KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Saturday, October 29, 2016

SERIKALI YASHTUKIA MCHEZO MCHAFU SIMBA NA YANGA, YAWATAKA MANJI NA MOO KUANZISHA TIMU ZAO




SERIKALI imeshtukia mchezo mbaya uliotaka kufanyika katika klabu za Simba na Yanga, hivyo imezitaka ziache mara moja mipango ya kutaka kuleta mageuzi ya mfumo wa uendeshaji.

Agizo hilo la serikali limekuja huku mfanyabiashara na Mwenyekiti wa Yanga, Yussuf Manji, akitangaza kuikodisha klabu hiyo kwa miaka 10 huku mwenzake, Mohammed Dewji wa Simba, maarufu kwa jina la Mo, akitangaza kununua hisa zaidi ya asilimia 50.

Katika agizo hilo lililotangazwa na Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Mohamed Kiganja, serikali imewataka Manji na Mo kuanzisha klabu zao kama alivyofanya mmiliki wa Azam, Said Salim Bakhressa badala ya kuzing'ang'ania Simba na Yanga.

Kiganja amezitaka klabu hizo kusitisha mara moja michakato yote inayoendelea ya kubadilisha umiliki wa timu kutoka kwa wanachama kwenda katika umiliki wa hisa na ukodishwaji hadi kutakapofanyika marekebisho ya katiba za Simba na Yanga.

Amesema klabu hizo zinapaswa kurekebisha katiba zao kwanza kabla ya kufanya mabadiliko hayo kwa mujibu wa Sheria ya Baraza hilo na Kanuni za Msajili namba 442 Kanuni 11 kifungu kidogo cha (1-9) .

Kiganja alisema kuwa mabadiliko hayo yanayoendelea kwenye klabu hizo tayari yameingia dosari baada ya baadhi ya wanachama kwenda mahakamani kupinga michakato hiyo kitu ambacho sio kizuri na pia sio ishara nzuri endapo yataachwa yaendelee.

"Tumesitisha michakato yote ya kubadili umiliki kutoka kwa wanachama kwenda kwa uwekezaji kwa timu za Simba na Yanga mpaka watakapofanya mabadiliko kwa mujibu wa katiba za klabu zao," alisema Kiganja.

 BMT imemtaka mdau au mwanachama yoyote anayetaka kufanya uwekezaji kwenye klabu hizo, ni vema angeanzisha timu yake kama  Bakhressa alivyoanzisha Azam FC ili kupunguza malalamiko kwa vile timu hizo zina wanachama wengi.
Kiganja alisema kuwa michakato hiyo ilitakiwa ianzie kwenye matawi nchi nzima ili maamuzi yawe ya wote kwani mabadiliko yoyote ndani ya klabu hizo lazima yafuate katiba zao.

No comments:

Post a Comment