KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, October 5, 2016

MALINZI: HATUWEZI KUITELEKEZA SERENGETI BOYS


Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amesema kwamba ataendelea kuwa karibu na vijana na Timu ya Tanzania ya vijana ‘Serengeti Boys’ licha ya kuondolewa na Congo kwenye harakati za kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana zitakazofanyika Madagascar, hapo Aprili, mwakani.

Mipango ya TFF kwa sasa inayoongozwa na Malinzi kwa sasa ni kuiiingiza timu hiyo kwenye program ya timu ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 20 maarufu kwa jina la Ngorongoro Heroes baada ya kuguswa na kilio cha vijana hao ambao walishindwa kujizuia kumwaga machozi mbele ya Malinzi ambaye alifanya kazi kubwa kuwatuliza pamoja na viongozi wengine.

Serengeti Boys ilipoteza mchezo dhidi ya Congo Oktoba 2, 2016. Kwa kupoteza mchezo huo dakika ya pili kati ya nne ya nyongeza baada ya kumalizika kwa dakika 90, kumefanya vijana hao wa Tanzania kuenguliwa kwenye mashindano ya kuwania kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika – fainali zitakazofanyika Madagascar.

Dakika moja ndiyo iliyoipoteza Serengeti Boys kufuzu kwa fainali hizo kwa bao la dakika ya 92 la lililofungwa na Mountou Edoward.

“Niko nanyi, najua mna group la WhatsApp, naomba msifute namba yangu. Iwe humo na mambo yenu mengi naomba mniambie humo, na nitayashughulikia iwe binafsi au kiofisi. Nawahakikishia sitawaacha,” alisema Malinzi alipowafariji vijana hao ambao wanatarajiwa kuingia leo saa 3.00 usiku huu kwa ndege ya Shirika la Ndege ya Rwanda.

“Umri wenu bado sana wa kucheza soka. Program za TFF, CAF na FIFA ziko nyingi pia mnaweza kupata nafasi ya kucheza Olimpiki na kuna michuano mingi, sitawaacha,” alisema Malinzi na kusisitiza ana imani na timu hiyo ambayo kwa dakika 90 za mchezo dhidi ya Congo walipambana kwelikweli kutetea taifa lao pendwa Tanzania.

No comments:

Post a Comment