KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, October 24, 2016

YALIYOJIRI KONGAMANO LA MABADILIKO YA UENDESHAJI WA KLABU ZA SOKA NCHINI


Kongamano la mabadiliko ya uendeshaji wa klabu za soka limefanyika Jumamosi Oktoba 22, 2016 kwenye ukumbi wa Uwanja Mkuu wa Taifa, Dar es Salaam.

Kongamano hilo lililoandaliwa na chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzani (TASWA) lilishirikisha wadau zaidi ya 60 nchini.

Kituo cha televisheni cha Azam kilionesha live (mubashara) kongamano hilo huku wajumbe wakikubaliana masuala kumi ya msingi.

Kwanza wajumbe walikubali kuwa kuna umuhimu wa kufanya mabadiliko sasa kwa sababu muundo unaotumika kuendesha klabu za soka una matatizo mengi.

Pili iliamuliwa klabu zijiandae vya kutosha kukaribisha mabadiliko hayo ikiwa ni pamoja na kuboresha utawala bora (governance) kwenye uendeshaji wa klabu.

Tatu mifumo yetu kama nchi inawezesha klabu kuwa na aina nyingi za mifumo ya kiuendeshaji hivyo wanachama waelimishwe kwa kina kuhusu mifumo hiyo ili wachague ulio bora zaidi kwa manufaa ya klabu zao.

Nne ili mabadiliko haya yafanyike kwa haki, inatakiwa wamiliki wa timu hizi (wanachama) waelimishwe  vya kutosha juu ya thamani yao ili wajitambue. Kwamba thamani ya klabu kubwa nchini haiwezi kulinganishwa na kiasi cha fedha kinachotolewa na wawekezaji hivyo wanachama wasiingie kwenye mabadiliko wakiwa wanyonge kwa sababu wao ndio wana mtaji mkubwa kuliko hela zinazoletwa kwa ajili ya uwekezaji.

Tano mabadiliko haya hayawezi kufanywa na wanachama na wawekezaji pekee bila kuishirikisha serikali. Hivyo klabu zinapojipanga kwa mabadiliko haya zihakikishe zinashirikisha serikali na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Sita mabadiliko haya yasifanywe kishabiki bali yafanywe kitaalamu ili  kutengeneza msingi Imara utakaoepusha migogoro hapo baadaye.

Saba kuelekea mabadiliko haya, hasa katika kipindi hiki ambacho uelewa wa wanachama ni mdogo, serikali inatakiwa kulinda maslahi ya walio wengi kwa kuingilia kati pale inapoona kuna mwelekeo wa kuwa na mabadiliko yanayominya maslahi ya walio wengi.

Nane mpira ni biashara ya kipekee ambayo mafanikio yake yanategemea jinsi washindani wanavyoshirikiana. Hivyo kuelekea mabadiliko haya wanatakiwa watumike wataalamu wa biashara ya mpira ili klabu zinapobadilika ziweke misingi itakayokubaliana na biashara ya soka.

Tisa  klabu zinao wajibu wa kulinda hadhi zake (brand) kwa sababu eneo hilo ndio msingi wa biashara ya mpira. Hivyo klabu zinapoelekea kwenye mabadiliko, lazima zizingatie hadhi zao zinalindwaje.

Kumi Chama cha Waandishi wa Habari na Michezo kiliombwa kufanya makongamao zaidi hasa kuhusiana na aina ya mabadiliko ambayo klabu zinaweza kuingia kwa sababu inaonekana wanachama ambao ndio wamiliki wa klabu hizi hawana uelewa wa kutosha hivyo inawapunguzia wigo wa kuchagua aina ya mabadiliko.

SHIJA RICHARD
KATIBU WA SEKRETARIETI

KONGAMANO LA MABADILIKO YA UENDESHAJI WA KLABU ZA SOKA

Oktoba 24, 2016.
…………………………………………..

TAARIFA KAMILI

UFUNGUZI

Kongamano lilifunguliwa na Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Mohammed Kiganja kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Prof. Elisante  Ole Gabriel.

Kiganja aliwataka wajumbe kujadili hoja badala ya watu au timu. Alisisitiza wajumbe wajadili mifumo na aina ya mabadiliko ambayo klabu hizi zinaweza kuelekea.

Pia aliwataka TASWA kuhakikisha Waandishi wake wanaripoti taarifa zenye weledi na zenye manufaa kwa familia ya wana michezo.

Aliongeza TASWA iunde kamati ya maadili kwa ajili ya kuwawajibisha wanachama ambao wanaenda kinyume cha maadili.

WACHANGIAJI

PROFESA PROSPER NGOWI- Chuo Kikuu cha Mzumbe

Katika mada yake, Profesa anasema wanachama na wadau kwa ujumla hawatakiwi kuogopa kufanya mabadiliko au kubadilisha namna ya kuendesha vitu kwa sababu hilo ni jambo la kawaida.

Hata hivyo akadokeza kuwa wanachama wa Simba na Yanga hawapaswi kuwa wanyonge kuelekea kwenye mabadiliko hayo kwa sababu mtaji wao ni mkubwa kuliko pesa zinazoletwa na wafadhili.

“….(Wanachama) Mtaji wao mkubwa pengine sio pesa. Mtaji wao mkubwa ni majina yaani brand ya timu hizi. Mtaji mwingine ni historia ndefu ya timu hizi ya zaidi ya miaka 80 na ‘fan base’ kubwa sana. Pia vikombe ambazo timu hizi zimeshida ni mtaji mkubwa sana katka meza ya majadiliano. Hii ni mitaji ambayo thamani yake ni kubwa kuliko pesa. Kwa hiyo wenye timu hizi hawapaswi kuwa wanyonge kifedha mbele ya wawekezaji. Thamani ya mitaji hii hasa brand ni kubwa kuliko pesa.”

Aliendelea kueleza, “Lazima waelewe kama wanakodisha timu hizi, wanatoa na kupokea masharti gani? Hawapaswi kupokea tuu bali nao watoe masharti. Waamue wanawakilishwa vipi katika uendeshaji wa timu hizi katika nyanja zote? Brand ya timu hizi zinalindwa vipi? Ni muhimu pia kujua kuwa kama mwekezaji atataka muda mrefu wa mkataba, Lazima wenye timu wawe na muda na nafasi ya kufanya marekebisho ktk makubaliano baada ya muda fulani, mfano miaka miwili au mitatu badala ya kusubiri hadi mwisho wa mkataba, mfano miaka 10”, anasema Profesa Ngowi ambaye ni mtaalamu wa masuala ya uchumi na biashara.

Profesa Ngowi anasisitiza kuwa kwa mtazamo wa kiuchumi na kibiashara mabadiliko ni jambo la kawaida na halipaswi kuonekana la ajabu.

“Jambo hilo linapaswa kuwa la kawaida kwa yeyote anayependa. Hakuna sababu ya kuogopa kufanya mabadiliko au namna ya kufanya mambo” anasema Profesa Ngowi.

Anaendelea kueleza jambo la msingi katika mabadiliko hayo ni pande zinazohusika hasa wanachama ambao ni wamiliki wa klabu kujua ni kipi wanachokitaka.

“Inavyoonekana wanachotaka ni hali nzuri ya kiuchumi ya timu zao. Sio jambo baya. Wawekezaji nao wanataka maslahi ya kiuchumi nalo sio jambo baya hata kidogo,” anasema Profesa Ngowi.

PATRIC MUSUSA – MENEJA WA MASOKO NA MIRADI KUTOKA SOKO LA HISA DSM (DSE)

Mususa anasema  klabu zinapotaka kuelekea kwenye mabadiliko hasa kwa matarajio ya kuingia kwenye soko la hisa, kwanza zihakikishe zinabadilisha mifumo yao iliyopo sasa ili iendane na mahitaji ya soko la hisa.

Anasema lazima zisajiliwe kuwa kampuni na Wakala wa Usajili wa Makampuni (BRELA) na pia ziandae taarifa za fedha.

Lazima zitatakiwa kuwa na Bodi ya Wakurugenzi (BOD) watakaochaguliwa na wanahisa ambao ni wanachama  wamiliki wa klabu hizo.

Kila mwanahisa atastahili kupata gawio la faida pale kampuni (klabu) yao itakapotengeneza faida na atakuwa huru kuuza hisa yake kama anataka  kuachanana na umiliki katika klabu hiyo.

ANGETILE OSIAH, KATIBU MKUU WA ZAMANI WA TFF

Angetile anasema klabu zikihitaji kubadilisha mifumo yao zinatakiwa kuzingatia utawala bora kwa kutofautisha majukumu sekretarieti na taasisi nyingine zilizopo ndani ya klabu.

Anasema ulimwengu wa sasa mchezaji ni rasilimali(asset) inayothaminishwa kwa fedha kwenye vitabu vya hesabu hivyo klabu lazima iwe na wataalamu watakaoweza kukabiliana na changamoto hizo za utaalamu na nyinginezo.

Anasema klabu lazima ziwe na kurugenzi za uendeshaji, habari, biashara, sheria, fedha na masoko na ziajiri wataalamu kwa ajili ya kuendesha shughuli hizi. Kurugenzi hizo zinahitaji wataalamu kama waliopo kwenye taasisi nyingine za serikali na makampuni binafsi.

Anaongeza kuwa uendeshaji wa klabu lazima uzingatie utawala bora kwa kuzipa Uhuru na mipaka ya kazi taasisi au idara zote zilizopo ndani ya klabu.

Anawakumbusha wadau kurejea azimio la Bagamoyo ambapo Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) lilileta utaratibu wa kutoa leseni kwa klabu zilizotimiza mashari.

Anasema masharti yanayotajwa yakiwemo kuwa na utawala bora, timu za vijana n.k kama yatazingatiwa, klabu nitakuwa katika nafasi nzuri ya kuchagua mfumo wa kujiendesha kama ni wa wanachama au wanahisa.

CHARLES NDAKI, Mtaalam wa Masuala ya Masoko

Ndaki anasema jina la timu (brand) ni rasilimali muhimu inayitakiwa kutunzwa na kuendelezwa kwa sababu ndio msingi wa biashara iliyopo katika soka.

Anasema klabu zinatakiwa kuweka mikakati ya kujipa upekee ili kujitofautisha na wengine kwa lengo la kutumia vizuri jina lake kibiashara.

Anasema kwa kufanya hivyo klabu itakuwa na wigo mpana wa wanachama na mashabiki (fun base) NA hivyo kuwa na uwezo mkubwa wa kufanya biashara kupitia jina la klabu.

MICHAEL WAMBURA – KATIBU WA ZAMANI WA TFF

Wambura anasema serikali ndio inayoweza kulinda maslahi ya wengi katika mabadiliko haya hivyo watumie vyombo vyake kuhakikisha yanafanyika mabadiliko yenye maslahi kwa walio wengi.

Anasema ni vyema mabadiliko yakafanyika kwa kuzingatia Sheria za nchi, TFF, CAF na FIFA hivyo aliviomba vyombo vinavyohusika, TFF, BMT na Wizara kuhakikisha zinawezesha mabadiliko haya kwa manufaa ya klabu, wanachama, wawekezaji na sekta ya michezo kwa ujumla.

HENRY TANDAU
MKUFUNZI WA FIFA

Anasema wadau katika mabadiliko haya lazima wajifunze mifumo minne ya kuendesha soka kablaya kuelekea mabadiliko

Anaongeza tatizo kubwa la wadau wa michezo hawapendo kujifunza wanaendesha klabu kwa mazoea.

Anasema biashara ya mpira ni ya aina yake kwa sababu ili ufanikiwe inahitaji ushirikoane na mshindani wako. Kutokana na upekee huo, biashara hii inatakiwa kuendeshwa na wataalamu wenye weledi nayo.

Anasema Azimio la Bagamoyo ndio lilitakiwa kuwa msingi mkubwa wa mabadiliko kwa sababu limeanisha vitu vingi vizuri ambavyo havijafanyiwa kazi.

Anaongeza kuwa japo tumechelewa lakini tulipofika tungeanza na Azimio la Bagamoyo kuelekea kwenye mabadiliko ya kweli.

JAMAL RWAMBOW, MJUMBE WA BARAZA LA MICHEZO LA TAIFA BMT

Anasema mabadiliko haya hawawezi kufanyika bila kuishirikisha serikali. “Itakuwa ni kujidanganya kuamini kwamba wawekezaji na wanachama wanaweza kufanya mabadiliko haya bila kuishirikosha serikali kwa sababu serikali ndio baba” anasema Rwambol.

Alitoa mwito kwa wadau kuishirikisha serikali na hasa kufuata maelekezo yaliyotolewa na BMT kuhusiana na utaratibu wa kufanya mabadiliko hayo kama klabu zi nataka kuelekea huko.

Mwishowe Katibu Mkuu wa TASWA, Amir Mhando aliahidi kwamba chama chake kitashirkiana wadau mbali mbali kuhakikisha makongamano kama hayo yanafanyika Mara kwa mara ili kutoa fursa kwa wadau ya kujifunza.

No comments:

Post a Comment