki mbili nchini Uturuki, anaamini mashabiki watapata burudani safi kutoka kwa mabingwa hao wa Kombe la Kagame.

Alivitaja viingilio katika mchezo huo kuwa ni sh. 30,000 kwa VIP A, sh. 20,000 kwa VIP B na sh. 15,000 kwa VIP C. Jukwaa la rangi ya chungwa kiingilio kitakuwa sh. 7,000/ wakati jukwa la rangi ya bluu na kijani mzunguko ni sh. 5,000.

WAMBURA AJITOSA TFF



KATIBU Mkuu wa zamani wa kilichokuwa Chama cha Soka nchini (FAT), Michael Wambura amechukua fomu kwa ajili ya kuwania uongozi katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, Wambura amechukua fomu ya kuwania nafasi ya makamu wa rais wa shirikisho hilo.

Wambura alisema wagombea wengine watano walichukua fomu za kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika shirikisho hilo na kufanya jumla ya wagombea waliojitokeza hadi sasa kuwa 26.

Aliwataja wagombea hao, ambao wote wanawania nafasi ya ujumbe wa kamati ya utendaji kuwa ni Mbasha Matutu, Muhsin Balhabou, Salum Chama, Titus Osoro na Zafarani Damoder.

Uchaguzi mkuu wa TFF umepangwa kufanyika Februari 24 mwaka huu, ambapo nafasi zinazogombewa ni ya rais, makamu wa rais na wajumbe 13 wa kamati ya utendaji.

Idadi kamili ya waliochukua fomu, nafasi wanazogombea zikiwa kwenye mabano ni Michael Wambura, Ramadhan Nassib na Wallace Karia (makamu wa rais).

Wanaogombea ujumbe, kanda zikiwa kwenye mabano ni Salum Chama (Kagera na Geita), Mugisha Galibona, Samuel Nyalla, Titus Osoro na Vedastus Lufano (Mara na Mwanza), Epaphra Swai na Mbasha Matutu (Shinyanga na Simiyu), Charles Mungodo, Elly Mbise na Twahili Njoki (Arusha na Manyara).

Wengine ni Yusuph Kitumbo (Kigoma na Tabora), Ayubu Nyaulingo, Nazarius Kilungeja na Selemani Kameya (Katavi na Rukwa), James Mhagama (Njombe na Ruvuma), Athuman Kambi (Lindi na Mtwara), Hussein Mwamba na Stewart Masima (Dodoma na Singida), Farid Nahdi (Morogoro na Pwani), Khalid Mohamed (Kilimanjaro na Tanga) na Muhsin Balhabou, Shaffih Dauda na Zafarani Damoder (Dar es Salaam).

Wakati huo huo, Said Mohamed amechukua fomu ya kuwania nafasi ya makamu mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu (TPL Board).

Tuesday, January 15, 2013

SIMBA YAMUUZA OKWI KWA MIL 480/-

KLABU ya Simba imemuuza mshambuliaji wake Emmanuel Okwi kwa klabu ya Etoile Du Sahel ya Tunisia kwa kitita cha dola 300,000 (sawa na sh. milioni 480 za Tanzania).

Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu' alisema kwa njia ya simu jana kutoka Oman kuwa, Okwi ametia saini mkataba wa kuichezea klabu hiyo kwa miaka miwili.

Kwa mujibu wa Kaburu, Okwi alitia saini mkataba huo jana jioni baada ya kufanya mazungumzo binafsi na viongozi wa klabu hiyo.

Kaburu alisema Etoile Du Sahel imeshakamilisha taratibu zote za kumsajili mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Uganda, ikiwa ni pamoja na kumalizana na Simba.

Makamu Mwenyekiti huyo wa Simba alisema, viongozi wa klabu hiyo ya Tunisia wameamua kumsajili Okwi baada ya kuvutiwa na kiwango chake katika mechi mbalimbali walizomshuhudia akiicheza Simba.

Alisema hafla ya utiaji saini mkataba huo kati ya Okwi na viongozi wa Etoile Du Sahel, ilishuhudiwa na Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage.

Kaburu alisema Etoile Du Sahel iliwasilisha maombi ya kumsajili Okwi kwa klabu ya Simba mapema mwezi huu kabla ya kumruhusu kwenda kufanya majaribio.

Okwi alijiunga na Simba miaka minne iliyopita akitokea SC Villa ya Uganda na kuiwezesha kufanya vizuri katika michuano ya ligi na ya kimataifa.

Mwishoni mwa mwaka jana, Simba iliamua kumuongezea mkataba wa miaka miwili mshambuliaji huyo baada ya kuwepo na taarifa kwamba, alikuwa akiwaniwa na klabu za Yanga na Azam.

Okwi alitia saini mkataba huo wakati wa michuano ya Kombe la Chalenji, iliyofanyika nchini Uganda, lakini haikuweza kufahamika kitita cha pesa alicholipwa, zaidi ya kuongezewa mshahara kutoka sh. milioni 1.5 hadi sh. milioni tatu kwa mwezi.

SUNZU AFANYIWA MAJARIBIO READING

LONDON, England BEKI wa kati wa kimataifa wa Zambia, Stopilla Sunzu yuko nchini England ambako anafanyiwa majaribio ya kucheza soka ya kulipwa katika klabu ya Reading.

Sunzu (23) kwa sasa anaichezea klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na anatarajiwa kuichezea Zambia katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zinazotarajiwa kuanza Jumamosi nchini Afrika Kusini.

Beki huyo wa kimataifa wa Zambia, anatarajiwa kutumia wiki moja kufanyiwa majaribio na Reading kabla ya kurejea kwenye kikosi cha Zambia.

Mabingwa watetezi Zambia wamepangwa kuanza michuano hiyo kwa kumenyana na Ethiopia. Taarifa iliyotolewa na tovuti ya Reading juzi ilisema kuwa, Sunzu alipewa ruhusa na Chama cha Soka cha Zambia pamoja na TP Mazembe ya kuondoka kwa muda kwenye kikosi cha timu ya taifa ya nchi hiyo ili kufanya mazoezi na Reading na kupimwa uwezo na makocha wa timu hiyo.

"Stoppila atajiunga tena kwenye kikosi cha Zambia baadaye wiki hii, kabla ya kucheza mechi yao ya kwanza ya fainali za Mataifa ya Afrika Jumatatu ijayo," ilieleza taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, licha ya kuichezea TP Mazembe ya DRC, Sunzu anafahamika vyema na Kocha Mkuu wa Reading, Brian McDermott kutokana na kuwepo kwenye kikosi cha vijana cha timu hiyo alipokuwa mdogo.

Reading ilisema kupitia taarifa hiyo kuwa, Sunzu atafanyiwa majaribio kwa siku nne ili makocha waweze kuona uwezo wake kabla ya kuamua kumsajili kwenye dirisha dogo.

Sunzu ni miongoni mwa wachezaji walioteuliwa kuwania tuzo ya mwanasoka bora wa Afrika mwaka jana.

Beki huyo ndiye aliyeifungia Zambia penalti ya mwisho katika mechi ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka jana na kuibuka na ushindi wa penalti 8-7 dhidi ya Ivory Coast.

Mbali na Sunzu, tayari Reading imeshamsajili beki Stephen Kelly kutoka Fulham, kiungo Hope Akpan kutoka Crawley na Daniel Carrico kutoka Sporting Lisbon ya Ureno wakati wa dirisha dogo.

TFF KUITAFUTIA STARS MECHI NGUMU

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limesema lipo katika mchakato wa kuitafutia mechi ya kirafiki ya kimataifa timu ya Taifa, 'Taifa Stars'.

Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, mchezo huo unaweza kufanyika Februari 6 mwaka huu, ikiwa ni tarehe iliyopangwa na Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA) kwa mechi za kirafiki.

Wambura alisema lengo la mechi hiyo ni kuipa mazoezi Taifa Stars kwa ajili ya kujiandaa kwa mechi yake ya michuano ya kuwania kucheza fainali za Kombe la Dunia za 2014 dhidi ya Morocco.

Taifa Stars na Morocco zimepangwa kumenyana Machi 22 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Wambura alisema lengo la TFF ni kutafuta timu yenye kiwango cha juu ili kuipa Taifa Stars mazoezi ya kiwango cha juu na kuwafanya wachezaji wajiamini.

Alisema Morocco ni timu nzuri na ambayo inashiriki katika fainali za mwaka huu za Mataifa ya Afrika, hivyo ni vyema Taifa Stars ikapata kipimo kizuri kabla ya kuwakabili wapinzani wao.

Tayari Taifa Stars imeshacheza mechi mbili za kirafiki hadi sasa. Katika mechi ya kwanza, iliichapa Zambia bao 1-0 kabla ya kufungwa mabao 2-1 na Ethiopia mjini Addis Ababa.

19 WACHUKUA FOMU TFF

WADAU 19 wa soka nchini wamechukua fomu kwa ajili ya kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), unaotarajiwa kufanyika Februari 24, mwaka huu.

Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, wadau wawili wameomba kugombea nafasi ya makamu wa rais wakati wengine 17 wameomba nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji.

Wambura aliwataja waliochukua fomu za kuwania umakamu wa rais kuwa ni Wallace Karia na Ramadhan Nassib, ambao kwa sasa ni wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF inayomaliza muda wake.

Aliwataja waliochukua fomu za ujumbe kuwa ni Shaffih Dauda, Athuman Kambi, Hussein Mwamba, Stewart Masima, Yusuph Kitumbo, Mugisha Galibona, Vedastus Lufano, Twahili Njoki, Charles Mugondo, Elley Mbise, Farid Nahdi, Ayubu Nyaulingo, Nazarius Kilungeja, Epaphra Swai, Khalid Abdallah, James Mhagama na Selemani Bandiho.

Ada kwa wagombea wa nafasi ya urais ni sh. 500,000, makamu wa rais sh. 300,000 na wajumbe wa kamati ya utendaji sh. 200,000.

Wagombea katika uchaguzi huo, wanatakiwa kuwa raia wa Tanzania, kiwango cha elimu kisichopungua kidato cha nne, uzoefu wa uendeshaji wa soka, wasiwe na hatia ya makosa ya jinai na umri usiopungua miaka 25.

Pia wanatakiwa wawe wamewahi kucheza soka, waamuzi, makocha au kuendesha soka katika ngazi yeyote wakati kwa nafasi ya urais na makamu wa rais, wagombea wanatakiwa kuwa na shahada ya chuo kikuu na uwezo wa kuwakilisha TFF ndani na nje ya nchi.

YANGA, BLACK LEOPARDS KUKIPIGA J'PILI

MABINGWA wa soka wa Kombe la Kagame, Yanga wanatarajia kucheza mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Black Leopard ya Afrika Kusini, itakayopigwa Januari 20 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, mechi hiyo itakuwa kipimo cha kwanza kwa timu hiyo baada ya kurejea nchini kutoka kambini Uturuki.

Mwalusako alisema maandalizi yote muhimu kwa ajili ya mechi hiyo, iliyoandaliwa na Kampuni ya Prime Time Promotions yanakwenda vizuri na wachezaji wana ari kubwa ya kuonyesha makali waliyoyapata walipokuwa Uturuki.

Yanga ilirejea nchini jana alfajiri ikitokea Uturuki ikiwa na kikosi cha wachezaji 27 na viongozi sita na Kocha Ernest Brandts ameamua kuwapa wachezaji mapumziko ya siku mbili.

Kwa mujibu wa Mwalusako, baada ya mapumziko hayo, timu hiyo inatarajia kuingia kambini kwa ajili ya kujiandaa na mechi hiyo na kufanya mazoezi kwenye uwanja wa shule ya sekondari ya Loyola iliyopo Mabibo, Dar es Salaam.

"Tunashukuru timu imerudi salama na wachezaji wote wapo fiti, isipokuwa wamepewa mapumziko ya siku mbili kabla ya kuendelea na mazoezi kwa ajili ya kujiwinda na mchezo wetu dhidi ya Black Leopord," alisema Mwalusako.

Yanga ilikwenda Uturuki kwa ajili ya kujiandaa na mzunguko wa pili wa ligi kuu ya Tanzania Bara, ikiwa ni pamoja na kucheza mechi tatu za kirafiki za kujipima nguvu.

Katika mechi ya kwanza, Yanga ilitoka sare ya bao 1-1 na timu ya daraja la tatu ya Arminia Bielefeld ya Ujerumani, ilichapwa mabao 2-1 na timu Dinzlispor FC ya Uturuki inayoshiriki ligi daraja la kwanza kabla ya kufungwa mabao 2-1 na Emmen FC ya Uholanzi.

TENGA ABWAGA MANYANGA TFF

RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Tenga, ametangaza kutogombea tena wadhifa huo katika uchaguzi mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika Februari 24, mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, Tenga alisema amefikia uamuzi huo ili kutoa nafasi kwa wadau wengine wa mchezo huo kuliongoza shirikisho hilo.

Tenga alisema muda wa miaka minane alioliongoza shirikisho hilo kwake unatosha na kutokana na umri alionao sasa wa miaka 58, anapaswa kupumzika.

Mchezaji huyo wa zamani wa klabu za Yanga,Pan African na Taifa Stars alisema, anaondoka madarakani huku akijivunia kujenga misingi imara ya uongozi ndani ya TFF na pia kumaliza migogoroya uongozi iliyokuwa ikitokea mara kwa mara miaka ya nyuma.

Tenga, ambaye aliingia madarakani mwaka 2006 alisema anamshukuru Mungu kwamba katika kipindi chote cha uongozi wake, ameweza kutimiza malengo yake na pia kurejesha amani na nidhamu ndani ya shirikisho hilo.

"Baadhi ya wajumbe wa mkutano mkuu wa TFF wamekuwa wakiniuliza rais vipi, utagombea, lakini nimewaambia mimi hapana kwa sababu mambo yote muhimu nimeshayafanya na kuyatimiza,"alisema.

Alisema chini ya uongozi wake, walifanikiwa kutengeneza katiba nzuri, inayofanana na ya Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA) kama ilivyo kwa klabu zote zinazoshiriki katika michuano ya ligi kuu pamoja na vyama wanachama wa TFF.

Tenga alisema chini ya uongozi wake, waliunda vyombo huru kwa ajili ya kufanya maamuzi, kupanua wigo wa wapiga na kuongeza kuwa, hakuna tatizo lolote linaloweza kutokea kuhusu soka likashindwa kupatiwa ufumbuzi na vyombo husika.

Alisema soka ya Tanzania imekuwa na mvuto kwa mashabiki wakati wa uongozi wake kutokana na kujitokeza kwa kampuni nyingi kuifadhili Taifa Stars na kwamba mashabiki wa soka wamerejesha mapenzi kwa timu hiyo, tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Rais huyo wa TFF alisema ameona ni vyema ajiweke pembeni ili kuwapa nafasi wadau wengine wa soka kuendeleza yale yote mazuri aliyoyaanzisha na pia kubuni mambo mapya kwa lengo la kukuza zaidi mchezo huo.

Amewashukuru wadau wa soka nchini na kampuni mbalimbali zilizojitokeza kudhamini mchezo huo kwa kumpa ushirikiano mkubwa wakati wa uongozi wake na kuwataka waendelee kufanya hivyo kwa viongozi wapya.

Tenga amewaomba radhi mashabiki wa soka nchini iwapo aliteleza wakati wa uongozi wake na kuongeza kuwa, ni kawaida kwa kiongozi yoyote baadhi ya wakati kufanya makosa na kisha kujirekebisha.

Ametoa mwito kwa wadau wa soka nchini kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu za kuwania uongozi wa shirikisho hilo ili waweze kupatikana watu watakaokuwa na mawazo mapya yatakayochochea maendeleo ya mchezo huo.

Alisema atakuwa tayari kutoa ushirikiano kwa kiongozi yeyote atakayechaguliwa kuwa rais mpya wa shirikisho hilo kwa kuwa anaamini bado mchango wake unahitajika katika kuendeleza soka ya Tanzania.

Tenga aliingia madarakani kwa mara ya kwanza mwaka 2006 baada ya kuwabwaga mwenyekiti wa zamani wa kilichokuwa Chama cha Soka nchini (FAT), Alhaji Muhidin Ndolanga na Michael Wambura.

Katika uchaguzi huo, nafasi ya makamu wa kwanza wa rais ilichukuliwa na Crescentius Magori wakati nafasi ya makamu wa pili ilichukuliwa na Jamal Bayser.

Tenga alirudi tena madarakani katika uchaguzi uliofanyika mwaka 2009 baada ya kumbwaga Jamal Malinzi. Katika uchaguzi huo, nafasi ya makamu wa kwanza wa rais ilichukuliwa na Athumani Nyamlani wakati makamu wa pili alikuwa Ramadhani Nassib.

KESHI: HAKUNA MWENYE NAMBA YA KUDUMU NIGERIA

LAGOS, Nigeria WACHEZAJI wa timu ya soka ya Taifa ya Nigeria wametahadharishwa kuwa, hakuna mchezaji mwenye namba ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo.

Tahadhari hiyo imetolewa na Kocha Mkuu wa Nigeria, Stephen Keshi alipozungumza na waandishi wa habari mjini hapa juzi kuhusu maandalizi ya timu hiyo kwa ajili ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika.

"Nataka wachezaji wenye njaa ya ushindi, wanaojituma na kujivunia kuichezea Nigeria,"alisema kocha huyo, ambaye pia aliwahi kuinoa timu za taifa za Togo na Mali katika fainali hizo zinazotarajiwa kuanza Jumamosi nchini Afrika Kusini.

"Ni vizuri kuwaona wachezaji wakipambana kuwania namba kwenye kikosi changu cha kwanza. Hakuna mwenye namba ya kudumu, lazima wapambane kupata namba na kuendelea nayo," aliongeza kocha huyo.

Kwa upande wake, nahodha na beki wa kati wa timu hiyo, Joseph Yobo aliseme anataka kuifikia rekodi iliyowekwa na Nwankwo Kanu ya kuichezea timu hiyo fainali sita za Kombe la Mataifa ya Afrika.

"Kutwaa ubingwa itakuwa kazi ngumu, lakini naahidi tutafanya kila linalowezekana kuonyesha uwezo wetu. Nawaomba Wanigeria waendelee kutuombea dua na kuiamini timu yao,"alisema beki huyo wa zamani wa Everton,ambaye kwa sasa anacheza soka nchini Uturuki.

Yobo alisema wanakwenda Afrika Kusini kwa ajili ya kupeperusha benderaya taifa lao na kuongeza kuwa, hawatabweteka hadi watakapotimiza lengo lao.

"Bahati nzuri ni kwamba tunaye kocha anayetuelewa na nina hakika wachezaji wapo tayari kuitumikia nchi yao,"alisema.

Yobo alisema lengo lao la kwanza ni kuhakikisha wanafuzu hatua ya makundi na baada ya hapo,ndipo watakapoanza kufikiria hatua ya robo fainali, nusu fainali na kucheza fainali.

Nigeria imeshiriki fainali 10 za michuano hiyo katika miaka 50 iliyopita, imeshinda fainali mbili, imeshika nafasi ya pili mara nne na nafasi ya tatu mara saba.

CHIPOLOPOLO YATAMBA ITATETE UBINGWA

LUSAKA,Zambia

KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Taifa ya Zambia,Herve Renard ametamba kuwa,watafanya kila linalowezekana kuhakikisha wanatetea taji lao la ubingwa wa michuano ya Mataifa ya Afrika.

Renard alisema juzi mjini hapa kuwa,wamefanya maandalizi ya kutosha kwa ajili ya fainali za michuano hiyo, zinazotarajiwa kuanza Jumamosi ijayo ikiwa ni pamoja na kucheza mechi nyingi za kujipima nguvu.

"Watu wengi hawaamini kama tunaweza kutwaa tena taji hili na hawataki kuaminisha hisia zao.Ni rahisi kusema kamwe Zambia haiwezi kutwaa tena taji hili,"alisema kocha huyo, ambaye alijijengea heshima kubwa baada ya kuiwezesha nchi hiyo kutwaa ubingwa wa michuano hiyo mwaka 2012.

 Renard alisema vipigo walivyopata kutoka kwa Tanzania,Saudi Arabia na Angola katika mechi za kirafiki walizocheza hivi karibuni havina maana kwamba kikosi chake ni dhaifu.

Alisema vipigo hivyo vimezidi kuifanya timu hiyo iwe imara na kubaini dosari zilizopo kwenye kikosi chake kwa ajili ya kuzifanyiakazi.

"Iwapo tutashindwa kutetea ubingwa, maana yake ni kwamba timu nyingine ilikuwa bora kuliko sisi. Lakini itakuwa vigumu kuifunga Zambia,"alisema kocha huyo na kuvishutumu vyombo vya habari vya nchi hiyo, ambayo vimekuwa vikikiponda kikosi chake.

Kupona kwa kiungo Rainford Kalaba,aliyekuwa akisumbuliwa na maumivu ya kifundo cha mguu, kumempa ahueni kubwa kocha huyo, ambaye pia atakuwa akiwategemea sana kipa Kennedy Mweene, beki Stopila Sunzu na mshambuliaji Christopher Katongo.

Wachezaji wengine nyota wanaotarajiwa kuwemo kwenye kikosi cha Zambia ni beki Emmanuel Mbola, kiungo William Njobvu na mshambuliaji, Jacob Mulenga, ambao walizikosafainali za mwaka 2012 kutokana na kuwa majeruhi.

Zambia imepangwa kundi C pamoja na timu za Ethiopia, Burkina Faso na Nigeria. Itacheza mechi yake ya kwanza Januari 21 mwaka huu kwa kumenyana na Ethiopia. Renard alikiri kwamba,mechi yao dhidi ya Ethiopia ni muhimu kwa vile iwapo watashinda, utakuwa mwanzo mzuri kwao katika kutetea taji hilo.

TAMASHA LA MA-STAR WA FILAMU JAN 26

SHIRIKISHO la Filamu Tanzania (TAFF) kwa kushirikiana na wanachama wake, limeandaa onyesho maalum litakalojulikana kwa jina la siku ya 'Ma-Star wa Filamu', linalotarajiwa kufanyika Januari 26, mwaka huu katika ukumbi wa Dar Live Mbagala, Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa TAFF, Simon Mwakifwamba alisema, onyesho hilo ni maalum kwa ajili ya kuchangisha fedha kwa ajili ya kujenga ofisi ya shirikisho hilo na kunua vitendea kazi muhimu vya ofisi.

"Katika moja ya changamoto za uendeshaji wa TAFF ni kutokuwa na ofisi pamoja na vitendea kazi muhimu ndani ya ofisi. Vifaa hivyo ni kama vile kompyuta, kabati za kuhifadhia nyaraka, mashine ya kudurufu nyaraka, viti na meza za watendaji," alisema Mwakifwamba.

Aliongeza kuwa, fedha zinazohitajika kwa ajili ya kazi hiyo ni sh.milioni 60, hivyo kwa kupitia onyesho hilo, wana uhakika wa kupata kiasi hicho cha pesa.

Mwakifwambva alisema onyesho hilo limepangwa kuanza saa sita mchana kwa burudani za watoto, ambazo zitadumu hadi saa 12 jioni na kiingilio kitakuwa sh.2,000.

Alisema burudani kwa ajili ya watu wazima zitaanza saa mbili usiku kwa kiingilio cha sh. 15,000 kwa viti vya VIP na sh. 7,000 kwa viti vya kawaida.

Alizitaja burudani zitakazokuwepo katika onyesho hilo kuwa ni pamoja na muziki kutoka kwa wasanii wa filamu wanaojihusisha na fani hiyo, kundi la Shilole Classic na vichekesho vya King Majuto, Kitale, Kingwendu, Snura na kundi lake, Hemed PHD, Masanja Mkandamizaji na Alex wa Michejo.

Aliwataja wasanii wengine wanaotarajiwa kutoa burudani katika onyesho hilo kuwa ni Jackline Wolper, Irene Uwoya, Aunt Ezekiel, JB, Rich Rich, Ray, Steve Nyerere na washereheshaji Ben Kinyaiya na Chiki Mchoma.

Kwa mujibu wa Mwakifwamba, onyesho hilo limedhaminiwa na kampuni za Baucha Records, Clouds Midia, Global Publishers, ASET, Times FM, Steps Entertainment na VANNEDRICK Tanzania ltd.

SIMBA KULIPA DENI LA TRA KWA MAFUNGU

UONGOZI wa klabu ya Simba umesema utalipa kwa mafungu deni la sh. milioni 50.7 inalodaiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Deni hilo linatokana na klabu hiyo kukwepa kulipa kodi ya Lipa Kama Unavyopata (PAYE) kwa ajili ya wachezaji wake wa kigeni waliosajiliwa na klabu hiyo kwa nyakati tofauti, ambao kwa muda mrefu walikuwa hawakatwi kodi.

Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, tayari uongozi wa klabu hiyo umeshawasiliana na TRA na kukubaliana kulipa fedha hizo kwa mafungu.

Mtawala alisema wanalikubali deni hilo na kwamba halikwepeki, lakini kutokana na klabu kukabiliwa na majukumu mengi hivi sasa, hawawezi kulilipa kwa mkupuo.

Alisema hiyo ndiyo sababu iliyowafanya wafanye mazungumzo na viongozi wa TRA na kukubaliana kulipa kwa mafungu hadi litakapomalizika.

Alisema lengo la Simba si kukwepa kulipa kodi hiyo. Hata hivyom Mtawala alisema Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ismail Aden Rage, anatarajia kuzungumzia kwa undani jinsi klabu yake itakavyolipa deni hilo na kulimaliza kabisa.

Wiki iliyopita, TRA kupitia kwa Kaimu Mkurugenzi wa Elimu kwa Walipa Kodi, Hamis Lupenja, ilisema kuwa, TRA inazidai klabu za Simba na Yanga jumla ya sh. milioni 253.7.

Kodi hiyo ni makato ya PAYE ya wachezaji wa kigeni waliosajiliwa na klabu hizo mbili kwa nyakati tofauti na ambao kwa muda mrefu walikuwa hawakatwi kodi kulingana na sheria za kodi nchini.

Lupenja alisema TRA inaidai Yanga sh. milioni 203 na tayari imekwishaifungia akaunti yake ya benki ya CRDB na kwamba akaunti ya Simba haijafungwa kutokana na viongozi wake kupewa muda wa kulipa deni wanalodaiwa.

Alisema hatua ya kuzifungia akaunti za klabu inakuja kutokana na klabu kushindwa kutekeleza wajibu wake na kuongeza kuwa, hatua itakayofuata ni kukamata mali za klabu.

Mwishoni mwa mwaka jana, TRA ilifunga akaunti ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutokana na kudaiwa sh. milioni 157,407.968 zilizotokana na malimbikizo ya makato ya PAYE ya makocha wa kigeni wa timu za Taifa.

'MFUMO WA UTEUZI WA WACHEZAJI TAIFA STARS MBOVU'

KOCHA Mkuu wa zamani wa timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars na Reli ya Morogoro, Dk. Mshindo Msolla amesema ni vigumu kwa timu inayofundishwa na makocha watatu wa kiwango kinachofanana kuweza kupatikana mafanikio.

Msolla amesema timu inapokuwa na makocha wa aina hiyo na iwapo hawatapeana majukumu, ni rahisi kukaribisha majungu na kuwachanganya wachezaji kwa vile kila mmoja atafundisha kwa mfumo wake.

Kocha huyo mkongwe, ambaye kwa sasa ni mfanyakazi katika Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, alikuwa akijibu swali aliloulizwa kuhusu mtazamo wake baada ya uongozi wa klabu ya Simba kuteua makocha watatu kwa ajili ya kuinoa timu hiyo.

Kwa sasa, Simba inafundishwa na Kocha Patrick Leiwig kutoka Ufaransa, anayesaidiwa na Moses Basena kutoka Kenya na Jamhuri Kihwelu.

Leiwig ameingia mkataba wa kuinoa Simba kwa miezi minane, akichukua nafasi ya Milovan Cirkovic kutoka Serbia, ambaye mkataba wake ulivunjwa baada ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa ligi kuu ya Tanzania Bara.

Basena aliwahi kuwa kocha mkuu wa Simba mwaka jana, lakini mkataba wake ulivunjwa kwa madai ya kutokuwa na vyeti wakati Kihwelu, maarufu kwa jina la Julio, naye amewahi kuifundisha timu hiyo kwa nyakati tofauti akiwa kocha mkuu na kocha msaidizi.

"Mimi naushangaa sana uongozi wa Simba kuwateua makocha watatu, ambao wana sifa zinazoshabihiana. Basena na Julio wameshawahi kuwa makocha wakuu katika klabu tofauti na kupata mafanikio, hivyo sifa zao zinafanana na za Leiwig. Wasipopamgiana majukumu, itakuwa ni kukaribisha majungu,"alisema Msolla.

Akitoa mfano, Msolla alisema kilichokuwa Chama cha Soka nchini (FAT), kiliwahi kumteua yeye, marehemu Syllersaid Mziray na Boniface Mkwasa kuwa wasaidizi wa aliyekuwa Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Burkhard Pape kutoka Ujerumani na matokeo yake ni kwamba kulikuwa na mvurugano mkubwa.

Alisema kutokana na kila kocha kuwa na mfumo wake, ilikuwa vigumu kuamua nani aanze kufundisha na wachezaji walikuwa na wakati mgumu wa kuamua wamfuate kocha yupi.

"Ilibidi tulipofika Rwanda kwenye Kombe la Chalenji, tuitishe kikao na kupeana majukumu, "alisema kocha huyo, ambaye kwa sasa ni mtaalamu katika masuala ya kilimo.

Akizungumzia mwenendo wa michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara msimu huu, Msolla alisema amefurahishwa na viwango vilivyoonyeshwa na timu za Azam na Coastal Union.

Alisema wachezaji wa Azam wanacheza kwa kujituma na kwa kutumia mfumo unaoeleweka, ndio sababu wamekuwa wakitoa upinzani mkali kwa timu zingine zinazoshiriki ligi hiyo.

Msolla alisema timu kongwe za Simba na Yanga nazo zinacheza vizuri, lakini kasi yao huwa ni katika dakika za mwanzo na baada ya hapo, wachezaji wanaonekana kuchoka kwa kukosa pumzi na nguvu mwilini.

Hata hivyo, Msolla amezipongeza Simba, Azam na Coastal Union kwa utaratibu ziliouanzisha wa kuwapandisha daraja wachezaji wao wa vikosi vya pili na kuongeza kuwa, iwapo utaratibu huo utakuwa wa kudumu, hazitakuwa na sababu za kusajili wachezaji kutoka nje.

Msolla alisema licha ya kuwepo kwa udhamini wa kampuni kubwa za biashara kwa Taifa Stars, kiwango cha timu hiyo bado kipo chini kutokana na viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuwa na maneno mengi kuliko vitendo.

"Hivi sasa kiwango chetu cha soka kinazidi kushuka chini. Hii ni kwa sababu uteuzi wa wachezaji wa Taifa Stars ni mbovu. Kwa ujumla, wigo na mfumo wa uteuzi wa wachezaji wetu ni mbovu,"alisema kocha huyo.

Akizungumzia ushindi ilioupata Taifa Stars dhidi ya mabingwa wa Afrika, Zambia katika mechi ya kirafiki mwezi uliopita, Msolla alisema ulitokana na bahati zaidi kwa vile timu haikuwa na wachezaji katika safu ya ushambuliaji ya kati.

Alisema ilishangaza kwa mchezaji kama Mrisho Ngasa, ambaye kwa kawaida hucheza kama winga wa pembeni, kuwa mshambuliaji wa kati na kuongeza kuwa, kilichofanyika ni ujanja ujanja kuliko ufundi zaidi.

Msolla alisema Tanzania imejaliwa kuwa na hazina ya wachezaji wengi wenye vipaji vya kucheza soka, lakini tatizo kubwa lipo katika ufuatiliaji wa vipaji, ambao ameuelezea kuwa bado ni mbovu na hautoa nafasi kwa wachezaji wengi, hasa waliopo mikoani kuonekana.

"Viongozi wetu wa soka wanapaswa kuacha ubinafsi na kuweka mbele zaidi maendeleo ya nchi. Vinginevyo, tutaendelea kubaki hapa hapa tulipo sasa,"alisema.

SIWEZI KUACHA MUZIKI WA INJILI-STARA

MWANAMUZIKI anayechipukia katika muziki wa Injili nchini, Stara Thomas amesema kamwe hawezi kuachana na muziki huo kwa sababu ni kazi ya kumtumikia Mungu.

Stara alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, uamuzi wake wa kupiga tena muziki wa kizazi kipya, hauna maana kwamba ameamua kuachana na muziki wa Injili.

Mwanamuziki huyo, ambaye mwaka jana aliamua kuokoka na kupiga muziki wa Injili, alisema kupiga muziki wa kizazi kipya kwake ni kazi ya ziada kwa ajili ya kujiongezea kipato.

"Nitafanya muziki wa kizazi kipya kama kazi, lakini siwezi kuacha muziki wa Injili," alisema mwanamuziki huyo, ambaye alijipatia umaarufu mkubwa wakati alipokuwa akipiga muziki wa miondoko ya zouk na rhumba.

"Nitaendelea kumtumikia Mungu. Nitakapomaliza kupiga muziki wa kizazi kipya, narudi kumtumikia Mungu. Nikipata pesa, naweza kuwasaidia wajane na kufanyakazi zingine za kijamii na za kanisa,"aliongeza mwanamama huyo mwenye watoto wawili.

Stara alisema kwake, kazi ni kazi, cha msingi ni kufuata na kuheshimu maadili ya dini na kumtumikia Mungu. Mwanamuziki huyo mkongwe aliachia albamu yake ya kwanza ya Injili mwaka jana, inayojulikana kwa jina la 'Nani mshamba', ikiwa na vibao vinane.

Mbali na kibao cha Nani alaumiwe, vibao vingine vilivyomo kwenye albamu hiyo ni Petro, Safari ya Wanaisrael, Niambie, Yesu alipokuja, Hauna jibu, Soma Biblia na Jesus You are the hero.

Stara alisema albamu hiyo ni mwanzo wa safari yake ndefu ya kupiga muziki wa Injili na amewataka wapenzi wa muziki huo kujiweka sawa kupokea nyimbo zake nyingine, ikiwa ni pamoja na kuanzisha bendi yake ya muziki huo.

Kabla ya kuamua kuyaweka maisha yake mikononi mwa Yesu, Stara alijipatia umaarufu mkubwa kutokana na vibao vyake maridhawa kama vile Sikia, Sitorudi nyuma, My body, Children rights na Nipigia, alioshirikishwa na msanii AT.

Awali, Stara alikuwa muumini wa dhehebu la Jamatrine, lakini kwa sasa ni muumini wa kanisa la Shalom lililoko Mbezi Salasala, Dar es Salaam