KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, October 3, 2016

SIMBA, YANGA HAKUNA MBABE





TIMU kongwe za soka nchini, Simba na Yanga, ambazo ni watani wa jadi, zimeshindwa kutambiana baada ya kutoka sare ya bao 1-1.

Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, mashabiki wa Simba walifanya vurugu kubwa baada ya kung'oa viti na kuvirusha uwanjani.

Tukio hilo lilitokea dakika ya 23 baada ya Yanga kupata bao la kuongoza lililofungwa na mshambuliaji Amis Tambwe, baada ya kupokea krosi kutoka kwa Mbuyu Twite.

Mashabiki wa Simba walilalamikia bao hilo kwa madai kuwa Twite aliushika mpira kwa mkono wake wa kulia kabla ya kufumua shuti lililotinga wavuni.

Aidha, picha za televisheni za pambano hilo lililokuwa likionyeshwa moja kwa moja, pia zilithibitisha kuwa ni kweli Tambwe aliushika mpira huo kwa mkono kabla ya kufunga.

Baada ya mwamuzi Martin Saanya kutoka Morogoro kupuliza kipenga kuashiria kwamba lilikuwa bao halali, ndipo mashabiki wa Simba walipoanza kung'oa viti na kuvirusha uwanjani.

Vurugu hizo zilidumu kwa dakika takriban tano, ambapo polisi wa kutuliza ghasia ilibidi watumie mabomu ya machozi kuwatawanya mashabiki hao.

Simba ilipata pigo baada ya kiungo na nahodha wake, Jonas Mkude, kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kumsukuma na kumwangusha mwamuzi Saanya.

Katika kipindi cha pili, licha ya kubaki na wachezaji 10, Simba walionyesha soka ya kiwango cha juu na kufanikiwa kusawazisha dakika ya 87 kwa bao lililofungwa na mshambuliaji machachari Shiza Kichuya.

Mshambuliaji huyo, ambaye alikuwa mwiba mchungu kwa mabeki wa Yanga, alifunga bao hilo kwa mpira mrefu wa kona uliotinga moja kwa moja wavuni.
 

No comments:

Post a Comment